Tumevurugwa: Tunahitaji muafaka wa kitaifa!

Tumevurugwa: Tunahitaji muafaka wa kitaifa!

LENGEJU BOB

Member
Joined
Nov 1, 2010
Posts
53
Reaction score
31
UTANGULIZI

Wahemga walinena, Mficha maradhi kifo humuumbua…Kuendelea Kujaza Maji kwenye ndoo iliyotoboka huku ukifahamua kuwa hayatajaa ni ujinga. Mungu ametupa akili na ufahamu, na hii ndiyo tofauti ya msingi kati ya sisi binadamu na viumbe hai vingine, kama wanyama na miti. Binadamu aliyekamilika hawezi kuanza safari ambayo hajui mwelekeo wala mwisho wake, lakini ni ujinga zaidi kuanza safari, ingawa ina mwelekeo, lakini unafahamu mwisho wake ni wa maangamizi. Kutokana na majukumu waliyonayo viongozi wetu, yale mema na yale yenye ukakasi, ambayo ndiyo mengi zaidi, kuna wakati akili zao huchoka na ubongo kugoma kufanya kazi. Pale zinapoachokea akili zao, ndipo akili za wananchi zinapaswa kuanzia. Ni dhambi kubwa kuweka mustakabali wa Taifa zima, lenye watu takriban milioni 50 kwenye mikono ya kiongozi mmoja au kikundi cha viongozoi wachache. Ni hatari kukabidhi matumaini ya vizazi 100 vijavyo kwenye mikono ya kamati kuu za vyama vya Siasa.


Kama kuna wakati nchi hii ilihitaji nuguvu hasa ya umma, basi wakati huo ni sasa. Sauti za watanzania zinahitajika sasa kuliko wakati wowote ule katika hostoria ya Taifa hili Tajiri mno. Kwa ujinga wetu au Pengine ni kutokana laana ya melfu ya vijana wanaharakati waliokufa kabla ya wakati, laana itokanayo maelfu ya watoto waliopoteza maisha kabla ya kuzaliwa, laana ya maelfu ya waamama waliopoteza maisha kwa kukosa huduma wakiwa katika harakati za kujifungua au laana ya mababu tuliowazika wangali wazima; Dhambi zetu kama Taifa, zimekuwa nyingi mno kiasi kwamba hatuna tena uwezo wa kuona wala kuelewa. Tumejazwa ujasiri wa kishetani wa kushangilia kwenye msiba na kulia kwenye sherehe. Tunawachekea, kuwabeba na kuwatukuza wale wanaouza nchi yetu, utu wetu na utaifa wetu, na tunawalaani wale wanaojaribu kutufumbua macho, kwamba nchi inauzwa, roho za watu zinawekwa rehani.
Yanayoendelea katika mchakato huu wa katiba yanathibitisha kiwango cha juu mno cha kiburi cha wenye mamlaka na kiwango cha juu mno cha ujinga wa watawaliwa. Wote tunajua kwamba Bunge hili maalumu halitaleta katiba ya wananchi lakini kila siku tunasoma magazeti na kuangalia TBC1 kujua maendeleo ya mchakato wa katiba. Viongozi wote wa vyama vya usiasa, viongozi wa didi, asasi za kiraia na kakundi ka watu walioteuliwa na watawala, lakini eti kakiwakilisha wananchi, nako kako bungeni. Wotw wanaendelea na mchakato ambao mwisho wake wanaujua. Labda wanasubiri maono kutoka kwa miungu au ndoto kutoka kwa mababu…Mtachapwa! Makala haya yamebeba maudhui ya kukatisha tama, lakini ndio ukweli kwahiyo nitausema, tena mchana na kwa Kiswahili fasaha.ukweli ni ukweli, hata kama hautakwi. Ndani ya makala haya nitachambua hali halisi ya pale tulipofikia katika mchakato huu wa katiba na hivyo kubashiri kisayansi, kule tunakoelekea . Kwa maoni yangu, gari imezama kwenye matope, haiwezi kutoka tena na ikiweza kuendelea na safari, itafika vipande vipande. Nitatumia madhui ya hotuza ya Warioba, mwenyekiti wa iliyokuwa tume ya Mabadiliko ya Katiba na pia nitatumia maudhui ya hotuba ya Mh. Rais Jakaya Kikwete. Nitaeleza ni kwanini hotuba hizi mbili zimetuvuruga na mwisho nitatoa maoni yangu, ushauri wangu na mapendekezo yangu kuhusu njia mbadala na muafaka ya kutoka hapa tulipo na kufika huko tuendako, kwa usalama. Tafadhali fuatana nami.


2.0 MAUDHUI YA HOTUBA (JK,WARIOBA)


Hotuba mbili za kihistoria zilizotolewa wiki iliyopita zilisimika maana kamili ya kile nilichokuwa nakitahadharisha. Hotuba ya warioba ni kama ilijenga, na ile ya Rais ni kama ilibomoa. Nini kimejengwa na nini kimebobolewa ni suala la mjadala. Simaanishi hapa kwamba kilichojengwa kilikuwa kizuri kwa asilimia mia wala simaamishi kilichobomolewa kilikuwa kibaya asilimia mia. La msingi hapa ni ukweli. Kwamba hotuba ya Warioba ilijenga na Hotuba ya Rais Jakaya Kiwete ilibomoa.. Muktasari wa yote hayo ndio umebeba mada ya makala ya leo….Tumevurugwa!

Alichowasilisha warioba ni maoni ya wananchi. Uwasilishaji wake umepewa kibali na sheria ya mabadiliko ya katiba, kwamba majukumu ya tume ni kuratibu ukusanyaji wa maoni ya wananchi, kuchataka maoni hayo, kutengeneza rasimu na kukabidhi drafti ya mwisho ya rasimu kwa njia ya uwasilishaji katika Bunge Maalumu la katiba. Hakuna alichofanya au kusema Warioba, ambacho hajaelekezwa na sheria. Hakuwasilisha mawazo yake, bali mawazo ya wananchi. Halikuwa jukumu la tume kuchambua maoni mazuri au mabaya. Kazi ya tume ilikuwa ni kukusanya maoni ya watu. Na katika mchakato wa kidemokrasia, hakuna mwenye mamlaka ya kuamua kwamba maoni fulani ya watu wengi hayafai. Wote tunakualiana kwamba tume imefanya kazi nzuri na inastahili pongezi. Kwa bahati nzuri, hata Rais Kikwete ameipongeza tume kwa kazi iliyotukuka.

Kwa mujibu wa ripoti ya Tume, matokeo ya kitawkimu yanaonyesha kati ya wananchi 38,000 waliotoa maoni yao kuhusu muungano visiwani Zanzibar, 19,000 walizungumzia suala la muundo wa muungano, huku zaidi ya nusu ya watu hao wakitaka marekebisho ya kikatiba yatakayowezesha uwepo wa serikali tatu. Kwa upande wa Tanzania bara, asilimia 61 ya wale waliotoa maoni yao juu ya muungano, walipendekeza serikali tatu. Aidha, kwa upande wa Zanzibar asilimia 60 walipendekeza muungano wa mkataba.Tume pia ilitoa matokeo ya kihoja, kwa wale wanaopendekeza serikali tatu na kwa ujumla, Tume imechakata hoja kadhaa za kwanini wananchi wanataka muundo wa muungano wa serikali tatu. Kwanza, tume imeweka wazi kuwa suala la muundo wa serikali tatu limechukua nafasi kubwa katika mjadala tangu tume ilipozindua rasimu ya kwanza ya katiba. Mjadala wa muundo wa muungano umekuwa mkubwa kiasi cha kufunika mapendekezo mengine yaliyomo kwenye Rasimu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kwa mujibu wa ripoti ya warioba, muundo wa serikali tatu haupunguzi uimara wa Muungano na kwamba muungani huo ni wa waananchi kwa manufaa ya wananchi.Tume pia imetanabaisha kwamba muundano wa serikali mbili waliotuachia waasisi wetu siyo huu uliopo sasa. Muungano wa sasa umebadilishwa mara nyingi na wakati mwingine bila ya kufanya marekebisho kwenye katiba, na hivyo kuacha masuala mengi yakiendelea kwenye serikali zetu mbili bila kuwa na uhalali wa kikatiba. Kwa maoni ya tume, waasisi wetu walituachia muungano wa nchi moja yenye serikali mbili, lakini kwa sasa tuna muungano wa nchi mbili zenye serikali mbili. Kutokana na mkanganyiko huo, tume inasema pande zote mbili za muungano zimeendelea na zitaendelea kulalamika. Wakati Tanzania bara wakilalamikia uwepo wa Zanzibar kama nchi katika muungano huku Tanganyika ikifutwa, Zanzibar inalalamika kwamba Tanzania bara imejificha katika koti la Serikali ya Muungano na hivyo kufaidika na masuala ya muungano. Zanzibari inalalamika kupunjwa katika faida kadhaa zitokanazo na muungano. Zanzibar inalalamika kutohusishwa katika maamuzi kadhaa yahusuyo muungano, na zaidi sana, Zanzibar inalalamikia kuongezwa kwa masuala ya muungano kila wakati ambapo sasa limeingizwa, tena kinyemela, suala la mafuta na gesi. Wanahoji mbona dhahabu na Tanzanite haijawahi kuwa suala la muungano toka kuasisiwa kwa muungano. Kwamba Tanzania bara imeendelea kuneemeka kwa rasilimali hiyo wakati wote peke yake, lakini sasa inapogundulika kuwa Zanzibar kuna hazina kubwa ya mafuta na gesi wanyang'anywe na kufanywa suala la uungano? Ripoti inamalizia kwamba malalamiko haya, yamekuwa yakitolewa kwa zaidi ya miaka 30 sasa na karibia tume zote zilizoundwa kujaribu kuchunguza na kutoa ufumbuzi wa suala hili, zilipendekeza muundo wa muungano wa serikali tatu kama suluhisho na mara zote maoni hayo ya kitaalamu yalikataliwa kwa sababu za msimamo wa kisera wa CCM, juu ya uwepo wa serikali mbili. Kwa bahati nzuri sana, maoni ya tume ya safari hii hayakutokana na utaalamu wa watu waliojifungia chumbani na kutoa maoni yatokanayo na nadharia za kifalsafa. Ni maoni ya wananchi.

Hotuba ya Rais kikwete ilipokelewa katika picha mbili tofauti. Ya kwanza ni picha ya Rais wa nchi anayehutubia bunge la wananchi na kuwataka wabunge kuwa makini katika kuchambua masharti ya Rasimu, akiwasihi wasome kifungu kwa kifungu, mstari kwa mstari na neno kwa neno, akisisitiza kwamba jukumu la bunge maalumu ni kuhakikisha linarekebisha kasoro zilizokona kuiboresha rasimu ili hatimaye ipatikane katiba bora, kwa manufaa ya wananchi wote. Hapo, alisimama kama Rais wa nchi, amiri jeshi mkuu, mwenye dhamana ya ubaba katika nchi. Lakini, kwa upande mwingine, ama kwa kujisahau ama kwa kuzidiwa na hisia za ukada wa chama na pengine umuhimu au ulazima wa maoni aliyodhani ni sahihi zaidi, japo ni maoni binafsi, Rais alichepuka kwa muda na kuvaa uenyekiti wa chama na kutoa maelekezo yenye kujenga zaidi msimamo na maslahi ya chama chake. Kwahiyo, sehemu Fulani ya hotuba yake, kwa kiasi kikubwa ilijielekeza katika kupangua hoja zilizotolewa na tume na kusimika mtazamo na mwelekeo mbadala. Kwa bahati mbaya sana, hoja zilizizopanguliwa ni muhtasari wa maoni ya wananchi na mtazamo na mwelekeo mbadala uliosomikwa na Rais ni maoni binafsi ya Jakaya Kikwete na msimamo wa kisera wa chama cha Mapinzduzi. Kwa bahati nzuri alijitahidi na kuweza kufafanua vema baadhi ya sababu anazosimamia katika maoni yake hayo, tena alifafanua kwa hoja. Kwa mfano, Rais alihoji uhalali wa kitakwimu wa matakwa ya wanachi ya serikali tatu. Kwamba kati ya watu 351,664 waliotoa maoni kwenye tume, ni watu 42,820 tu, ambao ni sawa na silimia 13.6 ndio walioonyesha kukerwa na muundo wa muungano wakati watu 303,844 sawa na asilimia 86.4 hawakuwa na tatizo la muungano. Hoja ni kwamba, iweje asilimia 13.6 itafsiriwe kuwa ndiyo watanzania walio wengi waliotaka muundo wa serikali tatu?

Hatahivyo, hili linajibiwa na hoja za tume yenyewe pamoja na wataalamu kadhaa wa masuala ya utafiti. Kwamba kwa ujumla ziko tafiti za aina mbili. Kwa lugha rahisi ziko tafiti zinazolenga kupata matokeo ya kitakwimu yaani namba au idadi (Quantitative Research), na ziko tafiti zenye kutafuta matokeo ya uzito wa hoja (Qualitative Research). Kwa hiyo, wakati katika utafiti takwimu swali linaweza kuwa ni watu wa ngapi? Katika utafiti-hoja swali ni kwanini au kwa sababu gani? Wataalamu wa masuala ya utafiti wanakubaliana kimsingi, kwamba kwa ukusanyaji wa takwimu zinazohusu maoni ya watu, nyenzo nzuri ya kutumia ni utafiti-hoja. Aina hii ya utafiti ndiyo iliyotumiwa na tume ya Jaji nyalali, na baadaye kuungwa mkono na Mwl, Nyerere, juu ya maoni ya wananchi ya ama kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa au kubaki katika mfumo wa chama kimoja. Kwa mujibu wa utafiti ule, asilimia 80 walitaka tubaki na mfumo wa chama kimoja wakati asilimia 20 walitaka tuingie katika mfumo wa vyama vingi. Wangezingatia matokeo ya utafiti wa kitakwimu, asilimia 80 wangeshinda na pengine mpaka leo CCM ingekuwa ni chama pekee cha siasa Tanzania. Lakini kwa kufuata matokeo ya utafiti-hoja, tume ilijiridhisha na kuaninisha kwenye ushauri kuwa, pamoja na kwamba waliotaka mfumo wa chama kimoja ni wengi kuwazidi wale waliotaka vyama vingi, lakini hoja au sababu walizotoa wale wachache zina uzito zaidi ya zile walizotoa wale wengi. Kumbukumbu zinaonyesha kwamba miongozi mwa sababu ziliyotolewa na watu wengi waliohitaji kuendelea kwa mfumo wa chama kimoja ni kwamba wamezaliwa katika chama hicho, chama kimewalea, chama kimeleta uhuru n.k. Wakati wale wachache walitoa hoja za Demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria; umuhimu wa kufikisha madaraka kwa watu na uwezo wa wananchi kuwajibisha viongozi wao. Hoja nyingine ya Rai Kikwete, mabyo pia ni hoja ya CCM na ya wote tunaotamani kuendelea kwa mfumo wa serikali mbili ni ukubwa wa gharama za kuendesha serikali tatu. Tume imetutoa hofu, kwamba gharama haitakuwa kubwa kwa jinsi inavyofikiriwa, hasa kwa kuwa kwa mapendekezo yaliyowasilishwa na tume, muundo wa serikali tatu utakuwa na watendaji wachache zaidi kwa maana ya wabunge na mawaziri kuliko huu wa sasa wa serikali mbili, ambapo kwa sasa kunahudumia takribani wabunge 380 wa bunge la Jamhuri na wale wa Baraza la wawakilishi wakati mapendekezo ya tume yana idadi ya wabunge wasiozidi 200 kwa mabunge yote ya nchi Tatu. Hivyo hivyo kwa idadai ya wizara, mawaziri na watendaji wa wizara. Tume pia imetoa ufafanuzi, kwamba suala la gharama si suala la msingi unapohitaji kupanua uwezo wa kuwahudumia wananchi kidemokrasia na kiutawala. Warioba ametoa mfano kuwa mikoa inaongezeka kila wakati, wilaya zinaongezeka, wizara zinaongezwa kila mara na haya yote yanaongeza gharama. La msingi linaloangaliwa ni umuhimu wa upanuzi wa wigo wa kuwahudumia wananchi na sio gharama zitkanazo na nia njema ya kuwafikishia wananchi huduma muhimu na za lazima. Tume inahitimisha kwamba kwakuwa muundo wa serikali mbili ndani ya nchi mbili umeshindwa na hauwezi tena kuisogeza nchi mbele, mahitaji ya mabadiliko ya kimfumo ni lazima na ni suala la lazima na lisiloepukika, bila kujali gharama za kufikia huko. Na kwa maoni ya wananchi, unapendekezwa mfumo wa Serikali tatu.

Kuhusu malalamiko ya masuala ya muungano, Rais kikwete ametangaza rasmi kwenye hotuba yake, kwamba kwa mujibu wa mapendekezo ya tume, masuala ya muungano yako saba tu na ambayo kwa uchache wake hayahitaji kuundiwa serikali ya tatu. Ameonngeza kuwa serikali zilizopo, yaani ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar, zimedhamiria na zinaweza kutatua kero zote za muungano, bila kuhitaji serkali ya tatu. Hilo ni tangazo zuri sana lenye kujaa matumanini. Swali ni je, serikali hizo zilikuwa wapi kwa muda wa zaidi ya miaka 30 ambapo wakati wote wazanzibari walikuwa wanalalamika na watanganyika kadhalika? Walikuwa wapi wasimalize kero hizo waje waibuke leo ambapo watu wanataka mchi yao? Tangazo hilo la Rais linapokewa kwa wasiwasi kwamba, msingi wake ni kutuliza hali ya hewa zaidi kuliko kuleta ufumbuzi wa kudumu wa migogoro mizito mno ndani ya muungano uliopo. Kwa taarifa tu, ni kwamba watu wa Zanzibar hawajawahi kutaka kuua muungano. Malalamiko yao miaka yote ni juu ya mgawanyo sawa na wa haki wa faida zitokanazo na muungano, ikiwa ni pamoja na kuipa Zanzibar mamlaka kamili ya kuamua mambo yake. Serikali ya Jamhuri imekuwa kiziwi na kipofu kwa zaidi ya miaka 30. Hoja ya kudai nchi yao imekuja baada ya kuona kelele zao za kuhitaji kuheshimiwa hazisikilizwi! Sasa wakubwa wameshikwa pabana, ghafla kila kitu kinawezekana!


3.0 UCHAMBUZI

Hebu tuchukulie kwamba Serikali mbili ziendelee. Kwamba kero za muungano zitatuliwe zote ndani ya muundo uliopo. Muundo upi huo? Wa nchi moja yenye serikali mbili au nchi mbili zenye serikali mbili? Kama ni chi mbili zenye serikali mbili kinachozaliwa ni muungano au ushirikiano? Nasema haya kwasababu Zanzibar tayari wamekamilisha mchakato wa kihistoria na kutengeneza katba inayoitambua Zanzibar kama nchi kwa maana ya mipaka ya kijografia na utaifa wa watu wake. Itawezekanane tuendelee na muundo wa serikali mbili bila kwanza kufanyia marekebisho makubwa katiba ya Zanzibar? Je wanzanibar baada ya kupiga hatua hiyo muhimu wako tayari kufanyia mabadiliko katiba yao? Au tutawalazimisha? Na tutawalazimisha kwa kutumia sheria au ubabe tu? Kwasababu Katiba ya Zanzibar imeshajiwekea yenyewe utaratibu wa kujibadilisha, ambao kimsingi unafuata hatua zote za uanzishwaji wake. Kwahiyo, kisheria, haiwezekani kubadili katiba ya Zanzibar kwa kikao cha siku moja. Je Unaweza kuwapa Zanzibar kila wanachohitaji na bado Zanzibar ikabaki mkoa maalumu ndanio ya Jamhuri?... Ni michanganyo na mivurugani tu!

Nimefuatilia kwa karibu sana mijadala inayoendeshwa na kamati ya maridhiano Zanzibar.Kamati ya maridhiano ni kamati yenye heshima kubwa kule Zanzibar. Ni kamati iliyoasisi na kuratibu maridhiano na mwafaka wa uhakika wa Kitaifa la Zanzibar, baada ya miafaka kadhaa ya huko nyuma kujaribiwa ka kushindwa. Tofauti na miafaka iliyowahi kujaribiwa huko nyuma iliyoshirikisha mtu wa tatu, yaani mpatanishi au wapatanishi toka nje ya Zanzibar, muafaka ulioratibiwa na kamati ya maridhiano uliwahusu wazanzibari peke yao, napengine hii ndiyo siri ya mafanikio yao. Amani, umoja na mshikamano wa Zanzibar ya sasa ni matokeo ya kazi nzuri ya kamati hii. Kwamba maalif seif na Shein wanakaa meza moja na kuongoza nchi kwa mafanikio makubwa ni matokeo ya kamati hii. Wazanzibari ambao huko nyuma waligawanyika vipande vipande, watoto wakiandikishwa skuli kwa itikadi za vyama, wagonjwa kutibiwa kwa kufuata idikadi za vyama na hata maziko ya wafu yalizingatia msiba ni wa chama gani, leo ni wamoja. Zanzibar tuliyoizoea kuona bendera za vyama mazikoni. Leo wameungana, wanapepea bendera ya Zanzibar badala ya vyama vyao, wanaimba wimbo wa Taifa la Zanzibar, wanajitambulisha kwa uzanzibari zaidi kuliko upemba na u-ungja. Ni matunda ya kamati ya maridhiano.

Kwa vyovyote vile, mwenye akili timamu hawezi kupuuza maoni ya kamati hii. Sasa kwa kadiri ya maudhui ya mijadala ya kamati ya maridhiano, wazanzibari wanataka nchi yao, yenye mamlaka kamili. Katika video iliyowekwa kenye mtandao wa ‘youtube' kuna kibwagizo cha wimbo unaosindikiza mikutano ya kamati ya maridhiano kinachosema "Tunatakla nchi yetu sasa tumechoka"! na kila anayesimama, kuanzia Rais (Seif), mawaziri, wawakilishi na wananchi…kauli mbiu ni moja tu…Tunataka nchi yetu. Waziri wa sasa wa sheria wa Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wote wanasisitiza Zanzibar yenye mamlaka kamili. Kwa bahati nzuri sana, wazanzibari ni wawazi, sio wanafiki, hawamung'unyi maneno kama sisi wa huku bara. Wanazungumza kwa Kiswahili fasaha na kwa sauti ya juu mchana kweupe, Tunataka nchi yetu. Kuwe na serikali moja, mbili, tatu au nane, sisi tunataka nchi yetu.
Kama nilivyogusia awali, kibwagizo hicho cha "tunataka nchi yetu" kimeasisiwa na viongozi wa wili wakuu wa Zanzibar, yaani Maalif Self na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, mwana wa muasisi wa mapinduzi na Taifa la Zanzibar. Hawa ndo walioamua kukaa chini, kutafakari uzanzibari wao, kuona madhila wanayoyapata kwa kisingizio cha muungano. Wamepima maslahi yao kama watu mashuhuri na umuhimu wa kujidhili ili kuwapatia wazanzibari heshima wanayostahiki. Wakaamua wasimshirikishe mtu asiye mzanzibari katika muafaka wenye manufaa kwa wazanzibari. Ikaandaliwa tume ya maridhano ya wanzanzibari iliyozaa Nchi ya Zanzibar inayojipambanua kwa mipaka yake kijiografia na utaifa.

Nikirejea somo la makala haya, ni ukweli unaojitegemea, kwamba Tumevurugwa vibaya. Kama taifa, hatukujipanga kuelekea kwenye huu mchakato. Tumekurupuka tu. Tumevamia mchakato huku tukiacha maswali mengi ya msingi hayana majibu. Tumetumia fedha na rasimimali za Taifa kukusanya maoni ya wananchi huku mamlaka za kiserikali na vyama vya siasa zikiwa tayari zina misimamo yao isioyumba. Hakukuwa na umuhimu wa kuundwa kwa tume ya kukusanya maoni kama hatukuwa tayari kukubaliana na maoni hayo. Hakukuwa na sababu ya kuunda Bunge la katiba lenye kazi ya kupinga kila hoja iliyotolewa na wananchi. Kitakachoendelea ni kwamba Bunge hili litapitisha muundo wa serikali mbili, hili ni suala la akili na mahesabu tu, angalia idadi ya wanachma wa vyama vya siasa katiba bunge, utapaja jibu la chama gani kitashinda. Baada ya hapo tutaingia kwenye kura ya maoni.Kipindi cha kura ya maoni kitakuwa ni kama uchaguzi mkuu. Gharama kubwa itatumika kushawishi watu wakubaliane na maoni ambayo hawakuyatoa. Wakikubali tunabaki na mfumo uliopo na wakikataa tutaingia kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa katiba iliyopo ambayo itazaa pia, mfumo uliopo. Tumetumia muda na gharama kubwa nyingi kujaza maji kwenye gunia. Binafsi sina la kusema, sioni wala sisikii tena. Kuhukusu suala la mchakato huu wa katiba maswali ni mbili au tatu, tatu au mbili, mbili za namna gani? Tatu zinawezekanaje? Sasa ndo tumekubaliana nini? Mbili au tatu? Nne au moja?, ipi bora?.... itaendeshwaje?. Halafu?..mbona haieleweki?............Tumevurugwa.


Sula hapa sio maoni ya mtu wala taasisi Fulani, hata mtu huyo akiwa mkubwa kumkaribia Mungu au taasisi ikiwa na nguvu kuikaribia Vatican. Suala ni mahitaji ya watu walio wengi. Mimi binafsi, pendekezo langu, kutoka moyoni ni muundo wa serikali mbili. Maoni yangu haya si maoni ya CCM wala ya Rais Kikwete. Kwa kusema hivi simuungi mkono mtu wala chama chochote. Simsaliti mtu wala chama chochote. Ni maoni yangu binafsi.. Jambo linalonisukuma kupendekeza serikali mbili ni hofu yangu mimi binafsi, ya changamoto zinazoweza kutokana na serikali tatu. Labda hii inatokana na ukweli kwamba pamoja na kuainisha hoja zenye mashiko za kupendekeza serikali tatu, si tume wala taasisi iwayo yoyote, iliyonishawishi bila shaka, kwa kutoa mchanganuo wa namna gasi hasa serikali tatu zitaendesha nchi hizi mbili, moja ikiwa kubwa sana na nyingine ndogo sana kwa maana ya idadi ya watu na eneo kijiografia, lakini zikiwa sawa kabisa kwa maana ya hadhi na mamlaka ya nchi (sovereignty). Napata shida kufahamu ni kwa namna gani kwa mfano, nchi hizi zitaendeshwa ikiwa kila nchi kati ya hizi tatu itashikiliwa na chama tofauti. Chukulia kwa mfano, CCM wameshika Tanzania, ikiongoza nchi kwa kufuata idikadi ya ujamaa na kujitegemea, Chadema imeshika Tanganyika, ikiongoza nchi kwa kufuata idikadi ya mrengo wa kati na CUF waikabate Zanzibari wakiiendesha kiliberali. Mchanganuo wa washirika wetu wa maendeleo utakuwaje? Misingi ya ukuaji wa uchumi wa nchi zetu utakuwaje? Hizo ni hofu zangu bimafsi tu, hazihusiani na maoni ya chama au kikundi cha watu. Cha ajabu ni kwamba, pamoja na mkanganyiko huo, pamoja na wasiwasi wangu huo, bado najikuta dhamira ikinielekeza kukubali kujaribu mfumo tofauti na huu wa sasa. Dhamira inanisukuma kwenda kusikojulikana kwamba kunaweza kuwa ni mahala salama au hatari. Dhamira yangu inanikataza kubakia mahala ambapo najua kwa hakika si salama. Nina wasiwasi wa kujaribu mfumo mpya ambao sina hakika kama utaniinua kiuchumi, kisiasa na kijamii. Lakini naogopa zaidi kubaki katika mfumo ambao nina uhakika umeshashindwa kuniinua. Pengine mchecheto huu si wangu peke yangu, ni wa watanzania wengi hasa wale wanaopendekeza mfumo wa serikali tatu. Hawana uhakika wa ni nini hasa kitajiri ndani ya mfumo huo, wanajaribu tu. Lakini kwao ni bora zaidi kujaribu mfumo wasio ujua kuliko kubaki katika mfumo wanaoujua, uliojaribiwa kwa zaidi ya miaka 30 na kushindwa mara zote! Mwandishi mmoja mahiri aliwahi kuandka kwenye makala moja wapo, kwamba kuelekea serikali tatu ni sawa na kuonja sumu. Nadhani alikuwa sahihi.Lakini Mtazamo wangu ni kwamba, kuelekea serikali tatu ni jaribio la kuonja sumu ambayo pia inaweza kuwa ni dawa. Kuna wanaodhani ni sumu na kuna wanaodhani ni dawa. Lakini hapa tuna mgonjwa ambaye ameshaugua kwa umri wote wa maisha yake na pengine amebakiwa na siku chache tu kupoteza maisha. Na mbele yake kuna kimiminika chenye utata, kwamba chaweza kuwa sumu au dawa. Afanyeje? Aamini kwamba ni sumu, asinywe na hivyo kujihakikishia kifo au aamue kunywa ili kama ikitokea kimiminika hicho ni dawa apone? Busara itamwongoza huyo mgonjwa kunywa hicho kimiminika. Matokeo ya kufa hayatofautiani na hali yake ya sasa, ya kwamba kwa hakika atakufa. Lakini ikitokea kile kimiminika kikawa ni dawa, atapona. Nashawishika kusema kuwa hapa ndipo tulipofikia kama nchi. Na kwasababu tulikurupuka kuanza huu mchakato, tumejinyima muda na fursa ya kuchunguza kama kile kimiminika ni dawa ama sumu.


4.0 KATUA ZA SULUHISHO

4.1 KUKUBALIANA NA UKWELI


Nini kifanyike sasa? Ni muhimu kujipa muda na fursa ya kuchunguza na kujiridhisha kwa uhakika kama kile kimiminika ni sumu au dawa. Jambo hili laweza kuonekana kama limekuja kwa kuchelewa. Lakini ni vema uchelewe kwa uhakika kuliko kuwahi kwa mashaka. Hatua moja wapo katika kujipa fursa hiyo ni Kujitambua, kama Taifa. Ni lazima Kwanza tukubaliane na hali halisi. Kwamba kwa hapa tulipofikia, hakuna katiba itakayotokana na matakwa ya wananchi, huu ndio ukweli ambao niko tayari kuusimamia kwa viapo vua mababu!...Angalia viashiria hivi, Sheria ya mabadiliko ya katiba ilichezewa mapema, Msimamo wa Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama Tawala uko wazi, Msimamo wa mwenyekiti wa Bunge maalumu hakuna siyeujua. Idadi kubwa ya wabunge wa Jamhuri ni wanachama wa CCM na wale wengine 201 wanaoitwa wawakilishi wa watu wameteuliwa na Rais, ambaye msimamo wake tunaujua. Rais ameshatoa maelekezo kwa wateule wake, ya nini kifanyike. Pili ni lazima tukubaliane na ukweli wa hatari iliyopo mbele yetu, kwamba tutalazimika kuendelea na serikali mbili huku Zanzibar ikibaki na msimamo wa kutaka nchi yake yenye mamlaka kamili, jambo ambalo ndani ya muundo wa serikali mbili haiwezekani. Kufikia hapo, mambo mawili yanaweza kutokea. La kwanza, ni ubabe kutumika kuilazimisha Zanzibar kurekebisha katiba yake (kama inawezekana) ili kuendelea kuwa mkoa maalumu ndani ya serikali ya Tanzania, au watu wachache wa Zanzibar wanaweza kununuliwa ili kusimika matakwa bandia ya wanzanzibari kukubaliana na mfumo wa serikali mbili utakaopoka kwa mara nyingine, mamlaka ya Zanzibar. Hali ikiwa hivyo, iko hatari ya wanzanzibari watakao kuwa hawajaridhika kutafuta njia mbadala ya kujitwalia mamlaka ya Taifa lao. Na kwakuwa wao wana uzoefu wa Mapinduzi, sidhani kama litakuwa suala gumu kwao….Mola aepushie mbali.


4.2 MUAFAKA WA KITAIFA

Tukishakubaliana na ukweli halisi na kujitambua katika mapana hayo, twende hatua ya pili, ambayo ni kutafuta muafaka wa kitaifa. Jambo la kwanza tunaloweza kufanya katika mazingira haya ni kuvunjwa kwa Bunge maalumu la katiba, kwanini? Kwasababu tunajua matokeo ya mchakato kabla hata hawajaanza kazi. Tunabashiri kwamba matokeo ya Bunge hili hayataakisi matwakwa ya wananchi walio wengi. Na hapa ndipo ninaposhangaa hata wapinzani wanafanya nini Bungeni wakati matokeo yako ubaoni. Pia, ni maoni yangu kuwa tumewapa wangunge maalumu kazi wasiyoiweza. Tumewapa kazi ya kuchambua Rasimu, lakini hawa wabunge sio wataalamu wa masuala ya katiba au muundo wa muungano, kwa maana ya sifa za uteuzi au kuteuliwa kwao. Tuliteua au kuchagua wawakilishi, sio wataalamu. Ni kweli, miongoni mwao wanaweza kuwepo wataalamu wachache, lakini hawapo Bungeni kwa madhumuni mahsusi ya kitaalamu, hasa katika masuala ya Katiba na hivyo hawalazimishwi sana kutumia utaalamu wao kwa maufaa ya wote. Hii ndiyo sababu tumeshuhudiambunge mmoja akatafsiri kanuni kwa manufaa ya kundi lake na mwingine akiibuka kwa hasira, kupinga, naye kwa manufaa ya kundi lake. Ingawa wako miongoni mwao ambao ni wataalamu, lakini mienendo na madhumuni ya uwepo wao Bungeni si ya kitaalamu.


Nashauri iundwe timu huru ya wataalamu mahiri wa ndani na nje ya nchi. Wataalamu wa masuala ya sheria, uchumi, Diplomasia, sayansi ya jamii n.k Timu hii ipewe jukumu la kuratibu upya mjumuisho wa maoni na sababu za maoni yote yahusianayo na muungano na muundo wa muungano. Mada yao iwe ni muungano tu. Timu hii ipewe uhuru kamili na tujiridhishe haiingiliwi na mkono wa dola wala vyama vya siasa. Timu hii itoke na mapendekezo ya kitaalamu, yenye kubeba suluhisho la muungano wetu na muundo wa serikali. Timu ianinishe umuhimu na faida za muungano, kama zipo. Swali la kwanza wanalotakiwa kujibu ni kwa kiasi gani na kwanini watu wa Tannganyika na Zanzibar ya sasa, bado wanauhitaji muungano. Kisha timu hii ichambue kitaalamu, muundo mmoja baada ya mwingine, kwa kutolea mifano nchi yoyote iliyounda mfumo mmoja wapo na kufanikiwa ama kufeli. Ichambue kitaalamu lakini kwa lugha rahisi sana, namna serikali itakavyoweza kuendeshwa ndani ya kila mfumo. Ianishe faida na hasara za kila mfumo, kwa kulinganisha na hali halisi ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania. Halafu mapendekezo ya timu hii yapigiwe kura na wananchi, ili wananchi ndio wachangue mfumo wa Muungano, kwa kuzingatia elimu waliyoipata ambayo kwa sasa hawana wala hawakuwa nayo wakati tume ikikusanya maoni, kwa mara ya kwanza. Matokeo ya kura yarudishwe bungeni ili bunge maalumu, litakaloundwa tena litengeneza katiba kwa kuchanganya na masharti mengine yasiyo na utata yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo kimsingi ni maoni ya wananchi ambayo hayahitaji tena kupigiwa kura na wananchi. Tukitaka ufanisi zaidi ni muhimu kufanyia marekebisho Bunge maalumu litakaloundwa mara ya pili. Tunaweza kubadili muundo wake kwa kuondoa ushiriki wa wabunge wote wa Jamhuri na wale wa Baraza la wawakilishi. Bunge, kama taasisi, linaweza kupewa nafasi ya kuteua wabunge wasiopungua 50 na wasiozidi 100 kutoka vyama vyote bara na visiwani. Wakaungana na hao 201 walioteuliwa na Raisi, ambao mimi sina shaka nao hata wakiendelea hawa waliopo sasa. Jumla tutakuwa na wawakilishi 251 au 301 wa wanachi. Ili hili lifanyike vema, ni muhimu kufanyia marekebisho, kwa hati ya dharura, sheria ya mabadiliko ya katiba, ili kuondoa baadhi ya kasoro za kisheria, kusimika wazi na rasmi mamlaka ya Bunge maalumu la kutunga katiba, kuondoa mtitiriko ukioko sasa na kuweka mpangilio mpya wa ushiriki wa kura ya maoni kwa suala la muungano pekee na kwamba Bunge maalumu la katiba ndilo lipewe kazi ya kutengeneza na kupitisha katiba ya Mpya.


Jambo la pili tunaloweza kufanya katika mazingira ya tahadhari ni kukubali kwamba Bunge hili liendelee na kazi waliyonayo, lakini matokeo ya bunge hili na yale ya kura ya maoni kwa utaratibu wa sheria ya sasa, yawe ni ya mpito, katiba itakayozaliwa sasa isiwe ni katiba ya kudumu. Kwa hiyo, ni muhimu katiba hii iwe nasharti linalozingatia umaalumu wake. Tunaweza kujipa muda, kama wa mika mitatu hadi mitano ya kujipima. Ili kutoa fursa kwa majaribio endapo bunge na wananchi watapitisha mfumo mgeni na ambao pengine waweza kuleta changamoto zizizobebeka, muda mfupi baada ya kuutumia. Ushauri wangu hapa ni kutengenezwa kwa katiba ya mpit (Interim Constitution) . Na katika kipindi cha muda tuliojiwekea kwenye katiba, tunajipa nafasi zaidi ya mdajala. Utafiti, elimu na kujiridhisha bila shaka yoyote. Haraka tuliyonayo sasa inatokana na tama ya kizazi hiki kufaidia na matunda ya katiba mpya. Tunasahau kwamba katiba tunayoiunda ni kwa manufaa yetu na kwa manufaa ya vizazi vingi vijavyo. Tunatengeneza katiba ambayo watu watakaoishi Tanzania miaka 200 ijayo watafaifiaka nayo. Tusitengeneze katiba kwa lengo tu la kukiondoa chama kilichomo madarakani au kwa lengo la chama kilichopo madarakani kujihakikishia kuendelea kutawala. Tuwe na maono makubwa zaidi kwa maslahi mapana zaidi.

5.0 HITIMISHO
Haya ni maoni yangu ambayo natamani kila mtanzania ayasome, kuyatafakari na kuyajibu binafsi. Natamani Rais Jakaya Kikwete asome aya kwa aya, mstari kwa mstari na neno kwa neno. Natamani viongozi wa serikali, vyama vya siassa, viongozi wa didi, taasisi za kiraia, wasomi, wanafunzi, wakulima, wafanya biashara, wasome maoni haya. Tuko katika kipindi nyeti mno katika historia ya nchi yetu. Ni muhimu kila mwenye mawazo akayaweka hadharani, akashirikisha ili sote kwa pamoja tushibe ufahamu na maarifa kuelekea kwenye kutengeneza na kujenga nchi iliyo bora. Tunapojaribu kutoa maoni yetu, tunaonesha upendo wetu kwa nchi, uzalendo wetu na kutimiza wajibu wetu kama raia wema. Kazi hii ni kubwa, si kazi ya mtu mmoja au kikundi cha watu. Si kazi ya Rais wa nchi walawanasiasa peke yao. Ni kazi inayopaswa kufanywa na kufuatiliwa na kila Mtanzania mwenye mapenzi mema. Hivyo, ingawa tuko katika hatua inayoonekana kama ni hatua ya kwenda mbele na sio kurudi nyuma, tusiache kutoa maoni tunayodhani yana manufaa na msaada kwa mwelekeo chanya wa Taifa letu. Inawezekana kujenga Tanzania imara kama kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake. Na tutimize wajibu wetu. Mungu Ibariki Tanzania na watu wake.


Imeandikwa na

Robert Victor Lengeju
Morogoro-Vijijini
+255 715901001/ 762341522
rlengeju@gmail.com
 
Walizoea sana kuvuruga na kutufunika macho lakini bahatimbaya Watanzania waleo wameona shule kuwadanganya ni ngumu.Kusema kweli hakukuwa nania ya dhati ya katiba mpya na bora ila kulikuwa na nia ya katiba mpya ila iliyo mbovu zaidi kwa manufaa ya utawala
 
Ni lazima wananchi tujitwalie fursa hii adimu ya kujenga nchi yetu..tusiwaachie wanasiasa kazi hii ngumu na muhimu mno!
 
JK mwenyewe ni kama alikuwa ana-test zari, then akakuta watu wamejipanga vilivyo, yeye mwenyewe akachomoa betri na kujizima data kama sio yeye...

Kiukweli alitukosea saana watanzania, rasilimali za taifa zikatumika ndivyo sivyo, ni mambo ya Kihuni tulifanyiwa.
 
Back
Top Bottom