Wakati wa jua mabondeni hakuna hatari na mtu anashawishika kujenga nyumba, kasheshe ni kipindi cha mvua za masika. Halafu hatujafikia viwango vya uokoaji vya mataifa kama yale ya Ulaya, ukisikia watu watano wamekufa baada ya nyumba kusombwa na maji ujue idadi kamili inaweza kufikia hata hamsini. Ni kweli kuwa inasikitisha sana kuona wajane wakivunjiwa nyumba zao na wakikosa hata ndugu wa kuwahifadhi, lakini twende mbele turudi nyuma miji yote duniani inajengwa kwa kuheshimu ramani zilizopo. Sisi tuliendekeza sana rushwa pale wizara ya ardhi, matokeo yake ndio huu mtafuruku unaoendelea.