Ushirikina wasababisha kifo cha kikongwe | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ushirikina wasababisha kifo cha kikongwe

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, May 10, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  May 10, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,611
  Trophy Points: 280
  KIILIMO cha kutumia mbegu bora, kufuata utaalamu, kuweka mbolea za kupandia na kukuzia, kimepeleka kilio nyumbani kwa kikongwe wa miaka 70, Kisinza Jiga, ambaye aliuawa kwa kucharangwa mapanga, huku wauaji wakimhoji kwa nini kalima sehemu ndogo na kuvuna zaidi yao waliolima sehemu kubwa.

  Mauaji hayo yalitokea juzi saa 4 usiku nyumbani kwa kikongwe huyo katika kijiji cha Mpeta, kata ya Muze, wilayani Sumbawanga.

  Mauaji hayo yalifanyika huku mkewe akisikia mumewe akiadhibiwa kwa kukatwa mapanga na maadui zake hao waliokuwa wakimuonea wivu wa maendeleo.

  Wauaji hao baada ya kufanya unyama huo, walinyofoa sehemu za siri za kikongwe huyo na kutokomea nazo kusikojulikana.

  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage alisema jana kuwa mauaji hayo yalifanyika juzi saa 4 usiku na kabla ya kufanyika unyama huo, wauaji walimfunika mke wa Jiga kwa blanketi na kuanza kumpiga mapanga mzee huyo.

  Baada ya kumdhibiti mama huyo, wauaji hao ambao hawajajulikana ndipo walipoanza kumshambulia kwa mapanga mzee huyo na aliumia zaidi sehemu za kichwani pamoja na sehemu nyingine za mwili.

  Kwa mujibu wa Kamanda Mantage, wauaji hao walipokuwa wakimcharanga mapanga mzee huyo, walikuwa wakimhoji kwa nini alilima sehemu ndogo na kupata kuliko wao waliolima maeneo makubwa.

  Baada ya wauaji hao kuhakikisha kuwa kikongwe huyo amekufa, walimkata nyeti zake na kutokomea nazo huku wakisikika wakidai kuwa nyeti hizi ndizo zitakazowasaidia na wao kupata mazao mengi msimu ujao wa kilimo.

  Habari kutoka eneo la tukio zinadai kuwa chanzo cha mauaji hayo ya kinyama ni wananchi wa kijiji hicho kukasirishwa na mafanikio makubwa ya kilimo aliyopata kikongwe huyo msimu huu baada ya kulima eneo dogo na kuvuna maradufu ya wakulima wengine waliolima maeneo makubwa huku wakihusisha mafanikio hayo na imani za kishirikina.

  Kwa mujibu wa Kamanda Mantage, hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kuhusu tukio hilo na Polisi inaendesha msako mkali kwa lengo la kuwabaini wote walioshiriki katika unyama huo ili wafikishwe mahakamani.

  Polisi imetoa mwito kwa wakazi wa mkoa huo kuwafichua wale wote wanaohusika katika matukio ya mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina ili kusaidia upelelezi na wakibainika wafikishwe katika vyombo vya sheria na kupunguza mauaji hayo.

  Tangu wakati wa msimu wa mwaka 2007/2008, Serikali imekuwa ikitoa mbegu na mbolea za ruzuku Mkoa wa Rukwa kwa nia ya kuboresha kilimo kiwe na tija kwa mkulima.

  Utoaji wa mbolea na mbegu hizo bora zenye ruzuku sio tu umekuwa ukimpunguzia mkulima gharama za kununua pembejeo hizo za kilimo, bali pia umekuwa ukiambatana na utoaji wa elimu ya kupanda kitaalamu ili mkulima alime eneo dogo na kuongeza mavuno.

  Hata hivyo, kutokueleweka kwa nia hiyo, kumekuwa kukisababisha kukataliwa kwa jitihada hizo kwa baadhi ya watu ambao wakati wa mavuno wamekuwa wakijilaumu kutofuata ushauri baada ya kujikuta walilima eneo kubwa na kupata mavuno kidogo kuliko aliyelima eneo dogo na kufuata ushauri aliyepata mavuno mengi.

  http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=7292
   
Loading...