Tuogope kuogopa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tuogope kuogopa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by baraka moze, Jun 6, 2012.

 1. b

  baraka moze Member

  #1
  Jun 6, 2012
  Joined: Apr 21, 2012
  Messages: 99
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 13
  WATANZANIA walio wengi, na hasa waliopo nje ya mfumo wa utawala wa CCM, wanaelekea kuwa na mwafaka kwamba mambo hayaendi ilivyo katika nchi yetu kwa sasa. Kwamba tulipo sipo tulipopaswa kuwa.

  Pengine kibaya zaidi ni kwamba haielekei kama tunakwenda ama tumesimama na kama tunakwenda haielekei kama tunakwenda tulipotaka kwenda. Kwa kifupi ni kwamba inaonekana tumepanda basi liendako tusikokwenda, na kwa hivyo haiwezekani tukafika tunapotaka kwenda.

  Mwafaka huu unathibitishwa na mambo mengi. Itoshe kutaja mawili kwa leo. Mosi, mazungumzo yasiyo rasmi katika sehemu mbalimbali, kama vile kwenye migahawa, vilabu vya pombe, kwenye taksi, maofisini na kwenye mabasi ya abiria, yamekuwa yakitawaliwa na kusutwa kwa Serikali ya CCM kwa sababu sio tu ya kushindwa kuleta ‘neema' iliyoahidi katika nyakati tofauti, lakini pia kwa kuharibu mambo ya msingi tuliyoyajenga kwa miaka kadhaa baada ya uhuru.

  Pili, ni kuungwa mkono kwa chama kikuu cha upinzani (CHADEMA) kwa kiwango ambacho, kwa vigezo vyovyote vile, hakijapata kuonekana katika historia ya mfumo wa vyama vingi hapa nchini.

  Hata hivyo bado kuna woga wa aina fulani unaotatiza baadhi ya Watanzania, hasa rika fulani, kusita kuunga mkono harakati za mabadiliko kwa kiwango cha kutosha. Ukichunguza kwa makini utagundua kwamba Watanzania hawa hakuna wanachokiogopa bali wanaogopa woga wenyewe! Watu wa aina hii wapo katika makundi makuu matano, ambayo nitajaribu kuyafafanua katika makala hii.

  Kundi la kwanza linajumuisha watu ambao wanaogopa kuunga mkono harakati za mabadiliko kwa kutokuamini kwamba matatizo yaliyopo yamesababishwa na utawala wa Chama cha Mapinduzi. Wanaamini kwamba Watanzania wote kwa umoja wetu tumesababisha matatizo tuliyo nayo na kwa hivyo si sahihi kukibebesha chama hiki lawama.

  Hata hivyo mantiki ya kutatua tatizo inatuelekeza kwamba ili uweze kulitatua tatizo hilo ni muhimu kulitambua tatizo lenyewe na chanzo chake. Katika kutambua chanzo huwezi kukwepa kutafuta mtu aliyesababisha tatizo hili. Ukishagundua tatizo na aliyelisababisha yakupasa kushughulikia vyote, tatizo lenyewe na yule aliyelisababisha. Kwa hivyo hatuwezi kuyashughulikia matatizo yanayotukabili bila kumshughulikia aliyeyasababisha.

  Kundi la pili linajumuisha Watanzania ambao wanakiri kwamba utawala uliopo umeshindwa, lakini je, hawa wengine wataweza? Kundi hili nalo wanaogopa woga na wanajaribu kutuaminisha kwamba kwa kuwa wale wengine hatuwajui tuendelee nao hawa (CCM) kwa kuwa zimwi likujualo halikuli likakwisha. Hakuna ambacho kundi hili wanakiogopa zaidi ya woga wenyewe, kwa sababu hao wengine hatuwezi kuwapima kwa sababu hatujawahi kuwapa fursa ya kutawala na kwa hivyo hatuna haki ya kuwahukumu. Jambo tulilo na uhakika nalo ni ukweli kwamba hawa waliopo wameshindwa, na kama wameshindwa wanapaswa kukaa pembeni.

  Kundi la tatu ni wale wanaokiri kwamba utawala huu uliopo ndio uliotufikisha hapa tulipo, lakini wanaamini kwamba ni utawala huu huu ambao wanaweza kuyatatua matatizo waliyoyasababisha. Kundi hili ni kikwazo zaidi katika harakati za mabadiliko kwa sababu linawaaminisha watu kwamba akili zilizosababisha tatizo ndio hizo zitumike kutatua tatizo hilo. Kundi hili pia linajumuisha watu ambao wanaamini kwamba tatizo la nchi yetu ni baadhi ya watu waliopo katika chama tawala na sio la kimfumo.

  Ni kundi la watu wanaoamini kwamba CCM haina matatizo, lakini watu wachache waliopo katika chama hiki. Ndio hawa ambao hushangilia pale ambapo Rais Kikwete huvunja baraza lake la mawaziri na kuwatoa baadhi ya watu na kuwaweka wengine. Lakini ukweli ni kwamba unapoingiza watu wapya katika mfumo ulioshindwa kuna uwezekano wa jambo moja kutokea kati ya mawili. Ama watu hao wapya wataweza kuubadilisha mfumo au mfumo utawabadilisha wao. Katika miaka 35 ya Chama cha Mapinduzi uzoefu umeonyesha kuwa kinachofanikiwa ni mfumo kuwabadilisha hao wapya walioingizwa katika mfumo ulioshindwa na wao kujikuta wameloweshwa matatizo ya utawala waliodhamiria kuubadilisha.

  Kundi la nne wamo watu wanaoshangaa na kuwatisha watu ambao wamefanikiwa kuushinda woga na kuamua kwa dhati kuwa sehemu ya mchakato wa mabadiliko. Watishaji hawa kimsingi hawajatumwa na mtu yeyote kutisha lakini wanaogopa tu woga usio na msingi wowote.

  Hawa ndio wanaowatisha wafanyabiashara walioamua kuunga mkono upinzani kwa kuwashangaa kwamba hawaogopi kukamatwa na TRA, au wafanyakazi katika sekta ya umma kwa kuwatishia kupoteza kazi zao. Kimsingi hawa nao wanaogopa woga kwani kuogopa kwao hakujajengwa katika msingi wowote lakini wanachangia sana kutatiza juhudi za kuleta mabadiliko yanayohitajika.
  Kundi la tano la watu wanaoogopa woga lipo ndani ya vyama vya upinzani. Hili ni kundi la watu ambao linawabatiza wanachama wenzao wa upinzani kwamba ni mamluki na wametumwa na CCM kuvuruga upinzani.

  Kwa hiyo mwanachama yeyote anayezungumza au kutenda kinyume cha mawazo ya wengi katika chama chake huonekana ni mamluki na kwamba ametumwa na CCM. Kundi hili nalo linatatiza harakati za mabadiliko kwa sababu linawafanya wanachama na viongozi wa upinzani waogope kukosea. Ukweli wa mambo ni kwamba bila kuwa na ujasiri wa kufanya makosa huwezi kufanya jambo lolote la maana. Ukiogopa kukosea utakuwa makini mno na matokeo yake hutaweza kujaribu kufanya chochote cha maana ili uweze kujifunza.

  Hivyo basi napenda kushauri mambo mawili ambayo nafikiri ni ya msingi katika harakati za mabadiliko hapa nchini. Mosi, matatizo yetu ni ya kimfumo na hayawezi kutatuliwa kwa kuwabadilisha watu katika nafasi za uongozi. Kwa maneno mengine ni kwamba ufisadi tunaolalamikia ni sehemu ya mfumo wa utawala uliopo na hatuwezi kuuangamiza bila kwanza kuuangamiza mfumo wa utawala.

  Matatizo ya nchi yetu yamefikia kiwango ambacho iliwahi kutokea Marekani kati ya mwaka 1929 na 1932. Katika miaka hiyo, taifa la Amerika lilikumbwa na matatizo makubwa ya kiuchumi kiasi cha Soko la Hisa la New York kufungwa. Benki, viwanda na maduka vyote vilifungwa, na kusababisha mamilioni ya Waamerika kupoteza kazi. Waamerika wote wakakubaliana kwamba moja ya chanzo cha matatizo yao ilikuwa ni utawala mbovu wa Serikali ya Republicans ambayo ilitawala kwa muda merfu, na wakaapa kuiangusha.
  Ilipofika kwenye uchaguzi wa mwaka 1932 Waamerika walikichagua chama cha Democrat kwa kishindo ambapo kilishinda katika majimbo 42 kati ya 50 na Rais Franklin D. Roosevelt (1882-1945) kuchaguliwa.

  Mara alipochaguliwa aliwataka Waamerika wasiogope chochote katika kujikwamua na matatizo ya kiuchumi isipokuwa waogope woga wenyewe!!

  Nchi yetu ilipofikia ni zaidi ya pale walipokuwa Waamerika mwaka 1932. Nasi vile vile katika kufikiria namna ya kujikwamua tulipokwama yatupasa tuushinde woga. Ni lazima tuunganishe nguvu zetu katika kuhakikisha kuwa tunabadilisha mfumo wa utawala kama hatua mojawapo katika kuyakabili matatizo yanayotukumba.

  Pili, inafaa kuwaasa wanachama na viongozi wa upinzani. Kwamba wanachama na viongozi wa CHADEMA, kwa mfano, sio malaika, ni Watanzania hawa hawa. Kwa hivyo watafanya makosa.

  Wanapofanya makosa si lazima wawe wametumwa na CCM. Wanaweza kufanya makosa kwa sababu tu ya upeo wa uelewa wao na wengine kwa ujinga wao na ni katika jitihada za kujifunza.

  Inapotokea wanalaaniwa kwamba wametumwa au ni mamluki wa CCM inawakatisha tamaa na wataogopa kujaribu. Hakuna hatari kama watu wakianza kuogopa kufanya makosa kwa sababu ndio itakuwa mwisho wa kufikiri.

  Kwa hiyo, wanachama na viongozi wa upinzani wanapokosea waaswe, waonywe na kurekebishwa kama ambao wamekosea kwa sababu mbalimbali. Kama hatuna ushahidi wa maana kwamba wametumwa na CCM hakuna sababu ya kuwapa majina ambayo yanawatenga na wanaharakati wenzao wa mageuzi.


  source:
  Kitila Mkumbo
   
Loading...