Tundu Lissu: Richmond ni ya Rais Kikwete

RUCCI

JF-Expert Member
Oct 6, 2011
1,701
1,714
Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu akihutubia Leo Mkutano wa kumnadi Edward Lowassa mgombea Urais wa CHADEMA (UKAWA) amesema Richmond ni ya Rais Jakaya Kikwete.

Aidha, amesema richmond sio ya mtu anayeongozana nae kwenye kampeni.

Magazeti leo yalimkariri Rais Kikwete alipokuwa Kigoma akisema mhusika wa Richmond ni yule anayeongozana na Lissu kwenye Kampeni.

TAZAMA VIDEO



Katika video hiyo,Tundu Lissu anasikika akisema maneno yafuatayo;

"Ndugu zangu wa Morogoro, Richmond ni ya Kikwete.. Richmond ni ya Kikwete narudia.. Richmond sio ya huyu anayetembea na Lissu kwenye kampeni, Richmond ni ya Kikwete. Sasa nimesema nataka nimnyamazishe. Sasa nipeni masikio yenu....".

======================

Morogoro/Dar. Siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kumtaka Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amtaje mhusika wa Richmond anayezunguka naye kwenye kampeni, Mbunge huyo wa Singida Mashariki ameibuka na kudai kuwa Rais huyo ndiye mhusika kwa kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kuteua na kuwawajibisha mawaziri.

Juzi, akiwa Kigoma, Rais Kikwete alieleza kumshangaa Lissu kumtaka amtaje mhusika wa Richmond wakati mtu huyo anazunguka naye kwenye mikutano ya kampeni na kumtaka amtaje la sivyo yeye (Rais), atamtaja.

Akihutubia mkutano wa kumnadi mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa, mwanasheria hiyo alianza kwa kusema: “Sasa ndugu zangu naomba leo nimjibu Kikwete na tumalizane na hii habari ya Richmond.

Alisema mkuu huyo wa nchi ndiye mhusika kutokana na mamlaka yake na; “si ya huyu Lowassa anayedai natembea naye kwenye kampeni. Hapa kwenye mkono wangu nina taarifa ya mwaka 2008 ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Richmond, Dk Harrison Mwakyembe, sasa ni miaka zaidi ya saba tangu isomwe bungeni.”

Lissu aliyekuwa akishangiliwa na umati wa watu waliohudhuria mkutano huo katika viwanja vya shule ya kiwanja cha ndege, alinukuu maelezo ya taarifa ya Mwakyembe kifungu kwa kifungu na kueleza namna ambavyo taarifa hiyo haikuweza kumtia hatiani Lowasa, bali aliwajibika kutokana na makosa ya watendaji wake.

Baada ya kueleza kwa kina taarifa hiyo, Mwanasheria huyo alisema Rais Kikwete ndiye pekee mwenye mamlaka ya kuwateua mawaziri, akisema alimteua Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha na ndiye mwenye mamlaka ya kuwawajibisha. Karamagi na Dk Msabaha walikuwa wameshika uwaziri wa Nishati na Madini kwa nyakati tofauti wakati wa sakata la Richmond na walijiuzulu pamoja Lowassa.

“Waziri mkuu Lowassa baada ya kutokea kwa sakata hilo alimwendea Rais Kikwete na kumweleza kuwa ‘kimenuka’ tuvunje mkataba baada ya wabunge wa upinzani kuchachamaa kuhusu sakata hilo, lakini alikataa na kumweleza kuwa hizo kelele za wapinzani zitaisha tu,” alisema.

Alisema baada ya Lowassa kujiuzulu mwaka 2008, tayari mashine za kutengeneza umeme zilishafika nchini na baada ya kujiuzulu haikufahamika zilikokwenda na kwamba baadaye mkataba wa Richmond ukahamishiwa kwa kampuni ya Dowans ambayo iliendelea kulipwa mabilioni ya shilingi.

Alimtaka Rais Kiwete awaambie Watanzania kwa nini Serikali yake iliendelea kuilipa Dowans mabilioni ambayo ilikuwa ya mfukoni na kwamba kama Lowassa alifanya makosa kwa nini hajapelekwa mahakamani kwa miaka minane tangu ajiuzulu.

“Rais Kikwete asitake kumaliza hizi siku chache za kampeni zilizobaki kwa shari na mimi na naomba niwaambie, Lowassa amefanya kazi katika umri wake wote wa miaka 62 ndani ya CCM na Serikali yake, lakini ameamua kuhamia huku kwa ajili ya kuleta mabadiliko na kuacha marupurupu yake yote,” alisema Lissu.

Lowassa apotezea

Aliposimama kuhutubia mkutano huo, Lowassa hakugusia kabisa suala hilo la Richmond na badala yake akaahidi iwapo atachaguliwa, serikali yake itafanya kila linalowezekana kuanzisha benki maalumu ya maendeleo kwaa ajili ya mama na baba lishe, vijana wa bodaboda na wamachinga ambao alisema watakuwa ni marafiki wakubwa wa serikali yake.

Alieleza kufurahishwa na umati huo akisema umemkumbusha siku alipowasili mkoani hapa kutafuta wadhamini, kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo kwa tiketi ya CCM.

Waziri mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye aliwataka wananchi kutobabaishwa na vitisho vinavyotolewa na viongozi wa CCM kuwa upinzani ukiingia Ikulu kutakuwa na machafuko.

Alisema serikali ya Ukawa ikiingia madarakani itahakikisha inasimamia mambo iliyoyaainisha kwenye ilani ya uchaguzi, tofauti na serikali ya CCM ambayo mbali na kuahidi maisha bora na kukusanya kodi za wananchi, bado hali imeendelea kuwa mbaya siku hadi siku.

Mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema Morogoro Mjini, Albanie Marcos aliahidi kusimamia viwanda mjini hapa vikiwamo vilivyobadilishwa matumizi, kurudi kuwa chini ya wananchi.

Kauli za wadau

Wakizungumzia kauli ya Rais Kikwete kuhusu Richmond, baadhi ya wasomi na wadau wa siasa nchini walisema hayo ni malumbano ya kisiasa.

Profesa Michael Ndashau wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema kauli za kulumbana kuhusu sakata la Richmond ni kufurahisha genge, kwa sababu kila siku maneno ni hayohayo.

Alimtaka Lissu kuweka bayana uthibitisho wa uhusika wa Rais mbele ya jamii ili wananchi wapate la kuamini.

“Lissu kasema, Kikwete kajibu, malumbano yanabaki palepale, mwenye nafasi nzuri ya kusema tena ambaye yupo upinzani ni Lissu, aeleze kwa ushahidi ili ambane mhusika maana bila uthibitisho yatakuwa yaleyale kulumbana bila kufikia mwisho.

Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema wote wawili wanaufahamu ukweli. Alisema hizo ni hadaa lakini hakuna kati yao asiyemfahamu mtuhumiwa wa Richmond, “Rais ametoa uhuru kwa Lissu amtaje, hivyo kama anamfahamu afanye hivyo, lakini anafahamika na siyo Baregu, Slaa wala Mbowe, wote wanamfahamu,” alisema Dk Bana.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alisema hilo siyo suala la Rais kumuagiza Lissu, bali alitakiwa afanye mwenyewe kwa sababu anayo haki ya kufanya hivyo.

“Rais kupitia vyombo husika ndiyo anatakiwa atoe amri mhusika achukuliwe hatua kama anamfahamu, ana kila sababu ya kufanya hivyo, kama alikaa kimya wakati huo, wakati huu haitasaidia?” alisema Bisimba.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema kujadili suala hilo sasa ni kuwanyima wananchi uhuru wa kujadili mambo ya msingi yenye tija kwa Taifa.

Chanzo: Mwananchi
 
Last edited by a moderator:
Sijui kuna Nini ????
 

Attachments

  • 1442337390988.jpg
    1442337390988.jpg
    36.6 KB · Views: 5,583

Similar Discussions

Back
Top Bottom