Umenikumbusha hadithi moja ambapo panya walipochoka kutafunwa na paka waliamua kufanya kikao kutafuta mbinu za kumdhibiti paka asiendelee kuwatafuna,wakati wanaendelea na kikao chao mara paka huyoo kaibukia kwenye kikao chao,mara sauti ikasikika chwiichwii kwa vile tayari paka alikuwa ameshafanikiwa kumdaka panya mmoja,badala ya panya kutumia mbinu walizokuwa wanapanga kwenye kikao kumdhibiti paka aliyekuwa anawatafuna,wote walitimkia shimoni kujificha, kilichofuata ni mwenyekiti wao kuhahirisha kikao kwa kuchungulia kutoka ndani ya shimo aliko kuwa amejificha na kumwacha paka akifaidi kula msosi wa panya mpaka leo hii.
Ni kweli watanzania wengi tunahitaji mabadiliko ya katiba kwa kuwa hata hii katiba mbovu iliopo haifuatwi,kila mtu ana mawazo mazuri sana na mipango mizuri sana ambayo inaweza ikatufanya tukapata katiba nzuri sana yenye kuwadhibiti wenye mamlaka wasijifanyie wanavyotaka wenyewe. Lakini hatuna uthubutu wa kusimamia mawazo yetu mazuri na mipango yetu mizuri ambayo tukiitekereza inaweza ikatupelekea kupatikana kwa katiba mpya ambayo itamdhibiti mwenye mamlaka kujifanyia chochote kile anachotaka pasipokuwa na hofu yoyote huku akijua kuwa kukubali katiba mpya ni sawa na kukitia mchanga kitumbua chake.
Hata kama kuna atakayejitokeza kuwaongoza wenzake kudai katiba mpya kwa manufaa ya nchi, ni kweli wengi watamuunga mkono, pia watakuwa naye katika kutoa ushauri wao, mawazo yao mazuri na mipango yao mizuri lakini linapokuja suala la wenye mamlaka ambao wanaona kitumbua chao kinaenda kutiwa mchanga kuanza kumshughurikia yule anayewaongoza wenzake kupata katiba mpya, wote walio kuwa wanampa ushauri mzuri na kupanga mipango pamoja,wanakuwa hawaonekani tena, wanamwacha akihangaika peke yake utafikri kazi aliokuwa anaifanya ilikuwa yake pamoja na familia yake.
Kama wote kwa pamoja tungekuwa tunasimama kwa pamoja na kwa nguvu moja kusimamia kwa pamoja kupigania kile tunachoamini kuwa ndicho sahihi,tunakinukisha mitaani kupigania haki yetu tunayonyimwa,mbona tungekuwa tumeshafanikiwa tangu zamani.
Wewe fikria nchi imetumia gharama kubwa sana kukusanya maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya na mamilioni ya watanzania katika maoni yao wakapendekeza uwepo wa katiba mpya,lakini maoni yote ya mamilioni ya watanzania yanakuja kuzimwa na kundi moja dogo tu,ambalo linafaidi keki ya taifa bila kujali gharama kubwa iliotumika kuzunguka nchi nzima kukusanya maoni hayo, na kwamba maoni wanayokwenda kuyasambaratisha yametokana na mamilioni ya watanzania.