TUNDU LISSU: Kuporwa kwa mafao ya Wafanyakazi ni dhambi ya Bunge au tunalishwa matango pori?

Wakubwa zangu salaam. Mimi ni Mbunge na kwa hiyo ninaweza kusemwa nina maslahi katika mjadala huu. Ninayo kweli.

Kwa vile 'mmetupiga' sana kwenye suala hili, ninaamini hamtajali sana nikijitetea mwenyewe, na kuwatetea wenzangu, hata kama hawajanituma.

Kuna hatari kubwa ya kutumia suala la mafao ya wafanyakazi kuwachonganisha Wabunge kwa wananchi, ili watu wenye agenda za kuua Bunge letu kama taasisi watimize matakwa yao. Naomba kufafanua.

Ni kweli kwamba utaratibu huu wa mafao hauwahusu Wabunge. Lakini sio Wabunge peke yao. Utaratibu huu hauwahusu pia Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote. Vile vile hauwahusu Mawaziri na Naibu Mawaziri wote, Rais na Makamu wa Rais.

Hawa wote sio 'wafanyakazi' kwa maana ya kisheria ya neno hilo. Ni watumishi wa kisiasa na mishahara na marupurupu yao yapo kwenye kundi la utumishi wa umma wa kisiasa.

Na sio wanasiasa tu ambao sio 'wafanyakazi.' Makamishna wa Tume mbali mbali zilizoanzishwa kwa mujibu wa Katiba au sheria mahsusi, na wajumbe wa Bodi mbali mbali za taasisi na mashirika ya umma nao sio 'wafanyakazi', na kwa hiyo hawahusiki na utaratibu huu wa mafao ya wafanyakazi.

Wote niliowataja hawalipwi pensheni wanapomaliza muda wao wa utumishi. Hulipwa kitu kinaitwa 'gratuity' (mtanisaidia Kiswahili chake), yaani malipo ya mkupuo mmoja wanapomaliza utumishi.

Viwango vya gratuity hiyo vinatofautiana kulingana na cheo cha mhusika. Kwa Wabunge mnaotusema sana ni 40% ya mishahara yote ya miaka mitano. Hicho pia ni kiwango cha Wakuu wa Wilaya ambao hamjawagusa kabisa kwenye mjadala huu.

Kwa Wakuu wa Mikoa na Naibu Mawaziri, gratuity yao ni 50% ya mishahara yote ya muda wao utumishi. Hawa pia hakuna anayewasema.

Kwa Mawaziri (na kama sikosei Naibu Spika) kiwango cha gratuity yao ni 60% ya mishahara yote ya muda wao wa utumishi. Hapa pia sijasikia malalamiko wala hasira yoyote.

Kwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Spika, hawa utaratibu wao ni mnono zaidi. Kwa mujibu wa Sheria ya Mafao ya Viongozi wa Kisiasa ya mwaka '99, Rais anayemaliza muda wake anatakiwa kulipwa 80% ya mishahara yote ya Urais wake; mshahara wake wote wa miaka miwili kwa ajili ya maandalizi ya kustaafu; na baada ya hapo ataendelea kulipwa 80% ya mshahara wa Rais aliyeko madarakani hadi atakapofariki dunia.

Mafao haya ni nje ya mafao mengine kama nyumba yenye furniture zote, magari, ofisi, walinzi na watumishi kadhaa wa ndani na wa ofisi. Sijaona wala kusikia mtu yeyote akimnyooshea kidole mtetezi wa wanyonge aliyeko Magogoni kwa sasa, wala kuhoji uzalendo au uadilifu wake.

Kwa Makamu wa Rais kiwango ni hicho hicho cha 80% ya mishahara yote na baada ya hapo pensheni ya kila mwezi ya 80% ya mshahara wa Makamu wa Rais aliyeko madarakani hadi kifo. Na hii pia ni nje ya nyumba, furnishings, gari, walinzi, watumishi, etc.

Kwa Waziri Mkuu na Spika ni 70% kwa utaratibu huo huo.

Ukiachia Wabunge, hakuna yeyote ambaye amewalalamikia wote hawa, pamoja na ukweli kwamba mafao yao ni makubwa kuliko ya Wabunge.

'Ignorance is bliss', Waingereza wanasema. Ujinga ni amani. Watu wetu wengi ni wajinga, hawaelewi nchi hii inavyoendeshwa. Kwa hiyo ni warahisi sana kuaminishwa kwamba Wabunge wao ndio wabaya, wasaliti, etc.

Wakishaamini kwamba Wabunge ndio tatizo, itakuwa rahisi zaidi kujenga hoja za kulidhoofisha Bunge letu zaidi ya lilivyo sasa. Tayari Serikali ya Magufuli imefanya na inaendelea kufanya mambo mengi yenye kulidhoofisha Bunge letu.

Je, nitahojiwa, Wabunge si ndio waliopitisha sheria hii ya kuwanyonga wafanyakazi na kujipendelea wao na wakubwa wenzao???

Jibu la haraka haraka ni ndio, sheria hiyo, na hizo nyingine zimepitishwa na Bunge.

Lakini suala la msingi ni je, kwa Katiba yetu ya sasa na Sheria zake, na kwa historia yetu ya kisiasa na ya kibunge ya tangu Uhuru, Wabunge hawa walikuwa na uwezo wa kukataa kupitisha sheria hizi???

Angalau tangu Katiba ya Jamhuri ya mwaka '62, Bunge la Tanganyika, na baadae Tanzania, limeendeshwa, kwa kiasi kikubwa, na Ikulu.

Bunge la mpaka mwaka '85 liliendeshwa na Ikulu ya Mwalimu Nyerere; la mpaka mwaka '95 liliendeshwa na Ikulu ya Mzee Mwinyi; la mpaka mwaka '05 lilikuwa kwenye mabawa ya Ikulu ya Ben Mkapa; la hadi mwaka '15 lilikuwa chini ya kivuli cha Ikulu ya Jakaya Kikwete, na Bunge la sasa liko chini ya udhibiti mkubwa wa Ikulu ya Magufuli. Huu ndio ukweli mchungu wa historia ya nchi yetu.

Kwa miaka yote hii, kwa sababu ya kivuli kirefu cha Urais wa Kifalme, Bunge letu limekuwa dhaifu sana. Bunge la aina hii, haliwezi - na halijawahi - kukataa Muswada unaopelekwa Bungeni na Ikulu. The very few, if any, exceptions only prove the general principle of our history.

Kwa hiyo, kuwalaumu Wabunge hawa kwa kupitisha sheria hii ya mafao ya wafanyakazi is simply to miss the point. Bunge la kondoo la miaka yote hii haliwezi kubadilika ghafla na kuwa Bunge la simba!!!

Nataka niwe wazi. Hapa ninazungumzia Bunge la wanaCCM. Sisi wapinzani tumekuwa wachache miaka yote hii tokea mwaka '95. Tumekuwa tunapinga mambo haya lakini, kwa sababu ya uchache wetu, 'tumefyekelewa mbali' na wale wanaosema: "Wanafiki waseme NDIYO!!!"

Na wanafiki wamesema 'NDIYO' kwa kila kitu walicholetewa na Ikulu ya Mwenyekiti wao wa Chama. Kwa hiyo, Sheria hii ya mafao ya wafanyakazi ni Sheria ya mpangaji wa sasa wa Ikulu pamoja na Wabunge wa Chama chao. Hili ni la kwanza.

La pili, na la mwisho kwa leo, linahusu sababu halisi ya mabadiliko haya ya sheria za mafao ya wafanyakazi.

Sababu halisi sio uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi wanaostaafu kama tunavyoambiwa na Mifuko yenyewe, au wakubwa wa Serikali hii. Hayo ni 'matango pori' wanayolishwa the blissfully ignorant.

Sababu halisi ni kwamba watawala wa CCM wameua mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kutapanya pesa za wafanyakazi kwenye miradi isiyokuwa na tija kwa wafanyakazi.

Pesa za wafanyakazi zimetumika kujenga 'White Elephants' kama majengo mengi na makubwa yaliyopo Dar Es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na kwingineko.

Kwa kiasi kikubwa, na kwa sababu mbali mbali, majengo haya hayapangishiki. Hivyo, licha ya kugharimu matrilioni ya shilingi, fedha za wafanyakazi hazitarudi.

Mifuko ya hifadhi ya jamii ndiyo iliyojenga UDOM; na tangu mwaka '09 CAG amelalamika kwamba Serikali imeshindwa kurudisha fedha hizo za wafanyakazi kwa sababu ama hakukuwa na mikataba au mikataba yenyewe haieleweki.

Pesa za wafanyakazi ndizo zilizojenga Ofisi ya Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi karibu na St. Peter's, Dar Es Salaam; nyumba za polisi Kurasini Dar; Machinga Complex Dar; Daraja la Kigamboni Dar, n.k.

Pesa za wafanyakazi zimetumika sana kuhonga baadhi ya Mawaziri na Wabunge kwa kuwapa miradi inayoitwa ya maendeleo, kama vile kununua mipira na jezi za michezo kwa timu za vijana kwa majimbo ya Wabunge na Mawaziri hao.

Waliofaidika na 'ukarimu' huu ni pamoja na Rais Magufuli mwenyewe, akiwa Waziri na Mbunge wa Chato. Hili nililizungumzia hata Bungeni takriban miaka minne iliyopita.

Lengo la hongo hizi ni kuwanyamazisha ili watu 'wapige' pesa za wafanyakazi. Ndio maana wala sio ajabu kwamba waliokamatwa na kushtakiwa kwa 'kupiga' pesa za mifuko ya hifadhi ya jamii sio akina Ramadhani Dau au Sanga wa iliyokuwa NSSF na LAPF, au akina AG Masaju na Naibu Spika Tulia Ackson waliokuwa Wadhamini wa Mifuko hiyo, bali ni wakurugenzi na mameneja wa kati wa Mifuko.

Wakurugenzi Wakuu na Wadhamini wa Mifuko, waliofanya maamuzi ya utapanyaji huu wa fedha za wafanyakazi, wamepandishwa vyeo na kuwa mabalozi au wabunge wa kuteuliwa na Rais au Majaji wa kuteuliwa na Rais pia.

Baada ya kuifilisi mifuko ndio watawala wakaanzisha hizi hoja za mara kuiunganisha, mara kubadili mfumo wa mafao, etc.

Suala muhimu lisilozungumzwa ni je, mifuko hii ina fedha za kulipa wafanyakazi wanaostaafu au kuacha kazi kwa sababu mbali mbali??? Pesa 'zilizokopwa' kujengea miradi hii na mingine mingi zimerudishwa lini?

Naomba kumalizia. Kutupiga Wabunge ni sawa sawa. Bunge lina sehemu yake ya lawama kwenye hili. Lakini ni Bunge peke yake??? Kwa utaratibu halisi wa utungaji sheria wa nchi yetu chini ya Katiba ya sasa, Bunge ndio lenye mamlaka haya yanayosemwa??? Mjadala na uendelee.

Tundu AM Lissu (MB)
Tienen, Belgium
Novemba 23, 2018

hahahahahaahahaaaaaaaaaaaa......

wamevuliwa nguo kina Dr. Dau!

how do they sleep at night hawa akina Dr. Dau?

wanapokuwa exposed kwamba walifuja, baka na kunajisi nchi iliyowapa elimu, neema, ma vyeo, mafao, mapensheni, ma heshima, ma kila kitu... na bado wakai run recklessly, wakaipiga kama majambazi, wanalalaje usiku??

na huyu Nyerere nae aliye design bunge dhaifu namna hii ili atawale peke yake, kwa nchi zilizoendelea sidhani kama angeitwa baba wa Taifa, kwa sababu kila legacy aliyoacha ndio kama hizi zinatumaliza, bunge dhaifu, rais mfalme, political police, jeshi kandamizi, li muungano uchwara lililotukosesha katiba mpya... you name it
 
ukisikia kauli za maafisa waaandaamizi wa majeshi wanavyoongea kuhusu awamu hasa baada ya sharia mpya ya mafao basi unajua dhahiri muda wowote hii nchi itavurugika..majeshi yetu yamevurugwa na hawana hamu tena na awamu hii
 
Uzuri wa huu mswada Hata ukiuunga mkono Leo bado kizazi chako, ndugu zako na jamaa zako watakuja kutuulaani siku za usoni.

Ndio maana wengi wetu Hata tuonaotetea Serikali kila siku hoja hii imetuhusu. Na kwakuwa tunaishi Kwa kutegemea mishahara na posho basi huu mswada ndio kiama chetu. Tukishastaafu tutakufa mapema mno kwasababu Hata gari na nyumba uliyepanga kujenga baada ya kustaafu hutaweza tena.

Anzeni kufanya kazi mbadala sasa maana yajayo yanahatarisha.
 
Bunge ni muhimili wenye mamlaka yaliyoclear sana kwenye katiba sema haliyatumii kwa sababu ya kujaa wabunge vihiyo na wahuni
Hakuna mamlaka kwa bunge, linalopitisha matakwa ya mtu, kwa ajili ya kukandamiza wenye mawazo tofauti na yeye. eg
Bunge limeperekwa gizani kwa takwa la mtu. Na bunge lilipojaribu kuchachamaa nini kilitokea ?! Aliwaita wabunge wa chama na kuwakoromea Dodoma. Je wabunge na bunge walifanya nini ?! KIMYAAA. Na wengine wakaanza kumuunga mkono kwamba wanabana za airtime . Really ?! Lengo ni wananchi wasione mawazo mbadala na kinzani.
 
ukisikia kauli za maafisa waaandaamizi wa majeshi wanavyoongea kuhusu awamu hasa baada ya sharia mpya ya mafao basi unajua dhahiri muda wowote hii nchi itavurugika..majeshi yetu yamevurugwa na hawana hamu tena na awamu hii
Na wao inawahusu?
 
Mhe. Lissu!
Nakusalim!
Nashukuru kwa ufafanuzi wako mrefu lakini ni fasaha kuhusu ulivyowatetea wabunge kwa ujumla.
Kwa upande wangu nikutaarifu kwamba sijawahi kulaani wabunge wote bali siku zote nalaumu 'Bunge la CCM'.
Hata hivyo ukubaliane nami kuwa leo ni mara ya kwanza kusikia mbunge akizungumzia sheria za pensheni Tanzania. Ingawa hukuzitaja sheria zenyewe.
Ili watu wasome na kuelewa zaidi ulichosema ninazitaja hapa:
1. Act No. 2 of 1999 (Public Service Retirement Benefits Act)
2. Act No. 3 of 1999 (Political Service Retirement Benefits Act)
Nalazimika kunukuu Katiba ya JMT 1977 ibara ya 9. hasa kifungu cha (j); Ibara ya 12. na ya 13. Kwasababu sheria mbili za pension nilizotaja hapo juu zinakiuka Katiba kwa mujibu wa Ibara hizo.
Kwakuwa miaka yote hatujasikia wabunge wa CCM au UKAWA kusema lolote bungeni kuhusu sheria hizi mbili za mafao ya uzeeni ambazo ndio chanzo cha ukiukwaji wa haki za wafanyakazi katika suala la pensheni, upande wenu upinzani hamuwezi kukwepa lawama.
Kwa misingi ya 'nitasema ukweli daima' mlipaswa kuziona kasoro hizi na kuzipinga!
Umesema 'ignorance is bliss' sawa, kama kweli hamkujua hizi sheria angalao mngesikia kilio cha wastaafu wa EAC cha miaka mingi sasa. Sijasikia mkiwasemea wazee hawa popote! Kwanini wasiwaone kama wasaliti sawa na wenzenu wa CCM?
Mwisho, nakubali uchache wenu upinzani hamuwezi kubadili au kufuta sheria nilizotaja. Lakini kunyamazia ni kama mnakuwa accomplices!
Tatizo hufuatiliagi hata bunge unaishia kuangalia clips za mitandaoni. Pitia hata Hansard ujionee kelele za wapinzani kuhusu stahiki za wafanyakazi. Msome marehemu Bilago, huyu huyu Lissu, wasome hata akina Slaa mwaka 2010 pengine utapata picha walivyolisemea jambo hiki. Msome Zitto Kabwe. Usiishie kutaja tuu sheria na kutupa lundo lako la lawama kwa "wabunge wote"
 
Swali ni kwamba kuna marais wastaafu watatu ambao wamekuwa wanalipwa pensheni zao kwa 80% ya mshahara wa Rais wa sasa kabla hajajipunguzia, kwahiyo pensheni za marais wastaafu zitapunguzwa pia? Kama ndio, kwa sheria ipi? Kwasababu sheria Na. 3 ya 1999 inasema hakuna mamlaka au chombo chochote kinachoweza kupunguza mafao ya Rais mstaafu.
Very good question. Hata huyu kusema kupunguza mshahara wake ni siasa za kijinga tuu. Hajapunguza hata senti.
 
Hoja ya Lissu ni kama analipaka mafuta bunge kwa kushindwa kutimiza wajibu wake kwa wananchi dhidi ya sheria hizi mbovu zinazotungwa na bunge ( siyo sheria ya mafao tu).

Hoja kwamba Bunge halina mamlaka au linaendeshwa kwa remote control ni hoja dhaifu kwa sababu kadhaa.

1 bunge linafanya kazi kwa mujibu wa katiba na siyo kwa mujibu wa matakwa ya rais

2 bunge ndiyo lenye mamlaka ya kutunga sheria hivyo linanafasi kubwa zaidi ya kuwalinda wananchi kupitia sheria linazotunga.

3 Bunge lina mamlaka ya kuisimamia serikali mojawapo ni kwenye hizi sheria serikali inazozipeleka bungeni

4 Bunge halishurutishwi kupitisha kila sheria inayopelekwa bungeni na serikali.

5 Bunge linamamlaka ya kuiwajibisha serikali kwa kupiga vote of no confidence kwa waziri Mkuu au impeachment kwa rais lakini executive haina mamlaka hayo

6 Wabunge ndiyo watetezi wa wananchi hivyo wao ndiyo ngao pekee ya wananchi kujilinda na maovu yoyote yanayoweza kusababishwa na Sera za serikali.

7 Wabunge wote kwa ujumla wao wanawajibu kwa wananchi kwa mujibu wa katiba bila kujali itikadi zao, bunge linapoapishwa linakuwa bunge la jamhuri na siyo la CCM au la CHADEMA hivyo collectively linawajibika kwa kuwatetea wananchi.

Kuna nadharia inajengwa na wabunge kuwa bunge halina linaingiliwa mamlaka yake na serikali japo hakuna ushahidi wa wazi unaoonyesha hivyo , tunaweza kusema kuwa hii dhana ni perceived na siyo actual na lengo lake ni kulipaka mafuta bunge ambalo halitumii mamlaka yake sawa sawa kwa mujibu wa sheria.

Kuna changamoto Moja iko wazi kwa bunge letu pale wabunge wanapochaguliwa hujenga dhana kuwa wao ni wabunge wa chama na siyo wawakilishi wa wanachama.

Wabunge wa ccm ( ambao ni wengi zaidi)huenda mbali zaidi nakujiona wao ni wabunge wa serikali hivyo huipigania serikali bungeni badala ya wananchi huu ni ugonjwa unaoweza kutibika tutafute tiba tu.

Kulitetea bunge kwenye dhahama hii ni kutowatendea haki wapiga kura wetu.

Namheshimu sana lissu ila sikubaliani na hoja yake ni malalamiko yasiyo na mashiko na yanalenga kulipaka mafuta bunge kwa uzembe wake kuwatetea wananchi.
Mimi naona unaongea nadharia ya bunge kinavyopaswa kuwa halafu pia unajijibu mwenyewe kulingana na yanayotokea bungeni....ni kams vile umemalizia kwa kufafanua vizuri hoja ya Lissu
 
Wanasiasa wanapiga hela tu..hawahitaji pension ....ndo maana unasikia mtu kachangiwa millioni kadhaa..etc...

Watanzania wa level chini, makapuku hali itazidi kuwa ngumu, hao wazazi wetu wanaotarajia kustaafu miaka ya karibuni wanatia huruma sana......

Lkn ndo serikali ya wanyonge hiyo.....tutaelewana tu......ni kukamuliwa kwa kwenda mbele..

Wakati mwingine unajiuliza hivi hao wanaandaa bills ya sheria kama hizi ni Watanzania wenzetu au labda ni class nyingine kabisa tofauti na sisi.....
SERIKALI YA WANYONGE HONGERENI
 
Hapa kidogo bado naweza kumpinga lisu.Tunajua kuwa n kweli bunge halina meno lakini likisimama lingeweza pinga hii sheria.mbona richmond na escrow bunge liliweza.
Wanasiasa ni selfish
Umempinga kwa hoja zipi? Unaelewa maana ya Muswada? Kuna muswada ya Escrow?

Wabunge wote wa ccm hawawezi kupambana kwa hoja na Lisu ndio sembuse wewe upanguws hoja za Lisu kwa paragraph tatu? Kichefuchefu.
 
Undani wa hiyo hoja, Lisu anaeleza sio wabunge tuu

Mchawi namba moja ni yule Mzee wa magogoni

Anatukumbusha pamoja na lawama zote kwa wabunge tusimsahau magufuli kwenye kundi la waliofanya uhujumu wa mfuko wa akiba za uzeeni kwa wafanyakazi

Mjadala unapaswa kuanzia kwa mwenyekiti wa ccm ambaye ndiye rais wa Tanzania kwa kusimamia maamuzi ya hovyo nakifisadi akisadiwa na wabunge wake wa ccm
Huyu chairman ni mzalendo namba moja, wakati mwingine ni lazima Watanzania wazamishwe vidole ili waweze kushtuka.
 
Not at all, halipunguzii lawama. Analilaumu kwa kutokuwa na meno. Soma vizuri, between lines, ndiyo maana tunasema Lisu is great. waliomuelewa ni wachache sana! Msome tena na tena! hatjawahi kuwa na bunge la maana anasema Lisu. Mabunge yote yanaongozwa toka Ikulu. Hili la sasa ndilo maiti kabisa, bado kuoza! basically anailaumu Ikulu kwa miaka yote kupora madaraka ya Bunge kama Jiwe anavyolitemea mate la sasa!
Kuna mipumbavu mpaka leo bado hawajamuelewa kwenye makinikia, saaa mapumbavu hayohayo usitalajie wamuelewe kwenye hili ambalo mchawi namba moja ni mwenyekiti wa ccm na ndio msaliti namba moja.
 
Back
Top Bottom