Uchumi wa Sanaa na Utajiri wa Wasanii

Hussein Massanza

JF-Expert Member
Dec 26, 2012
918
1,994
Ubora wa sanaa ni kielelezo cha maendeleo ya nchi. Wasanii wanapokuwa na maisha mazuri na wakawa wanaishi maisha ya msanii (kuishi kisanii), ni dalili kuwa nchi husika ina mwamko mzuri wa kiuchumi. Utajiri wa wasanii ni utajiri wa jamii, ni utajiri wa nchi.

Hapa madhumuni ni kuchambua uchumi wa sanaa unavyoweza kuibeba jamii kwa upana wake. Mwisho kabisa, tutakubaliana kuwa kuna umuhimu mkubwa sana jamii ikiwa na wasanii wenye uwezo mkubwa wa kifedha na nguvu ya kumiliki mali.

Kabla ya yote, nieleze kuwa sanaa inapotumika vizuri, hufanya kazi kama mhimili huru unaosimamia dola. Katika nchi ambayo Bunge linakosa meno dhidi ya udhaifu wa serikali, vyombo vya habari navyo vikawa kimya, sanaa inaweza kuwa nyenzo imara zaidi ya kuwasiliana na jamii na kuieleza jinsi mambo yalivyo hayapo sawa.

Sanaa kwa kushirikiana na vyombo vya habari na Bunge, inaweza kuwa daraja rahisi la jamii kujua udhaifu wote wa serikali au hata uimara wake. Hapa ni suala la namna ya kuitumia sanaa. Mwananchi anaweza asiwe mfuatiliaji wa Bunge, hasomi magazeti na hataki kusikiliza taarifa za habari lakini nyimbo anasikiliza. Filamu anaangalia.

Ndiyo maana inaelezwa kuwa ukitaka uiue jamii yoyote ile, basi haribu mfumo wake wa sanaa na wasanii wajikite kwenye mambo mengine bila kumulika matatizo ya jamii wanayoishi. Inaweza kuchukua miaka 30 kubadili fikra za wananchi lakini tungo na msimamo wa wasanii kwa mwezi mmoja, zinatosha kufanya mabadiliko makubwa.

Wasanii wakiamua kuwa na msimamo mmoja na kusema wanataka mgombea fulani awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kisha waamue kumfanyia kampeni ya nguvu, hata atokee nani hataweza kuipiku nguvu hiyo. Matajiri wamwage fedha, hawatafanikiwa kuuzima moto huo. Wasanii wakiamua iwe na inakuwa.

Bahati mbaya sana wasanii wenyewe huwa hawajui nguvu waliyonayo. Ni kwamba wakiwa pamoja na kutoa msimamo wa pamoja, tamko lao linaweza kutikisa nchi kuliko wabunge kususia vikao vya Bunge. Katika nchi nyingi, jambo ambalo wanyonyaji hufanya kwanza ni kuwagawa wasanii ili wasiwe na maono yenye kushabihiana. Wao kwa wao wawe hawaelewani.

Ni kama hapa Tanzania kwa hali iliyopo sasa, wapo wachache wanaopata promo mbuzi kwa sababu maalum. Wanapewa promo ili watumike kuuhalalisha mfumo dhalimu uliopo, hao ndiyo huwaponda wenzao wanaolalamika kuwa hawauzi, kwamba muziki wao haukubaliki ndiyo maana wanaponda mfumo.

Kwa kawaida wanaotumika kutuliza upepo ni wachache sana, kwani kwa Tanzania hakuna msanii anayeweza kusimama na kujisifu kwamba anakula halali kulingana na wingi wa jasho lake. Kila mmoja anatambua kuna mfumo kandamizi, mfumo unaonyonya jasho la wasanii. Ila nafuu kidogo inatumika kusaliti wenzao.

Ndiyo zao la kuwepo wasanii wa muziki wa kizazi kipya wanaojitambulisha kuwa wao ndiyo wapo kwenye mstari sahihi, wakiwa na Chama cha Tanzania Urban Music Association (Tuma) na wengine Tanzania Flavor Unit (TFU). Ni mgawanyo tu, huwezi kuwatawala wasanii bila kuwagawa.

Mtaalamu wa sanaa za maandishi, aliye pia Mkurugenzi wa Tume ya Utamaduni na Sanaa (NCCA), nchini Philippines, Malou Jacob, aliwahi kuliambia kongamano la kimataifa la sanaa lililofanyika Australia kuwa sanaa ni tiba yenye njia nyingi.

Alitolea mfano kwamba aliwatumia ipasavyo wasanii wa Philippines kuitibu jamii iliyokumbwa na mafuriko nchini humo na kufanikiwa kwa kiwango kikubwa. Anasema kuwa jamii ilipona majeraha ya dhiki baada ya mapinduzi mwanzoni mwa miaka ya 2000 kupitia wasanii.

Hapa tunakubaliana bila shaka kuwa wasanii ni nguvu kubwa. Muhimu ni kuwafanya wao wenyewe wajitambue na wajiamini, kisha na jamii yenyewe iwaamini kwamba wakitumika inavyotakiwa katika mambo ya maana, wanaweza kuchagiza matokeo chanya.

UCHUMI WA SANAA:
Kuna uchumi mkubwa sana ndani ya sanaa. Ni vigumu kuuona au hata kuufikia kama soko lake linakuwa limebanwa. Lazima soko liwe jepesi na huria, wasanii watengeneze fedha na hapo ndipo itakuwa rahisi kuona manufaa mapana ya kiuchumi ndani ya jamii na taifa kwa jumla.

Ukiachana na faida nyepesi ambazo watoto wa shule za msingi hukaririshwa kwamba manufaa ya sanaa ni kuelimisha na kuburudisha. Ni wakati mwafaka sasa itambulike kuwa sanaa ni fedha, ni uchumi. Inatosha kuwa mkombozi wa bajeti za serikali na kutoa mchango wa thamani katika Pato la Ndani la Taifa (GDP) na jumla katika Pato la Taifa (GNP).

Laiti kila raia angejua thamani ya sanaa, angetamani kuona kila msanii mwenye kipaji na aliye na jitihada za kufanikiwa, basi anafanikiwa na kutengeneza fedha ili kurahisisha mirija mingi ya uchumi kupata mtiririko wenye afya. Sanaa ni kilainishi (grisi) cha uchumi wa sekta nyingine nyingi.

Kwa mantiki hiyo, mafanikio ya sanaa ni msisimko wa uchumi kwa taifa.

Tunayajua haya, ndiyo maana tunatoa miongozo na tunashupalia uwepo wa soko huria, wasanii wa Watanzania wafanye biashara bila longolongo, watengeneze fedha, wafikie daraja la kuitwa matajiri ili tuone raha yake.

Wasanii wanapofanya biashara na sanaa ikapita kwenye mkondo wake barabara, husisimua uchumi wa sekta ya Viwanda na Biashara.

Huitangaza nchi na kuchagiza kivutio cha wageni kutembea kibiashara au kitalii, hivyo kuipa nguvu sekta ya Utalii. Wasanii wanapotajirika, huwezesha kupanuka kwa sekta ya Uwekezaji na kutanuka kwa sekta za Ajira na Elimu.

Wasanii wapovuna stahili ya jasho lao na kutengeneza fedha za kutosha, inaweza kupunguza msongamano wa wananchi wanaojibana kutibu njaa katika sekta isiyo rasmi, kwani wengi wa waliopo huko, wana vipaji sana lakini hawavitumii kikamilifu kwa kuona na kuamini kwamba maisha kwenye sanaa ni magumu na hayalipi.

Biashara ya sanaa inaposhika nafasi stahiki na kujaa kwenye mifereji yake, inaweza kuchangamsha ubunifu kwa watu na kufanikisha kutengeneza ajira, badala ya kufikiria kuajiriwa tu. Mafanikio hasi ya wasanii wa Tanzania, ni sababu ya vipaji vingi kupotea.

Watu wanashindwa kufikiria na kubuni njia ya kutengeneza fedha kupitia sanaa kwa sababu ya kuona jinsi wasanii wanavyoishi kwa tabu. Inahitaji mtu mwenye akili ya uthubutu kama mwendawazimu, ndiye anaweza kuona kitu fulani hakilipi na kimewapotezea dira wengi, kisha naye akifanye kwa kuamini kitampa mafanikio.

Ni ndoto ya kila mtu kuwa na maisha mazuri, kwa hiyo watu huangalia maeneo ambayo yanalipa. Mathalan, huko nyuma ilikuwa ndoto ya kila mtoto kuwa daktari, injinia na rubani kwa sababu ilionekana ndiyo mafanikio yanayotazamika na kupigiwa mfano. Siku hizi, vijana wengi wanatamani kuwa maofisa wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania).

Sababu ni kwamba wanaona jinsi maofisa hao wanavyofanikiwa ndani ya muda mfupi. Wanaiba kwa kutengeneza mirija ya rushwa kwa wafanyabiashara, kwa hiyo ndani ya kipindi kifupi, watu wanapiga hatua kubwa. Umiliki wa majumba, magari ya kifahari na uwekezaji mwingine.

Hiyo ndiyo sababu ya vijana wengi kutamani kuingia huko. Nao wawe maofisa wa TRA. Tulishashuhudia watu zaidi ya 70,000, kwenda kufanyiwa usaili Idara ya Uhamiaji. Hiyo ni kuonsha namna gani ajira zilivyo ngumu. Ukweli ni kwamba katika idadi hiyo ya watu, wapo wengi wenye vipaji lakini ni ngumu kuvionesha wala kuvitumia kwa mfumo uliopo.

Ni wakati mwafaka sasa, unapotembelea shuleni na kumuuliza mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari, matarajio yake nini kwa maisha yake ya baadaye, naye ajibu kuwa yeye ana kipaji, kwa hiyo anatamani kuwa msanii maarufu wa kimataifa, mwenye mafanikio na kutengeneza fedha nyingi. Msanii kwa kawaida mkondo wake ni maisha ya burudani. Starehe kwa sana!

Ni vigumu leo hii, umuulize mtoto anataka kuwa nani baadaye, naye akujibu kwamba anaota kuwa msanii mkubwa kwa sababu anapozungumza na wazazi wake, wanamwambia kazi nzuri ni zipi. Uinjinia, udaktari, urubani, ubunge na ajira nyingine ambazo ni rasmi kwa sasa.

Mzazi mwenyewe anajua kwamba wasanii wanahangaika na njaa. Hii ndiyo sababu mpaka leo, kila unapomuuliza swali msanii anayetambulika, alipotoka mpaka kufika alipo, atakwambia kwamba wazazi wake hawakutaka kabisa awe msanii. Si kwa sababu ni fani mbaya la hasha! Wanaona sanaa ni kupoteza muda, ni uhuni tu! Laiti wangeona mafanikio ya wasanii, wasingewakataza watoto wao hata kidogo.

Tena wangewaunga mkono pale wanapoona wanaonesha vipaji wakiwa wadogo kwa sababu ya kuamini kwamba watakuwa watu mashuhuri na wenye utajiri mkubwa. Mama yake Justin Bieber, alipoona mwanaye ana kipaji cha muziki, alimnunulia guiter kwa sababu ya kuamini mwanaye anapita njia ya mafanikio. Leo hii anafaidi matunda ya kipaji cha mtoto wake. Ifike wakati, wazazi wote wawe na imani hiyo na wawekeze kwenye vipaji vya watoto wao.

UTALII:
Bila kuzunguka, hapo ulipo unaweza kutafakari ni kwa namna gani sanaa imeweza kuitangaza Nigeria. Anzia filamu zao, tasnia yao ya filamu (Nollywood), imeweza kuwatangaza kwa kiasi gani? Unaweza tu kupata jibu la haraka kwamba taifa hilo limetangazika kwa kiwango ambacho siyo cha kawaida wala cha chini.

Kama filamu za Nigeria zimeweza kuteka soko la Afrika na dunia kwa kiasi fulani, haiwezi kukufanya uumize kichwa sana kujua kwamba taifa hilo, limeweza kupata matangazo mengi kupitia sanaa ya maigizo, na zaidi kuvuta watalii kutoka pande mbalimbali za dunia.

Baada ya hapo jaribu kuwaza, ni kwa kiasi gani kundi la P-Square limefanikiwa kuifanya Nigeria kuwa taifa linalotajwa mara nyingi na watu mbalimbali duniani kila yanapoibuka mazungumzo au majadiliano ya kukua kwa muziki barani Afrika? Je, unaweza kuona matunda ya wanamuziki kufanikiwa?

Tangu mwaka 1983, Nigeria ilishaanza kung'ara kimataifa kupitia sanaa. Kuchomoza kwa mwanamuziki Sunny Ade, kisha kampuni kubwa ya muziki duniani ya Island Records kubeba jukumu la kutangaza muziki wa staa huyo, kuanzia albamu yake "Synchro-System" hadi ziara zake, kulifanya watu wa mataifa mbalimbali kuanza kuifuatilia Nigeria.

Ongezea mafanikio ya 2face Idibia, D'Banj, Davido, Iyanya na wengine wengi. Jumlisha na ukweli kwamba zama hizo hakukuwa na mtandao mkubwa wa mawasiliano kama ilivyo sasa. Kisha pata jawabu ni kwa kiasi gani, sanaa imeiweka Nigeria kwenye ramani ya dunia.

Ukweli kwamba kiwanda cha filamu Nigeria (Nollywood), kinashika namba tatu kwa utengenezaji na uuzaji wa filamu duniani kwa sasa baada ya Hollywood, Marekani na Bollywood, India, ukupe pointi nyingine ya nyongeza kuwa sanaa ni mtaji mkubwa nchini Nigeria.

Bila shaka mpaka hapo, utakuwa umeshajiridhisha pasipo shaka kuwa sanaa imechangia ukuaji wa sekta ya utalii nchini humo kwa kiasi kikubwa sana. Mamilioni ya watu huingia Nigeria kila mwaka kwa ajili shughuli mbalimbali za utalii lakini zaidi kuona na kujifunza namna wasanii wa nchi hiyo wanavyofanya sanaa za filamu na muziki.

Juni 2000, Benki ya Dunia kwa kutambua umuhimu wa sanaa na nguvu yake kwa ukombozi wa kiuchumi kwa vijana wenye vipaji na jamii kwa jumla, ilifanya kongamano la kujadili njia za kusaidia maendeleo ya muziki kwa nchi sita za Bara la Afrika, ambazo ni Afrika Kusini, Zimbabwe, Ghana, Nigeria, Senegal na Mali.

Kwa nyongeza tu hapo ni kuwa nchi zote ambazo zimetajwa, kutoka mwaka 2000 hadi 2010, kila moja ilikuwa imeshtengeneza wanamuziki ambao, uwezo wao wa kifedha kwa kulinganisha na sarafu ya Tanzania, ni haki kuwaita mabilionea.

Swali; Kama Benki ya Dunia inaweza kuwekeza kwenye sanaa Afrika kwa kuamini inaweza kuwa mkombozi wa kiuchumi katika uwanja mpana, ni kwa nini Tanzania mpaka leo, hakujawa na dhamira ya dhati ya kuifanya sanaa kuwa sekta rasmi na iweze kutumika katika mageuzi ya kiuchumi?

Tangu mwaka 2000 baada ya kongamano hilo la Benki ya Dunia, Ghana imefanikiwa kuingiza fedha nyingi katika Pato la Ndani la Taifa kupitia sanaa, hasa baada ya wanamuziki wake kufanikiwa kupenyeza kazi zao katika mataifa mbalimbali duniani. Afrika na nje ya Bara ya Afrika.

Ushuhuda mkubwa ambao Ghana inao kupitia maajabu ya sanaa ni kutanuka kwa sekta ya Utalii baada ya wasanii wa nchi hiyo kufanikiwa kutamba kimataifa. Leo hii, nchi hiyo imekuwa ikipokea mamilioni ya wageni ambao wamekuwa wakiitembelea vivutio mbalimbali, ikiwemo sanaa lakini sababu kuu ni kwa kuvutiwa na kazi za wasanii na kusoma sanaa ya Afrika.

John Collins, mkufunzi katika Shule ya Sanaa za Maonesho katika Chuo Kikuu cha Ghana, aliandika kitabu kinachoitwa Ghana and the World Music Boom, ndani yake alielezea mafanikio ya Ghana kiutalii, baada ya wasanii wa Ghana kufanikiwa kutamba nje ya mipaka ya nchi hiyo.

Aliandika kuwa mwaka 2003, Ghana ilianza kuwa na ingizo kubwa la wageni, hivyo kuinufaisha sekta ya Utalii. Katika maandishi yake, alisema kuwa jumla ya watu 550,000 waliingia nchini humo, ikiwa ni mara mbili zaidi ya kabla sanaa haijawa na umaarufu wa kimataifa.

Collins aliongeza kuwa mwaka 2004, idadi ya watalii ilipanda kwa 100,000 zaidi hadi kufikia 650,000. Yaani kadiri sanaa ya Ghana ilivyokuwa inavuma kwenye soko la kimataifa, ndivyo na wageni walivyomiminika nchini humo kushuhudia "yaliyomo", hivyo kuwa na matokeo mazuri katika ingizo la pato la kigeni.

Kwa mujibu wa Collins, hivi sasa Ghana inapokea mamilioni ya wageni kila mwaka kutokana na mchango mkubwa wa sanaa. Na inatambulika rasmi kwamba sanaa nchini Ghana inawezesha sekta ya Utalii kushika nafasi ya tatu kwa kuingiza fedha za kigeni baada ya dhahabu na mbao.

Kabla ya sanaa kuchukua nafasi pana, mpaka mwaka 2000 sekta ya Utalii ilikuwa na wastani wa kuingiza dola milioni 350, mwaka 2004 baada ya mwamko mkubwa wa sanaa, Utalii ulifikisha ingizo la dola milioni 800. Kwa sasa utalii kila mwaka nchini Ghana, unatengeneza wastani wa zaidi ya dola bilioni 3 ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 5.

Hiyo ni tathmini ya Ghana. Ni wazi kwamba hapa Tanzania inawezekana kabisa kufikia hatua nzuri na kuona matokeo ya faida ya sanaa katika Utalii kama wasanii watafanikiwa. Kujitangaza inahitaji fedha, msanii wa Kitanzania hawezi kujulikana kila kona ya Afrika, Ulaya, Asia, Marekani, Australia na kwingineko kama hajitangazi. Na bila pesa atajitangaza vipi?

Huu ni wakati mwafaka kwa mamlaka za Utialii kama Tanapa, Bodi ya Utalii na kadhalika, kuamua kwa dhati kabisa kuwawezesha wasanii wa Tanzania, wadhamini kazi zao, watengeneze fedha na wawasaidie kwenda kujitangaza nje ya nchi. Baada ya hapo kutakuwa na matokeo yanayoonekana.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alimchukua msanii wa filamu Tanzania, Aunty Ezekiel, walikwenda Marekani kufanya kile ambacho walikisema kuwa ni kutangaza Utalii. Makosa hapa ni ya kufikiri; Wamarekani wangapi wanamjua Aunty Ezekiel? Yalikuwa ni matumizi mabaya ya fedha. Kabla ya Aunty kutumika, alipaswa kutangazwa yeye kwanza.

Ni kwa sababu Tanzania yetu haina utaratibu wa kufuatilia wageni wanaokuja nchini. Ila kwa hakika, kuchomoza kwa mwanamuziki Nasibu Abdu Juma ‘Diamond', kumekuwa na matokeo ya ujio wa wageni wengi, kuja nchini kununua kazi zake (ingawa kimagumashi) na kwenda kuziuza kwao.

Mazungumzo yangu na wauzaji CD za muziki na filamu, wanathibitisha kuwa kuna kundi la watu kutoka Comoro, Sudan, Ethiopia, Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda, DRC, Congo Brazzaville na kwingineko mpaka Afrika Magharibi. Miongoni mwao wapo mpaka ma-DJ ambao mbali na kazi za Diamond, hufuatilia za wanamuziki wengine wa hapa nchini ili kwenda kuboresha ladha ya kazi zao.

Malebo Ishaka ni muuza CD Kariakoo, aliniambia: "Mafanikio ya Diamond nje ya Tanzania, yamesababisha ujio wa wageni wengi na kwa kweli biashara inakwenda vizuri kila wanapokuja. Wapo wafanyabiashara wanaokuja kununua CD kwa wingi, tena kwa jumla, nao husema wanakwenda kuzirudufu ili wakauze kwenye nchi zao na kupata faida.

"Kwa kawaida huanza kuulizia nyimbo za Diamond na baadaye hutaka kujua wanamuziki wengine ambao wanafanya vizuri. Kuna ma-DJ, hawa hutaka mseto wa nyimbo za wasanii wa Tanzania ili wakawarushe katika madisko yao. Kimsingi wageni wanakuja na CD wananunua ila sababu kubwa ni Diamond. Wanakuja Tanzania kwa sababu wanajua ndiyo nyumbani kwao Diamond, na kwa hivyo hata muziki wake unakuwa rahisi kuupata."

Malebo anaongeza: "Wakati Kanumba (marehemu Steven Kanumba) alipokuwa anatikisa katika soko la filamu, vilavile watu mbalimbali walikuwa wanakuja nchini kutoka mataifa tofauti kufuata filamu za Kanumba na za Watanzania wengine, nao walikuwa wanakwenda kuuza.

"Kanumba alipofariki dunia, idadi ya watu waliokuja nchini kufuata filamu zake iliongezeka zaidi ya maradufu. Watu walikuwa wengi sana. Hata sasa watu huwa wanakuja lakini si kwa idadi kubwa kama kipindi kile. Mahitaji yao ni filamu za JB (Jacob Stephen), Ray (Vincent Kigosi), Dk. Cheni (Mahsein Awadhi), Jully Tax na wengine japo siyo sana."

Hapa ni kuonesha kuwa kama biashara ya kazi za sanaa itakuwa rasmi na kuwekewa utaratibu wenye sifa za kutambulika kiserikali, inaweza kusababisha utambuzi sahihi wa idadi ya wageni wanaowasili nchini kwa matilaba ya sanaa na kadhalika.

Lakini hiyo ni kuonesha kuwa sanaa ikitumika vizuri na wasanii wakawezeshwa kufanya kazi yenye faida na kujitangaza kimataifa, inatosha kuwa mwarobaini wa wa sekta ya Utalii. Ni rahisi sana kuukuza Utalii na kuingiza fedha nyingi za kigeni kama wasanii watawezeshwa kujitangaza ndani na nje ya nchi.

VIWANDA NA BIASHARA:
Kazi za sanaa zinategemea viwanda kwa utengenezaji wake. Pale wasanii wanapotengeneza fedha, huutafsiri mzunguko wa sanaa kwamba ni mzuri na kwa hivyo, huchagiza mwamko wa sekta ya Viwanda na Biashara.

Hivi sasa, viwanda vya kazi za sanaa havichanui wala kuonekana kwa sababu wasanii hawana fedha. Mzunguko wake ni mbaya na soko limebanwa. Wizi na ufisadi vimetamalaki.

Wasanii wanapokuwa na fedha ni fursa nzuri kwa wafanyabiashara mbalimbali. Mathalan wenye maduka ya nguo, watauza sana kwa sababu kubadili mwonekano ni sehemu ya sanaa. Lazima abadili mavazi katika maonesho yake kwa lengo la kujipa heshima na thamani zaidi ya kibiashara.

Katika eneo hili, wabunifu wa mavazi ambao nao ni wasanii, hupata kazi zaidi kwa ajili ya kuwapendezesha wenzao katika sanaa tofauti, hususan waigizaji na wanamuziki. Hoja iliyopo hapa ni kuwa mbali na sababu za kibiashara lakini mafanikio katika aina fulani ya sanaa, husisimua mwamko wa sanaa nyingine.

Wasanii wanapokuwa kwenye maonesho yao, wafanyabiashara wa vitu mbalimbali, hujitokeza kuuza chakula, vinywaji, mavazi na hata nakshi za aina tofautitofauti. Hii ni sehemu ya biashara, ingawa inaweza kubeba tafsiri ya soko la ajira kwa upana wake.

Katika kipengele hiki, unaweza kupata neno la "uchumi wa ubunifu". Jokate Mwegelo ‘Jojo' kupitia ‘brandi' yake ya Kidoti, ameweza kuingia mkataba na Wachina kwa ajili ya kutengeneza na kuuza bidhaa zenye nembo ya Kidoti. Mkataba huo thamani yake ni zaidi ya shilingi bilioni 8 na unahusu zaidi mavazi.

Hapa ni kuonesha kwamba Jokate amewavutia Wachina kuwekeza katika soko la Tanzania. Yupo pia Sheria Ngowi ambaye ubunifu wake wa mavazi umeshavuka mipaka ya nchi. Ni suala la njia tu, uchumi wa sanaa ni mpana na ni rahisi.

Kuna biashara ya mahoteli. Wasanii wa filamu wanapokuwa kwenye shughuli za kurekodi, mara nyingi hulazimika kukaa kambini. Kwa mantiki hiyo hukodi hoteli na kuingiza kipato kwa mmiliki na kodi.

Katika mataifa mengine ambapo sanaa inalipa, wasanii hukodi hoteli hata mbili au tatu kwa mkupuo na kuzitumia kurekodi filamu au tamthiliya kwa kipindi cha miezi. Ni suala la uwezo wa kifedha tu, Tanzania itawezekana kufika huko kama wasanii wataweza kutengeneza fedha.

Biashara ya mahoteli, inagusa pia wageni ambao hutembelea nchi kwa sababu mbalimbali, kama kitalii, kibiashara na kadhalika, nao hulala kwenye mahoteli. Uchumi unatanuka.

Makampuni ya kibiahara nayo hutaka kufanya biashara kupitia sanaa kwa kudhamini maonesho, au kuingia makubaliano na wasanii kwa mikataba ya ubalozi wa matangazo (endorsements). Michakato yote hiyo ni biashara na kodi inapaswa kulipwa.

Kila onesho la wasanii lenye sura ya kibiashara linalipiwa kodi. Mamlaka ya sanaa, kwa mfano Baraza la Sanaa la Taifa, hutoza fedha kwa ajili ya kutoa vibali. Hiyo yote ni mirija inayowezesha serikali kuvuna fedha kupitia sanaa.

Sanaa ikiwa vizuri huongeza kipato katika vyombo vya usafiri na vituo vya mafuta. Wanaokwenda kwenye maonesho watapanda dalala na taksi, hivyo kulipa nauli. Wapo watakaopanda vyombo vyao lakini nao hununua mafuta.

Tanesco huingiza fedha kupitia umeme ambao unatumika kwenye kumbi za burudani. Yanapowashwa majenereta, biashara ya mafuta inakuwa imefanyika.

UWEKEZAJI:
Jokate na Wachina wanaingia hapa na kuleta maana iliyonyooka kabisa. Jokate ni mwekezaji wa ndani na Wachina kutoka nje. Faida iliyopo hapa mbali na mzunguko wa kibiashara kutokana na uwekezaji huo, serikali inanufaika kwa kutoza kodi uwekezaji wenyewe na biashara zake.

Katika sekta ya uwekezaji, sanaa inapofanikiwa wawekezaji mbalimbali hujitokeza na kujenga majumba ya maonesho, kumbi za burudani na starehe. Upo uwekezaji mpaka wa vyuo vya sanaa kwa sababu sanaa inapolipa, huongeza hitaji la watu kuisomea kwa undani zaidi fani ili waifanye kwa weledi.

Hivyo basi, uwekezaji wa sanaa unaenda sambamba na kutanuka kwa elimu. Kwa msingi huo, mafanikio ya wasanii, yatakuwa na matokeo makubwa kabisa kwamba Chuo cha Sanaa Bagamoyo hakitoshi. Ila hivi sasa kinatosha kwa sababu hakuna hitaji kubwa la wasomi wa sanaa.

Kuna uwekezaji wa studio na makampuni ya usambazaji. Inawezekana kampuni ya nje ikatamani kuwekeza kwa msanii wa hapa nchini kama ambavyo staa wa Marekani mwenye asili ya Senegal, Akon alivyosaini makubaliano na Kundi la P-Square kupitia ‘lebo' yake ya Konvict Music

Mfano mwingine ni D'Banj wa Nigeria alivyosaini mkataba na ‘lebo' ya Good Music, inayomilikiwa na rapa wa Marekani, Kanye West. Lazima kwanza mwanamuziki aoneshe mafanikio ya awali ndipo ataweza kupata mikataba mikubwa ya makampuni makubwa ya nje.

Maprodyuza wakubwa wa muziki na hata wa filamu, hawawezi kuja Tanzania kuwekeza kwa sababu soko lake lina giza. Hakuna mwekezaji anayeweza kuingiza uwekezaji wake kwenye mazingira ambayo haoni fursa ya kutengeneza fedha itakayolipa gharama na kumpa faida.

AJIRA:
Msanii mwenyewe ni ajira. Anapofanikiwa ataajiri watu ili wamsaidie kufanya kazi zake. Kazi zake zinapoingia sokoni, kuna mnyororo mrefu wa mauzo mpaka kumfikia mnunuzi wa mwisho. Kila anayehusika katikati ni ajira tosha.

Msanii mwenye mafanikio lazima aajiri walinzi, madereva, mameneja na watumishi mbalimbali watakaorahisha kazi zake. Leo hii kuna kelele kuwa filamu za Kitanzania zinakosewa tafsri (subtitles), kama msanii angekuwa na fedha za kutosha angeajiri mkalimani aliyebobea.

Ndiyo maana inabainishwa kuwa msanii mmoja anaweza kutengeneza ajira za watu mpaka 200. Kama wasanii 1000 watafanikiwa kufanya vizuri kibiashara, wanaweza kutengeneza ajira za watu 200,000 na zaidi.

Ripoti za nchini Afrika Kusini zinabainisha kuwa asilimia tano ya raia wa nchi hiyo, wameajiriwa kupitia mnyororo wa sanaa. Hata hivyo, upo mjadala kuwa utafiti makini haujafanyika, kwani kuna uwezekano mkubwa waajiriwa wakawa asilimia kubwa zaidi ya hiyo.

Kwa mujibu wa Collins, mpaka mwaka 2007, utafiti rasmi ulikuwa unaonesha kuwa sanaa ilifanikisha ajira za watu zaidi ya 400,000 nchini Ghana. Na kwa kasi iliyopo sasa kwa sababu sanaa ya Ghana inakua kwa kasi, upo uwezekano ajira za sanaa zikawa zimefika 600,000 mpaka 700,000.

Jokate baada ya kusaini dili la mabilioni na Wachina, lilifanya aongeze idadi ya wafanyakazi. Sheria Ngowi hafanyi kazi zake peke yake, anao watu anashirikiana nao. Akina Khadija Mwanamboka, Mustafa Hassanali, Asia Hidarus, Ally Remtullah, Martin Kadinda na wengineo, kuna watu wanafanya nao kazi. Huko ndiko kupanuka kwa soko la ajira.

KUKUA KIBIASHARA KWA VYOMBO VYA HABARI:
Kama wamiliki wa vyombo vya habari wangekuwa wanaelewa kwa upana jinsi mafanikio ya wasanii yanavyoweza kuongeza fedha kwenye akaunti zao, hakika wangekuwa wakali sana kwa watangazaji na ma-DJ wao wanaowabana na kuwaminya wale ambao wanagoma au kushindwa kutoa rushwa.

Wasanii wenye mafanikio hujiongoza wenyewe. Hata bila mapromota, wanaweza kuandaa maonesho yenye mafanikio kwa kuwatumia mameneja na maofisa wao. Msanii ni kampuni. Katika onesho hilo atahitaji matangazo, kwa hiyo atalipa vyombo vya habari ili vicheze na kuchapisha matangazo yake.

Kwa kawaida wasanii wanapofanikiwa hukuza ushindani. Na kitafiti ni kuwa mafanikio ya msanii huendana na idadi ya mashabiki. Aliyefanikiwa sana maana yake ana wafuasi wengi na hao ndiyo wateja wake. Msanii na shabiki wake ni sawa na mfanyabiashara na mteja wake.

Msanii mmoja atakuwa anaandaa onesho lake ukumbi A, mwingine B, yupo atakayefanyia C, yupo wa D na kadhalika. Wote hao watalipa mtangazo ya redio, televisheni na magazeti. Kwa hiyo vyombo vya habari vitaongeza fedha na kutanuka zaidi kibiashara.

Ukiachana na hoja hiyo ya matangazo, mafanikio ya wasanii hukuza pia idadi ya wasomaji kwenye magazeti, wasikilizaji redioni na watazamaji katika televisheni. Shabiki anampenda msanii wake, kwa hiyo atasikiliza redio na kutazama runinga inayocheza wimbo wa msanii anayempenda. Atasoma gazeti lililondika habari ya msanii wake.

NI MUHIMU SANA WASANII KUWA MATAJIRI:
Baada ya kupitia maeneo yote, sasa unaweza kurejea tena kusoma mwanzo mpaka hapa katika somo hili la Uchumi wa Sanaa na Utajiri wa Wasanii, kisha rejea tena, bila shaka tutakubaliana kwamba sanaa siyo sekta ya kuchezewachezewa, wala haipaswi kupuuzwa hata kidogo.

Sasa tutakuwa pamoja na kuelewana pasipo ubishi pale tunaposema kwamba ni muhimu wasanii wakawa matajiri kwa ajili ya ukombozi mpana wa vijana katika soko la ajira na mzunguko mzuri wa kiuchumi.

By Luqman Maloto
 
Dah uzi mrefu na mzur. Ikumbukwe pia ni wasinii wa Hollywood walicheza nafas kubwa kumfanya Obama awe rais kwa mihula miwili. Pia hapa bongo ni haohao walimsaidia huyu bweeegee tunaye
 
Back
Top Bottom