Tumia mizozo ya watoto kuwajenga kitabia

Tumia mizozo ya watoto kuwajenga kitabia

Sema Tanzania

JF-Expert Member
Joined
May 18, 2016
Posts
251
Reaction score
466
Kama wazazi, sio jambo geni kuona watoto, hasa waliofuatana, wakigombana mara kwa mara na wakati mwingine kupigana kabisa na kufanyiana vitendo vya kukomoana. Wengi wetu tunaweza kukumbuka matukio mbalimbali ya kugombana na ndugu zetu pindi tulivyokuwa watoto. Hali hii ni ya kawaida lakini huwapa wazazi wakati mgumu sana hasa pale watoto wanaposhindwa kukaa kwa amani na mzazi kujikuta akiwa hakimu muda wote. Kesi za mara kwa mara zinachosha kwakweli na wazazi wengine hujikuta wakichelewa nyumbani au kuwaweka watoto shuleni muda mrefu ama shule za bweni ili kuepuka adha ya kuwa hakimu nyumbani.

Mara nyingi, mzazi hujikuta akiegemea upande mmoja na kumtetea mtoto mmoja huku akiona kwamba mwenzake ndiye mkorofi. Pengine unambandika mtoto majina kama ‘mtundu’ au ‘mkorofi’ bila kujua kuwa unavyozidi kumuita majina haya, unampa nafasi ya kuwa mkorofi zaidi. Inawezekana kuwa yeye huwa sio mwanzilishi wa kila ugomvi na hana namna ya kujitetea kwa kuwa imeshajulikana kuwa yeye siku zote ni mkorofi.

Watoto ni werevu sana na wana uwezo wa kukusoma na kutumia udhaifu ulionao kwenye mambo fulani kama mwanya wa kuwaonea wenzao. Pia, watoto wanajua kuwa mama/baba ‘anamsikiliza na kumjali fulani zaidi yetu’. Ingawa wote ni wanao, mara nyingi kuna mmoja au wawili wanaokuwa karibu na wewe zaidi na wakisema kitu unakichukulia hatua. Ingawa hii ni hali ya kawaida, tukumbuke kuwa watoto wanaona na kuelewa hili na huweza kutumia mwanya huu kuwaonea na kuwasingizia wenzao. Hii ni hali ya kawaida kwa watoto wanapokua wakitafuta utambulisho wao.

Ugomvi wa mara kwa mara huwaathiri watoto kisaikolojia; hasa wale wanaokuwa wanyonge kwa wenzao. Huwaathiri kimasomo, huathiri mahusiano yao na wengine, huwafanya wasijiamini na kuwa na hisia kuwa wao ni wakosaji kila mara. Ugomvi ukizidi sana, huweza kupelekea msongo wa mawazo hali ambayo inaweza kumsababisha mtoto kujidhuru, kukimbia nyumbani ama kutaka kwenda kuishi na ndugu mwingine wa karibu. Epuka kuwa muamuzi wa mashitaka yao kila wakikwaruzana, epuka kumpa mtoto jina kutokana na tabia yake, epuka kupendelea upande mmoja zaidi maana wote wanastahili kupendwa, kusikilizwa na kuthaminiwa.

Jitahidi kujiwekea mfumo mzuri wa kuwa mwamuzi wa haki bila kupendelea upande mmoja pale watoto wako wanapofarakana. Jaribu kuwaachia wenyewe wasuluhishe kwa usimamizi wako. Pasipo kuwahukumu, unaweza kuwakalisha chini na kuwasikiliza na kisha kurudisha swali kwa kila mmoja, ‘Je kama wewe ungefanyiwa hivyo ungejisikiaje? Ni ipi namna sahihi ya kushirikiana na mwenzio?’ Unaweza pia kuweka sheria kuwa kila wakizozana wanapata adhabu wote kama kuosha vyombo kama ni kulingana na uwezo, uelewa na umri wao.

Wajenge watoto kuwa wamoja siku zote. Waeleze umuhimu wa undugu na kuishi kwa amani, waeleze namna unavyojisikia pale wanapopigana na kuzozana kila mara na uwaambie namna unavyofurahi wakicheza pamoja kama ndugu. Wafundishe watoto kuombana msamaha na kupatana pasipo kujali nani mwenye kosa. Ni vyema uwe mfano wa hili; waombe msamaha wewe kama mzazi pindi unapowakosea. Ni ngumu ila ni fundisho jema kwao kama watu wazima wa baadae. Mwisho, kumbuka kuwa haya mafundisho hayatatekelezwa haraka; yatachukua muda ila hayataondoka akilini mwao. Siku zote watakua wakijua kuwa wanapaswa kuishi kwa amani na kupendana.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia kurasa zetu za Facebook, Instagram and JamiiForums: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
 
Hili swala la ugomvi ,limesababisha wife aniombe tuwapeleke boarding, yaani uhakimu umemshinda ,wanatembezeana vifinyo,vikumbo,mabanzi yaani ni malalamiko kila mara
 
Umeandika ya maana Sana.

Kuna watoto wawili wanapenda Sana kupigana lakini Kati ya hawa wawili mmoja mdogo ndiye mkorofi Sana na mkubwa akirudisha mapigo mama yao hukasirika Sana na kumwita yule mtoto mkubwa kua ni muuaji na maneno mengine yasiyostahili kwa mtoto na wakati mwingine humuadhibu kabisa.

Hiyo hali imepelekea yule mtoto mkubwa kua mnyonge Sana na yule mdogo akiona mkubwa anapigwa hufurahia Sana na sio kwamba mama yao hajui kuwa yule mdogo ni mkorofi anajua ila sijui kwanini hupendelea upande mmoja.
 
Hili swala la ugomvi ,limesababisha wife aniombe tuwapeleke boarding, yaani uhakimu umemshinda ,wanatembezeana vifinyo,vikumbo,mabanzi yaani ni malalamiko kila mara
Habari. Asante kwa kutuletea ushuhuda huu hapa jukwaani, tafadhali, ungana nasi hapa hapa kujua mengi zaidi
 
Umeandika ya maana Sana.

Kuna watoto wawili wanapenda Sana kupigana lakini Kati ya hawa wawili mmoja mdogo ndiye mkorofi Sana na mkubwa akirudisha mapigo mama yao hukasirika Sana na kumwita yule mtoto mkubwa kua ni muuaji na maneno mengine yasiyostahili kwa mtoto na wakati mwingine humuadhibu kabisa.

Hiyo hali imepelekea yule mtoto mkubwa kua mnyonge Sana na yule mdogo akiona mkubwa anapigwa hufurahia Sana na sio kwamba mama yao hajui kuwa yule mdogo ni mkorofi anajua ila sijui kwanini hupendelea upande mmoja.
Asante kwa ushuhuda huu. Ni imani yetu kwa kupitia makala haya, sasa unaweza kuwapa elimu hii adhimu. Kwa maelezo zaidi unaweza kutupigia simu kupitia namba 116 tuzungumze.
 
Shukrani,wakati mwengine inawahusu sana wazazi wa kambi maana wanakuwa watesaji wakati walijichagulia,kumbe Ni kukosa maarifa sahihi ya malezi.
 
Back
Top Bottom