Unapaswa kujitofautisha ili ufanikiwe

Peter Mwaihola

JF-Expert Member
Jun 23, 2022
227
333
Kuna siku tulikuwa kwenye tukio moja la kindugu pembeni kidogo alikaa kaka yangu mmoja tukaanza kupiga stori moja mbili tatu kulingana na uhusiano wetu kama ndugu pamoja na jamii kwa ujumla.

Wakati tunaendelea kupiga stori aliniuliza una mpango gani kuhusu maisha yako ya mbeleni, utaishi wapi utaendelea kubaki kijijini maana ni kwa muda mrefu sikuoni mjini?

Kwa utulivu na umakini nikamjibu kuwa ni kweli kwa wakati huu nimekuwa mtu wa kukaa sana kijijini kwa sababu ya majukumu na hatua ya maisha ninayopitia inakuwa ni vigumu kwenda mjini kutembea tu na kurudi hivyo najipanga ili nikienda iwe jumla nisiwaze tena habari za kijijini.

Akanikatisha kwa kusema inawezekana una majukumu lakini kuna wakati unaweza ukamuachia mtu kitu unachokifanya na kisiharibike wewe ukaendelea na maisha mengine.

Nami nikamjibu kuwa maisha ya mjini na kijijini hayafanani hivyo jambo la kuhamia mjini ni jambo nyeti kwangu linalohitaji maandalizi ya rasilimali wezeshi hasa mtaji kabla ya kwenda huko ili nisiteseke kwa sababu sina wa kumtegemea naamini katika uwezo wangu kwanza.

Akasema mjini kuna fursa nyingi sana kuliko kijijini na sio kila aliye mjini alienda na mtaji hapana wengine walianzia kuchoma chipsi mtaani na wakafanikiwa.

"Hivyo maisha ya mjini yanaweza kukupa changamoto ya kupambana zaidi na kufikia malengo yako kwa wakati hasa ukiwa mtu mwenye elimu kama wewe" alisema.

Nami nikakubaliana na kauli yake lakini nikasisitiza kuwa kila mtu ana uwezo wa pekee na fungu lake la bahati ambalo Mungu amempangia hivyo siwezi kujua nini kinaweza kutokea lakini ni vema kuchukua tahadhari kabla ya kuanza maisha mapya.

Basi baada ya majibizano hayo alinipa funzo moja lenye mfano halisi ndani ya jamii hususani maisha ya vijana wa mjini.

Akasema kuna vijana wengi waendesha bodaboda mjini lakini ukiwaangalia unagundua kuna wenye malengo na wale ambao wanafanya kazi hiyo kwa mazoea hawatamani kufanikiwa zaidi ya pale walipo.

"Ukiwa msomi unaweza hata kuendesha bodaboda lakini ukaifanya kazi hiyo kwa malengo na ikawa kazi yako ya kupita tu kuelekea mafanikio makubwa" alisema.

"Bodaboda msomi ambaye anataka kufika mbali zaidi hawezi kuweka muziki kwenye chombo chake kwakua utamkosesha kusikia sauti za wateja wakiita. bodaboda msomi mwenye malengo chombo chake hakina muziki na anatembea pasipo kuvaa spika sikioni "earphones" ili asikose kazi".

Alisema kuna waendesha bodaboda vyombo vyao vina mziki mkubwa na wao wanavaa earphone masikioni hata mteja akiita wanapita tu hawasikii kitu, hivyo wanaonekana wameridhika na kazi hiyo hawataki kupata mafanikio mengine zaidi.

Alisema mtu ambaye anafanya kazi ambayo haipendi hawezi kuifanya kwa starehe ataifanya kwa malengo ili apate pesa akanye kazi nyingine iliyobora zaidi.

Mwisho akamalizia kwa kusema sio bodaboda tu wanaopaswa kujitofautisha kwenye kazi zao bali hata watu wengine waonaofanya kazi ambazo ni mapito kwenye maisha yao ili waende kwenye kazi bora zaidi za kudumu na manufaa.

Peter Mwaihola
Photo_1709994207380.jpg
 
Back
Top Bottom