Tutafika Salama Mke wangu

Tutafika Salama Mke wangu

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
34,143
Reaction score
79,573
TUTAFIKA SALAMA MKE WANGU.

Na, Robert Heriel

Miaka ilienda nayo haikurudi, muda ukapita wala hatukuuona tena. Ahadi nilizomuahidi sasa aliziona ni ndoto ya mchana. Ndoto za alinacha kamwe zisizotimia. Loooh!

Niite Taikon wa Fasihi, Dereva wa Bus katika barabara mbovu.

Awali niliwahi kumuahidi tutaishi maisha mazuri, nikamuahidi majumba makubwa ya kifahari, magari ya gharama, nguo za malkia, na hata safari za Dubei, Marekani, na Ulaya, zote hizo zilikuwa ahadi zangu kwake.

Nakumbuka wakati nikimuahidi mambo hayo alikuwa akinitazama uso wake ukiwa na tabasamu, bila shaka alipenda ahadi zangu. Aliniona mimi ndiye ninayefaa, naam mimi ndiye ninastahili kumfikisha katika ndoto zake. Basi akapanda Basi langu, nililokuwa naliendesha, nia na dhamira nimfikishe katika ndoto zake.

Basi akapanda ndani ya Basi langu, mimi nikiwa Dereva yeye akiwa Kondakta.

Basi langu lilikuwa kuukuu lisilo namvuto, lakini maneno yangu yalimvutia mno si ajabu ndio maana akayaacha Mabasi mazuri ya kisasa yanayovutia.
Maneno mazuri huleta hamu, huiosha nafsi kwa nafasi, huleta utamu usiodumu, Maneno matamu hayana hatamu, na kamwe hayadumu kwani ni simu iuayo ufahamu.

Nikatia gia pia safari ikaanza nikiwa na Mke wangu. Tulikuwa wawili tuu, basi gari letu halikuwa na Redio wala Luninga, palikuwa kimya mngurumo wa gari ukikera masikio ya mke wangu. Sisemi mimi sikukerwa lakini siku zote chako ni chako wala si cha mwenzako. Lile Basi lilikuwa langu hivyo nisingeweza kuliponda, hivi ningelipondaje ikiwa sina jingine, ikiwa hilo hilo ndilo nililompakizia mke wangu.

Tambarare tulilifurahia, tambarare katika safari yetu, Magurudumu ya gari yalichekelea tambarare ile. Wote tulikuwa kimya, lakini uso wa Mke wangu ulijawa na hofu, pengine alifikiri kuwa hakufanya uamuzi wa busara kupanda gari yangu. Lakini pumzi aliyokuwa anaivuta ilimpa moyo kuwa mbona hata gari yangu inaenda vizuri tuu. Basi ndivyo ilivyo, Kujifariji huleta tumaini, na tumaini huleta amani ya moyo.

Mimi na usukani, mimi na gia, gari nikaliendesha macho yangu yakiwa mbele kama dereva mbobevu. Umakini wangu ulimfanya Mke wangu apunguze hofu, lakini pengine angefikiri kuwa Dereva makini ndani ya Gari bovu. Lakini sisemi alifikiri hivyo bali hayo ni mawazo yangu.

Baada ya muda kupita tulipanda kwenye kamlima, hapo ndipo kizaa zaa kikazaa kimbembe. Awali Gari lilinguruma kwa nguvu rurururuuruuuu! Huku moshi mbaya mweusi ukitoka nyuma ya gari. Nikajitaihidi na kujitahidi, nikaonyesha ufundi na ujuzi, lakini gari ikagoma kupanda Mlima. Wala usifikiri ulikuwa mlima mkubwa, hata haukuwa hivyo, basi tuu gari langu lilikuwa bovu tena kuukuu.

Hamad! Kufumba na kufumbua gari ikaanza kurudi nyuma baada ya kushindwa kupanda kale kamlima. Nilishika breki holaa! Haaa! Jamani Gari ndio lilianza kuserereka kurudi kinyume nyume. Ajabu ni kuwa mwendo wa kinyume nyume ulikuwa wa kasi zaidi ya ule mwendo wa mbele tuliokuwa tukiendesha tukiwa tambarare.

Kumbe nyuma kuna nguvu zaidi, kunavuta zaidi, kurudi nyuma ni kwa kasi zaidi kwenye maisha kuliko kwenda mbele.

Basi nilichoamua kukifanya ni kushika usukani na kulielekezea gari lifuate Barabara kusudi lisije likatoka nje ya barabara na kuanguka. Sitaki kukumbuka kelele za Mke wangu jamani alivyokuwa akiogopa pale gari lilivyokuwa linarudi kinyuma kwa kasi. Jamani alipiga mayowe, alilia mara kwa mara alishika vizuri ndani ya gari kuogopa kupelekwa huku na huku na gari langu. Sauti yake iliugusa moyo wangu, iliumiza nafsi yangu, ilinitesa sana. Niliumia kuona Mke wangu akiwa anapata mateso kwa sababu yangu. Loooh!

Sasa na mimi jasho lilinitoka, niling'ata mdomo na kutoa macho nje nikihangaika kuliweka gari vizuri. Jambo moja kwa muda ule lilikuwa ni kuokoa maisha yangu na mke wangu kipenzi.

Ikawa Kheri gari likapunguza mwendo pengine ni kwa sababu lilimaliza kushuka kinyume nyume kale kamlima tulikokuwa tumekapanda kidogo. Huuh! Tulipumua tukiwa hatuamini. Lakini mke wangu licha ya kutokuamini lakini hakutaka kuendelea kuwa ndani ya gari langu, kilichotokea kilimtosha.

Basi tukashuka, mahali pale palikuwa hapana makazi ya watu, kulikuwa na vichaka tuu na mapori. Basi tukakaa mahali pale mimi nikitengeneza gari kwani halikutaka kuwaka tena. Huku tukisubiri msaada kwa wenye magari wengine watakaopita. Waliokuwa wakitokea tulipokuwa tunaenda, na waliokuwa wakienda tulipokuwa tunaelekea.

Mke wangu alianza kulalamika, alianza kunung'unika, alinipa maneno makali, sipendi kumlaumu, alikuwa na haki. Mahali pale kulikuwa na jua kali sana, hapakuwa na miti ya kupumzikia zaidi ya vichaka vifupi. Tulisubiri msaada mpaka tukachoka, gari nayo ilitugomea.

Punde kwa mbali tuliona Gari ikija, lilikuwa gari zuri mno. Lilikuwa la gharama sana. Mke wangu alipoliona lile gari likija aliamka upesi uso wake ukifurahia, aliona msaada umefika. Basi lile Gari alikuwepo Kijana wa rika langu ndiye alikuwa akiendesha, alikuwa pekeake.

Akasimama.

Alinisalimu, kisha akauliza kunashida gani, baada ya sisi kujieleza, naye akajieleza jinsi atakavyotupa msaada. Sikutegemea kama angemtongoza Mke wangu nikiwa nasikia kwa masikio yangu, kwa macho yangu. Ati alijifanya anajua nahau na misemo, methali na mafumbo akinifumbia mimi mjinga alafu mke wangu mwerevu afumbue.

Sikatai kijana yule alinishinda kwa mali, pengine na muonekano uliong'arishwa na pesa zake, mbaya zaidi alikuwa akichanganya lugha, sijui kingereza mara kireno.

Ilimradi aonekane wa maana mwenye wadhifa.

Mke wangu nilimuona akilaghaiwa na shetani moyoni, tamaa ilijaribu kumuambia, acha kuchezea nafasi, mkubalie huyo.

Mimi sikuwa najua kingereza, wala kireno wala lugha yoyote ile ya kimataifa, isipokuwa lugha Mama na lugha ya kiswahili. Nami nikachanganya kiswahili na kilugha, nikichagua maneno matamu ya vijana yaliyokuwa yanavuma kwa wakati ule ilimradi nami nionekane nimo kwa habari za ujanja wa lugha za vijana. Masikini! nilimuona mke wangu akitoa tabasamu la kunicheka, alinicheka kwa dharau. Niliumia sana. Lakini sikuonyesha maumivu yangu usoni.

Basi nikasema; Tutafika salama Mke wangu, haijalishi gari tulilopanda ni bovu, haijalishi tuvuka milima na mabonde kiasi gari, haijalishi watu watatucheka na mkweche mkweche wetu lakini lazima tufike salama.

Basi yule kijana akacheeka mpaka machozi akiwa ndani ya gari lake amefungua kioo cha dirisha la gari lake. Hapo akasema ati mimi sina hadhi ya kuwa na mwanamke mzuri kama alivyo mke wangu.

Kwa huzuni nikajikaza, nikamwambia ondoka nisije nikaleta madhara hapa, masikini kumbe nilimchimba mikwala mtu anayejiweza, akatoa bastola, akaninyooshea. Hapo hofu ikanipiga, nikahisi ule ndio ungekuwa mwisho wangu. Ajabu ni kuwa Mke wangu akaingiwa na utu, akanionea huruma, akasimama mbele yangu kusudi kama yule kijana akiachia risasi imlenge yeye. Hapo Yule kijana alipoona hivyo akatutukana wote kisha akachapa lapa.

Nikakumbatiana na Mke wangu nikitweta, nilinong'ona kwenye sikio lake tukiwa tumekumbatiana; Nitakupenda Mke wangu siku zote za maisha yangu. Ahsante kwa kunisaidia.

Nikajaribu mara ya mwisho kutengeneza gari, Mungu sio athumani gari likafaa. Safari ikaanza tena, wakati huu nikamwambia mke wangu, yeye aendeshe gari alafu mimi nitakuwa nyuma nasukuma. Mke wangu akanijibu, yeye tangu kuzaliwa hakuwahi kuendesha gari hivyo asingeweza muda ule. Nikamwambia nitamfundisha pale pale, Looh! Taikon anataka kumfundisha mwanafunzi na siku hiyo hiyo aendeshe gari.

Akakubali, nikamfundisha, kuendesha gari. Basi akaanza kupanda kale kamlima mimi nikisukuma kwa nyuma. Hapo baadhi ya wenye magari walituokuwa wakitupita na kupishana nasi walikuwa wakitushangaa, wengine wakituzomea, basi ilimradi kila mtu na akili yake.

Hatimaye, tulipanda kale kamlima, lakini wakati wa kuteremka Mke wangu hakujua namna ya kulisimamisha gari ili nipande. Gari likaserereka mimi nikilikimbiza kwa nyuma, nilichoka gari likawa limefika chini kabisa umbali wa nusu maili. Nikatembea nakulifikia, kisha nikalidandia.

Mke wangu alifurahia kuendesha gari ingawaje lilikuwa gari bovu, aliendesha bila umakini kwani hakuwa na uzoefu. Alipiga vigele gele kwa shangwe, kumbe mwanamke hufurahi akiwa sehemu ya uendeshaji wa gari lako katika safari yenu ya maisha, hapendi kuwa abiria.

Basi jioni ilikuwa imeingia tukiwa tumechanja mbuga na safari ikiwa imebaki kidogo kufika.
Nikachukua usukani, sasa nikaendesha kama mwanamume, kwa kasi kubwa na umakini wa hali ya juu. Ili niwahi kufika, mke wangu alikuwa anasinzia, hofu yake ilikuwa imepungua.

Taa za gari letu hazikuwa zinamulika vizuri, hatukuweza kuona umbali mrefu. Basi Mke wangu hofu yake ilianza tena. Hasa pale wenye magari makubwa waliokuwa wanapishana nasi wakituwashia full light, hali iliyopelekea sisi tusione njia. Walitufanyia makusudi kutumulika, huku wakitudhihaki. Lakini tulikaza moyo.

Mvua kubwa ilianza kunyesha, hali iliyopelekea barabara kujawa na matope kwani ilikuwa barabara ya vumbi. Looh! Gari yetu ilishindwa kwenda, matope yalilizuia. Hatimaye tukasalia tupo porini, baridi ikitupiga, na mbu wakitung'ata.

Basi nilitoka nje ya gari nikamwambia mke wangu mimi nitakuuwa nasukuma yeye atie gia, basi tulikazana tukakaza, nilichafuka kwa matope jamani ili gari linasuke kwenye yale matope, mvua ilininyeshea mpaka ikakatika, baada ya masaa mawili, tulifanikiwa kuliondoa lile gari kwenye matope. Mke wangu alinipa pole kwa kuhangaika kule.

Tukatia Gia na gari ikaanza tena safari. Kwa mbali tuliuona Mji, naam ndio mji tuliokuwa tunaelekea. Hapo moyo wangu ukafurahi, lakini kabla furaha yetu haijafika mbali tairi la gari la nyuma likapasuka, hiyo ilikuwa ni usiku wa saa tatu.

Safari ikaishia hapo, Nikamwambia mke wangu, tulale, alafu kesho tutabadilisha tairi.

Tukakumbatiana tukalala.

Tutafika salama, haijalishi ni vikwazo gani tunapitia, haijalishi ni mambo gani mazito tunapitia. Licha ya gari yetu kuwa bovu lakini tutafika salama.

Usimuache Mumeo au mkeo kwa sababu ya ugumu wa safari yenu ya maisha, usiache shule, au mafunzo ya kijeshi kwa sababu ya ugumu wake, jambo moja ni kuwa utafika salama.

Usiache kufanya kazi licha ya mshahara, au malipo ni kidogo, au watu wanakucheka nayo, kaa ukijua utafika salama.

Usiache kuongoza watu kama wewe ni kiongozi kwa kuogopa maneno ya wasiokupenda, neno moja kwako, utafika salama.

Na atukuzwe yule anayeipigania safari yetu. Tutafika salama kwa kuwa hatuko peke yetu.

Basi tukalala.......!

Ulikuwa nami:

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300

Hadi wakati mwingine.
 
Nikisoma kazi zako na kufananisha na Charles Dickens au William Shakespeare.....big up man
 
Similar Discussions

Back
Top Bottom