Udhaifu wa serikali ni udhaifu wa rais

Udhaifu wa serikali ni udhaifu wa rais

Joined
May 28, 2013
Posts
91
Reaction score
17
Udhaifu wa Rais ni udhaifu wa Serikali
----------------------------------------------

Katika ukurasa wa 50 wa kitabu cha Uongozi Wetu
na Hatima ya Tanzania, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliandika hivi: "Rais Mwinyi ni mtu mwema na mpole, lakini ni kiongozi dhaifu; na upole wake unatumiwa na watu ambao wala si wema wala wapole kuhatarisha umoja na amani ya nchi yetu."

Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika, alitamka maneno haya: "Tumefika hapa kwa sababu ya udhaifu wa Rais Jakaya Kikwete, kwa uzembe wa Bunge na kwa sababu ya upuuzi wa CCM."

Kauli hizi mbili zinafanana kwa kiasi kikubwa. Mwalimu Nyerere alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwathibitishia Watanzania kwamba rais alikuwa dhaifu. Hata rais mwenyewe alikiri kimya kimya. Akachukua hatua za kurekebisha baadhi ya yale yaliyomfanya Mwalimu Nyerere amuite kiongozi dhaifu.

Hivyo ndivyo John Malecela alivyopoteza Uwaziri Mkuu; na Horace Kolimba akapoteza Ukatibu Mkuu wa CCM. Sijawahi kumsikia kiongozi yeyote wa CCM au Serikali akimlaumu Mwalimu Nyerere kwa kauli ile; bali watu wengi wamekuwa wakijipendekeza kwa
Mwalimu Nyerere, wakitaka ionekane kauli yake ilikuwa halali kwani ni ya mtu aliyekuwa anamsema mdogo wake!

Lakini ilipofika zamu ya Mnyika kutoa kauli kama hiyo kuhusu Rais Kikwete, wakazuka watu wa kusema mbunge "amemtukana rais." Eti rais ni kama baba, hata kama angeweza kushauriwa na kukosolewa kwa upole, nidhamu na heshima. Propaganda hii ilianzishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu, William Lukuvi, ikadakwa na Naibu Spika, Job Ndugai, ikaenezwa na wakongwe wengine hata ikawagusa baadhi ya wanahabari na wanasiasa, hasa wale wanaoogopa kuzomewa au kuonekana wabaya.

Bahati mbaya ni kwamba karibu wote hawa wamesikika mara kadhaa wakimsema rais kwamba ni dhaifu. Wanayasemea kwenye vikao visivyo rasmi, kwenye vijiwe na kwenye vilabu vya pombe.

Mnyika amewazidi ujasiri akayasema hadharani. Amekataa unafiki wa kumsifia rais hadharani na kumsema vibaya pembeni. Aliktaa kufuta kauli yake, akataka kumbukumbu za kibunge zimnukuu kwamba Rais Kikwete ni dhaifu. Na kutokana na uzito wa kauli yake, ndiyo maana maneno yake hayo yamejadiliwa sana wiki hii, na ndiyo yametupatia nukuu ya wiki, ingawa yaliyozungumzwa bungeni yalikuwa mengi. Na ingawa Naibu Spika hakumpatia Mnyika fursa ya kufafanua hoja yake juu ya udhaifu wa Rais Kikwete, yeye alitumia fursa nyingine akafafanua alichomaanisha.

Aliandika hivi: "Ubovu wa bajeti hii ni matokeo ya udhaifu wa Rais Kikwete, yeye ndiye aliyesaini Mpango wa Taifa wa miaka mitano kama kiongozi mkuu wa nchi, tena kwa wino mwekundu kama Amiri Jeshi Mkuu. Na yeye ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri, bajeti hii iliyoacha kuzingatia mpango wa taifa imepita kwenye baraza aliloliongoza, pia kushindwa kutekelezwa kwa bajeti iliyopita ni matokeo pia ya udhaifu wa taasisi ya urais. "Pia kwa mujibu wa Katiba, rais ndiye ambaye anapeleka bajeti bungeni, waziri mwenye dhamana anapeleka tu kwa niaba.

Rais amepewa mamlaka makubwa juu ya bajeti ibara ya 99 imeweka mipaka kuhusu mambo ambayo Bunge lina mamlaka nayo,
huku ibara ya 90 inasema Bunge likikataa bajeti rais ana mamlaka ya kuvunja Bunge. Hivyo Rais Kikwete anapaswa kumwagiza Waziri wa Fedha bajeti iondolewe, irudi kwenye baraza la mawaziri ikafanyiwe marekebisho!" Je, haya ndiyo "matusi" ambayo nimesikia baadhi ya wanapropaganda na wanaswa na propaganda,wakiwamo hata wachungaji, wanasema kwa kumlaumu Mnyika? Au tuulizane swali la msingi: Rais wa nchi anaweza kuwa dhaifu? Au tuulize hivi: ni jambo lisilotarajiwa kwa mbunge yeyote kujadili udhaifu wa rais, kama amejiridhisha kwamba udhaifu huo upo? Au yawezekana watu wanamtazama Mnyika kwa umri na kimo chake. Au wanajadili suala hili kwa kusingizia tu "maadili na utamaduni wetu?" Lakini kauli ya Mnyika inapaswa kutafsiriwa kisiasa.

Ni kauli ya mwanasiasa dhidi ya wanasiasa na mfumo wa kisiasa asiouamini. Nimekutana na watu wengi serikalini na nje ya serikalini wanaoamini kwamba rais ni dhaifu, lakini wanadai kwamba Mnyika angeyasema kwa staha; au asingeyasema kabisa, au angeyafuta baada ya kuambiwa hivyo na Naibu Spika.

Lakini wanaosema hivyo wanasahau au wanapuuza Ibara ya 100 ya Katiba yetu mbovu inayosema: "Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika mahakama au mahali popote pengine nje ya Bunge.

"Bila ya kuathiri Katiba hii au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika, Mbunge yeyote hatashitakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya Bunge au alilolileta bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au vinginevyo." Na kama tunafika mahali tunadhani mbunge kutamka kuwa rais ni dhaifu ni tusi; ni maneno gani yanafaa kutumia badala ya neno dhaifu? Na katika kuimba sifa za rais, tunamsaidia rais au nchi? Tunaondoa udhaifu wake au tunaudumisha? Lakini ni vema tuulizane pia.

Hivi mawaziri wanadhani kwamba rais hawezi kuwa dhaifu kwa sababu tu ni bosi wao? Au wanadhani kwa sababu rais ni bosi wao, kusifu udhaifu wake ni kudumisha uzalendo kwa taifa? Na kwa madaraka makubwa aliyonayo rais katika katiba ya nchi, hivi udhaifu wake binafsi wa kiuongozi au kiuamuzi, hauathiri uwezo wa taasisi nzima ya urais? Hauidhoofishi serikali yake? Ukweli ni kwamba udhaifu wa timu ni udhaifu wa kocha au kapteni.

Udhaifu wa jeshi ni udhaifu wa kamanda. Udhaifu wa serikali ni udhaifu wa rais. Kwa jinsi Katiba yetu ilivyo, rais anapokuwa imara taifa linakuwa imara pia. Akiwa dhaifu linakuwa dhaifu pia. Kwa jinsi tunavyokiona CCM na serikali, hapo walipofikia chini ya uongozi wa Rais Kikwete, nitawashangaa sana wana CCM na wapambe wao kama wataendelea kumshambulia Mnyika kwa kusema ukweli wanaousambaza wao kwenye vikao visivyo rasmi.

Na kama watu wanajadili ukali aliotumia Mnyika katika kutoa kauli yake hiyo, na hata kukasirika, wanapaswa wajiulize kulikoni hata Mnyika, mpole, muungwana na makini kama tunavyomjua afike hatua ya kuwa mkali kiasi hicho! Hicho kilichosababisha ukali wa Mnyika ndiyo hoja inayopaswa kujadiliwa kwa kina.

Na kinachoonekana hapa, ni kwamba ukali wa wabunge na wana CCM dhidi ya Mnyika, si lazima iwe kauli yake dhidi ya rais, bali kwa vile Mnyika aliigusa CCM akisema ni legelege. Ni kwa sababu aliligusa pia Bunge kwamba ni zembe.

Lakini tuseme ukweli, kama wabunge wa CCM wangesimama kidete kuikosoa na kuisimamia serikali bila kujikomba kwa rais, "madudu" mengi tunayoshuhudia leo yangekuwapo? Hivi kama Bunge lingekuwa na makali ya kuisimamia CCM bila kujali itikadi, badala ya "kuiomba" itekeleze hili na lile, tungekuwa katika hali hii dhalili ya umaskini, ujinga na maradhi yasiyopungua? Hivi kama kauli mbaya dhidi ya rais wanazotoa baadhi ya wabunge wa CCM na viongozi wengine wa serikali zingekuwa zinatolewa kwa uwazi na kwa dhati, rais na serikali yake wangeshindwa kujisahihisha na kuboresha utendaji kazi? Kimsingi, alichosema Mnyika si kipya.

Nakumbuka hata mimi niliwahi kukisema nikimtetea Rais Kikwete katika kipindi cha televisheni ya Star, mwezi mmoja uliopita. Nilisema siamini kama Rais Kikwete ni mtu mbaya. Nilisema kwamba siamini kama ana nia mbaya na serikali. Nilisisitiza kwamba kwa haya yanayotokea, na kwa kuwa kwa hulka Rais Kikwete ni mpenda sifa, anakuwa amewekeza nguvu na akili zake zote, lakini uwezo wake unaishia hapo! Na bado naendelea kuamini hivyo.

Kuna uwezo mdogo wa kubuni, kufikiri na kutenda katika serikali yake. Huu nao ni udhaifu. Na kama kuna udhaifu mahali fulani, lazima kuna mahali unakoanzia au unakoishia. Katika hili la uongozi wa serikali na CCM, nani aulizwe kama si Rais Kikwete? Nani asemwe kama si Rais Kikwete? Nani amseme kama si mbunge?
 
Thread ni nzuri mno ila hujaipangilia mkuu...pia hii thread ni mwiba mchungu sana kwa magamba Hahaha hahaha
 
Huyo mnyika wako ni mhuni, mwambie ajifunze adabu kwanza ndio ulete maneno yake ya kihuni hapa
 
Back
Top Bottom