Tusilalamike tu, tutafute mwarobaini wa rushwa

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
Tusilalamike tu, tutafute mwarobaini wa rushwa




Na Mhariri





KATUNI%28176%29.jpg

Maoni ya katuni.



Kasi ya kuongezeka kwa vitendo vya rushwa nchini ni moja ya malalamiko yanayotolewa kila siku na wananchi wa kawaida, viongozi wa makundi ya kijamii na wa kisiasa.
Vitendo vya rushwa vinalalamikiwa kuwa ndicho chanzo cha kutokua kwa uchumi wa nchi yetu hivyo kuwaacha wananchi katika lindi la umaskini.
Malalamiko dhidi ya rushwa yameanza muda mrefu na muda mfupi baada ya serikali ya awamu ya tatu kuingia madarakani, Rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa, aliunda Tume ya kuchunguza na kubaini vyanzo vya rushwa, iliyoongozwa na Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Jaji Joseph Warioba.Kuundwa kwa Tume hiyo kulipongezwa na wengi wakiwemo washirika wa maendeleo wa nchi yetu.
Watanzania wengi walijiunga pamoja na washirika wa maendeleo, ambao hutoa fedha za walipa kodi wao kuchangia bajeti yetu, waliamini kuwa serikali ya awamu ya tatu ilikuwa imedhamiria kwa dhati kukomesha rushwa na kuwaletea maendeleo wananchi. Tume hiyo ilifanya kazi kubwa kwa kubainisha mianya ya rushwa. Ripoti kubwa iliyoandaliwa haikuficha kitu, kiasi kwamba ilizitaja taasisi zinazoongozwa kwa rushwa. Aidha, iliwataja baadhi ya wahusika kwa majina na wengine haikuwataja majina moja kwa moja, lakini walijulikana.
Ripoti hiyo ilionekana kuwa ingekuwa mwongozo mzuri na uliokamilika katika vita dhidi ya rushwa nchini.
Baada ya Jaji Warioba kuwasilisha ripoti yake iliyokuwa na mapendekezo lukuki, wengi walitarajia kuwa serikali ingeanza mara moja kuitekeleza kwa kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu watuhumiwa wa rushwa.
Hata hivyo, serikali haikutekeleza mapendekezo ya Tume hiyo, badala yake ikawataka wananchi kupelekea ushahidi kwa vyombo vya dola kuhusu wanaowatuhumu kwa vitendo vya rushwa.
Malalamiko kuhusu kasi ya vitendo vya rushwa na ufisadi yameendelea hususan baaada ya kuibuliwa kwa kashfa kadhaa zikiwemo za EPA, Richmond, Meremeta, Tangold, Deep Green na nyingine zilizosababisha kupotea kwa mabilioni ya fedha za walipakodi nchini. Tusingependa kutaja malalamiko yote yanayotolewa na jamii kuhusu rushwa, lakini kwa ujumla kila inapotokea mikusanyiko ya makundi ya jamii, malalamiko dhidi ya rushwa ni jambo linalotawala mazungumzo iwe katika semina, makongamano, mikutano na warsha.
Kwa kutaja machache, juzi wakati wa kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) jijini Dar es Salaam, washiriki wengi walionyesha wasiwasi wao kuhusu kasi ya rushwa nchini.
Akifungua kongamano hilo, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alisema vitendo vya rushwa vinaongezeka kwa kasi kubwa na kwamba imefika hatua ambapo watu wanaopata utajiri kwa njia za rushwa wanaheshimika na kuonekana kama mashujaa katika jamii. Sitta aliishauri serikali ijielekeze kwenye kutibu chanzo cha rushwa badala ya kusubiri kuwakamata wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Alisema inasikitisha kuona baadhi ya watu wametajirika kwa kula rushwa na sasa wanaonekana mashujaa kwenye jamii. Alisema kuna umuhimu wa kubuni mikakati shirikishi na endelevu ya kukabiliana na adui rushwa ambayo hudhoofisha maendeleo.
Alisema kukithiri kwa rushwa kumesababisha hata zile nchi zilizojaliwa utajiri na rasilimali nyingi kuendelea kuwa maskini na hatimaye kukumbwa na machafuko.Alisema hali hiyo inatokana na ukweli kuwa rasilimali huwanufaisha wachache katika jamii na kuwaacha wengi katika minyororo ya umaskini.
Washiriki wengine walibainisha kuwa kukosekana kwa uwazi ni sababu kubwa inayochangia rushwa. Kwa mfano, Balozi wa Sweden nchini, Staffan Herrstrom, alisema rushwa inasambaa zaidi panapokuwa na mazingira ya usiri na kuwanyima wananchi taarifa.
Suala la kukosekana uwazi pia lilizungumziwa na Mbunge wa Kibaha, Dk. Zainabu Gama (CCM), ambaye alisema rushwa inaenea kwa kasi kutokana na mambo mengi ya serikali kufanywa kwa siri likiwemo suala la mikataba. Tunakubaliana na hoja zilizotolewa katika kongamano la juzi, lakini tunawashauri Watanzania kuwa kulalamika sio suluhisho dhidi ya rushwa, bali njia inayofaa ni kupendekeza njia za kukabiliana nayo.
Baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa tunaamini kuwa yatasaidia katika kupata mwarobaini wa tatizo la rushwa nchini. Jambo la msingi ni serikali kupokea na kuyafanyia kazi mapendekezo yanayotolewa na wananchi ya kupambana na rushwa.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom