Fundi Mchundo
Platinum Member
- Nov 9, 2007
- 9,187
- 7,285
Mahakama yaamuru azikwe Kikristu
2008-04-04 08:43:26
Na Simon Mhina
Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, imeamuru mwili wa marehemu Paul Goliama (40), uzikwe kwa imani ya Kikristo na kuwaonya Waislamu wasivuruge mazishi hayo.
Hukumu ya mgogoro wa mazishi ya Goliama ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi Emilius Mchauru wa mahakama hiyo, huku ulinzi mkali wa polisi wenye bunduki mikononi ukiwa umeimarishwa.
Magari mawili Land Rover Defender yalikuwa yamejaa askari hao ambao pia walizunguka eneo la mahakama kuhakikisha kuwa utulivu unakuwepo.
Kesi hiyo ilivuta watu wengi waliokusanyika kuanzia saa 6:00 mchana jana hadi ilipomalizika saa 10:15 jioni.
Goliama alifariki Jumanne ya wiki iliyopita na mazishi yake yalipangwa kufanyika Ijumaa iliyopita katika makaburi ya Sinza, lakini ulizuka mtafaruku wa kugombea maiti yake baada ya Waislamu wa Msikiti wa Swafwa kudai alikuwa Muislam wakati jamaa zake walisisitiza kuwa aliacha Uislamu na kurudi kanisani.
Vurugu hizo zilitokea katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Sinza baada ya ibada kumalizika, na waumini kujiandaa kwenda makaburini kwa maziko.
Hali hiyo ilipelekea uongozi wa kanisa hilo kuomba msaada wa polisi ili kutuliza vurugu na kutafuta muafaka, lakini ilishindikana na polisi wakashauri kuwa suala hilo lifikishwe mahakamani ili kupata muafaka wa kisheria.
Familia ya marehemu ilifungua kesi ya madai katika Mahakama ya Kinondoni na ilianza kusikilizwa Jumatatu wiki hii, na upande wa wajibu madai walifungua kesi katika Mahakama ya Kisutu, lakini ilifutwa kwa kuwa kulikuwa na kesi nyingine ya msingi iliyofunguliwa katika mahakama ya wilaya.
Ushahidi wa wadai uliowasilishwa na wakili wao, Mutakyahwa Charles ulithibitisha kuwa marehemu Goliama alikuwa Mkristo na kwamba hadi anakufa alikuwa muumini wa dini hiyo.
Ushahidi huo kama daftari la waumini wa Usharika huo lililotolewa kama kielelezo ulionyesha kuwa marehemu alirudia dini yake ya Kikristu Juni 2006.
Aidha maelezo ya mkewe Bi. Agnes Goliama, kuwa mumewe alikuwa muumini wa Kikristu ni ushahidi uliothibitisha kuwa alikuwa muumini wa dini hiyo.
Akizungumzia madai yaliyotolewa na upande wa wajibu madai, hakimu Mchauru alisema ushahidi uliotolewa na upande wa wajibu madai, umeonyesha kuwa marehemu alibadili dini ili aweze kumuoa binti wa Kiislamu ambaye ni Atala mwaka 1996 na kwamba hakuwa na dhamira halisi ya kuwa Muislam.
Alisema anaamini hivyo kwa kuwa marehemu baada ya kuachana na Atala, alirudia dini yake ya Kikristu na kuoa binti mwingine wa dini hiyo, Agnes, mwaka 2003 na mtoto waliyempata walimpa jina la Kikristu.
Aidha alihoji ushahidi uliotolewa na upande wa Waislam kuwa iwapo marehemu alikuwa muumini wao, iweje wasifahamu alikuwa mgonjwa hadi anafariki?
Alifafanua kuwa utata upo kwenye ushahidi juu ya ndoa kwa kuwa hawakujua kuwa ndoa ya Atala na Goliama ilivunjika na pia hawakueleza iwapo alikuwa na mtoto na waliieleza mahakama kuwa mtoto aliitwa Aina wakati vielelezo vinaonyesha kuwa anaitwa Anna.
Hakimu Mchauru akitoa ufafanuzi wa barua iliyotolewa mahakamani hapo kama ushahidi iliyodaiwa iliachwa na marehemu huyo ili atakapokufa azikwe Kiislamu, alisema ana mashaka na barua hiyo kwa kuwa haikuwa na sehemu ambayo Goliama aliandika azikwe Kiislamu.
Pia alisema haikuwa na nakala kwa kiongozi wala jamaa yeyote na badala yake mwenye barua hiyo ni Imamu Othman Njama wa msikiti wa Swafwa.
Alisema kisheria marehemu alichokifanya ni kuandika wosia akiagiza anachotaka atendewe atakapokufa kulingana na imani yake ambayo wakati huo ilikuwa Uislamu.
Baada ya hukumu hiyo iliyosomwa kuanzia saa 7:30 hadi saa 10:30 jioni, Waislam hao walionekana kutoridhika na kudai kwamba watakata rufaa.
Walisema hawakuridhika na hukumu hiyo kwa maelezo kuwa hakimu aliyeitoa amefanya hivyo kwa lengo la kuwatetea Wakristo wenzake.
Bw. Omar Hashim aliyejitambulisha kuwa ni kiongozi wa Vijana wa Jumuiya ya Kiislam Mkoa wa Dar es Salaam, alisema mbali na kukata rufaa, watafukua mwili huo na kuuzika kwa mujibu wa taratibu, sheria na dini yao kwa kuwa kushindwa kufanya hivyo ni dhambi.
Alifafanua kuwa kwa vile marehemu walisali naye msikitini na kuwaachia wosia, wasipopigania kumzika kwa imani aliyotaka hawawezi kuepuka adhabu ya Mwenyezi Mungu siku ya Kiama.
Baada ya hukumu hiyo kutolewa, msafara wa waombolezaji ulielekea nyumbani kwa marehemu Sinza huku wakiimba nyimbo mbalimbali za miziki ya Injili na mapambio.
Waombolezaji hao walionekana kuwa na nyuso za furaha na huku wakiimba kwa shangwe.
``Hakuna tena majonzi sasa ni furaha,`` alisema mmoja wa waombolezaji.
Hata mama mzazi wa marehemu huyo, Bi. Anna Goliama, alitoka mahakamani akiwa anarukaruka kwa furaha. Jamaa zake walipiga honi na miziki wa Injili na mapambio yalipamba msafara wa waombolezaji.
Marehemu Goliama anatarajiwa kuzikwa leo ambapo ndugu wanatarajia kupata nakala ya hukumu na kuiwasilisha polisi ili wakabidhiwe mwili wa ndugu yao.
SOURCE: Nipashe
Hii inawezekana imeishatoka kule kwenye mambo ya dini. Ninachojiuliza ni vitu viwili:
1) Mbona hatusikii watu wakigombania kuuguza?
2) Huyo Mungu atakuadhibu kutokana na utakavyozikwa(ambacho kiko nje ya uwezo wako maana ndio yameisha kukuta) na siyo ulivyoishi?
Mimi naona ni aibu kubwa watu kugombania mwili wa marehemu. Kama alikuwa muislamu au mkristu itajulikane mbele ya huyo ajuaye yote. Kwa vile ndugu zake ndio inaelekea walikuwa wanaishi naye na waliishafanya mipango ya mazishi wangeachiwa tu. Hao masheikh hawaitendei haki dini yao kwa kuendelezea huu ugomvi. Wauache MWILI wa marehemu ukapumzike wakati ROHO yake inakabiliana na tusiyoyajua.