Ujangili watikisa Bunge | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ujangili watikisa Bunge

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MziziMkavu, Aug 12, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Aug 12, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,616
  Likes Received: 4,617
  Trophy Points: 280
  Kiongozi mtandao wa ujalingi atajwa
  [​IMG] Idara ya Wanyamapori yanuka rushwa  [​IMG]
  Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa


  Vitendo vya ujangili vimelitikisa Bunge huku Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni ikiibua malumbano baina yake na Serikali baada ya kumtuhumu mtu aliyemtaja kwa jina moja la Lazaro ambaye ni mmoja wa viongozi wa CCM wilayani Karatu kuwa mshirika wa ujangili.

  Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa, aliyaeleza hayo bungeni jana alipokuwa akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani baada ya kuwasilishwa kwa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha.

  Alisema Lazaro anamiliki silaha aina ya Rifle 375 na kwamba ni mshirika wa mtandao mkubwa wa ujangili nchini unaoongozwa na mtu aliyemtaja kwa jina la Bryson Baloshingwa.

  Alisema Baloshingwa ni kiongozi wa mtandao wa ujangili kwa kufadhili uwindaji wa faru na biashara haramu ya meno ya tembo; uharamia unaofanyika katika hifadhi za Serengeti, Katavi, Tarangire, Ziwa Manyara na Ngorongoro.

  Msigwa ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), alisema Baloshingwa anafadhili pia majangili wanaoua wanyama katika mapori ya akiba ya Ugalla, Rungwe, Moyowosi na Maswa.

  Alisema inashangaza kwamba wafadhili na majangili wanafahamika kwa majina lakini hawachukuliwi hatua na pindi wanapokamatwa hufunguliwa kesi rahisi zenye dhamana hivyo huachiwa kwa dhamana.

  "Usalama wa tembo uko hatarini kutokana na serikali kutochukua hatua dhidi ya ujangili wa tembo pamoja na taarifa hizi kuwepo serikalini na viongozi wa CCM kushiriki katika ujangili," alisema.

  Msigwa alisema mtuhumiwa anayedaiwa kuratibu mtandao wa ujangili alikamatwa Juni 11, mwaka huu kwa RB namba MUG/RI/1330/2012 akiwa kituo cha Polisi Kibondo lakini baada ya kufikishwa Mugumu pamoja na mtuhumiwa mwenzake walifunguliwa kesi za kuazimisha silaha ambayo ni rahisi kupata dhamana.

  Alisema washirika wake ambao hawana ushawishi wa fedha walifunguliwa kesi ya ujambazi wa kutumia silaha.
  Alisema Julai 9, mwaka huu mtuhumiwa Baloshingwa alitolewa rumande kwa kibali maalum, akapelekwa mahakamani na kisha kupata dhamana ambapo pia alisafirishwa hadi Kigoma anakoishi kwa gharama za serikali.


  "Kambi ya Upinzani inasikitishwa na utendaji wa mamlaka za serikali na serikali yenyewe; pamoja na kuwepo kwa taarifa hizi, imeendelea kuwaacha huru watuhumiwa hawa bila kuchukua hatua madhubuti na kuendelea kumaliza maliasili za nchi," alisema Msigwa.

  Alisema mwenendo wa mtandao wa ujangili umegubikwa na rushwa hadi serikalini ndio maana watuhumiwa wanapokamatwa huachiwa bila kufuata taratibu za kisheria.

  Alisema ujangili unatishia ustawi wa Hifadhi za Taifa na mapori ya akiba na kuitaka serikali iiruhusu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mazingira ya rushwa na kuchukua hatua stahiki kwa watakaobainika.

  Aidha, Msigwa pia alihoji ripoti ya uchunguzi wa bodi ya Ngorongoro akiwemo Makamu Mwenyekiti wake ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, ambayo ilichunguzwa na tume mwaka mmoja uliopita bila kutoa ripoti.

  Kadhalika, Msigwa aliitaka serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu uhalali wa mkataba kati ya kampuni ya uwindaji ya Game Frontiers of Tanzania Limited iliyoingia mkataba wa siri na kampuni ya Uranium resources PLC na Western Metals Limited kwa ajili ya kufanya utafiti wa urani kwenye hifadhi ya Selous.

  Hata hivyo, alisema idadi ya vitalu imeongezeka wakati tafiti zinaonyesha kupungua kwa idadi ya wanyama kwenye mapori na hifadhi mbalimbali nchini.
  Kwa upande wake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ilieleza kuwa Idara ya Wanyamapori inanuka rushwa na ufisadi wa kutisha na kushauri kwamba serikali ianzishe Mamlaka ya Wanyamapori kama sheria inavyotaka.

  "Kuanzishwa kwa Mamlaka hii kutapunguza kwa kiasi kikubwa mianya ya rushwa na ufisadi uliobobea katika idara hii," alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli.

  Hata hivyo, katika kipindi cha jioni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alikanusha tuhuma

  zilizotolewa na Msigwa akieleza kwamba Lazaro aliyetajwa kuwa ni Mwenyekiti wa CCM wilayani Karatu si kweli kwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Karatu ni John Tipa.

  Alisema kiongozi huyo hana silaha yoyote na wala hahusiki na ujangili au uharamia wowote.
  Alisema anachofahamu ni kwamba Lazaro aliyetajwa anaweza kuwa ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu (Chadema).

  Alisema taarifa zinaonyesha kwamba Februari mwaka 2010, gari yenye namba SM 4117 mali ya Halmashauri ya Karatu inayoongozwa na Chadema ilikamatwa na nyara za serikali zilizokuwa zikisafirishwa na Diwani wa Kata ya Lotya (Chadema) pamoja na Ofisa Wanyamapori wa Halmashauri hiyo na watu wengine saba.

  Alisema watu hao walikutwa na silaha mbalimbali ikiwemo shotgun na bunduki aina ya Rifle namba 257 ambazo zote zipo Polisi huko Ngorongoro.

  Lukuvi ambaye alisimama kuomba mwongozo wa Spika ili kumtaka Msigwa athibitishe au afute tuhuma hizo, alikitaka pia kiti cha Spika kisimamie kanuni za Bunge ili kikomeshe tabia ya baadhi ya wabunge kuwatuhumu baadhi ya wananchi ambao hawana uwezo wa kujitetea ndani ya Bunge.

  Akieleza kuhusu mwongozo huo, Naibu Spika, Job Ndugai, alionya tabia ya wabunge kuwatuhumu viongozi au wananchi ambao hawana uwezo wa kujitetea ndani ya Bunge kwa kuwa ni kinyume cha kanuni.

  Alisema kutokana tuhuma hizo, atapeleka hotuba ya Msigwa kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili iijadili na kushauri hatua za kuchukua dhidi ya Msigwa na wabunge wengine wenye tabia ya kutaja majina ya watu wasio wabunge ndani ya Bunge.
  Awali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kaghasheki, akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, alisema serikali itaanzisha utalii wa usiku na utalii wa tufe katika Hifadhi za Katavi, Ruaha na Mikumi.

  Alisema wizara yake pia itajenga maabara ya kisasa ya utafiti wa nyuki na itaanza ujenzi wa kituo cha kumbukumbu na taarifa kwenye mapango ya Amboni.
  Katika mwaka huu wa fedha, Wizara hiyo imeomba kutumia Sh. 77,249,692,390 ambapo ni Sh. 12,712,682,390 za miradi ya maendeleo, Sh. 37,871,639,000 za matumizi mengineyo na Sh. 26,665,371,000 za mishahara.

  Imeandikwa na Restuta James, Sharon Sauwa na Moshi Lusonzo, Dodoma  CHANZO: NIPASHE

   
Loading...