Uliimi huuma kuliko meno

BabuK

JF-Expert Member
Jul 30, 2008
1,845
329
ULIMI una uwezo wa kuuma kuliko meno.

Methali hii inatukumbusha kwamba maneno anayotamka mtu yaweza kuleta maumivu au kumwumiza mtu sana.

Yatushauri kupima maneno kabla ya kuyatamka yasije kuwaudhi na kuwakera wenzetu. Maneno tutamkayo wakati mwingine huwa kero kwani hupotosha maana. Maneno mengi ya Kiswahili yamo vitabuni lakini kwa uvivu wa kusoma, tunatumia maneno yasiyokuwamo.

Neno ’siahi’, kwa mfano, ni ukelele mkali; yowe, unyende, konzi, ukemi, unyange, kibe, ukwenje. Pia siyahi.

’Rumenya’ ni hali ya mwanamume kuhama na kuishi na mwanamke; wekwa kinyumba na mwanamke; mwanamume wa kinyumba. ’Pukachaka!’ ni neno litumiwalo kubeza au kudharau kitu kwa kutokithamini kabisa; yasini! lo! po! ’Pukute’ ni wali uliopikwa kwa kumwaga maji kabla ya kukauka ili punje zisishikane.

Laiti lugha ya Kiswahili ingetiliwa mkazo kuanzia nyumbani kisha shuleni na hatimaye mitaani, wanafunzi wasingekuwa wanashindwa mitihani ya Kiswahili.

Maneno yamo mengi ila watumiaji ni wachache, kama ilivyosemwa katika Biblia Takatifu ”mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache” (Mt. 9:37).

Neno ’pukusa’ lina maana tano: 1 Tunzo apewayo mwari. 2 Toa zawadi kwa mtu kwa ajili ya jema alilofanya; tunza, tuza, tunukia, hongeza, -pa, zawadia. 3 Angusha kitu kama vile matunda, maua au majani kwa kutikisa mti au mmea; popa, angusha, tupa, vurumisha, pukuta, lenga, dekua, vungumiza, vurumiza. 4 Fanya vitobo na kutoa ungaunga kama wafanyavyo wadudu katika nafaka, mbao, nk.; bonga, bungua, toboa. 5 Pukuchua, kokoa, goboa, pukusa, konyoa.

’Poza’ (kitenzi sielekezi) fanya kuwa baridi, fanya ipoe; tuliza mtu aliyekasirika, liwaza, burudisha, fariji, pomoa, pumzisha, furahisha, tabaradisha, lainisha. ’Poza’ (nomino) malipo anayolipwa mtu aliyetendewa kosa ili kumtuliza; dia, fidia, ridhaa.

Pia gongomea, zima. ’Kundavi’ ni shanga nyingi zilizotungwa pamoja na kuwa kama mkanda na huvaliwa kiunoni na wanawake. Mara kadhaa vyombo vyetu vya habari hutangaza, kwa mfano, ”Leo tunaadhimisha kifo cha ...” au ”tunaadhimisha siku ya ukimwi/kifua kikuu/malaria.”

Je, neno ’adhimisha’ linastahili kutumiwa kukumbuka kifo au maradhi? ’Adhimisha’ (kitenzi elekezi) fanya sherehe ya kukumbuka tukio fulani kama vile siku ya kuzaliwa, kufunga ndoa, n.k.; kuza, tukuza, sherehekea, furahia, kumbuka, sifu, heshimu.

Je, tunafurahia vifo au maradhi? Matukio ya ajali, vifo na maradhi hayaadhimishwi bali huwa kumbukumbu; makumbusho. Kwa hiyo kumbukumbu za matukio hayo huitwa kumbukizi. ’Kizalia’ ni kitu au jambo alipatalo mtu kama vile ugonjwa, tabia n.k. kutokana na kurithi kwa wazazi; alama katika mwili ambayo mtu huzaliwa nayo.

Mara nyingi watu wanapokuwa na hasira, hutulizwa kwa kuambiwa ”tuliza munkari” wakiwa na maana ya kupunguza mori (hasira, hamaki). Neno hili kwa hakika lina maana mbili: 1 Kitu kinachokatazwa, kitu kibaya, kitendo haramu, jambo ovu.

Maana nyingine (kidini) ni mmojawapo wa malaika wanaoaminiwa kuwa huwahoji maiti kaburini. ’Mmasihiya’ ni Mkristo ambaye pia huitwa ’Nasara.’ Wengi ni ’Wamasihiya’ na Manasara’. Kwa lugha ya Kisambaa, Wakristo huitwa ’Wamasiya’ na mmoja ’Mmasiya.’ Huu ndio uzuri wa lugha za Kibantu unaokifanya Kiswahili kuwa tajiri wa maneno.

’Tarika’ (kidini) ni mafunzo ya dini ya Kiislamu yanayotokana na uongozi wa shehe au kiongozi fulani wa dini na yaliyojengeka kwa njia za ufanyaji ibada lakini ambayo hayatoki n-nje ya misingi ya dini hiyo.

Pia kundi la watu wanaofuata mafunzo hayo. ’Tariki’ ni njia; shika tariji wende zako/shika njia wende zako; ondoka wende zako. Kufa ’upinda’ ni kufa kwa kawaida; fariki. ’Mtagusano’ ni hali au kitendo kinachoingilia kingine; maingiliano. Mtagusano baina ya viongozi na wachezaji una manufaa kwa vilabu.

’Mtaguso’ ni mkutano maalumu wa Makardinali wa Kanisa Katoliki ambao huweza kubadili sheria za Kanisa hilo. ’Mtang’ata’ ni eneo la pwani ya Tanga kutoka Machui hadi Kigombe ambapo huzungumzwa Kimtang’ata.

’Tasa’ ni neno lenye maana ya: 1 Mwanamke au mnyama wa kike asiyeweza kuzaa; gumba. 2 Namba isiyoweza kugawanyika kwa namba nyingine yoyote isipokuwa yenyewe na namba moja kama vile 1, 3, 5, 7, na 11. 3 Chombo kama bakuli kitumikacho kunawishia mtu maji, tuwasi, towasi na 4 fanya kitu kisieleweke vizuri; tatiza, tanza, tinga, tatanisha, babaisha, kikisa, kanganya.

Pia koroweza, rabishi, bumbuaza, hangaisha, sumbua, zongomeza. Kadhalika hero, upatu (wa shaba). ’Tasua’ ni (ku)fumbua jambo lililofumbwa; tanzua, fundua, tatua, dadavua, tatanua, futu, zongoa, hozahoza, fumua, funua.

Pia sema bila kuficha; sema waziwazi, fichua, fafanua, fahamisha, dhihirisha, sherehi, ainisha, changanua, bambanua, onesha, tafsiri. ’Makiwa!’ ni neno aambiwalo mtu aliyefiwa kwa lengo la kumpa pole kwa msiba uliomfika; yatima, mwanamkiwa.

’Jitanibu’ ni jitenga; jiweka mbali na watu au mji; hepa, jibari, jibanza, jiepushe. ’Guda’ ni kutoa sauti ya kitu kinachocheza ndani ya kitu kingine: Nazi imekauka sana mpaka inaguda. Pia ni mahali ambapo vyombo vya baharini huegeshwa; gati.

Kitendawili: Ngalawa mbili zanibeba – Viatu

Chanzo: IPPMEDIA
 
Back
Top Bottom