Urusi yajitoa ICC

Urusi yajitoa ICC

kalulukalunde

JF-Expert Member
Joined
May 27, 2016
Posts
1,056
Reaction score
1,086
Urusi imesema kwamba inaondoa rasmi saini yake kutoka kwenye sheria inayounda mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, ICC, siku moja baada ya mahakama hiyo kuchapisha ripoti inayokishutumu kitendo cha nchi hiyo kutwaa eneo la Crimea nchini Ukraine kuwa ni cha kimabavu.

Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imetoa tangazo siku ya Jumatano kwa amri ya Rais Vladimir Putin, ikisema kwamba mahakama hiyo imeshindwa kufikia matazamio ya jumuiya ya kimataifa na kushutumu kazi za mahakama hiyo kwamba ni za upande mmoja na zilizokosa ufanisi.

Nchi hiyo ilisaini makubaliano ya Rome mwaka 2000 na ilikuwa ikishirikiana na mahakama hiyo, lakini haijaridhia mkataba huo na kwa hiyo ikaendelea kubaki nje ya mamlaka ya mahakama hiyo. Hii ina maana kwamba, kitendo hiki cha sasa, pamoja na kwamba ni ishara tu, lakini hakibadili mambo mengi kiuhalisia.

“Hii ni alama tu ya kukataa na kusema mengi juu ya tabia ya mtazamo ya Urusi kuelekea haki na taasisi za kimataifa,” akisema Tanya Lokshina wa Human Rights Watch. ”Katika uhalisia haibadili kitu, lakini ni tangazo linaloonyesha mwelekeo wan chi hiyo, inaonyesha kwamba Urusi haina tena nia ya kuridhia mkataba huo siku za usoni au kushirikiana na mahakama hiyo.”

Mwezi Januari, wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ilisema kwamba ilikuwa ikifikiria juu ya mtazamo wake kwa mahakama hiyo baada ya mahakama hiyo kutoa uamuzi wake juu ya vita baina ya nchi hiyo na Georgia.

Wakati huo, msemaji wa wizara hiyo, Maria Zakharova alisema, “Urusi ilisimama katika msingi wa kuanzishwa kwa ICC, na kupiga kura ianzishwe na siku zote imekuwa ikishirikiana nayo. Urusi ilitumaini kwamba ICC itakuwa ni kitu muhimu katika kuhakikisha utawala wa sheria na utulivu katika mahusiano ya kimataifa.

“Kwa bahati mbaya, akilini mwetu, hili halikutokea. Kwa maana hiyo, na kutokana na uamuzi wake wa karibuni, Shirikisho la Urusi litalazimika kufikiria upya mtazamo wake kwa ICC.”

Siku ya Jumanne, mahakama hiyo ilichapisha ripoti ambayo inatambua kutwaliwa kwa Crimea kama kitendo cha kivita baina ya Urusi na Ukraine, na kusema kuwa kitendo hicho ni kukalia kimabavu.

“kulingana na habari zilizopatikana, hali huko Crimea na Sevastopol ni sawa na mgogoro wa kivita baina ya Urusi na Ukraine,” ripoti ya awali kutoka kwa mwendesha mashtaja wa ICC Fatou Bensouda ilisema.

“Urusi ilitumia wanajeshi wake kuingia na kutwaa maeneo yaliyoko katika ardhi ya Ukraine bila kupewa ruhusa na serikali ya Ukraine.”

Urusi imekuwa ikisisitiza kwamba Crimea iliamua yenyewe kujiunga na Urusi baada ya kupiga kura ya maoni, lakini waangalizi wa kimataifa wanasema kwamba kura hiyo iliandaliwa kwa haraka haraka, haikufikia viwango vya kimataifa, na ilipigwa kipindi ambacho wanajeshi wa Urusi wakiingia katika peninsula hiyo. Baada ya kukataa kwa nguvu kwamba wanajeshi wa nchi hiyo hawakuhusika katika kutwaa sehemu hiyo, lakini Putin alikuja kukubali baadae.

Urusi pia huenda ikawa na wasiwasi juu ya mahakama hiyo kuwa na mamlaka nchini Syria, ambako majeshi yake yamekuwa yakishutumiwa mara kwa mara kwa kufanya uhalifu wa kivita katika miezi ya hivi karibuni. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human rights Watch na mashirika mengine yamekuwa yakitaka matukio ya nchini Syria kufanyiwa uchunguzi na mahakama ya ICC.

Kitendo cha Moscow kimekuja wakati wa kipindi kibaya kwa mahakama hiyo, baada ya mataifa matatu ya barani Afrika – Gambia, Burundi na Afrika Kusini – kutangaza kuwa zinaondoa saini zao kwa madai ya kuwa mahakama hiyo imekuwa ikizionea nchi za Afrika.

Raia Mwema

Maoni yangu

Imefikia hatua sasa inabidi, ICC iangalie umuhimu na uhalali wake wa kuwepo, kwa maana imekuwa inashutumiwa kuwa ina kazi ya kuwahukumu viongozi wa kiafrika pekee,

Wako wapi walioua raia nchini Libya, Iraqi amabapo sasa kila mtu anajua wazi kuwa vita vya kumuondoa Gadafi zilikuwa kwa ajili ya masalahi ya nchi za magharibi na marekani, hivyo hivyo kwa Iraqi lakini mahakama hiyo ipo kimya mpaka leo?

Na sisi kama taifa tujitathimini kama kuna umuhimu wa kuend4elea kuwa mwanachama wa mahakama hiyo inayotumiwa na ulaya na marekani kama fimbo dhidi ya viongozi wa kiafrika wanaotufautiana nao kimsimamo na mtazamo.
 
Back
Top Bottom