Tumpate mrithi wa Kikwete nje ya CCM

KunjyGroup

JF-Expert Member
Dec 7, 2009
352
26


Ansbert Ngurumo

amka2.gif

KATIKA utafiti na mijadala yangu na makada kadhaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), nimegundua mambo mawili ya msingi.
Kwanza, wana-CCM wenyewe, wakiwamo makada waandamizi, wanakiri kwamba chama chao kimechafuka na kimeathirika sana kisiasa.
Wanasema chama chao kimeshuka umaarufu kwa umma, hakina mvuto; na kwamba kama nchi hii ingekuwa na mfumo wa uchaguzi ulio huru na wa haki, CCM isingechaguliwa tena.
Lakini hawayasemi haya katika vikao rasmi. Hawayasemi hadharani, bali katika mazungumzo ya kawaida, lakini yanayotoka mioyoni mwao. Wanasema kweli.
Wanajua kwamba wananchi wameichoka CCM. Lakini faraja waliyo nayo ni kwamba wanahisi watachaguliwa tena mwakani kwa sababu vyama vya upinzani havijaweza kujipenyeza kwa nguvu za kutosha na kukita mizizi katika vijiji, mitaa na vitongozi vyote nchini.
Wanajua kuwa vyama vya upinzani havijulikani kama CCM. Na kwa kuwa nchi hii haijawahi kutawaliwa na chama kisicho TANU au CCM, wananchi hawajafikishwa mahali pa kuona kwamba wasio katika CCM wanaweza kushika dola na nchi ikatawalika vema. Kwa hiyo, faraja hii ya wana-CCM imejijenga katika ujinga wa umma na unyonge wa upinzani. Lakini wanajua pia si kwamba vyama vya upinzani ni vinyonge kuliko CCM.

Tofauti kubwa ya sasa kati ya CCM na vyama vya upinzani vinavyoonekana (CHADEMA au CUF) ni kwamba CCM imeshika dola; inatumia kodi ya wananchi kuwanyanyasa wananchi wanaoipinga na hata wanaoiunga mkono serikali. Siku ikipoteza nguvu za dola itakuwa chama dhaifu kiasi cha kukosa hata wabunge 10 nchi nzima.
Niliwahi kusema haya huko nyuma, na sasa nasisitiza tena. Yaliyotokea kwingine, Kenya na Zambia, kwa mfano yatatokea hapa kwetu. Nguvu ya UNIP ya Kenneth Kaunda na KANU ya Daniel arap Moi, ilinyauka ghafla na kutoweka siku ile ile vyama hivyo vilipoondoka Ikulu. Jeuri ya watawala iligeuka kuwa unyonge usiomithilika. Vyama hivyo sasa vinaishi nje ya Ikulu, vikiwa katika homa ya uchaguzi na kivuli cha kifo cha kisiasa.

Kwa mantiki hiyo hiyo, CCM isiyoshikilia Ikulu, haiwezi kuwa na ubavu wa kivibeza vyama vingine, kwa sababu yenyewe ni dhaifu zaidi. Lisilojulikana kwa mtu yeyote sasa ni lini CCM itaondoka madarakani, lakini dalili zinaonyesha kwamba siku hiyo haiko mbali.
Maana kama walivyo wana-CCM wetu hawa, wana-KANU na wana-UNIP walikuwa wanajiamini kwamba wangetawala milele.
Hadi siku ya uchaguzi uliowaondoa madarakani, waliamini kwamba wangeshinda wao. Sababu ilikuwa moja tu – mazoea. Hawakuwahi kushindwa kabla ya hapo, hasa kwa kuwa mifumo ya uchaguzi ilikuwa inaendeshwa na wao, na iliwapendelea wao.
Lakini kwa kuwa walishachokwa na umma, walishakosa mvuto, walifanya siasa za kutumia nguvu za dola kuliko ushawishi wa itikadi, sera na utendaji adilifu na makini; waliwachimbia wapinzani kaburi lenye kina kirefu mno, wakatumbukia wao. Sasa inawawia vigumu kutoka!
Huko ndiko CCM inakoelekea. Wanaoamini katika mazoea kwa kuwa hawajawahi kuona upinzani unatawala, hawaelewi ninachosema.
Wanaodhani upinzani ni dhaifu kwa kuwa hawajui kuwa nguvu ya sasa ya CCM ni matumizi ya dola, wanaweza kubeza hoja yangu hii.
Lakini walio makini, hata viongozi wenyewe wa CCM, wanajua ukweli wa hoja hii. Ndiyo maana wanafanya kila jitihada kuhakikisha CCM inabaki madarakani kwa kuzingatia na kutekeleza suala la pili nililogundua na ambalo sikubaliani nalo. Nalo ni kwamba, mtu pekee wa kuivusha CCM 2010 ni Rais Jakaya Kikwete.

Wanadai kwamba CCM hakikubaliki mbele ya umma, lakini bado inaweza kuchaguliwa kwa sifa za mgombea anayekubalika. Wanadai Rais Kikwete anakubalika.
Na hawasemi kwamba Kikwete hana udhaifu. Wanakiri kwamba amekuwa kiongozi dhaifu kuliko wote waliomtangulia. Lakini amefanikiwa kujenga umaarufu binafsi kwa muda mrefu, na kuwafanya watu wampende na kumwonea huruma hata kama ameshindwa kazi.
Lakini kwa chama kutegemea kibebwe na mtu aliyeshindwa kazi, ni kuishi kwa matumaini yanayofananishwa na ramli ya kisiasa. Bahati nzuri yao, vyombo vya habari na taasisi kadhaa za utafiti nchini vimetumika kisiasa kueneza propaganda kwamba rais anafanya kazi nzuri tu, bali anaangushwa na wasaidizi wake.

Vyombo hivyo hivyo vimeshindwa kutufafanulia rais anafanya kazi kwa kutumia nyenzo gani na watu gani. Vimeshindwa kutwambia kwamba udhaifu wa mawaziri wenyewe unatokana na uteuzi mbaya unaofanywa na rais.
Vimekataa pia kutueleza kwamba hata akishawateua, wanapofanya vibaya na ‘kumharibia’ anakosa kabisa uwezo wa kuwachukulia hatua. Je, ni sahihi kumsifia kiongozi anayeshindwa kufanya uteuzi mzuri wa wasaidizi na washauri wake, na badala yake tukawalaumu washauri wake?
Bahati mbaya, kazi hii imekuwa pia sehemu ya majukumu ya kihuni ya watumishi wetu wanaotambulika kama mashushushu au makachero.
Badala ya kutumika kusambaza taarifa muhimu za kuliokoa taifa, wamekuwa wanatumika sana kusambaza na kufuatilia taarifa za kutunga za kumsaidia mtu mmoja ambaye udhaifu wake wa kiuongozi ndiyo sababu kuu ya nchi hii kuporomoka na kudoroa kiuchumi; kuibuka kwa makundi hasimu ndani ya chama tawala na serikali, na kulifikisha taifa mahali pa kukabiliwa na ombwe la uongozi.
Naamini kwamba kama vyombo hivi vya habari na usalama wa taifa vingekuwa vinajali taifa katika uzito unaokubalika; kama vingekuwa vinaona masilahi ya umma katika maisha ya wanyonge na maskini wa nchi hii; kama vingekuwa vinaona madhara ya ufisadi kwa taifa, na vikatambua kuwa watawala ndio wamekuwa vinara na walezi wa ufisadi huo, visingetumia rasilimali zetu kuwalinda.
Sana sana vingewashauri wabadilike au vingesambaza na kufuatilia taarifa za kuwadhoofisha na kuwaondoa, huku vikijenga mazingira ya kuwawezesha wengine wenye nguvu kuchukua nafasi ya walio dhaifu.
Na hata pale ambapo washauri wa rais wameonekana kushindwa kazi au hata kumpotosha, vyombo hivi ndivyo vingetumika kumshauri kiongozi mkuu mwenyewe, na hata kumlazimisha kuchukua hatua kali kulinusuru taifa.
Si tu kulinusuru taifa bali hata kumnusuru yeye binafsi hata kwa kumwambia aachie ngazi kwa heshima kabla mambo hayajaharibika ili taifa liweze kupiga hatua. Si jambo la kujivunia kama vyombo hivi vya habari na usalama wa taifa vinatumika kujenga, kutetea na kusimika udhaifu wa viongozi badala ya kuuondoa; huku vikifanya jitihada za kuwadhoofisha na hata kuwaondoa walio na nguvu ambazo taifa hili linazihitaji kupiga hatua ya kimaendeleo.

Vyombo hivi, kama vingesimamiwa kitaalamu na kizalendo, ndivyo vingetusaidia kuubomoa mfumo mkongwe wa utawala wa nchi hii. Vingetusaidia kuwabomoa watawala wabovu na kuwashauri wapumzike kabla mambo hayajaharibika zaidi.
Vingesaidiana na wananchi wenye nia njema na taifa hili kujenga na kusimika mfumo mpya unaoendana na enzi hizi za karne ya 21.
Kwa maana nyingine, udhaifu wa makusudi wa vyombo hivi ndio unawafanya makada wa CCM leo waone kwamba ingawa kiongozi wao ni dhaifu na hakubaliki kama zamani (kwa sababu za kujitakia), bado anaonekana kuwa ndiye pekee anayeweza kukibeba chama chake kushinda uchaguzi mkuu.
Maana mantiki inakataa. Kama tumekwama kwa sababu ya kukosa uongozi madhubuti, inawezekanaje tufikiri na kukubali kwamba hao waliotukwamisha ndio wanaostahili kushinda tena katika uchaguzi? Kwanini tuwang’ang’anie walioshindwa?
Inawezekanaje, kwa mfano, kwamba ndani ya CCM hakuna mwanachama anayekubalika, anayeuzika na mwenye uwezo wa kuongoza nchi kuliko Jakaya Kikwete?
Yaani, kama Rais Kikwete (kwa utendaji huu wa miaka minne) ndiye taswira halisi ya uwezo na mafaniko ya CCM, tutakuwa waongo tukisema chama kimeishiwa talanta za uongozi? Kama huyu ndiye sampo wa viongozi bora wa CCM, na ndiye pekee anayeweza, tutapata wapi maneno makali zaidi ya kuwatukana watu makini ndani ya CCM?
Je, tutakuwa na makosa gani tukisema inatosha, tutazame kwingine? Kama CCM haina mgombea mwingine mwaka 2010, wakati makada wake wakikiri kwamba chama chao kimekosa mvuto kwa umma, tunakuwa tunalitendea haki taifa hili kumng’ang’ania aliyeshindwa aendelee kutawala, hata kama yeye anataka?
Jambo moja ni dhahiri. Kinachowafanya wengi wao wajipendekeze kwa rais ni unafiki binafsi na kujipendekeza. Wanaogopa mamlaka yake ya kikatiba kitaifa na katika CCM, maana ndiye kiongozi wa vikao vikuu vya maamuzi makubwa yanayohusu pia masilahi yao binafsi kisiasa.
Na wanajua kuwa wanapokuwa na mgombea ambaye yuko madarakani, atatumia nguvu zote za dola kujipa ushindi kupitia mifumo ile ile inayoandaa na kuratibu uchaguzi. Wanataka ushindi hata kama hawana mkakati wa kuutumia kuleta maendeleo ya taifa.
Lakini kama wanakiri kwamba wameshindwa kazi, na kama wanaamini kwamba chama kina hazina kubwa ya talanta za uongozi, kuna ubaya gani wakaanza mchakato rasmi na usio rasmi wa kupata uongozi utakaolikwamua taifa hili kutoka kwenye lindi la maradhi, ujinga, umaskini na ufisadi? Kama wana-CCM wanaipenda nchi hii, kwanini wanakosa ujasiri wa kusema ukweli daima (kama kanuni yao mojawapo inavyosema), wakatusaidia kutafuta mbadala wa Kikwete katika chama chao? Lakini haya yote yanaleta ujumbe mwingine mzito kwa taifa. Enzi za kutawaliwa na CCM zimekwisha. Na kama enzi za CCM zimekwisha kwa nini tusishirikiane sasa kutafuta mbadala wa uongozi wa kitaifa nje ya CCM? Au bado tunadhani haiwezekani?


MAONI YENU MWANA JF....
 
Back
Top Bottom