Uongozi hufanikiwa kwa wananchi kujitambua, kuunga mkono, kukosoa

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
viongozi.jpg


WANADAMU wakishakuwa zaidi ya mmoja katika eneo fulani na wakawa na lengo la aina fulani linalofanana, ili mambo yao yande vyema, wanalazimika kuwa na uongozi.

Hata taasisi ya ndoa ambayo ni muunganiko wa mke na mume inatakiwa kuwa na kiongozi pia, na kwa mujibu wa vitabu vya dini, Mungu alishamchagua mwanamume kuwa kiongozi wa familia. Ninajua wanarakati wa haki za wanawake hawakubaliani sana na hili lakini hii si mada yangu. Jamii za wanadamu toka kuumbwa kwa Adamu (kwa mujibu wa maandiko), zimekuwa zikiongozwa na watu, baadhi wakiwa na mitume na manabii waliotumwa na Mwenyezi Mungu.

Hawa walikuwa na karama zaidi na maelekezo maalumu anayotaka muumba ili binadamu sisi tuyafuate kwa ajili ya ustawi wetu wa hapa duniani na maisha baada ya hapa (ahera). Ukiachana na mitume, viongozi wanadamu baadhi yao wamekuwa na karama au vipaji madhubuti na hivyo kutoa mchango mkubwa wa kuendeleza jamii walimoishi kiasi cha kukumbukwa sana kutokana na mabadiliko chanya walioleta katika jamii zao hata baada ya kuondoka duniani. Hata hivyo, wapo viongozi waliofanya vibaya kwa kudidimiza jamii zao.

Katika kizazi hiki, mmoja wa viongozi wa mfano ni Nelson Mandela ambaye kabla hajatiwa gerezani na utawala wa wazungu wachache kule Afrika Kusini, alisema wazi kwamba ataendelea kupigania upatikanaji wa jamii huru ambamo watu wote wataishi kwa upendo, uelewano, furaha, amani, na haki sawa.

Zipo taarifa kwamba walowezi wa Afrika Kusini walikuwa tayari kumwachia huru Mandela kwa masharti ya kutopigania uhuru wakidhani ni ‘mganga njaa’ tu lakini yeye akawaambia ni afadhali kufungwa kuliko kuishi akiwa huru yeye binafsi huku akipewa manufaa fulani na makaburu wakati jamii yake ikiwa haiko huru.

Alipotoka jela baada ya miaka 27, alirudia maneno yaleyale, kwamba mapambano ya kumkomboa mtu mweusi Afrika Kusini hayatokoma mpaka mazingira ya usawa yapatikane. Makaburu walipoamua kurejesha uhuru kwa wananchi wote ili na wao wawe huru, Mandela akawa kiongozi wa kwanza wa nchi hiyo mzalendo. Lakini, pamoja na madhila aliyopata yeye mwenyewe na yale ya weusi wenziwe, hakulipiza kisasi.

Mengi yalifanikiwa katika uongozi wake wa mpito katika kujenga Afrika Kusini mpya na kuleta umoja, kwa vile wananchi walimwelewa, wakajitambua na wakamuunga mkono. Nchi hiyo inaendelea vizuri sasa. Tukirejea hapa nchini mwetu, Mwalimu Julius Nyerere kwa kushirikiana na wananchi wenzake, alifanikiwa kuongoza harakati za kusaka uhuru na hatimaye tukakabidhiwa uhuru wetu hapo mwaka 1961, tukijitangaza taifa huru la Tanganyika na baadaye, ili kusaka umoja zaidi, tukaungana na wenzetu wa Zanzibar.

Mwaka 1967 uongozi wa Mwalimu ulitangaza Azimio la Arusha ambalo baadhi ya wachunguzi wa mambo wanasema lililenga pia kuwabadilisha fikra viongozi wazalendo ambao baada ya uhuru walitaka sasa kuvaa viatu vya wakoloni wazungu, kwa maana ya kutaka kutumia nafasi zao za uongozi kufaidi jasho la walalahoi kadri wanavyoweza. Azimio hilo lilijielekeza katika kujenga nchi isiyo na matabaka na kuweka maadili makali ya uongozi wa umma.

Wananchi walijitambua, wakaliunga mkono kwa maandamano na vitendo ingawa pia halikukosa wakosoaji. Ingawa wakosoaji walifanikiwa kuliondoa Azimio la Arusha ‘kimyakimya’ kupitia Azimio la Zanzibar, Mwalimu Nyerere amefariki dunia akiamini kwamba hakuna dosari yoyote katika Azimio la Arusha. Hata hivyo, Mwalimu alisema kwamba Tanzania inaweza kukataa Siasa ya Ujamaa inayosisitizwa katika Azimio hilo la Arusha lakini akasema haiwezi kukataa msimamo wa pili wa Azimio hilo ambao ni kujitegemea.

Baada ya Mwalimu, nchi yetu ilipata kiongozi mwingine baada ya kustaafu. Tukawa na Ali Hassan Mwinyi na kama alivyowahi kusema yeye mwenyewe, kila zama na kitabu chake. Mwinyi alituongoza vizuri, akaendelea kuimarisha tunu za nchi yetu ambazo ni pamoja na kuwa nchi isiyo na matabaka kama ya ukabila, nchi ya amani, umoja na upendo . Lakini ni katika zama zake, wakosoaji wa Azimio la Arusha walikuja na Azimio la Zanzibar na bila shaka walikuwa na nia njema kutokana na mahitaji ya ‘zama’ hizo.

Baada ya Mwinyi, akachukua Benjamin Mkapa hatamu za uongozi wa nchi yetu mwaka 1995, kipindi ambacho pia nchi ilikuwa imeondoka kwenye siasa za chama kimoja na kuingia kwenye demokrasia ya vyama vingi.

Awamu yake ambayo ilipewa jina la Uwazi na Ukweli ilijielekeza pia katika kupambana na rushwa na kubinafsisha mashika ya umma. Haya yote yalifanywa kwa nia njema kulingana na mahitaji ya zama hizo ambapo mashirika kadhaa yalianza kuonekana mzigo, lengo likuwa ni kuyafanya yaimarike zaidi katika mikono ya sekta binafsi. Awamu ya nne ilikuwa chini ya Jakaya Kikwete.

Huu ni utawala ilioanza na kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya. Ulijenga imani kubwa kwa wananchi ambao waliupa kila aina ya uungwaji mkono. Rais Kikwete ataendelea kukumbukwa kwa uungwana wake na kuipeleka nchi mbele kadri alivyoweza. Hata hivyo, katika tawala hizo zilizopita kuanzia ya Mwinyi hadi ya Kikwete, kuliibuka mambo yasiyopendeza na ambayo ilikuwa ni lazima uongozi wa sasa uyakomeshe.

Haya ni pamoja na kugundulika kwa kuuzwa kwa mashirika ya umma kwa bei ya kutupwa, baadhi ya mashirika hayo, hususan viwanda kugeuzwa kuwa maghala na mitaji ya wajanja kukopea pesa kwenye benki pamoja na madude mengine ya kifisadi kama kashfa za EPA, Meremeta, Escrow, Richmond na kadhalika. Pia, pamoja na nia nzuri ya Azimio la Zanzibar lililoruhusu viongozi wa umma kuwa na haki ya kufanya biashara, maadili ya viongozi yaliwekwa kando, dhana ikiwa kwamba viongozi wetu wa ngazi mbalimbali wangeweza kujiongoza wenyewe.

Lakini sote tumeshuhudia namna maadili ya viongozi yalivyoporomoka katika kipindi hicho kiasi kwamba sekta ya umma haikuwa tena inatoa matumaini ya kujenga nchi iliyo moja, nchi inayomjali mkulima, mfanyakazi na mvuja jasho.

Ilikuwa inaelekea kuwa mithili ya nchi ya manyang’au ambayo kila lenye nafasi linagombea kukimbia na sehemu ya mzoga bila kujali wengine! Nchi ilikuwa imefikia pabaya ambapo tofauti ya kipato cha wananchi wa kawaida na matajiri au viongozi wao kilikuwa kikubwa sana, hali ambayo hata Spika aliyepita wa Bunge la Muungano, Anne Makinda, alisema kilikuwa kinatishia amani ya nchi baina ya walio nacho na wasio nacho.

Sasa tumeingia kwenye uongozi wa Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli. Kinachoonekana ni kwamba Rais Magufuli ameyaona mambo yaliyojitokeza katika awamu zilizopita yanayotupeleka pabaya na ameamua kuyavalia njuga. Ameona namna nchi ilivyokuwa inatumbukia kwenye ufisadi ambapo rasilimali za nchi ziliwanufaisha wachache. Ameona namna sekta ya umma ilivyokuwa sasa hawaitumikii tena wananchi wa kawaida bali matajiri wachache.

Ameona namna upendo baina ya walio nacho na umma ulivyokuwa unazidi kupotea. Sasa anarekebisha nchi irejee katika msitari. Moja ya vitu ambavyo vinafanya wananchi wawe karibu na viongozi wao ni pale wenye madaraka wanapoamua kwa dhati kushirikiana na wananchi kuondoa zile kero zinazowasumbua kwa muda mrefu ama hata zile za dharura. Hakuna ubishi kwamba kuna waliokuwa wakineemeka na mambo ya hovyo yaliyokuwa yanaendelea kujichimbia mizizi katika nchi yetu na ambao usiku na mchana watataka kukwamisha juhudi za kutupeleka mahala salama.

Ufisadi uliokuwa unafanyika nchini ikiwa ni pamoja na kukwepa kodi unaonesha fika kwamba nchi hii kufika kwenye lengo la kujitegemea kama alivyokuwa akihubiri Mwalimu ingekuwa ndoto. Lakini ninachoamini, wananchi wanajitambua na walio wengi wanaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kupambana na ufisadi na kurejesha hadhi ya sekta ya umma.

Tunachopaswa kujua wananchi ni kwamba ni lazima tutoe ushirikiano wa kutosha kwa viongozi wetu kwani wana nia njema kabisa. Lakini tukumbuke kwamba hawa si malaika. Wanaweza kufanya makosa kwani hata viongozi waliopita walikuwa na nia njema pia lakini kuna makosa yalijitokeza hadi tukafika tulikofika. Kwa makosa tutakayoyaona, tusiyafumbie macho. Muda wa kukosoa ni sasa na viongozi wetu mkubali kukosolewa.
 
Kauli mbiu ya awamu hii haieleweki vizuri. Kazi bila dira matunda yake hayatabiriki, yanaweza kuwa mazuri au mabaya. Waifanyie marekebisho kauli mbiu yao iakisi matokeo ya kazi au matarajio ya taifa.

Hapa Kilaza Tu.
 
Kauli mbiu ya awamu hii haieleweki vizuri. Kazi bila dira matunda yake hayatabiriki, yanaweza kuwa mazuri au mabaya. Waifanyie marekebisho kauli mbiu yao iakisi matokeo ya kazi au matarajio ya taifa.

Hapa Kilaza Tu.

dira maana yake au na wew ni kilaza nin labda , unajua dira ni dubwasha flani kubwa hivi, tumia muda wako japo kidogo kusoma majarida mbalimbali
 
Kauli mbiu ya awamu hii haieleweki vizuri. Kazi bila dira matunda yake hayatabiriki, yanaweza kuwa mazuri au mabaya. Waifanyie marekebisho kauli mbiu yao iakisi matokeo ya kazi au matarajio ya taifa.

Hapa Kilaza Tu.
Mzungusha mikono huwezi kuelewa
 
Naona wanapropaganda mmekuja kupoozesha moto wa wanafunzi wa UDOM na Jesca .
 
Back
Top Bottom