Miongoni mwa vitu ambavyo unapaswa kufahamu kuhusu Diwani ya Amani ni kwamba hiki ndio kitabu pekee kilichochanganya aina zote za washairi wa zama hii waliohai.
Humu ndani kuna wale washairi wakongwe wa A-list kutoka nchini Kenya kama Mzee Thomas Koskei, Mzee Mohamed Khamis wa Takaungu, Mzee Ludovick Mbogholi na Mahmoud Sharifu almaarufu Swahibul Iman, lakini pia kuna washairi mahiri damu changa wanaofanya vizuri na kuvuma sana kwa sasa kwenye ushairi wa Kiswahili nchini Kenya kama Swalehe Hussein (Mzora), Valentine Omondi, Halili Malenga, James Obiero ,Mwalimu Oyugi Stephen, Moses Chesire na Kezia Macharia.
Kabla sijawataja baadhi ya wakongwe na washairi chipukizi wa Tanzania bara na visiwani ambao kwamba wino wao umehusika kikamilifu katika kutengeza Diwani hii ya kihistoria hebu tazama shairi hili namba 58 la gwiji wa Ushairi wa kiswahili Tanzania ambaye kwa hakika yeye ndiye miongoni mwa kile kizazi cha kale kilichobahatika kupata barka ya umri hata siye vijana wa kisasa kuweza kumuona na kunufaika naye, huyu ndiye yule gwiji aliyetunga shairi maarufu la Mvaa koti si lake na mashairi mengine mengi yaliyovuma miaka ya themanini wakati wa kizazi cha dhahabu cha Ushairi wa kiswahili nchini Tanzania.
Huyu mwamba ni Rakhisi Filisi anayetambulika pia kama Nassor Mohammed ama Mzee wa Khairati kutoka Uvumba Kibada, na shairi lake laitwa "Kwanza Tuchunge Amani"
SHAIRI Namba 58
KWANZA TUCHUNGE AMANI
Kama huchungi amani, japo unadai haki,
Kwa fujo na tafarani, kwako amani hutaki,
Iwe fujo mitaani, ndio njia ilobaki,
Amani huzaa haki, kwanza tuombe amani.
Amani haki huzaa, mtakapo hamtaki,
Hili mkilikataa, hali mbaya tutabaki,
Haki kama mshumaa, kwenye fujo hauwaki,
Amani huzaa haki, kwanza tuombe amani.
Amani kwetu muhimu, tuache ubaramaki,
Amani inaghalimu, ikienda haibaki,
Hukaribisha mabomu, likirushwa hulidaki,
Amani huzaa haki, kwanza tuombe amani.
Haki kwenye mtihani, zinaporushwa fataki,
Ataijadili nani, watu wa kwenye handaki,
Amani ina thamani, wote tuombe ibaki,
Amani huzaa haki, kwanza tuombe amani.
Amani natuitunze, kama kinywa na mswaki,
Wasojua wajifunze, nakumuomba Razaki,
Na nchi tusiiponze, sisi watu si samaki,
Amani huzaa haki, kwanza tuombe amani.
Baada ya hapo tusonge mbele kwa kuangalia shairi la Mwalimu wa Sanaa aliyewahi kufundisha chuo cha Sanaa Bagamoyo gwiji wa Ushairi Mzee Mustafa Merere liitwalo Ibilisi wa Imani.
SHAIRI Namba 59
IBILISI WA IMANI
Akili tuliza moyo, woga wangu ni Manani,
Tabia mbaya uchoyo, kizazi cha mumiani,
Watu leo koyokoyo, hawakumbuki hisani.
Mali nguvu ya shetani, ibilisi wa imani.
Vurumai ya amana, utu hauna thamani,
Chuki mzazi na mwana, japo yumo mwanandani,
Njozi naota laana, gharika lenye tufani,
Mali nguvu la shetani, ibilisi wa imani.
Imepotea huruma, mja nusu punguani,
Mgonjwa hana huduma, roho kaweka rehani,
Utiriri wa dhuluma, umeshika usukani,

Upweke ni ukafiri, undugu una nishani,
Dini haina kadiri, utashi wa upagani,
Njia panda ya fakiri, mkabala wa jirani,

Hatima mchuma janga, mwiko kula na mtani,
Mchamungu au mwanga, lishe dua na ubani,
Kirago chako mchanga, joho vazi la kafani.

Kwa mwenye kupenda na kuujua Ushairi ataelewa ukubwa wa mtifuano wa hoja, ulumbi na ujagina uliomo kwenye kitabu, kupitia mashairi haya mawili yaliyopakana kwenye mpangilio wa kurasa za kitabu cha Diwani ya Amani.
Ajabu ilioje kitabu kama hiki kuwa ni bure kabisa sababu pekee ikiwa ni mapenzi na uzalendo uliomo kwenye vifua vya washairi hawa 63 wa Afrika Mashariki waliojitoa kukamilisha kazi hii.
Tukipata wasaa katika makala ijayo tutawataja wakongwe wakubwa migogo ya ushairi na vijana mahiri malenga wasifika kutoka Tanzania bara na visiwani walioshiriki katika Diwani hii.
Kwa mawasiliano, maoni na ushauri wasiliana na
+255689969098.