Ushuhuda: Kwa akina Dada tu

MTAZAMO

JF-Expert Member
Feb 8, 2011
19,643
33,427
Huu ushuhuda nimetumiwa na mtu nikaona ni share nanyi! Najua yupo mtu utamfaa ...

KILICHOPATIKANA KWA MAOMBI, KITALINDWA KWA MAOMBI!

Nilianza kuhisi tatizo baada ya kuona mbona kama vile ilikuwa nipate ujauzito lakini bila bila? Nikapotezea! Mmh tena ikatokea nikaona bila bila tena. Mmh sasa tayari taa nyekundu zikawaka kichwani, mmh kwa hiyo ina maana na mimi sitozaa tena? Ndio nina watoto wawili wangeweza kutosha kabisa bila taabu ila kujua kuwa nimezingatia vigezo vyote halafu tena haishiki..., hiyo mbaya..! ikafika mahali hali hii ikawa rasmi kuwa pamoja na yote yakiyokuwa yakiendelea mimba hazishiki.

Basi ikapita miezi kadhaa hola! Mara mwaka holaa! Wa pili nao ukapita mweh eti mimi siwezi tena kuzaa? Mbona neno hili ni gumu kwangu. Mungu wangu na ninavyowajua walimwengu uwiii ilitosha kuumiza moyo wangu. Walimwengu wanaumiza kuliko tatizo lenyewe! Walimwengu mweh ntauweka wapi uso wangu...!

Basi kwa vile jambo hili limekuwa tayari niko na utumishi ndani yangu, ikanisaidia sana kuapply mambo ambayo nilishayafahamu yangenisaidia ikiwemo na kutomtegemea mwanadamu wala kutojifunua kwa namna yeyote ile kwa mwanadamu hata awe na ukaribu na wewe kiasi gani hata akwambie anakupenda kiasi gani... so katika masumbuko yote yale moyoni mwangu, maana jambo hili la kushindwa kubeba mimba lisikie kwa jirani, acha tu hayo maumivu yake; NILIAMUA KULIBEBA MWENYEWE NIKAKAA KIMYA KABISA SIKUTAKA KUMSHIRIKISHA YEYOTE YULE.

Nikuombe tu kama unamfahamu mwenye changamoto hii jitahidi sana usiwe kiherehere kumuuliza maswali yoyote yahusuyo changamoto yake, we muombee sirini inatosha! Halafu usije ukamtenda vibaya au kumsemea vibaya akijua na ama kwa kumsemea kwa watu; don't! Narudia Don't! Kwanza unamjeruhi sana halafu machozi yake hayatokuacha salama... Muombee tu!

2‭0‬19, ikiwa ni mwaka wangu wa nne kusubiri bila kufanikiwa kubeba ujauzito, nikaamua kubadilisha maombi yangu na kuweka nguvu kuubwa zaidi rasmi kuliombea jambo hilo na safari hii nilikuwa na ombi kuu moja tu ''Mungu kuna nini, mbona sipati ujauzito?'' Nikashikana na hilo ombi mpaka siku moja nikaota ndoto kuwa nilikuwa napambana kuvuka barabara fulani hivi iliyokuwa imejaa popo wengi mno waliokuwa wapita hapo barabarani kwa nguvu na kasi kubwa kiasi cha kuzuia kabisa watu wasiweze kuvuka maana watakujeruhi tu hata kukatisha maisha, basi mi nikavaa ujasiri na kuvuka huku nilijitahidi kwa shida sana kuwakwepa wasinipate, ilikuwa ngumu mno nikafanikiwa kuvuka pakubwa tu, ile nataka kumaliza tu pale, kumbuka nilikuwa navuka kwa kulala chini maana popo walikuwa wengi mno na wakali sana... mara popo mmoja akanigonga eneo la kiuno mkono wangu wa kulia pale pale usawa wa mji wa mimba mrija wa kulia.

Aliponigonga nikawa na mimi nimefika upande wa pili wa barabara na kunyanyuka na kukimbia mbali, ila tayari nilikuwa na maumivu kiunoni, nikashtuka usingizini ndoto imeishia hivyo, na kiunoni kuna maumivu sehemu ile niliyogongwa..!'' Mi nafahamu elimu ya ndoto kwa sehemu, na ninafahamu kuota popo haikuwa ndoto nzuri kabisa nikajua kuna shida tayari tena ipo katika ulimwengu wa roho , nikamshukuru Mungu na kuingia kwenye maombi. Maana sasa tayari nilikuwa nimepata majibu nina tatizo gani, basi rasmi tena nikaongeza kuomba safari hii nikishughulikia shida niliyokuwa nimeifahamu kupitia ndoto.

Nikiwa katika hali ya maombi ili kutafuta mpenyo kwenye hitaji langu, mwaka huo wa 20‬19, Emaus kulikuwa na kongamano ka kitaifa ka huduma ya maombezi ambapo kwa mara ya kwanza alikuja Padre fulani kutoka Botswana, kama muhubiri kwenye kongamano hilo. Mambo kama haya mi huwa napendaga sana kuhudhuria lakini safari hii nilivutiwa zaidi kuhudhuria kwa sababu ya uwepo wa huyu mtumishi ambaye nilishasikia sifa zake nzuri kitambo sana kupitia rafiki yangu fulani basi ikanisukuma kwenda kwa ajili ya kupata vya huyu mtumishi.

Kweli bana, yaani siku ya kwanza tu kumsikiliza mweh nikasema hapa kuna cha mno, sio kwa mahubiri yale... nikatishe tu kusema baada ya kupambana sana kutaka kuonana naye nilifanikiwa kumuona nilikuwa na mambo mengine kabisa ya kumwambia lakini nikajikuta nimemueleza ndoto ya popo na mimi kutokushika ujauzito kwa takribani miaka minne sasa. Straight akaniambia you know what, adui anataka usizae lakini kwa jina ka Yesu utazaa! kamata eneo ulilogongwa nikuombee...!

Ilisemwa sala fupi tu pale, kisha nikaondoka. Ndio mtu pekee ambaye nilipata amani kumwambia shida yangu na ni vile kwa sababu ni wa nchi nyingine ndio maana nikawa na amani kumfuata niwe mkweli kabisa...! Watumishi wengi siku hizi japo sio wote, shida ya mtu ni mtaji wa kumsema kwa watu na kumuongezea maumivu kitu ambacho sikutaka kabisa kukishiriki ni heri nipambane kwa jinsi nyingine lakini sio kumwambia mwanadamu... basi nikawa tu mtu wa kuomba mwenyewe nakung'ang'ana sana.

Mweh nimepita aisee! Nimepita! Kuna wakati nikiona mjamzito njiani, tayari machozi yameshafika shavuni nafuta chap nisifaidishe wengine, nilimlilia Mungu sana mno. Wakati fulani kuna msalaba ulikuwa unazunguka kwenye maparokia, ukafika kwetu tukaupokea kwenye jumuiya zote na jumuiya yangu nikapata bahati msalaba ukapokelewa nyumbani kwangu na kukesha hapo mpaka kesho yake tulipoutoa kwa misa... nakumbuka jinsi nilivyopata nafasi kukaa mimi na msalaba tu baada ya watu kumaliza mkesha wakaenda kujiandaa na misa yooh yale maombi niliyoomba na ule msalaba mweeeh na tena nilikuwa nipo kwenye siku zile za wanawake, yaani hadi nilitoa pad nakufanya vitu very mysterious nikiomba mno kwa machozi makali nikimwambia Mungu ikimpendeza nisivae tena ile nipakate watoto wangu... Kwa kifupi maombi ndio yakiyokuwa faraja yangu. Kilikuwa kipindi kigumu sana kwangu acha tu!

Nikaendelea hivyo na mwaka wa tano ukafika 2‭0‬2‭0‬. Ndipo siku moja nikaamua niende hospitali nione hili tatizo kama liko mwilini pia na liko kwa kiasi gani. Nikaenda hospital kubwa tu nikaandikiwa ultrasound pamoja na HGS kipimo cha mirija. Basi nikapewa maelezo na vitu vya kufanya kuweza kupatiwa vipimo, nakumbuka jinsi mpimaji alivyonicounsel kuhusu hicho cha mirija, mpaka nikaogopa.. na akasema usije kwenda kugoogle utakatishwa tamaa etc etc kweli aisee siku ya kupima ndio nikajua kwa nini alinicounsel vile mweh kina mama wenzangu poleni sana tuna mapito mengi sana.

Kipimo kiliniumiza mno, maumivu yake duu nilitokwa machozi hadi huruma ! Nimemaliza kupima ilikuwa siku ya ijumaa na tayari muda ulikuwa umeenda sana, daktari bingwa wa kusima majibu alikuwa mmameshaondoka kwa hiyo ingenilazimu kurudi j3 ili kusomewa majibu na dr. Mi nikajiongeza nikamshika mpimaji anipe tu majibu nijue nini kimeonekana, tatizo lipo ama la ndio ilikuwa hitaji langu. Mweh niliahtuka na hali ya mpimaji, mmh nikahisi kitu.. alikataa kabisa kuniambia akasema nimsubiri dr yeye kazi yake ni kupima tu yaani hata ile nuru ya usoni haikuwepo tena! Duh hali tete.Nikavaa ujasiri nikamwambia yule mpimaji ''Kaka

yangu nikwambie tu, majibu yoyote uliyoyapata MIMI NITAZAA!!!'' Akasema sawa kama wewe unaimani ni vizuri kushika imani. Jumatatu asubuhi tayari nilikuwa kwa daktari anisomee majibu yangu, Dr akaniangalia akaniuliza, una watoto wangapi? Nikamwambia, akanijibu bila kupepesa macho, '' Mshukuru Mungu tayari una watoto, maana kwa majibu haya huwezi tena kushika ujauzito na wala usijeukapoteza hela zako, haitowezekana wewe hutozaa tena'' Duuuuu! Eti umesemaje? Unajua nilimuona dr ni mkatili hata kusema kwa huruma mweh! Nikamuuliza ina maana hakuna hata dawa ninayoweza kujaribisha?

Akaniambia tatizo lako linaonekana limekaa muda mrefu na halikupatiwa tiba, maana mrija wa kulia ( ule wa popo) ni kama haupo umeharibika kabisa na wa kushoto umeziba kabisa, labda tujaribu dawa ambayo itakubidi uje siku ya tatu ya mzunguko wako wa mwezi ndio tuone kama itazibua! Ndani yangu nilikuwa na nguvu aaah! Mimi Annamaria yule anayeamini katika uwezo wa nguvu za Mungu, yule aliyemuona Mungu akimshindia kwenye mengi tena ya kustaajabisha sana!

Haya ni maneno ya daktari (mwanadamu) sio mwisho wa maisha nayavunja kwa jina la Yesu! Nikafungua kinywa kwa ujasiri nikamwambia na huyu pia kuwa dr haijalishi ulichoniambia, I am a believer, mimi NITAZAA! Akawa kama anataka kubishabisha sikumpa nafasi nikamshukuru nakuondoka. Ndani yangu nikasema nasirudi kutafuta dawa yoyote! Sirudi.

Sasa ni kama ile vita imerudi upyaa, mbichi kabisa yaani! Nikaanza kukumbuka ahadi zote za Mungu! Nikakumbuka shuhuda nilizowahi kusikia zilizoinua imani yangu! Nikakumbuka uwezo wa Mungu na ishara na miujiza yake...

Basi nikasema hii vita! Sio tu ya kiroho hii pia ni ya kimwili. Maana wengine hawazai lakini wakienda kupima huwa hawakutwi na tatizo lolote , tofauti na mimi naonekana nina tatizo kubwa mpaka mpimaji kashikwa hofu kakataa kabisa kuniambia! Kwa kadiri ya imani yangu nikasema nitainua imani kwa matendo nione mwisho wa jambo hili. Hapo ilikuwa mwanzoni mwa mwezi wa pili.

Kwaresma ya huo mwaka iliyokuwa siku kadhaa baadae, asikwambie mtu vile ilikuwa kwangu, nafungaga kwaresma zote, lakini ile!!! Yayayah nilikuwa na hasira kuu na adui! Yaani ile ya ama zake ama zangu! Nilifunga kwa kuuma mno mno! Aaah nilijiongezea mateso na kujinyima niutiishe moyo wangu hali nikimlilia Mungu anikumbuke!

Mambo mengine ni magumu isipokuwa kwa kufunga na kuomba...! Ungeniona kipindi hiko! Mweh! Niliisha! Nilipauka! Nilikonda! Nilikuwa ovyo, rafu sana! Maana hata saluni niligoma kwenda! Hakuna nywele iliingia kichwani, nivua mapambo yoote, no mahereni. No kuvaa kokoko. Nilivaa nguo nyeusi mwanzo mwisho yaani niliacha viwalo vyote nikaamua kuvaa nguo zilizokuwa na weusi tu! Sikula nyama yeyote wala maziwa wala mayai siku zote 46.

Nilikuwa nafunga hadi jpili yaani kali kali na niliacha kabisa vitamu ice cream, soda, pipi biscuit cakes vyote ilikuwa NO! Nilikuwa nafungua saa 12 nakula mlo mmoja tu wa kichovu mpaka kesho tena... huku nikiomba tu. Kwaresma ikaisha nikamaliza mfungo lakini nikaendelea na maombi yaani nilikuwa naomba ovyo ovyo tu saa nyingine vinaumana naliiia mweh ndio yakawa maisha yangu hayo...

Mungu wangu siku moja sikujua kabisa saa ngapi imetokea eti mimba imeingia, nilichojishtukia ni kule kutema mate sana na uchovu mwingi mno. Kila saa nataka nilale tu mmh nikasema ina maana mimi ni mjamzito? Nikaanza kujifuatilia kwa karibu! Kweli bwana mwezi ukapita bila zile siku! Haaaa nikasema nataka uhakika, nikaamua kupima...! IMOOOOO

Siwezi kuelezea nikaeleweka ile hali niliyokuwa nayo! Miaka mitano ya mateso yakutamkiwa hutozaa usipoteze hela zako huwezi (mweh maneno haya nayakumbuka yalivyoniingia hadi kwenye mfupa) sasa nina habari nyingine! Sasa mimba imoo bana hahaha naucheka wakati ujao! Adui ameshindwa, yule aliyeniharibia sirini ni wakati wa kumponda hadharani!

Alizani amenizika kumbe mimi ni mbegu alikuwa ananiotesha....! Na sasa sio tu nimeota, NIMEPATA NA UZAO!!! Basi kwa ujasiri mkubwa clinic nikafanya hospital ile ile na kwa daktari yule yule aliyesema haiwezekani! Nilipokutana naye alikosa kabisa cha maana cha kuniambia!! Angeongea mbele ya Yesu mshinda kaburi?? Akabaki kuniuliza we unaimani sana ee? Unasali kanisa gani? Basi tu nikaachana naye kwa jicho la 'siku nyingine usirudie tena'

Hivi ninavyoandika ni zaidi ya mwezi mtoto wangu wa kike nimeshajifungua niko naye nyumbani! Nikimtazama siachi kumwambia Mungu asante! Mimi sio mnigeria kwamba wao ndio kila ukiingia mtandaoni unasoma tu shuhuda zao, hata sie tunaweza! Wala mimi sio wa dhehebu fulani yale yanayosifika kuwa na nguvu zaidi kiroho, MIMI NI WA KAWAIDA TU MKRISTU KAMA WENGINE AMBAYE NIMEAMUA KUYAFANYIA KAZI MAFUNDISHO NINAYOJIFUNZA KANISANI! Hivyo tu!

Mimi sina tofauti na wewe rafiki! Fanya kitu juu ya hitaji lako na acha kutazama watu watakupunguzia mwendo! Watu wanaMANENO lakini MUNGU analoNENO la kukusaidia!!!

Nimeshinda tena! Yesu kanifanya mshindi. Yaani najiskia vizuri huku ndani! Acha kabisa! Nimeshaimba nyimbo zote! Nimeshacheza style zote. Ingekuwa nimejianika kwa walimwengu si tu wangekuwa mwiba lakini hata ushindi huu wangepaza sauti '' mimi ndio nimesababisha hadi akapata mtoto'' yoh! Tuheshimiane jamani!

Kwenye litania ya bikira Maria, kunasifa moja isemayo 'Mama mstaajabivu' kwa kiingereza ni Mother most amiable/amicable! Basi kwa kibali cha pekee this beautiful baby is named after that!
anaitwa #Amicable! call her Amica #Mstaajabivu.

Unaweeza kufanya! Unaweeza kutenda! Yaliyo makubwa, Unaweeza Yeesu...!

Asante Yesu.
 
Hahaha ... ukiona binadamu anaamua kusimulia mapito yake bila kujali watu watamchukuliaje kwa utukufu wa Mungu msome utaokota kitu! Inawezekana isiwe sasa lakini ipo siku unaweza kuhitaji such courage.
Nakubaliana na wewe Mungu ni mwema
 
hapo ndio mke wangu ananishangaaga...mm nikiwa na shida nasaligi mwenyewe na kufunga mwenyewe hata wakati mwingine simwambiagi aisee shida hata iwe kubwa namna gani inaisha kama miujiza...sema madhara yake sasa yule aliekuloga au kukupitisha hiyo njia anaweza kufa ghafla sana kama anaendelea kupambana na ww
 
hapo ndio mke wangu ananishangaaga...mm nikiwa na shida nasaligi mwenyewe na kufunga mwenyewe hata wakati mwingine simwambiagi aisee shida hata iwe kubwa namna gani inaisha kama miujiza...sema madhara yake sasa yule aliekuloga au kukupitisha hiyo njia anaweza kufa ghafla sana kama anaendelea kupambana na ww

Isije ikawa wanadamu walifunga kwa ajili ya Jiwe maana naye kafa ghafla sana
 
Daah inatia huzuni nimeisoma yote

Hadi nimehairisha kutoka leo jioni kwenda kuwatapeli wanaume wa mikoani pale sokoni karume
 
Back
Top Bottom