Ugomvi wa zuberi mtemvu na julius nyerere 1958

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,266
Utangulizi

Baada ya kupokea picha hii kutoka katika nyaraka na picha alizoacha marehemu Ali Msham picha ambazo alinipatia mwanae Abdulrahman Ali Msham na kwa kuzingatia pia kabla sijapatapo kuona picha ambayo Zuberi Mtemvu alipiga na Nyerere imenijia hamu ya kuweka hapa historia ya hawa wazalendo wawili ambao baadae walikuja kuwa maadui wakubwa kila mmoja akimwita mwenzake "kibaraka."



img260.jpg
Kushoto John Rupia Makamu Rais wa TANU, Julius Nyerere Rais wa TANU na
Zuberi Mtemvu Katibu Mwenezi wa TANU

Ilikuwa miaka ya 1980 tuko nyumbani kwa marehemu Bi. Mluguru bint Mussa, mama yake Ally Sykes Mtaa wa Lindi. Pametokea msiba. Bi. Mariamu, shangazi yake Bwana Ally Sykes amefariki. Watu wamejazana mtaa umefungwa wanasubiri muda wa mazishi. Bwana Ally mwenyewe kakaa jamvini kazungukwa na jamaa zake wa Gerezani, wamekukuja kuungananae katika msiba wa shangazi yake. Watu ni wengi sana. Bwana Ally yeye mwenyewe ni mzishi sasa leo limemfika ndugu zake wamemwitika kwa wingi sana, wamekuja kumzika. Bwana Ally kuniona ananita nende nikakae nae mbele. Basi nanyanyuka pale nyuma nilipokuwa kwa unyonge maana umma mzima unaniangalia huyu anaeitwa mbele pale ana umuhimu gani. Katika lile jamvi alokuwa Bwana Ally ni "nani aliye nani katika mji wa Dar es Salaam," Waingereza wanasema "Who is Who" wenyewe watoto wa Gerezani na Dar es Salaam wametanda. Sasa Bwana Ally anawanadia watu, "Nyie mnamjua huyu? Mtoto wa Said pale Kipata mwandishi hodari sana…"


Utambulisho umekwisha nakaa pembeni Ally Sykes na Zuberi Mtemvu wanashambuliana kwa maneno. Bwana Ally kalalamika kuhusu hali ya nchi mambo hayendi vyema. Zuberi Mtemvu kadakia anawashahidisha watu, "Jamani mnasikia Ally analalamika ati mambo hayendi sawa…" Mtemvu anaangua kicheko cha kejeli huku akitingisha kichwa. Watu sasa weshakuwa hadhir wanasubiri Mtemvu atasema kitu gani? "Huyu Ally na marehemu kaka yake (Mungu amrehemu) walikuwa wanashirikiana na Nyerere kukipiga vita chama changu kife, leo Ally huyu huyu keshageuka ati nchi imeharibika…"Wasikizaji wanacheka wengine wanamuunga mkono Bwana Ally wengine Zuberi Mtemvu. Bwana Ally hakubali kushindwa anarudisha kombora, "Ala kumbe Congress bado mko hadi leo nilidhania tulishakumalizeni." Vicheko. Mzee mmoja kwa mbali anaita, "Ally sikiza bwana, Congress tupo sana. Congress ni mwamba usiovunjika." Vicheko vinaendelea. Hii "Congress ni mwamba usiovunjika," ni maneno yaliyokuwa katika nyimbo ya Congress wakati wa harakati za kudai uhuru.


Kwangu mimi pale nilikuwa nasoma na kupata mazingatio. Nilikuwa nikiifahamu vema historia ya Zuberi Mtemvu na mwalimu wangu alikuwa Ally Sykes. Nilikuwa nimemsoma Mtemvu katika nyaraka za Sykes. Mtemvu ni mmoja wa wanachama wa mwanzo shupavu na msomi kabisa kujiunga na TANU. Katika nyaraka za Sykes kuna "note" ya mwaka 1954 aliyoandika Zuberi Mtemvu kwa penseli kumpelekea Ally Sykes akimtaarifu kuwa kakutana na Ally Mwinyi Tambwe na amemweleza kuhusu chama kipya cha siasa kinachotaka kuanzishwa. Katika "note" ile Mtemvu anamfahamisha Ally Sykes kuwa Ally Mwinyi Tambwe kakubali kukiunga mkono chama hicho kipya. Mtemvu alimjulisha Ally Sykes kuwa Tambwe kukubali kujiunga na TANU lilikuwa jambo zuri sana. Tambwe, Mngazija wakati huo alikuwa katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika. Tambwe alimwahidi Mtemvu kuwaingiza TANU wanachama wengine wanaounga mkono harakati zile.


Mtemvu alimfahamu Nyerere siku zile za mwanzo alipokuwa akija Mtaa wa Kipata kwa Ally Sykes. Baba yake Mtemvu, Mzee Mwinshehe Manga Mtemvu, alikuwa amejenga nyumba yake nyuma ya nyumba ya Kleist Sykes, baba yake Ally. Mtemvu alikuwa na kipaji cha kuzungumza kama alichokuwanacho Nyerere, Bibi Titi na Sheikh Suleiman Takadir. Mtemvu alikuwa na kipaji cha kuweza kushawishi na kuwashirikisha watu katika harakati. Takriban mwezi mmoja baada ya kuundwa kwa TANU Nyerere na Mtemvu walikwenda kuifanyia kampeni TANU huko Morogoro ambako ndiko ilipokuwa asili ya ukoo wa Mtemvu. Baba yake Mtemvu, Mzee Mwinshehe, alikuwa ameongea na baadhi ya wezee wenzake kuhusu TANU. Ijapokuwa Nyerere alijaribu kwa uwezo wake wote kuwafikishia watu ujumbe wa TANU matokeo hayakuwa mazuri. Katika barua ambayo Mtemvu alimwandikia Ally Sykes mnamo Agosti, 1954 aliwaelezea watu wa kabila lake kama "wagumu." Mtemvu alimuelezea Ally kwa ufupi juu ya mkutano wao na Nyerere Morogoro mjini na aliomba apewe mara moja kadi 200 za TANU. Ally aliwaandikia na kuwapa kadi za uanachama wa TANU, Mtemvu na Tambwe na akamwambia mdogo wake Abbas, awaalike wote wawili kwenye mkutano wa uzinduzi wa tawi la TANU la Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Arnatouglo ambao ulikuwa ufanyike Jumamosi inayofuata. Nilipokuwa nawatazama pale mazikoni Ally Sykes na Zuberi Mtemvu walivyokuwa wakitaniana nilizidi kupata uhakika kuwa kwa hakika wazalendo hawa walikuwa wakijuana vyema na historia yao ni ndefu na inatoka mbali.


Si watu wengi sana wenye kujua kuwa ni Nyerere ndiye alimshauri Mtemvu aache kazi serikalini ajiriwe na TANU. Mtemvu alikubali ushauri ule na akaacha kazi. Kwa ajili hii basi Mtemvu akaja kuwa katibu wa kwanza wa TANU na Waingereza wakimchukulia Mtemvu kama mtu mwenye siasa za upande wa kushoto sana katika TANU. Hivi ndivyo ilivyokuwa Zuberi Mwinshehe Manga Mtemvu akaja kuwa mmoja wa viongozi wa juu katika TANU. Katika siku za mwanzo nafasi ya katibu mwenezi ilikuwa ikishikwa na viongozi mbali mbali baina ya Mtemvu Denis Phombeah, Oscar Kambona, Iddi Faizi Mafongo na Stephen Mhando. Mtemvu akiwa katibu mwenezi alikuwa na kazi ngumu ya kuwashawishi na kuushirikisha umma katika harakati za kudai uhuru na kusajili matawi ya TANU. Ili kampeni ya kuwaingiza wanachama katika TANU ifanikiwe na ujumbe wake uwafikie wananchi ilibidi TANU ifanye mikutano ya hadhara. Kwa bahati mbaya serikali ikawa haitaki kutoa kibali kwa TANU ifanye mikutano. TANU ilijikuta katika hali ambayo haiwezi kuwasiliana na umma kuutayarisha katika harakati za kudai nchi yao. Katika hatua kadhaa za ujasiri Mtemvu alifanya mikutano ya hadhara bila ya kupata kibali cha serikali. Nyerere mtu wa hadhari hakutaka kuonekana anavunja sheria. Alifahamu kwamba vitendo kama hivyo vingesababisha matatizo kutoka serikalini.


Jambo kama hilo lilikuwa sawa na kuikaribisha misukosuko bila sababu ambayo ingeathiri TANU na uongozi wake wote. Nyerere, kama rais wa TANU, alikuwa amepokea barua kadhaa kutoka kwa Chief Secretary, T. Griffith-Jones, kuhusu mikutano isiyokuwa na kibali aliyokuwa akiifanya Mtemvu. Lakini kwa hakika kwa TANU kunyimwa haki ya kuitisha mikutano ilikuwa sawasawa na kuifunga mikono. Hakukuwa na namna nyingine TANU ingeweza kufanya ili iwasiliane na watu. Kuacha kufanya mikutano TANU ingebakia dhaifu na harakati zingekufa. Mtemvu alikuwa akifahamu kuwa serikali ilikuwa imedhamiria kabisa kuiua TANU ingali bado changa. Akiwa bado amenaswa katika kitendawili hicho cha kibali cha kufanya mkutano, Mtemvu alipata nakala ya mkutano wa 674 wa Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa ambayo Attorney General, Gratten Below, alifafanua juu ya msimamo wa serikali kuhusu suala hilo. Mwanasheria Mkuu aliarifu kwamba watu wanaweza kuanza shughuli za chama mara tu maombi ya usajili ya chama cha siasa yatakapowakilishwa; na wanaweza kuendelea na shughuli za siasa mpaka majibu kutoka kwa Msajili Mkuu yamepokelewa kwamba tasjili imekataliwa. Uongozi wa TANU katika makao makuu ulisisimka kwa taarifa hiyo iliyofukuliwa na Mtemvu. TANU daima itamkumbuka Mtemvu kwa juhudi zake za kuiingiza TANU Mafia ambako alihutubia mikutano iliyofurika watu. Nyerere alimwambia Mtemvu watu wa Mafia watakuelewa wewe zaidi ya mimi.


Bahati mbaya sana Mtemvu alitupana mkono na Nyerere na TANU mwaka 1958 pale serikali ya kikoloni ilipoandaa uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria ambao viti vilikuwa vishindaniwe kwa misingi ya utaifa. Kulikuwa na viti kwa ajili ya Wazungu, Wahindi na Waafrika. Masharti mengine ya kumwezesha Mwafrika kupiga kura yalimtaka awe na kipato cha paundi mia nne za Kiingereza kwa mwaka, awe na kiwango cha elimu ya darasa la kumi na mbili na awe ameajiriwa katika kazi maalum. Haya yalikuwa masharti magumu na yaliyoonekana kama hayataweza kukubalika na TANU. Mtemvu hakuona mantiki ya kuwaingiza Wazungu na Waasia katika Baraza la Kutunga Sheria na hakuficha msimamo wake na kwa hakika wanachama takriban wote wa TANU walipinga kura tatu. Wana TANU walikuwa na kauli mbiu yao wakisema kuingia kura tatu ni sawasawa na "kujipaka kinyesi." Mtemvu na wengi waliokuwa wakimuunga mkono walisisitiza, "Afrika kwa Waafrika." Lakini hili jambo likawa linasubiri uamuzi wa mkutano mkuu wa TANU wa mwaka 1958 ambao ulikuwa ufanyike Tabora.


TANU ilifanya mkutano wake mkuu wa mwaka wa 1958 mjini Tabora kuanzia tarehe 21-26 Januari kujadili miongoni mwa mambo mengine ikiwa ishiriki katika uchaguzi chini ya masharti haya ya kibaguzi yaliyowekwa na Waingereza au wasuse. Mkutano ule ulitishia kuigawa TANU katika kambi mbili hasimu. Kambi moja ni ile ya wenye siasa za wastani waliopendelea kushiriki katika uchaguzi na ile ya pili ni ile ya wenye msimamo mkali waliotaka uchaguzi ususiwe kabisa. TANU ilinusurika na kile ambacho kingeweza kuwa mgogoro ndani ya chama ambao ungewafanya wale wenye msimamo mkali kama Sheikh Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU katika makao makuu, na Zuberi Mtemvu, wakati huo katibu mwenezi wa TANU, kufanya mapinduzi ambayo yangekigawa chama kama isingelikuwa busara ya Julius Nyerere, Rais wa TANU na mkakati wa siri alioupanga na viongozi wa TANU Tanga, Mwalimu Kihere na Sheikh Rashid Sembe.


Lakini kumuelewa Mtemvu na hisia za wanachama wa TANU, fikra za uongozi wake na nguvu zilizokuwa zikidhibiti siasa Tanganyika wakati ule wa ukoloni, na ili kuelewa kwa nini kura tatu ilileta mgogoro na kutoelewana katika uongozi hata kupelekea TANU kumegeka kwa mara ya kwanza na Mtemvu kuanzisha chama kingeine cha siasa, inatubidi turudi nyuma tufuatilie mwanzo wa siasa mjini Tabora, mahala ambapo TANU ilifanya uamuzi wake ya kihistoria na kuwanasa Waingereza katika mtego wao wenyewe. Tunahitaji kuyatazama mambo kwanza kuanzia Tanga mahali ambapo Nyerere na uongozi wa TANU pale Tanga walikutana kwa siri kuweka mikakati ya mkutano wa Tabora. Baada ya kufanya hivyo tufichue jambo moja baada ya jingine katika ule mkutano ambao wajumbe wa TANU walikutana katika ukumbi wa Parish wa Kanisa Katoliki, Tabora. Hii itatuwezesha kujua kwa nini mkutano mkuu huu ulikuwa muhimu. Akiiandikia Fabian Colonial Bureau, Katibu Mwenezi wa TANU, Zuberi Mtemvu ambae alikuwa amelichambua jambo hili la utatanishi wa kura tatu aliandika maneno haya,"Katika nchi kama Tanganyika, utajiri na elimu vimo mikononi mwa wageni. Mwafrika ni maskini na hana elimu. Upigaji kura wenye masharti magumu yaliyoegemezwa kwenye mali na elimu utawaathiri Waafrika peke yao bila kuwagusa Wazungu na Waasia hata kidogo. "


Ungozi wa TANU makao makuu kulikuwa na watu wengi ambao wasingeweza hata kidogo kusimama kama wagombea katika uchaguzi chini ya masharti yale. Makao makuu ya TANU palikuwa na viongozi kama hawa, Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, Bibi Titi Mohamed, John Rupia, Elias Kissenge, Dossa Aziz, Julius Mwasanyangi, Michael Lugazia, Ramadhani Chaurembo, Hussein Mbaruk, Clement Mtamila, Idd Tulio, Mzee Salum, Idd Faiz Mafongo, Idd Tosiri, Haidari Mwinyimvua na Rajabu Diwani.Katika hawa ni wachache tu ndiyo waliokuwa na sifa za kusimama kupigiwa kura au kupiga kura. Na hali ilikuwa kama hivi Tanga, Tabora, Dodoma na mahala pengine kwingi nchini Tanganyika. Kwa hiyo ilikuwa ni jambo la wazi kabisa kuwa TANU ingesusia uchaguzi wa kura tatu. Mkutano wa Tabora ulikuwa uamue ikiwa TANU itashiriki katika uchaguzi na kushindana na UTP au ingesusia uchaguzi huo na hivyo kumpa mshindani wake mkubwa na hasimu wake ushindi wa bure bila jasho.


Mkutano wa Tabora kwa shida sana uliamua kuwa TANU ishiriki katika kura tatu. Baada ya kutia saini kwa Azimio la Tabora Mzee Fundi Mhindi, Nyerere, Dossa, Mwalimu Kihere na Mohamed Mangiringiri waliondoka pale Parish Hall na kwenda mjini kutafuta simu ili kumpigia Zuberi Mtemvu makao makuu Dar es Salaam kumuagiza awatangazie wananchi kuwa TANU imepiga kura kuingia katika uchaguzi wa kura tatu. Mangiringiri alimchukua Nyerere hadi kwa mwajiri wake wa Kiasia, G. B. Somji kupiga simu kwa Mtemvu. Siku iliyofuata wakati mkutano bado ukiendelea Mtemvu alituma simu ya maandishi kwa rais wa TANU, Nyerere kupitia ofisi ya TANU Tabora, akitangaza kujiuzulu kwake kutoka TANU na kuanzishwa kwa chama kipya - African National Congress (ANC). Chama cha Mtemvu kilikuja kujulikana kama "Congress" neno ambalo kutokana na vyama vyote viwili jina hili lilikuja kunasibishwa na usaliti. Mtemvu akimshutumu Nyerere kwa kusaliti dhamana aliyokabidhiwa na TANU na wananchi; na Nyerere akimshutumu Mtemvu kwa kuacha mapambano na kujiunga na upinzani ili kudhoofisha TANU, na hivyo kusaliti harakati za kudai uhuru. Msimamo wa Mtemvu ulikuwa "Afrika Kwa Waafrika" - hakuna mgeni atakayekubaliwa kuitawala Tanganyika.


Mtemvu alikuwa amelenga kwenye serikali ya Waafrika watupu ndani ya Tanganyika huru. Ujumbe wa Mtemvu ulipokelewa katika ofisi ya TANU mjini Tabora na mara moja tarishi alipanda baiskeli kupeleka ujumbe ule mkutanoni kule Parish Hall. Nyerere aliwasomea wajumbe wa mkutano mkuu ile simu kwa sauti. Ilikuwa ni habari za kustusha. Hatua hii ya Mtemvu ilikuwa ya pekee katika historia fupi ya TANU. Hapakuwahi kutokea kiongozi wa chama kujiuzulu na kuanzisha chama cha upinzani. Mtemvu alikuwa mpinzani wa kura tatu toka mwanzo na Nyerere aliufahamu msimamo wake. Katika maandalizi ya mkutano wa Tabora ilikuwa Mtemvu ndiye atakaeongoza hoja ya "kwa nini lazima TANU ikatae pendekezo la kura tatu". Lakini baadae Nyerere alimshawishi Mtemvu abaki nyuma Dar es Salaam kuendesha makao makuu kwa kuwa haitakuwa busara kwa viongozi wote kuondoka na kuiacha ofisi bila kiongozi wa juu ofisini. Nyerere alimshawishi Mtemvu akubaliane na ushauri wake na kuhusu hoja ya upinzani wa kura tatu, Nyerere alishauri hoja hiyo aachiwe Amos Kissenge aiwasilishe kwenye mkutano wa Tabora.


Vita kati ya Mtemvu na Nyerere inasemekana ilikuwa imeanza siku nyingi na Nyerere alijaribu kushinikiza atolewe Kamati Kuu ya TANU lakini hili lilipingwa vikali na John Rupia, kwa hiyo Nyerere hakufanikiwa lengo lake. Miezi michache kabla ya uhuru Rais wa Congress, Zuberi Mtemvu akiwahutubia wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Karl Marx mjini Leipzig, Ujerumani ya Mashariki, Mtemvu alibashiri kuwa kutolewa kwa uhuru wa Tanganyika kwa uongozi wa TANU, hautabadili chochote kwa kuwa wanaoingia madarakani wameamua kushirikiana na walewale wanyonyaji wa zamani na hii itavunja nguvu za wazalendo na matumaini yao. Siku za mwisho za Mzee Mtemvu alikuwa anakuja nyumbani kwa mwanae Abbas Mtemvu akitokea Morogoro ambae tukiishi jirani. Nikitoka kazini njia ya kwenda kwangu ilikuwa inapita mbele ya nyumba yake. Nyakati za jioni Mzee Mtemvu alikuwa akipenda kukaa nje kupunga upepo. Nikifika pale nilikuwa nakwenda kumwamkia na hapo tutaanza gumzo. Ilikuwa akinishinda kwa hoja basi mimi humchokoza kwa kumwambia, "Lakini baba unajua kuwa historia ya uhuru wa Tanganyika imekuweka wewe katika kundi la wasaliti?" Hapo ninakuwa nimechokoza nyuki. Mzee Mtemvu atanijibu, "Msaliti mimi au Nyerere aliyetoa nchi kwa walewale waliokuwa wakitutawala?" Hapo atazungumza sana na mwisho huagana nikenda zangu. Mtemvu na Nyerere kuanzia mwaka wa 1958 walinuniana hawakuzungumza hadi mwisho wa maisha yao na kisa cha ugomvi wao kilikuwa ni kura tatu.
 
Ni yapi yalikuwa maisha ya Mtemvu baada ya kuanzisha chama chake, na ilikuwaje akapotea kwenye siasa za Tanganyika, na kipi kilifanyika baada ya kufutwa vyama vingi

Asante
 
Asante sana Mohamed Said kutukumbusha historia haswa nafasi ya Zuberi Mtemvu ktk harakati za uhuru.
 
Ule mkutano uliofanyika Tabora ulipo-mention kuwa umefayika Parish ya katoliki unamaanisha kuwa kuna influence yoyote ya sehemu ulipofanyika mkutano na maamuzi yaliyofikiwa au ndo kama kawaida yako na nyimbo zako za udini?
 
Mkuu unaweza kututajia hoja/critical points Hata tatu zilizoshawishi mkutano kukubaliana na kura tatu?
 
Blac kid,
Angalia kwenye kitabu cha Abdul Sykes mjadala ulivyokwenda.
 
Tourmaline,
Kwa kauli yake Mzee Mtemvu alinambia kuwa TANU ilikuwa na nguvu
sana hakuna mtu angeweza kupambananayo.

Chama.chake hakikuweza kuhimili.
 
Tourmaline,
Kwa kauli yake Mzee Mtemvu alinambia kuwa TANU ilikuwa na nguvu sana hakuna mtu angeweza kupambananayo. Chama.chake hakikuweza kuhimili.

Hivi mzee huyu abbas mtemvu ndio huyu mbunge wa temeke
 
mzee hii umeiweka sawa bila biaseness, mi nafurahia sana historia zikiwa rational kama hivi mkuu....

big up, naomba more pics tafadhal.
 
Nimeona jina la Julius Mwasanyagi. Huyu mzee hataki kabisa kumsikia Nyerere, walitofautiana mwalim akamweka jamaa kifungo cha nyumbani karibu 20yrs. Alipostaafu nyerere na yeye akaachiwa. Akawa sasa kila sehemu akiomba kazi ananyimwa, akaishia kuwa mwalim pale highlands high school Iringa akifundisha economics na commerce
 
Nimeona jina la Julius Mwasanyagi. Huyu mzee hataki kabisa kumsikia Nyerere, walitofautiana mwalim akamweka jamaa kifungo cha nyumbani karibu 20yrs. Alipostaafu nyerere na yeye akaachiwa. Akawa sasa kila sehemu akiomba kazi ananyimwa, akaishia kuwa mwalim pale highlands high school Iringa akifundisha economics na commerce

Kabla ya hapo, Julius Mwasanyagi alikuwa mwalimu Songea Secondary School, 1968. Alikuwa anafundisha historia baada ya kupata degree yake Makerere ambako alifundishwa na Professor Ali Mazrui. Wanafunzi wa Songea Secondary School wakati ule, miongoni mwao ndugu wawili wa Oscar Kambona, wanamkumbuka pamoja na alivyotofautiana na Mwalimu Nyerere. Nina hakika kwa sababu nilimfahamu mzee huyo pamoja na wazee wengine nyakati zile.
 
Jembepori,
Unanipitishia hukumu nini niseme na nini niache?
Hiyo "rationality" ni ipi?

Ni ile ya Chuo Cha Kivukoni ya kuigeuza historia ya TANU?
Umewahi kuandika chochote kikachapwa?
 
Back
Top Bottom