Uadilifu katika uongozi na dira ya maendeleo

Yona F. Maro

R I P
Nov 2, 2006
4,202
218
THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF – Chama Cha Wananchi)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI APRILI 28 2009
UADILIFU KATIKA UONGOZI NA DIRA YA MAENDELEO​


Watanzania tuna stahiki kuwa na dira ya taifa ya kujenga nchi inayoheshimu haki za binadamu, yenye misingi mizuri ya demokrasia ambapo raia wote watu wazima na wenye akili timamu wana haki ya kushiriki kikamilifu katika uamuzi wa masuala yanayohusu maisha yao na hatma ya nchi yao. Kila raia popote alipo awe na haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa kiongozi toka ngazi ya kitongoji/kijiji/mtaa mpaka uongozi wa taifa.

Kujenga umoja wa kitaifa wa kweli ambako hamna ubaguzi wa aina yeyote wa jinsia, kabila, rangi, dini au ulemavu. Kuhakikisha kuwa serikali inaheshimu dini zote na inajenga mazingira ya waumini wa dini mbali mbali kuheshimiana na kuvumiliana.

Kuhakikisha kuwa kila mwananchi ana uwezo au anawezeshwa kupata milo mitatu kwa siku. Hatua za maksudi zichukuliwe kuhakikisha kuwa kina mama waja wazito na watoto wachanga wanapata lishe bora kwani mtoto mchanga asiye na lishe bora ananyimwa haki ya kujenga mwili, kinga ya mwili na ubongo wake ili aweze kushiriki kikamilifu katika kujielimisha na kujiendeleza na kufikia uwezo wake aliojaliwa na Mwenyezi Mungu.

Kuhakikisha kuwa kila raia ana haki na anapata huduma za msingi za afya. Hatua maalum zichukuliwe kuhakikisha kuwa huduma za uzazi anapatiwa kila mama mja mzito ili kupunguza vifo vingi vya kusikitisha vya kina mama wajawazito.

Wazee wengi baada ya kulitumikia taifa kwa muda mrefu wanaishi katika umaskini wa kutisha. Watoto wao hawana kipato cha kutosha na maadili ya kuwalea wazee yameporomoka. Kama taifa ni muhimu turejeshe na kujenga maadili ya kuwaheshimu na kuwaenzi wazee. Tuweke utaratibu wa kitaifa wa hifadhi ya wazee itakayohusisha jamii kuwalea wazee wetu.

Elimu ndiyo ufunguo wa maisha. Ili kujenga taifa linalojiamini, watoto wote wa Tanzania wawe na haki ya kupata elimu bora ya msingi na ya sekondari. Taifa lijenge utamaduni wa kuamini kuwa elimu haina mwisho na kila raia ajiendeleze kielimu hasa kwa kutumia vizuri teknolojia ya habari na mawasiliano.

Elimu ya wasichama ni nyenzo muhimu ya kuleta haki sawa kwa wananchi wote na kuhakikisha kizazi kijacho kinakuwa na fursa sawa katika kuleta na kuneemeka na maendeleo. Wasichama wengi hawamalizi masomo yao kwa sababu ya uwezo wa fedha wa wazazi, mila zilizopitwa na wakati zinazowabagua wasichama na wanawake, mazingira mabovu ya shule kama vile kutokuwa na vyoo vya wanawake mashuleni.

Kuwaelimisha wasichana na wanawake kushiriki katika soko la ajira ni nyenzo muhimu ya kuvunja mduara wa umasikini unaorithisha umaskini toka kizazi kilichopo na kinachofuata.

Ili kufanikisha mabadiliko ya kiuchumi, kuongeza tija na ajira, Taifa litoe kipaumbele maalum katika kuendekeza elimu ya sayansi na teknolojia.

Kujenga uchumi wa kisasa wenye ushindani kimataifa na utakaohimili misukosuko ya utandawazi, unaokua kwa kasi bila kuharibu mazingira na wenye manufaa kwa wananchi wote. Wananchi wahisi na waone kuwa uchumi wa taifa unatoa fursa sawa kwa wananchi wote. Tofauti za vipato vya wananchi visiwe vikubwa mno huku tukizingatia kutoa motisha kwa raia kuwa wabunifu na wajasiramali hodari. Mikakati ya kukuza uchumi itafanikiwa iwapo itatoa fursa kwa wananchi wote kufaidi matunda ya kukua kwa uchumi.

Haiwezekani watanzania kuondokana na umaskini bila kukuza uchumi unaoongeza ajira. Ikiwa pato la taifa la mwaka 2007 lingegawanywa sawa sawa kwa kila Mtanzania, kila mmoja wetu angepata dola za kimarekani 428 kwa mwaka sawa na dola 1.17 kwa siku au shilingi za Tanzania 1340/- kwa siku. Bila kukuza uchumi umaskini uliokithiri utakuwa tatizo la kudumu. Katika suala la kukuza uchumi hakuna miujiza. Uchumi unakua kwa kuongeza elimu, ujuzi na utaalamu wa wafanyakazi, ongezeko la raslimali na vitendea kazi, na kuongezeka kwa ufanisi na tija katika uzalishaji na utoaji huduma. Kukua kwa uchumi kunahitaji uongozi imara na utawala bora, mikakati na mipango mizuri ya maendeleo na utekelezaji mzuri wa mikakati na mipango hiyo. Mpaka hivi sasa hatuna Dira ya maendeleo na mikakati madhubuti ya utekelezaji inayoeleweka kwa wananchi wote. Dira ya Maendeleo ya 2025 ilitayarishwa na wataalamu kuliko kuwashirikisha jamii kwa ujumla, haileweki kwa wananchi wengi na haitumiwi kuhamasisha wananchi katika ujenzi wa taifa letu. Ukosefu wa uongozi ni kizingiti kikubwa kinachozuia kupitia, kuchambua na kubuni dira ya maendeleo inayozingatia hali halisi ya nchi yetu na mabadiliko ya uchumi duniani. Chama cha CUF kupitia mijadala na Wananchi kinaandaa Vision for Change – Dira ya kuleta mabadiliko itakayoonyesha njia ya kuleta haki sawa kwa wananchi wote na kujenga uchumi unaokua na kuleta neema kwa wananchi wote.

Ombwe la Uongozi linadhihirika kwa kushindwa kwa uongozi kwa CCM na Rais Kikwete katika mapambano dhidi ya ufisadi. Ufisadi ni matumizi ya dhamana na wadhifa uliopewa na umma kwa manufaa yako binafsi. Inajumuisha kudai na kupokea rushwa, matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za umma na kuiba fedha za umma. Rushwa ni adui wa haki, na pia ni adui mkubwa wa maendeleo. Rushwa ni saratani (cancer) inayoua uchumi na kuwanyima wananchi haki ya maisha mazuri na maendeleo. Chanzo kikubwa cha rushwa ni ukiritimba wa madaraka, mishahara midogo ya watendaji serikalini, maamuzi yasiyofuata taratibu zinazoeleweka na kutowajibishwa kwa wanaoshiriki katika vitendo vya rushwa. Vita dhidi ya rushwa itafanikiwa ikiwa ukiritimba wa madaraka utaondolewa, maamuzi ya kiserikali yatafuata taratibu zilizo wazi na zinazoeleweka na kuwaadabisha wanaoshiriki katika rushwa.

Mfumo wa rushwa unapunguza uwekezaji wa vitega uchumi ulio makini na kwa hiyo kupunguza ongezeko la ajira na ukuaji wa uchumi. Kwa wawekezaji makini rushwa ni mbaya kuliko kodi kubwa kwa sababu haitabiriki na mtoaji hana uhakika kuwa aliyepokea atatimiza ahadi ya kutoa huduma iliyolipiwa rushwa.

Kukithiri kwa rushwa kunaathiri utumiaji mzuri wa vipaji vya ujasiriamali. Wafanyabiashara wenye vipaji vizuri wanatumia uwezo wao kupata utajiri kwa njia rahisi za rushwa badala ya kuwa wavumbuzi wa njia bora za kuongeza uzalishaji, tija na faida katika shughuli halali za kiuchumi.

Rushwa inapunguza uwezo wa misaada kutoka nje kusaidia kukuza uchumi na kupunguza umaskini badala yake inachochea nchi na serikali kuwa tegemezi milele. Kwa sababu ya rushwa mikopo na misaada ya nje haijengi miundombinu imara kama vile barabara, ufuaji na ugavi wa umeme, huduma za maji, afya na elimu. Rushwa inafanya gharama za miradi kuwa kubwa mno. Uchambuzi wa mradi wa kusimamia mali ya asili (Management of Natural Resources Programme (MNRP)) iliofadhiliwa na serikali Norway 1994 – 2006 na kugharimu dola milioni 60 umeonyesha kuwa hadi nusu ya fedha hizo dola milioni 30 zimetafunwa kifisadi.

Rushwa inasababisha nchi iwe na miundombinu na huduma hafifu. Rushwa inahatarisha afya na maisha ya wananchi. Madawa hafifu au yaliyopitwa na wakati yanaingia nchini na kutumiwa na raia. Vifaa vibovu kama vile nyaya za umeme zinaingizwa nchini na kusababisha ajali zinazoweza kuunguza nyumba na kupoteza maisha ya watu. Maghorofa na madaraja yanajengwa bila kuzingatia viwango.

Rushwa inapunguza mapato ya serikali. Wafanyabiashara na makampuni yanatumia rushwa kukwepa kodi na kuipunguzia uwezo serikali kutoa huduma muhimu kwa wananchi kama vile elimu na afya.

Rushwa ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali inachangia kuwepo kwa mikataba mibovu katika sekta mbali mbali ikiwemo madini inayoihujumu serikali. Mikataba inaandaliwa kwa makusudi iwe na gharama kubwa kwa serikali kama itaitekeleza na gharama kubwa zaidi ikiwa itaivunja. Upande wa pili ukivunja mkataba haupati gharama kubwa.

Rushwa inaendeleza matumizi mabaya ya fedha za umma. Miradi mikubwa yenye mianya ya rushwa inapendelewa zaidi kuliko matumizi yatakayochochea maendeleo ya watu. Uongozi wa Benki Kuu ulichangamkia sana ujenzi wa minara pacha (twin towers) kwa gharama kubwa bila shaka kwa sababu ya rushwa. Inawezekana kuwa robo ya gharama ya majengo hayo ingeweza kukidhi makao makuu yenye taratibu zote za kiulinzi wa Benki Kuu. Serikali ingeweza kutumia robo tatu iliyobaki kuanzisha kama mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo na Benki ya Maendeleo ya Viwanda.

Athari mbaya zaidi ya rushwa ni mmomonyoko wa maadili ndani ya serikali na katika jamii. Kuwepo kwa rushwa miongoni mwa viongozi waandamizi wa serikali kunaathiri uadilifu kwa watendaji wote wa serikali. Kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali amejitajirisha kwa rushwa, kwa nini Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya naye asitafute mbinu za kujitajirisha hata kama rushwa hiyo itaongeza gharama za kupambana na UKIMWI? Kama wakubwa wanakula basi wadogo watataka alau walambe. Mwanasheria Mkuu mmoja wa Serikali inasemekana alitoa agizo lisilo rasmi kwa maafisa wake kuwa kila mtu ale kwenye meza yake mwenyewe. Saratani ya rushwa inaathiri mfumo mzima wa serikali.

Najua kwamba hivi sasa kumekuwepo na hisia kwamba Serikali ya Rais Kikwete iko makini katika kupambana na ufisadi kutokana na kesi dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi zilizofikishwa Mahakamani. Mimi binafsi siamini kwamba kesi hizo zitafika popote. Naziona kama ni mchezo mchafu wa kisiasa wenye lengo la kuwahadaa Watanzania na jumuiya ya kimataifa waone hatua zinachukuliwa lakini baadaye kusitokee jambo lolote la maana. Inawezekana kabisa zina malengo ya kuifanya Serikali ya CCM ionekane inapambana na ufisadi na hivyo kutumiwa kama kete ya kuombea kura katika uchaguzi mkuu wa mwakani lakini baada ya hapo zife kidogo kidogo. Mfano mzuri wa haya ninayoyaeleza ni kupeleka kesi Mahakamani dhidi ya Sailesh Vithlani ya kupokea rushwa ya dola za Marekani milioni 12 (shilingi bilioni 15.6) kutoka kampuni ya BAE ili Tanzania inunue rada ya bei mbaya ya dola milioni 40 (shilingi bilioni 52.0) badala ya rada ya dola milioni 5 (shilingi bilioni 6.5) wakati mtuhumiwa ameshafanyiwa mipango na kuondoka nchini. Vigogo waliokuwa serikalini wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kuisababishia serikali kupoteza mapato na siyo kwa kosa la kupokea rushwa. Na wao wanajitetea kuwa walikuwa wanatimiza amri ya Rais ambaye hawezi kufikishwa mahakamani. Hawakushtakiwa hata kwa kuwa na mali isiyoelezeka kwa mapato yao halali.

KAULI YA MENGI
Mwenyekiti wa IPP Media ametoa kauli anayodai kuwa anamuunga mkono Rais Kikwete katika vita anayoingoza ya kupambana na Ufisadi. Amedai kuwa kuna mafisadi wakubwa 10 na ikiwa mafisadi papa watano aliyowataja kwa majina watashughuliliwa ipasavyo tutamaliza tatizo la ufisadi Tanzania. Majina aliyoyataja ni wananchi wenye asili ya kiasia. Maelezo ya Bwana Mengi ni kuwa watumishi wa serikali au wanashawishiwa au kulazimishwa na mafisadi wakubwa, mfumo wa maamuzi na watendaji serkalini siyo tatizo la msingi la ufisadi.

Kauli ya Bwana Mengi haisaidi vita dhidi ya rushwa na kwa kweli inaidhoofisha na kupoteza malengo. Udhaifu na ukosefu wa uongozi imara wa Rais Kikwete ndio uliochangia kuenedelea kwa rushwa. Kama Rais Kikwete angekuwa imara katika uongozi wake kwani Richmond isngetokea kwa kuwa Baraza la Mawaziri chini ya Uenyekiti wake liliamua CDC Globeleq ifanye kazi ya kufua umeme wa gesi baada ya marekebisho machache ya makubaliano ya serikali na kampuni hiyo. Waziri Mkuu na Wizara ya Nishati na Madini wasingeweza kubadili maamuzi ya Baraza la Mawaziri bila Rais kuafiki mabadiliko hayo.

Rais Kikwete angeweza kuingilia suala la ufisadi wa EPA mwezi Septemba 2006 wakati wakaguzi wa mahesabu ya Benki Kuu, Delloitte and Touche, walipoibua na kutoa ushahidi kuwa kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd ilichota kwa nyaraka za kughushi dola milioni 30 toka akaunti ya EPA. Pamoja na Waziri wa Fedha kuelezwa tatizo hili, Gavana Balali hakuziiwa kuwafukuza wakaguzi wa mahesabu. Uteuzi wa wakaguzi wapya ulifanyika baada ya shinikizo la nchi na mashirika yanayotoa misaada.

Mwezi Machi 2008 Mwanasheria Mkuu wa serikali alipelekewa barua na taasisi ya Uingereza inayochunguza ufisadi mkubwa ikiwataja kwa majina maafisa wawili wa ngazi za juu wa serikali mwaka 1999 wanaotuhumiwa kuhusika na kupokea rushwa katika sakata la serikali kununua rada ya bei ya ya juu ya dola milioni 40. Mpaka hivi sasa maafisa hao hawajafikishwa mahakamani.

Bwana Mengi kumsifia Rais Kikwete kuwa mpambanaji dhidi ya ufisadi siyo ujasiri bali ni kujipendekeza kwa bei rahisi kwa kuwa hivi sasa Rais Kikwete yuko madarakani na akishamaliza kipindi chake na kuachia wadhifa bila shaka atamponda vilivyo.

Kwa kutaja majina matano ya watu wenye majina ya Kiasia kuwa ndiyo mafisadi papa na wakishughulikiwa ufisadi utakisha nchini, Bwana Mengi anacheza karata ya ubaguzi wa rangi. Kwa kusikia majina hayo umma wa Watanzania unashawishiwa uamini kuwa tatizo la ufisadi Tanzania limeletwa na "wahindi wachache." Hawa watano wakikamatwa na kuzuia wengine wasiibuke tutakuwa tumemaliza kazi. Hii ni dhana potufu na ni ya hatari hasa ukuzingatia kuwa baadhi ya wananchi wengi wana mashaka na uzalendo wa raia wenye asili ya kiasia . Anatumia vita dhidi ya ufisadi kupanda mbegu ya ubaguzi. Maamuzi na kutowajibika ndani ya serikali ndiyo chanzo kikubwa cha kuongezeka kwa rushwa na siyo "wahindi wachache." Tukipanda mbegu za ubaguzi wa rangi tutateleza na kuingia katika ubaguzi wa kidini na wa kikabila.

Kwa kuwa Bwana Mengi anaonyesha kuwa ana mahusiano mazuri na ya karibu na Rais Kikwete, jambo la busara, ilikuwa kuchukua ushaidi alionao kuhusu mafisadi papa na kuupeleka kwa Rais Kikwete na kwa TAKUKURU. Kama Rais na TAKUKURU hawatashughulikia ushahidi huo, ndipo angejitokeza na kueleza umma kuwa nimempa Rais Kikwete ushahidi niliyonao wa mafisadi papa, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Tatizo la ufisadi ni la mfumo. Kutokuwa na uwazi katika maamuzi na ukosefu wa uwajibikaji. Rais Mkapa anapaswa kuwajibika alau kwa kuwaomba radhi Watanzania kwa ufisadi mkubwa uliotokea katika kipindi chake. Rais Kikwete awajibike kwa kushughulikia kesi kubwa za ufisadi. Mwaka 2008 TAKUKURU ilikamilisha uchunguzi wa kesi 7 za rushwa kubwa kubwa na kupeleka kwa DPP, Mkurungezi wa mashtaka. Mkurungezi wa mashtaka bila shaka baada ya kushaurina na Rais alitoa kibali cha kesi moja tu ndiyo ipelekwe mahakamani.

Ni matumaini yangu kuwa baada ya kukosoa kauli ya Bwana Mengi, hatatumia umiliki wake wa vyombo vya habari kuagiza kususia kuwaeleza Watanzania harakati za kisiasa za Chama cha CUF za kuwaunganisha Watanzania kujenga nchi itakayokuwa na haki sawa kwa wote bila kujali rangi, dini, kabila au jinsia na itakayojenga uchumi unaotumia vizuri mali ya asili kutoa ajira kwa wingi na kuleta neema kwa wananchi wote. Akifanya hivyo naye pia atakuwa anaendeleza ufisadi.

HAKI SAWA KWA WOTE
Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti wa Taifa
The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi)
DAR ES SALAAM
28 Aprili, 2009
 
Back
Top Bottom