Tunadai hatua zichukuliwe wakati wenye kuchukua hatua ni sisi wenyewe | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tunadai hatua zichukuliwe wakati wenye kuchukua hatua ni sisi wenyewe

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Endaku's, Nov 19, 2008.

 1. E

  Endaku's JF-Expert Member

  #1
  Nov 19, 2008
  Joined: May 25, 2007
  Messages: 322
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 35
  Novemba 19, 2008  Kwa ndugu na majamaa,
  Ushagoo,
  Danganyika.

  Mpenzi Frank,

  Vipi mpenzi wangu? Wajikunyata vipi na hali ya mvua? Mimi mzima lakini wiki hii najisikia niko mbali zaidi na wewe maana mama bosi kanipeleka kwao, eti akienda huko wageni watakuwa wengi hivyo lazima nimsaidie mama yake katika kupika. Kwa hiyo sasa mi mwenzio nina macho mekundu utadhani mchawi maana mama yake hataki kubadili maisha yake.

  ‘Sikiliza mwanangu. Nimepika humuhumu tangu niolewe. Wewe umestawi na upishi wangu huohuo. Mambo ya kusimama na umeme sitaki’

  Na kweli anajua kupika. Naona hutamtambua Hidaya wako kwa kunawili. Napungua tu kwa kutafuta kuni asubuhiasubuhi. Najua unafikiri nini, kwamba naweza kubebwa na kunawili kote huko lakini tunaenda kundi maana wageni wanaokuja kila siku si chini ya kumi.

  Kwa hiyo pole mwenzangu. Najua wewe na wenzio mmekuwa walevi wa umbea wa wanene utadhani haya maigizo ya Wazungu kwenye luninga. Lakini wiki hii ni mambo ya wembamba tu. Sina habari bosi na wenzie wamefanya nini wala wamefanyiwa nini. Badala yake michapo yangu yote ina harufu ya shamba, au kama wenzetu Wakenya wanavyosema, harufu ya ushagoo!

  Lakini harufu ya ushagoo ina utamu wake pia. Kwanza mpenzi nadhani watu hapa mkoani wanafurahia kweli tunavyoweka pua juu kuangaza mafisadi wa angani. Sisemi tusiwaangaze. Lakini tukiangalia juu tu tuwaone ndege wanaotudondoshea uchafu kichwani, tunasahau funza wanaotula miguu hadi tutashindwa kutembea. Kwani huko kwetu hakuna vifisi na vifisadi? Na wakati tunadai wanene wakuu wachukue hatua dhidi ya ndege wachafu, na sisi tumechukua hatua gani kuondoa funza miguuni mwetu?

  Kwa mfano yule afisa ardhi bado yupo? Tena yeye akilewa kazi yake kupita barabarani akitamba kwa sauti anavyoweza kulewa kutokana na hongo za wenye uhanga wa kupata viwanja. Si anatangaza mwenyewe? Na ni kweli na hata kaka yangu akatapeliwa hivihivi na yeye, lakini watu wote na akili zetu tumefanya nini? Tunadai hatua zichukuliwe wakati wenye kuchukua hatua ni sisi wenyewe.

  Hata MB akashtuka. Huko Bongo hana haja ya kutetemeka kwa sababu anatetemekewa kila siku. Akitaka chakula cha ng’ombe, anapewa papo hapo wakati wenzie wote wanasota kwenye foleni. Au dereva wake akiruka foleni na kusababisha msongamano, hana shida maana kwanza trafiki wanatetemekea gari lenyewe na wanapomtambua ndani ya gari inabaki shikamoo kumikumi badala ya kushika gari kwa makosa yale.

  Lakini hapa kijijini ni suala lingine. Hawamjui na kwa kuwa ni mwanamke basi ndiyo zaidi. Wanafikiri wanaweza kumkomesha kabisa. Kwa mfano juzi nilimwona MB anataka kupasuka maana tumbo lake lote lilikuwa linatetemeka kama ugali usioiva.

  Shida ilianza alipoamua kutumia pikapu ya kaka yake kwenda mjini. Pikapu yenyewe wasiwasi lakini bosi alikuwa amebaki na lishangingi lake la wanene na ka Rav ka MB kalikuwa kamegoma, sijui kama nako kamezoea mno maisha ya raha. Hivyo MB hakuwa na jinsi maana alikuwa anakwenda kumwona dada yake hospitali. Basi yeye na mtoto mmoja wa shangazi yake ambaye anakaa huko wakapanda mbele, mtoto wa shangazi akiendesha na mimi nilipanda nyuma na chakula cha mgonjwa nifaidi hewa safi.

  Huko njiani tulisimamishwa na malaika wa barabarani. Mavazi meupeee … roho … Tena ilikuwa wazi jamaa anatafuta pesa maana alikuwa peke yake bila dalili ya kitabu cha risiti wala nini. Amebeba tu lile bunduki ya mwendo kasi.

  ‘Unaona. Unakwenda kilomita 80.’

  ‘Kwani kuna shida gani?’

  ‘Huoni nyumba. Hapa unapaswa kwenda 50?’

  Hapa MB alifanya kosa kwa kuanza kubembeleza (na mimi nilishangaa maana sijawahi kumwona MB akibembeleza!’

  ‘Samahani kaka, tunawahi hospitali.’

  ‘Eti nini mama? Kuwahi hospitali maana yake ni kuvunja sheria? Lipa faini.’

  Kuona ubembelezaji umeshindwa MB akaanza kufoka.

  ‘Nilipe faini ya nini? Bango la mwendo kasi liko wapi?’

  ‘Ohooo, unabishana na mimi? Wajidaaaai mjuzi wa sheria. Basi tuone nani mkubwa hapa.’

  Wakaanza kugombana hadi MB akaamua kutumia silaha ya mwisho.

  ‘Lakini wewe unajua mimi ni nani?’

  ‘Sijui na sitaki kujua.’

  ‘Mimi ni mke wa mheshimiwa wazi ….’

  ‘Na mimi ni Julius Nyerere. Nyinyi wanene mnatafuna kila kitu huko juu na sisi tukitaka vikaranga tu vya watoto wetu mnawaka moto kama kifuu cha nazi. Sasa wanipa ujira wangu au nikupeleke utaje wewe ni nani mbele ya mkuu?’

  Kuona mambo yanazidi kuharibika, yule mtoto wa shangazi alimwambia malaika waende huko nyuma ya gari huku mama anatweta kwa hasira. Na mbele yangu mwenyewe akatoa noti za pembetatu. Waziwazi! Bila kujali nani anapita wala nini. Bila risiti. Aliporudi ndani, mama alitaka kumfokea lakini ilikuwa wazi amefurahi shida imekwisha tuweze kuwahi hospitali. Mtoto wa shangazi akamwambia kila siku yule malaika anashuka kutoka mbinguni na kukaa pale ili awatoze watu ushuru binafsi waweze kuingia mbinguni.

  Kurudi huko kijijini stori ikazaa stori zingine. Afisa ardhi na mambo zake, bosi wa kata naye akawa na vyake, mwalimu mkuu na mitihani, tabia ya mganga mkuu wa hospitali na mabinti wadogo, mwenyekiti wa chama cha ushirika … yaani ilionekana wazi kwamba ile VVUF, vile virusi vya ufisadi vya fyatu wako Makengeza kweli vinaambukiza hadi kijijini. Na kwa kuwa njaa ni kali zaidi basi kila mtu kaambukizwa moja kwa moja. Ndugu zake MB wakawa wanalaani na kumwuliza MB kwa nini serikali haitupi macho huko ushagoo. Ndiyo maana wanaitwa Wadanganyika huko.

  Lakini wakati kila mmoja anashindana na mwenzie kutoa stori za vijifisadi, kijana mmoja akaanza kucheka. Niliambiwa anasoma Kidato cha Nne katika shule ya karibu. Wacha wazee wakasirike!!

  ‘We kijana shika adabu yako. Wakati wazee wanaongelea vya maana unacheka? Watoto wa siku hizi!’

  Lakini kijana hakutishika.

  ‘Samahani wazee lakini hawa mafisadi wote unaowaongelea si vijana.’

  ‘Yaani unatuambia sisi wazee ndio mafisadi?’

  Walitaka kumshambulia na kumnyamazisha papohapo lakini niliona MB kakunwa. Sijui akakumbuka ukorofi wa binti yake mwenyewe.

  ‘Mwache aseme tumpime.’

  Kijana wa watu akawaangalia wote kisha akasema:

  ‘Paukwa …’

  Wazee walitaka kukasirika tena lakini kijana aliwaambia kwamba anafuata mtindo wao. Hadithi hufunza eti.

  ‘Hapo zamani ya siku hizi simba na chui walikuwa marafiki sana. Na walikuwa wakulima mashuhuri wa mihogo. Shida ilikuwa kwamba ndani ya kijiji kile alikuwepo fisi ambaye alikuwa hataki kufanya kazi. Basi kila simba au chui wakilima vizuri anatokezea usiku na kula mihogo yao. Tena alikuwa haiishii hapo. Alikuwa anabeba magunia na kuvuna zaidi ya nusu ya shamba lile. Basi kesho yake, simba au chui wakienda shamba na kukuta hivi, wacha wangurume! Wacha wafoke! Na kila ikitokea hivyo fisi anajificha kwa muda mrefu hadi mingurumo ipoe. Hata hivyo kwa nini atoke wakati anashiba ile mihogo. Akiona mambo yamepoa anatokezea na kufanya vilevile.

  Basi siku moja simba na chui walikuwepo kwenye mataputapu wakilalamika sana tabia ya sungura.

  ‘Kwa nini hachukuliwi hatua?’

  Wakati huo wakamsikia kobe akicheka.

  ‘Yaani wewe simba … wewe chui … na nguvu zenu zote mnamngoja nani mwingine amchukulie hatua yule fisi? Kweli?’

  Hapo watu walikuwa wanasikiliza kwa makini lakini kijana aliishia hapo tu.

  ‘Samahani wazee na nguvu zenu zote …’

  Watu wakatazamana. Na kweli mpenzi. Wanaotula tunawajua. Hawa wa ushagoo tunakaa nao kabisa. Tunamngoja nani mwingine awashughulikie?

  Mpenzio mdanganyika wa ushagoo.

  Hidaya

  Moral of the Story !
  Mambo mengi madogo madogo yanatokea Saana katika maisha yetu mitaani na mara nyingi watu tunalaumu tuu serikali ,yes kwa namna mmoja serikali inawajibika lakini pia wananchi tunapoombwa rushwa tunafanyaje ? Tuwashe moto kwenye kila jambo ambalo ni haki yako ulipate unavyostahili tuache kuhonga hongo ovyo sisi wenyewe kwa kutoa rushwa kwa wanaoweka mazingira ya kuomba rushwa tunawadekeza ,ni ngumu lakini tukianza itawezekana naitakuwa tabia na baadae kuwa mfumo wetu wa maisha,asilimia kubwa twaweza punguza rushwa!
   
 2. E

  Endaku's JF-Expert Member

  #2
  Nov 19, 2008
  Joined: May 25, 2007
  Messages: 322
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 35

  Source :Raia Mwema - Muungwana ni Vitendo
   
 3. b

  benezer Member

  #3
  Feb 20, 2014
  Joined: Feb 10, 2014
  Messages: 5
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Ni wazo zuri sana lakuanzisha vikoba
   
 4. b

  benezer Member

  #4
  Feb 20, 2014
  Joined: Feb 10, 2014
  Messages: 5
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Natafuta mtu mwenye mtaji wake tuungane kuwekeza kwenye gereji-kibaha
   
Loading...