Ukuta wa gereza

Ukuta wa gereza

FEBIANI BABUYA

JF-Expert Member
Joined
Mar 5, 2022
Posts
2,229
Reaction score
4,345
STORY: MIAKA 15 NYUMA YA UKUTA WA GEREZA
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: +255621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE 18+

UKURASA WA KWANZA
MLANGO WA GIZA
Kwenye kuta ambazo zilionekana kuchoka, hazikuwa zimepakwa rangi kwa muda mrefu lakini zilikuwa imara kwa sababu ya ubora wa ujenzi ambao ulitumika kuziandaa zilisikika kelele nyingi watu wakishangangilia kwa furaha kubwa. Ni eneo ambalo lilikuwa na kiza maeneo mengi, ni sehemu chache tu ambazo zilikuwa na taa ambazo zilifanya maeneo hayo kuonekana vyema.

Watu walikuwa na raha, walilipuka kwa furaha kubwa wakiwa wanashuhudia baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yanaendelea humo ndani, haikuwa furaha ya watu kushinda maisha bali wengi wao walikuwa wakipata burudani kubwa ambayo iliwafanya watu hao kuweza kufurahia siku zao ambazo walibahatika kuzipata hapa duniani. MLANGO WA GIZA, ulikuwa ni ulingo maalumu wa siri ambao ulikuwa unaendesha mapigano ya hatari yasiyo rasmi. Eneo hilo halikuwa tu hatari kwa sababu ya kutofuata sheria na taratibu za nchi bali uhatari wake zaidi ulikuwa unakuja kutokana na kwamba watu walikuwa wanafia kwenye hilo eneo, ulikuwa ni ulingo ambao watu walikuwa wanapigana ili kuweza kuuana.

Walikuwepo matajiri ambao walikuwa wanaenda kuangalia mapambano hayo, hao walikuwa wakitoa pesa nyingi ili kuweza kuona damu za watu zinamwagwa hivyo wapiganaji hawakuwa mbali kuweza kuhakikisha wanajibebea pesa hizo kwa kuua wenzao. Maisha yaliwafundisha ukatili, hawakuwa na sehemu nyingine ya kuweza kwenda zaidi ya kuzipigania kesho zao kwa kutoa nafsi za watu wengine.

“Hili jengo lina thamani kubwa kwa watu wa burudani, watu ambao wapo nje ya hapa hawawezi kuelewa ni kipi kinaendelea humu ndani lakini nakiri kwamba hii dunia ina watu ambao hawakupaswa kuzaliwa, huwezi kuwa na roho ya kuua wenzako kwa namna kama ile”

“Ndugu yangu usiilaumu dunia wala wanadamu, kuna namna maisha yanatufundisha mambo mengi na kuweza kuwa na maamuzi tofauti, hata hawa wauaji huenda wakiwa bado wadogo hawakuwahi kuwaza hata siku moja kwamba wangekuja kuishia eneo kama hili kwa ajili ya kumwaga damu za watu. Ukiwa na machaguo mengi kwenye maisha yako unaweza ukawa unawalaumu lakini siku ukiishiwa machaguo unaweza ukajikuta unakuwa mmoja wao na ndipo maisha huwa yanabadilika moja kwa moja. Na jambo baya zaidi kuhusu damu ya mwanadamu ukiimwaga siku moja tu inaanza kukupatia hamu kubwa ya kuendelea kuimwaga kila siku kwahiyo mpaka siku unakuja kushtukia jambo kama hilo unakuwa umechelewa pakubwa na dunia inakuwa sio sehemu salama kwa upande wako”

“Mhhhhh nawaza namna tulivyo na binadamu wakatili humu ndani, sijajua kama dunia ingekuwa vipi ingetokea watu wote wakawa hivi”

“Huenda labda haujaitembelea dunia kwa undani wake na kuwajua watu waliopo, kuna watu ni wakatili zaidi ya hapa ila huwa wanayafanya mambo yao kimya kimya ili wasiweze kutambulika na mtu yeyote. Watu wa-siri ndio ambao wanapata mafanikio makubwa kwenye maisha kwa sababu hakuna mtu ambaye anakuwa pale kwa ajili ya kuwafuatilia tofauti na watu ambao wanapiga makelele muda wote huwa hawafiki mbali. Haya majumba kila siku yanatoa maiti za kutosha serikali haijui na hata wale ambao wanajua wananyamazishwa na nguvu ya noti sasa unahisi yatafika wapi? Sisi ambao ni wakamalia kama mimi na wewe hapa tunaingiza pesa za kutosha kuhusu hili, wapiganaji wanaingiza pesa za kutosha wakiwa wanawafurahisha matajiri ambao ni wadhamini wakubwa wa haya mashindano, sasa unategemea haya mambo yataacha? Pesa ina nguvu kubwa ndugu yangu, hata wewe hapo ikiwekwa pesa ambayo inatosha kuishawishi nafsi yako kuna siku unaweza kutuma watu wa hatari kama hao kuja kuniua ama kuninyooshea bastola na hautakumbuka kama wewe ni mkatili bali utaangalia kwanza kuiridhisha nafsi yako”

“Mhhhh nadhani ni muda wa kuangalia ngumi sasa, haya mambo tuyaweke kabatini kwa sasa kwa sababu maongezi yetu yanaelekea mahali ambapo sio salama kwa ukubwa huu tulio nao” walikuwa ni matajiri wawili ambao walikuwa wamekaa viti vya juu vya heshima ambako sio kila mtu alikuwa anaruhusiwa kufika. Walikuwa ndani ya ulingo wa mapigano, ulingo ambao ulikuwa ni hatari kwa watu ambao walikuwa wana mpango wa kuishi maisha marefu. Ulingo huo ulikuwa unaendeshwa kwa usiri mkubwa, vyombo vya sheria havikuwa na taarifa ya uwepo wake hivyo kufanya mauaji kuwa sehemu ya kawaida ya eneo hilo. Halikuwa eneo ambalo lilikuwepo kwa ajili tu ya burudani bali ilikuwa ni sehemu kwa ajili ya mauaji.

Wapiganaji walikuwa wanapanda ulingoni kuuana, yule ambaye angefanikiwa kuua watu wengi angeondoka na pesa za kutosha. Ilikuwa ni michezo ya kamari lakini kwa wakati huo huo ilikuwa sehemu ya burudani kwa matajiri wenye pesa nyingi ambao walikuwa wanaenda kwa siri humo ndani kufurahia huku wakiwa makini kutoonekana kwenye macho ya watu wengi kwani nje ya hapo walikuwa ni watu ambao walikuwa wakiigiza kuwa wema mbele ya jamii hivyo hawakuwa tayari kuona maisha hayo yakiwaharibia nje ya hapo. wanaume hao wawili ambao walikuwa wanaizungumzia michezo hiyo walikuwa wakikumbushana kuhusu uwepo wao humo huku mmoja akionekana kuwa na maelezo mengi zaidi kuhusu mambo ambayo yalionekana kama kuanza kumshtua mwenzake hivyo akaamua wageukie ulingoni kuweza kushuhudia mapambano ambayo yalikuwa yakiendelea.

ULINGONI
Mwanaume mmoja ambaye mwili wake ulikuwa umetuna, lilikuwa pande la jitu huku akiwa kifua wazi alionekana akitamba kila sehemu ndani ya ulingo ule ambao sakafu yake ilikuwa ni zege. Haikuwa na mvutiko wa kuweza kusaidia mpiganaji akianguka chini, lilikuwa limewekwa zege ili kurahisisha watu hao kuuana. Bwana yule alikuwa akitamba baada ya kuivunja shingo ya mwanaume mwenzake na damu zikawa zimetapaa eneo hilo. Kwa usiku huo alikuwa amefanikiwa kuwaua watu watatu ndani ya dakika kumi na tano tu pekee hivyo alikuwa ameshinda zaidi ya shilingi za kitanzania milioni mia moja ndani ya hizo dakika kumi na tano. Ule uhatari ambao alikuwa nao ndio ambao uliwafanya wengi kuanza kusita kusimama naye, ilikuwa ukiingia pale ulingoni ni lazima uweze kupoteza thamani yako ya kuendelea kuwa hai.

Promota alikuwa akitamba wakati ambao watu walikuwa wamefurika kwa furaha kubwa, shangwe ilikuwa inapigwa kila kona watu wakitaka ngumi ziendelee kupigwa lakini wahusika walikuwa wanaogopa. Ilikuwa inatangazwa kwamba kama kuna mtu alikuwa anahitaji kuweza kuzipata pesa hizo alitakiwa kwenda kumuangusha bwana huyo ili aweze kuondoka nazo kwa wakati huo lakini kulikuwa kimya. Watu wote walitulia wakati wakisikilizia ni nani angeweza kuingia, waliamriwa kuweza kuketi kwa sababu hiyo ili kama kuna mhusika ambaye angeweza kwenda hapo aweze kuonekana na kutambulika kirahisi. Watu wakiwa wameanza kukata tamaa ya kupata burudani kwa usiku huo, alisimama bwana mmoja ambaye alikuwa amevaa vesti fupi kwenye mwili wake, mwili wake ulionekana kukomaa kiasi lakini hakuwa mtu wa kutisha, kusimama kwake kuliwashangaza wengi lakini kuliwapa burudani kwa wakati mmoja kwani walijua wanaenda kupata burudani ila hofu yao waliamini burudani hiyo isingeweza kudumu kutokana na mtu mwenyewe alivyokuwa.

Kila kona ulitawala ukimya, kila mtu alibaki ametulia tu wakiwa hawana la kuongea, kila mtu ni kama hakuwa akiamini kama bwana yule kweli alikuwa anahitaji kwenda ile sehemu kwa ajili ya kupigana na jitu lile hasa baada ya kuona wenzake wakiwa wanauliwa. Alitembea taratibu kuelekea kwenye ule ulingo hali ambayo ilimfanya hata mpinzani wake abaki anashangaa, hakuonekana kuwa mtu wa aina yake hivyo hakuelewa ni kipi kilimfanya mwanaume yule aweze kujisogeza pale kuweza kupambana naye usiku ule.

“Una uhakika na haya maamuzi yako?” ilikuwa ni sauti kutoka kwa promota kuhitaji kupata uhakika kwa bwana yule.

“Umesema nikishinda naondoka na shingapi usiku huu?”
“Mpaka sasa ni milioni mia moja za kitanzania”

“Nipe dakika mbili tu namuua huyo mtu” sauti yake ilisikika kwa watu, kuna ambao walishangilia na ambao walizomea. Watu walitaka burudani hivyo promota alimuonyeshea mkono bwana huyo wa kwamba kama alikuwa anautaka ulingo basi nafasi ilikuwa ni yake kuweza kuonyesha manjonjo yake wakati huo”

Yule bingwa wa ulingo aliona kama dharau kijana kama yule kumuendea kimasihara namna ile kwa kuwa hakuwa kwenye levo yake. Alimkimbilia kwa nguvu zote na kwenda kukita mguu wake juu ya kichwa chake lakini alimkosa mguu ukashuka mpaka chini kwenye zege, aligeuka na kumuona kijana yule akiwa pembeni anaichezesha miguu yake taratibu huku akizimezea mate zile milioni mia moja ambazo aliahidiwa kama akipata ushindi. Alimfuata tena kwa nguvu zote ambazo zilikuwa zimechanganywa na hasira za kutosha, mkono ulikita kwenye kamba akaukwepa, alipangua ngumi kali yenye maumivu ndani yake akayumbia pembeni.

Aliona mikono inakuja tena upande wake akajivuta kwa nyuma na kuunyoosha mguu wake mpaka kwenye kamba, alijirusha na Kamba ikamsaidia akapishana na mwanaume yule ambaye alienda kupiga hewa ila wakati anageuka alikutana na ngumi kali ya koromeo kutoka kwa kijana yule. Ile ngumi ilimfanya kupatwa na hasira akiwa amejishika eneo hilo akakohoa na kujiweka sawa ili arudi tena. Zile hasira zilimfanya kutumia nguvu kuliko akili hivyo alienda na mwili mzima bila hesabu nzuri, alikuwa anakimbia lakini alishangaa hata kijana yule naye anamfuata kwa kasi zaidi yake, alipo msogelea kijana yule alijizungusha kama anataka kuruka sarakasi ya juu hivyo bwana yule akayumbia kushoto kwake kumkwepa ili amtwishe ngumi nzito lakini mwenzake alimdanganya kwa kumuuza kijinga.

Ndiyo kwanza tunaanza sehemu ya kwanza kabisa ya simulizi hii ya MIAKA 15 NYUMA YA UKUTA WA GEREZA, kuna mengi ya kuyasoma humu ndani kuhusu uhalifu, maisha yanavyo wabadilisha watu, namna watu walivyo tayari kufanya jambo lolote kwa ajili ya maisha yao, uhalifu, siasa, mapenzi na namna pesa inavyo-yabadilisha maisha ya watu.

Nyuma ya kalamu nipo mwenyewe FEBIANI BABUYA

SIMULIZI HII INA VIPANDE 117 vilivyoshiba haswa..... Unaweza kuipata vyote kwa SHILINGI 5000 TU ZA KITANZANIA ambapo utachagua kama unataka kwa vipande au PDF.....

Hata kama pesa yako haipo kamili unaweza ukaanza kusoma kidogo kidogo kuanzia shilingi 1000.

KARIBU KWENYE ULIMWENGU WANGU WA KUFIKIRIKA WA KIJASUSI....

Unaweza kulipia kwa namba hizi hapa 👇

0621567672 (HALOPESA).... WhatsApp

0745982347 (M-PESA)

0714581046 (TIGO-PESA)

0689440143 (AIRTEL MONEY)

36316279 (LIPA NAMBA (M-PESA) inapokea mitandao yote)

FEBIANI BABUYA

Miaka 15.jpg
 
Back
Top Bottom