SoC02 Usikubali kukatishwa tamaa

Stories of Change - 2022 Competition
Jun 27, 2020
6
3
(Kwenye kila sababu elfu za kukata tamaa, ipo sababu moja ya kuendelea kupambana!)

Na; Mashaka Siwingwa

Katika maisha haya ya kila siku kuna mambo mengi ambayo tunakuwa tunapitia wakati tunapambana kusaka ridhiki. Hata hivyo, yapo mambo mbalimbali ambayo yamekuwa yakitukwamisha kusonga mbele. Jambo kubwa na la msingi sana katika harakati za kusaka mafanikio ni binadamu wenzetu, zaidi ni watu wetu wa karibu nasi. Wakati mwingine watu ambao tunaamini kwamba wanaweza kuwa sehemu ya faraja kwetu ndiyo ambao wamekuwa kikwazo kwetu.

Pengine umekuwa ukishangaa na kujiuliza sana kwa nini unapitia changamoto za namna hiyo! Nataka nikwambie kwamba haupo peke yako unayepitia changamoto za namna hiyo. Wapo watu wengi sana na mashuhuri ambao walisifika kwa matendo yao mema kwa jamii lakini bado ilifika wakati wakaonekana siyo kitu tena kwa watu ambao waliwasaidia na kuwatetea kwa namna mbalimbali.

Katika kukuonya usikubali kukata, kukatishwa tamaa ama kurudishwa nyuma kwa namna yoyote ile nataka nikupatie mifano ya watu kadhaa ambao walikuwepo kabla yangu na yako na pengine walikuwa na msaada mkubwa kwa jamii zao kunizidi mimi au wewe lakini bado waliishia kukatishwa tamaa na kuvunjwa moyo japokuwa hawakukubali.

Yesu Kristo, huyu ni moja ya watu ambao walijitoa wao wenyewe bila kusukumwa na mtu yeyote kuja kuukomboa ulimwengu. Watu wa imani hasa wakristo watakuwa wananielewa hapa. Lakini ulimwengu ambao kwao ndiyo alikuja kuutetea na kuukomboa haukuona thamani yake. Ulimdhihaki na kumuona kama mtu aliyekosa kazi ya kufanya.

Hatimaye watu mbalimbali walimfanyia hila na kumtesa na mwisho akafariki msalabani. Kimsingi ni kwamba watu hao hao ambao alikuwa akiwatetea na kuwapambania ndiyo hao hao waliogeuka baadaye na kumuadhibu. Sasa wewe ni nani hata usipigwe vita na kurudishwa nyuma!

Pia, tunamuona mtu kama Martin Luther King Jr namna alivyopambana kwa ajili ya watu wenye asili ya Afrika (Wamarekani weusi). Huyu ni moja ya watu ambao walipambana kwa jasho na damu, katika mvua na katika jua kuhakikisha kwamba wenzake wanaishi maisha ya furaha na amani katika ardhi ya Marekani. Ni moja ya watu ambao walitumia rasilimali za kila namna na walitumia nguvu nyingi sana kupambana lakini bado angalia namna alivyolipwa. Tunaona kwamba mkombozi na mpambania haki huyu anakuja kulipwa mauti tena na moja ya watu ambao alikuwa akiwapambania na kuhitaji uhuru wao.

Aidha, mtu mwingine hapa ni shujaa wa India Mahatma Mohandas Gandhi, ni mtu ambaye historia yake inajieleza. Anatambulika kwa ushujaa wake na namna alivyolipambania taifa na watu wake. Alifanya hivyo kupitia juhudi na maarifa aliyokuwa nayo. Lakini bado alionekana wa kawaida sana na watu walimbeza kila siku. Ipo mifano mingi sana ya kujifunza hapa lakini kimsingi ni kwamba huna sababu ya kukata tamaa na watu hawana budi kuendelea kukupiga vita na kuhakikisha kwamba hufiki popote.

Unachotakiwa kufanya ni kutokumdharau yeyote na kumpa heshima kila mtu ili siku unapofanikiwa kila mtu ajione yeye ni mpumbavu. Heshima yako ipo katika kutokata tamaa baada ya kurushiwa maneno lukuki yenye kukatisha tamaa, kejeli na dharau za kila namna. Ukiwa mtu wa kusikiliza kila unachosemwa huwezi kufika popote na utaishia njiani. Maadui zako watajiona mashujaa sana kwa kukufanyia fitina na kufanikiwa kukukwamisha. Usikubali kurudi nyuma hata iwaje.

Pia, jenga urafiki na watu ambao unauhakika hawawezi kukunafikia kiwango cha kuleta madhara kwenye shughuli zako. Waepuke mapema sana marafiki ambao una uhakika wao ndiyo chanzo cha kuzuia mafanikio yako. Huna haja ya kuendelea kuwa karibu nao japokuwa huwezi kuwatenga na kuachana nao kwa ghafla kama chafya. Anza kupunguza mazoea nao taratibu na ipo siku wao wenyewe wataona hawana umuhimu tena kwako.

Kwenye kila sababu elfu moja za kukata tamaa tafuta sababu moja tu ya kuendelea kupambania ndoto na mipango yako. Ni dhahiri kwamba una mipango mikubwa sana na ndiyo maana ndugu, jamaa na marafiki zako wanapambana kuhakikisha kwamba hufiki popote. Unachotakiwa kufanya wewe ni kutafuta sababu moja tu kati ya hizo elfu moja za kukata tamaa ambayo unajua ni chanzo na motisha kwako ya kusonga mbele. Usikubali kukata tamaa kwa namna yoyote ile.

Zitumie changamoto zao kujiboresha na kujiimarisha kila siku. Wakati mwingine utawasikia watesi na maadui zako wakisema kwamba huwezi kufika popote, bidhaa yako ni mbaya na haivutii, wewe siyo mkarimu kwa wateja na kadharika. Kwenye changamoto za namna hii na nyingine nyingi unaweza kuzitumia na kujiboresha kwa pale ambapo haukuwa vizuri. Wakati mwingine unakuta yale yanayozungumzwa na watesi wako juu yako ni halali tatizo ni kwamba wanasemea pembeni tu. Yatumie hayo kujiimarisha na kujiboresha zaidi na zaidi kwani kwa kufanya hivyo hata thamani yako itaongezeka.

Mshirikishe Mungu wako kwenye changamoto na kila jambo unalopitia. Nafikiri hili ni takwa la imani na dini zote kumtegemea Mungu katika kila jambo. Kuna wakati mwingine unakuta unapitia changamoto ambazo kwa namna ya kawaida ni ngumu kuzitatua na katika hali ya kibinadamu unaona kabisa kushindwa katika kila jambo. Wakati mwingine unakuwa unaona ni kama vile upo mwenyewe unayepitia changamoto za namna hiyo. La hasha!

Ni watu wengi sana wanaokuwa wanapitia changamoto ya namna hiyo lakini kwa bahati nzuri ni kwamba kila mtu amepewa namna yake ya kuzibeba na kuzishughulikia changamoto zake. Mpe Mungu wako mamlaka ya kushughulikia changamoto zako. Mkumbushe kwamba una mzigo mzito wa kuubeba na hivyo unahitaji kupewa mabega imara ya kuubeba mzigo huo.

Hauna kabisa sababu ya kukata tamaa. Endelea kupambania ndoto na maono yako kwa namna yoyote ile.

Ahsante!
 
Back
Top Bottom