Ukweli ulivyo ukitaka kumdanganya mwafrika, mdanganye msomi

KDS

Member
Apr 27, 2013
46
15
UKWELI ULIVYO UKITAKA KUMDANGANYA MWAFRIKA, MDANGANYE MSOMI
Na Victor Makinda- Imechapishwa kwenye Gazeti la RAI (Oktoba 26- November 1, 2017)

Afrika ni bara la giza. Sio giza lenye maana ya giza, la hasha. Giza kwa maana waafrika walio wengi wana uoni hafifu kuhusu kesho yao. Waafrika tulio wengi hatuangalii kesho na kesho kutwa na hata siku baada ya siku hiyo. Wengi wetu tunaangalia leo.

Ni nadra sana kumkuta mwafrika akipanga malengo ya namna mjukuu wake ataishi. Akijitahidi sana atapanga malengo ya namna mtoto wake ataishi, na kuna baadhi hawafikirii kabisa hata vile ambayo mtoto wake ataishi. Wapo waafrika wengi ambao wanaamini kuwa kila mtoto huzaliwa na bahati yake, hivyo hawajishughulishi sana kuipanga kesho ya mtoto huyo. Kazi pekee waifanyayo ni kupata mtoto na sio kupanga namna nzuri ya malezi sambamba na mipango madhubuti ijayo. Jiulize ndugu msomaji kama umejaaliwa kupata mjukuu au lah, je umewahi kuifikiri kesho ya mjukuu wako na kizazi chako kijacho? Jibu hapa litakuwa hapana na kama wapo wenye fikra za baadae za vizazi vyao, hao wanahesabika tena ni kwa uchache mno. Hi ndio sababu tunasema Bara la Afrika ni bara la giza. Ndio, Waafrika tunaona karibu, fikra zetu na mitazamo yetu ni ya karibu mno na tumejivika upofu wa makusudi wa kutoona mbali. Sababu ni nini?

Huenda labda ni mifumo yetu ya elimu haituwezeshi kuwa wapana wa kuijua na kuithamini kesho. Au kiwango cha juu cha ubinafsi ndicho kinachotufanya tusikifiri kuhusu nafsi za wengine na kuishia kufikiri nafsi zetu. Ni ubinafsi, ndiyo Ubinafsi mara zote huzaa usaliti na kutothamini wengine. Waafrika tunasalitiana, tunaumizana, tunanyanyasana, tunauana kwa ajili ya ubinafsi. Wafanyao hivyo hasa hasa ni waafrika wasomi.

Kichwa cha makala hii kimeeleza kuwa ukitaka kumdanganya Mwafika mdanganye mwafrika msomi. Kauli hii sio yangu mimi ni kauli na imani ya watu waishio nje ya bara la Afrika na hata ndani ya bara hili la giza. Hii ni kauli imani na mtazamo mkubwa waliojijengea watu waishio nje ya bara la Afrika. Wamerekani wanaamini hivyo. Wahindi, Waarabu na Waislaeli wanaamini hivyo. Waingereza, Wafaransa, Waitaliano na watu wote waishio bara la Ulaya wanaamini hivyo. Ndiyo wanaamini njia nzuri, nyepesi na rahisi kabisa ya kufanikiwa kupata chochote ukitakacho kutoka nchi yoyote barani Afrika ni kuwatumia wasomi wa Kiafrika. Naam, Afrika ni vigumu sana kumdanganya Mwafrika asiyesoma, ni rahisi sana kumdanganya mwafrika msomi. Na tujiulize swali, kwanini iwe rahisi kumdanganya mwafrika msomi iwe vigumu kumdanganya Mwafrika asiye msomi?.

Ukweli ulivyo mwafrika asiye msomi anapungukiwa sana na kiwango cha ubinafsi. Mwafrika asiye msomi anapungukiwa sana na kiwango cha tamaa, uchu wa mali na madaraka na ni mwepesi kuridhika. Kinyume chake Mwafrika msomi ni mwenye utajiri wa viwango vya tamaa, uchu wa mali, ubinafsi na madaraka. Mwafrika asiye msomi nimwenye kutilia shaka kila jambo nani mdadisi mno. Mwafrika msomi anajua ukweli ulivyo lakini kwa kuwa ameshiba ubinasfi, tamaa uchu wa mali na madaraka hufumba macho, hujitia upofu na uziwi. Hujaa kiburi cha kutaka kupata yeye pasi kuangalia wengine. Hutumia mwanya wake wa usomi kutaka kuishi maisha bora na kujilimbikizia mali pasi kuliangazia kundi kubwa la wasio na elimu na walio na hali duni za maisha. Naam, Ukweli Ulivyo Mwafrika kadili anavyopata elimu na kuzidi kuelimika katika nyanza na sekta mbali mbali, ndivyo anavyoongeza kiwango chake cha ubinafsi na tamaa, uchu wa mali na madaraka.

DHANA YA WAAFRIKA KUWAAMINI WAAFRIKA WASOMI.
Dhana hii Waafrika wasio wasomi kuwaamini Waafrika wenzao wasomi ndiyo kabuli hasa la mateso, manyanyaso, dhurma, laghai, ukandamizaji, uporwaji na ufukarishwaji wa jamii pana ya kiafrika ambavyo haikubahatika kupata elimu.

Koo nyingi za Kiafrika hazikubahatika kupata elimu ya kigeni. Kwa bahati mbaya sana wakoloni walitunyima waafrika fursa pana ya kupata elimu kwa ujumla wetu. Wachache kutoka baadhi tu ya koo na jamii fulani fulani ndio waliobahatika kupata elimu ya kigeni. Watu hao waliobahatika kupata elimu hiyo ya kigeni waliaminiwa na wazungu. Kwa kuwa waliaminiwa na wazungu ilituaminisha Waafrika kuwa ukiwa msomi ni mtu mwenye kuaminika. Matokeo yake Waafrika tulio wengi tunawaamini sana ndugu zetu walio wasomi tukidhani kwa kuwa ni wasomi basi watakuwa na uwezo wa kupembua, kutafakari, kubainisha na kuainisha masuala ambayo yapo kinyume na haki za biniadamu na maendeleo. Sivyo ndivyo. Na ndivyo wazungu waaminivyo. Hutumia mwanya huo kutulaghai kupitia watu tunaoowaamini ambao sio waaminifu.

Pasipo kujua kuwa wasomi hawa wa Kiafrika, baada ya kupata elimu na kuelimika, viwango vyao vya unafiki, ubinafsi na tamaa ya mali vimeongezeka mara dufu. Hawa wamekuwa chanzo cha kutuuza na kutuangamiza na kuzidi kutukandamiza katika lindi la umaskini wa fikra na kipato. Kosa jingine kubwa ambalo waafrika tusio wasomi tumelifanya na tunaeendelea kulifanya ni kuwaamini wasomi hawa wa Kiafrika kuwa wanaweza na kufaa katika nyanza za uongozi. Kwa sasa moja ya sifa za kuwa kiongozi ni kuwa na elimu ya kigeni ya kiwango fulani. Tena kuna baadhi ya nyazfa zinataka elimu ya Shahada au shahada ya uzamili au uzamivu. Bila kujua hawa wenye shahada za uzamili na uzamivu, viwango hivyo vya elimu vimewafanya kutokuwa Waafrika. Wamebaki Waafrika kwa kuwa walizaliwa ama kuishi barani Afrika. Roho zao na nafsi zao zimekengeuka mno. Zimekengeushwa na usasa na Umagharibi. Hawana uzalendo kwa nchi zao na kwa jamii walizotoka. Wamejaa ubinafsi uliotamalaki.

Sina chuki na wasomi, hapana. Siwachuki wasomi. Sisemi ni wasomi wote wa kiafrika wapo hivyo, laha hasha, wapo wasomi wachache a kiafrika ambao wana uchungu na uzalendo uliotukuka kwa Afrika na Waafrika wenzao. Lakini walio wengi wasomi wa kiafrika uzalendo kwao ni msamiati mkubwa. Wanatumia usomi na ujuaji wa wao wa mambo kutudanganya na kutuuza mchana kweupe. Hawana tena huruma na sisi waafrika wenzao. Tamaa zao, ubinafsi wao ni mauti kwetu.

MIKATABA NA UBINAFSI WA WASOMI WA KIAFRIKA.
Nchi nyingi za kiafrika zinalalamikia mikataba mibaya mno baina ya nchi hizo na wawekezaji wa mataifa ya Ughaibuni. Tunayo mifano mingi. Hapa kwetu Tanzania, baada ya kumpata moja katika wasomi wachache waliobaki na moyo wa kizalendo wa kiafrika, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Mafuli, ameangazia tena kidogo tu juu ya mikataba ya uchimbaji wa madini baina ya Tanzania na wawekezaji katika sekta hiyo muhimu. Kilichobainika kila moja nishahidi. Ni madudu yaliyopindukia. Wasomi tuliowaamini walisaini mikataba kana kwamba walikuwa wamefumba macho au walikuwa gizani! Imebainika kuwa tumeibiwa matrilioni ya shilingi na makampuni haya ya kigeni. Na hii katika sekta ya madini tu. Bado maeneo mengine. Tujiulize swali, ni nani aliyeingia mikataba hiyo feki ya hovyo na yenye kufukarisha jamii. Jibu ni Waafrika/watanzania wasomi walio na utajiri wa ubinafsi na uchu wa mali, waliopungukiwa na uzalendo na huruma kwa jamii ya kitanzania. Walio na fikra za giza kuhusu kesho ya Taifa hili. Walio na upeo mkubwa wa ubinasfi wa matumbo yao, watoto wao na nyumba zao ndogo. Wametuuza.Wameuza rasilimali ambayo ingekuwa mkombozi wetu katika lindi la umaskini uliotopea. Nakasirika sana.

Hali ni mbaya, umaskini ni wa kutisha, Hospitali hazina madawa, pembejeo za kilimo ni shida. Maradhi yanatuandama, makazi duni, hatuna miundombinu mizuri ya uhakika. Mungu ametujaalia rasilimali hii ya madini, lakini Watanzania wenzetu, wasomi tena wa viwango vya juu kabisa, ambao wamesoma kwa kodi zetu, tumewaamini kuwapa madaraka na mamlaka, wanatusaliti kwa kusaini mikataba isiyo na tija kwetu kwa ajili ya ubinasfi wao, inauma sana.

Nini kifanyikeili Waafrika tuondokane na kadhia hii ya wasomi wa Kiafrika kutuuza na kututweza kwa ajili ya ubinasfi wao uliopindukia….
 
Back
Top Bottom