Tunatatua migogoro yetu kwa mitutu ya bunduki! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tunatatua migogoro yetu kwa mitutu ya bunduki!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Bishop Hiluka, Nov 18, 2011.

 1. Bishop Hiluka

  Bishop Hiluka Verified User

  #1
  Nov 18, 2011
  Joined: Aug 12, 2011
  Messages: 4,101
  Likes Received: 1,425
  Trophy Points: 280
  IMEKUWA ni kawaida kuona ama kusikia polisi wakiwashambulia kwa risasi za moto na mabomu
  wananchi waliogoma, wanaoandamana, wanafunzi wa vyuo vikuu waliogoma, wafanyabiashara
  ndogondogo wasioridhishwa na taratibu za watawala, wananchi wanaoishi maeneo ya migodi
  wanaodai haki zao huku wakiwa hawaridhishwi na ‘uporaji’ wa urithi wao huo, na migogoro mingine
  mingi katika sehemu tofauti za nchi.

  Matukio ya aina hii katika nchi hii yamekuwa ni ya kawaida na hayajaanza leo, yamekuwa yakitokea
  mara kwa mara katika sehemu kadhaa nchini, hasa katika miji mikubwa. Na mara zote kumekuwepo
  taarifa za watu ama kujeruhiwa au taarifa za mauaji ya watu kadhaa.

  Matukio haya yametamalaki kila pembe ya nchi yetu, kuanzia kwenye maeneo ya migodi, vyuo vikuu,
  hadi kwenye maeneo ya wafanyabiashara ndogondogo maarufu kwa jina la machinga.

  Kwa hali inavyoonekana, Serikali haioni tena umuhimu wala haja ya kutafuta suluhu kwa kufanya
  mazungumzo na makundi mbalimbali ya kiraia na kijamii inapotokea pande hizo mbili zinapotofautiana,
  na imeamua kutumia njia inayodhani inafaa 'ya mitutu ya bunduki na mabomu' kwa kutumia vikosi vyake
  vya ulinzi kama njia muafaka ya utatuzi wa migogoro inayojitokeza!

  Kibaya zaidi ni kwamba, mauaji haya yanazidi kujitokeza katika Serikali ambayo imejivika joho la utawala
  bora na kudai kuwa imebobea na kuitekeleza dhana ya utawala bora kwa vitendo.

  Wakati huko nyuma ingeliwezekana watu kujiuzulu kwa mauaji na manyanyaso kwa wananchi kama
  ilivyotokea kwa Ali Hassan Mwinyi akiwa waziri, siku hizi hata polisi wanapodhihirika kutumia nguvu kubwa
  ambayo haikuhitajika katika kuua wananchi hakuna hatua wanazochukuliwa.

  Nakubaliana kabisa na kauli ya Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Yuda Thadeus Ruwa-Inchi,
  wa Kanisa Katoliki, pale alipowataka viongozi wa serikali kutambua kuwa amani na usalama haviwezi kulindwa
  wala kudumishwa kwa kutumia nguvu kubwa za jeshi na matumizi ya silaha kali, bali ni kwa kila kiongozi
  kuwatendea haki watu wake.

  Mfano hivi karibuni, katika kipindi cha siku saba tu kumekuwepo matukio yaliyowahusisha polisi na wananchi
  ambapo polisi walitumia risasi za moto na mabomu hata pale ambapo hakukuwa na haja ya kufanya hivyo.

  Hapa jijini Dar es Salaam, polisi waliwatia nguvuni wanafunzi 46 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa
  kuandamana kuishinikiza Serikali kuwapa wenzao 1,000 mikopo ya elimu ya juu. Kabla ya kuwakamata,
  polisi walitumia mabomu na kutoa vipigo kwa wanafunzi hao waliokuwa wanaelekea sehemu za Ubungo
  kupeleka ujumbe huo kwa wananchi.

  Eneo hilo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam liligeuka uwanja wa mapambano baina ya jeshi la polisi na
  wanafunzi wa chuo hicho walioandamana kushinikiza kupatiwa mikopo ya elimu. Hata hivyo, vurugu
  hizo zilisababisha shughuli zote za chuo hicho kusimama kwa saa kadhaa.

  Kuna picha fulani niliiona ambayo kwa kweli haikunipendeza kabisa, ambapo askari wawili wa kiume
  walionekana kumdhalilisha mwanafunzi wa kike, huku wenzao saba wakiwa wameelekeza mitutu ya
  bunduki kwa mwanafunzi huyo!

  Jijini Arusha polisi walikuwa katika mapambano makali na viongozi na wafuasi wa Chadema waliowatia
  mbaroni na kuwafungulia mashtaka kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria na kukataa
  kutii amri halali ya polisi.

  Na huko Mbeya, risasi na mabomu vilitawala sehemu kubwa ya jiji hilo na kusababisha kifo cha mtu
  mmoja na kujeruhi watu kadhaa. Vurugu hizo zilitokana na operesheni iliyofanywa na askari wa Jiji la
  Mbeya iliyokuwa na lengo la kuwaondoa wafanyabiashara wadogo (Wamachinga) katika mitaa ya jiji hilo.
  Katika vurugu hizo, watu 235 walikamatwa na polisi.

  Mapambano hayo yaliyoanza majira ya saa 2.30 asubuhi katika maeneo ya Mwanjelwa na kusambaa kwa
  kasi katika mitaa mingi ya jiji hilo, yalisababisha kufungwa kwa barabara zote na hakukuwa na gari linaloingia
  ama kutoka katikati ya jiji.

  Polisi zaidi wakiwa na silaha waliwasili na kuanza kuwashambulia wananchi kwa risasi bila kujali kama ni
  mfanyabiashara ama watembea kwa miguu. Katika mapambano hayo, mtu mmoja Abel Mwalukali, alipigwa
  risasi katika mkono wake wa kulia uliovunjika vibaya, na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa
  matibabu. Pia kuna taarifa ya watu wengine kupigwa risasi za moto na kujeruhiwa.

  Lakini pamoja na mapambano hayo, vurugu hizo zilizoendelea bila kukoma na jeshi la polisi kwa kushirikiana
  na JKT kambi ya Itete hawakufanikiwa kutuliza ghasia hizo. Pongezi za pekee ni kwa Mbunge wa Mbeya Mjini,
  Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu kwa kuacha kikao cha Bunge mjini Dodoma na kwenda mjini Mbeya
  ambako alifanikiwa kuzima vurugu hizo kwa njia ya kidiplomasia.

  Kwa kweli Sugu ametoa somo kubwa sana kwa viongozi wa Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama
  kuwa, wananchi wanahitaji kiongozi anayewasikiliza na kutafuta suluhisho la matatizo yao, na kamwe migogoro
  haiwezi kuzimwa kwa mitutu ya bunduki.
   
Loading...