Tujikumbushe kidogo kizaa zaa cha Sakata la IGP Mahita na Chama cha CUF

Konzo Ikweta

JF-Expert Member
Oct 3, 2013
735
1,464
MIAKA hiyo ya 2000, uliibuka mgogoro mkubwa sana kati ya Chama cha CUF na Inspekta jenerali wa jeshi la Polisi, Omar Mahita wakati huo chama cha CUF kilikuwa ni chama kikubwa sana cha pili tukiacha kile cha CCM ambacho kilikuwa na ndicho mpaka leo ni Chama namba moja kwa ukubwa nchini Tanzania.

Kizaazaa chenyewe kilianzia pale Mahita alipokituhumu Chama cha CUF kwamba kilikuwa nyuma ya ongezeko la vitendo vya ujambazi vilivyopamba moto nchini miaka ile. Kwamba kwa jinsi fulani Chama hicho kilikuwa kikiendesha kwa siri vitendo hivyo ili kuikomoa Serikali ya Kikwete ,baada ya kushindwa Vibaya katika uchaguzi Mkuu uliopita.

Lengo kuu likiwa kuiharibia haiba yake mbele ya jamii ya watanzania, akaongeza pia kwamba ajenda nyingine ya CUF ilikuwa kumchonganisha yeye Mahita na Rais Kikwete ili aonekane hafai, kwa vile ama ameshindwa kudhibiti uhalifu na hasa ujambazi, au anaihujumu Serikali kwasababu ambazo hazikupata kuwekwa wazi.

Miongoni mwa mbinu zilizokuwa zikitumika kwa Maelezo ya Mahita ni pamoja na kueneza Uvumi mitaani kwamba yeye binafsi anashirikiana moja kwa moja na majambazi. Akaweka wazi kwamba uhasama wote huo ni kwa vile CUF inamtuhumu yeye kuwa alichangia kwa kiasi kikubwa katikati kushindwa kwao uchaguzi.

Mwishoni akaonekana kuchomwa na maneno yake, akaweka wazi kwamba yeye angeondoka madarakani kwa nguvu za Mungu pekee na kuwa haogopi mtu yeyote ,tena Akashindwa kujizuia akisema kwamba CUF kamwe haitaweza kuingia Ikulu hata kama yeye hatakuwepo Polisi.

Baada ya hotuba hiyo ya kushtusha ,sio CUF pekee waliotoa misimamo yao ,hata wanasiasa wa vyama vingine waliingilia kati na kuitaka Serikali kuunda tume kuchunguza tuhuma hizo ili sheria iweze kufuata mkondo wake. Kwa upande wao CUF waliibuka kwa nguvu na kufanya maandamano makubwa wakimtaka Rais amtimue kibarua Mahita mara moja. Kadhalika waliahidi kwenda mahakamani kufungua kesi dhidi yake kwa kuchafuliwa jina mbele ya jamii.

Kwa upande wake Serikali haikusema lolote zaidi ya kukana kuhusika na maneno ya Mahita kupitia Waziri wa wa usalama wa Raia .Baada ya hapo ikafuatia mikanganyiko zaidi ndani ya jeshi la Polisi. Kwanza ni juu ya utajiri binafsi wa Mahita na jinsi alivyoupata ,Lakini zaidi umri wake na tarehe ya kustaafu kwake.

Tukasikia kupitia aliyekuwa msemaji wa jeshi la Polisi, Aden Mwamunyange ,Kwamba Mahita alikuwa amemwandikia Rais barua tangu mwaka 2005 akiomba kustaafu. Mwamunyange akaitaja tarehe rasmi ya kustaafu kwa bosi wake ,huku akitoa vielelezo vya umri na tarehe yake ya kujiunga na jeshi .

Ilikuwa iwe tarehe nne mwezi wa tano mwaka 2006 Hata hivyo tarehe hiyo ikabatilishwa tena na Mahita akastaafu kabla. Wachambuzi wa mambo walisikika walidai kwamba , "Katika akili za kawaida tunaweza kabisa kuamini kwamba Mahita alistaafu chini ya shinikizo fulani. Kadhalika tunaweza kukisia sababu kwamba kama sio sakata lake na CUF ,basi ni tuhuma zilizokuwa zikimkabili juu ya kuulea uhalifu nchini. Au Serikali kuamua kumaliza mizozo kwa busara ya kuung'oa mzizi wa fitina, yote yanawezekana."

Kwa vyovyote hili ni miongoni mwa sakata zito zilizowahi kuikumba nchi yetu na si vyema kulisahau bila kukumbushana kidogo kwa wale ambao hawakulisikia. Tukichukulia kipindi hicho CUF kilikuwa ni chama kikubwa sana cha pili baada ya CCM,

Katika sakata lile ulikuwa ni mzozo ulioanzia sio baada ya hotuba ya Mahita wala baada ya uchaguzi Mkuu kama alivyodai Mahita, lakini zaidi mzozo wao uliwaathiri zaidi wananchi wa Tanzania kuliko ulivyowaathiri wao wenyewe. Mzozo wao ulikuwa ni mzizi mrefu ulioanzia mbali ambao ulikuja kuchipua tu pale upande mmoja ulipozidiwa mbinu za mapambano ya kimya kimya na kuamua kutumia jazba na makelele ,ambayo moja kwa moja yaliupa turufu upande mwingine.

Kipindi kile CUF Ilikuwa imesheheni wasomi wajuzi wa hila, wanatafakuri, na wanasiasa wazoefu, pia Mahita hakuokotwa barabarani kuwa IGP, ana Historia ndefu ya utumishi wa umma uliojaa uwezo wa uongozi, uadilifu, uzoefu na kila sifa kumfanya Rais amteue yeye miongoni mwa mamia ya waliokuwepo ndani ya jeshi la Polisi.

Sakata hili lilipamba moto tukiwa katikati ya simanzi juu ya ongezeko la ujambazi nchini, lililoitia Serikali hasara ya mabilioni ,Lililopoteza roho za watu wengi wakiwa vilema ,yatima au wajane hata leo. Katika kutafuta mchawi ndipo wakubwa hawa walipoanza kutajana.

Minong'ono ikaenea mitaani kwamba Mahita yuko nyuma ya uhalifu huo, Naye akaweka wazi kwamba anawajua wanaoeneza minong'ono hiyo ,na sababu za kufanya hivyo. Akakitaja chama cha CUF kwamba ndio wahusika wakuu wa ujambazi huo, na akatoa Ushahidi mintarafu wa visu vilivyokamatwa na jeshi lake vikiingizwa nchini na chama hicho.

Wachambuzi wa mambo waliwahi kuhoji, ni nini kilimsukuma Mahita kutamka jambo la hatari kama lile ambalo hata Serikali yenyewe ilikana kuhusika nalo. Pamoja na Historia ndefu ya uongozi wa kijeshi iliyojaa sifa lukuki ,lakini wachambuzi wa mambo waliwahi kudai kwamba Mahita alikuwa na tatizo la kuropoka, mara nyingi alionyesha kushindwa kuzuia jazba yake na kujikuta akiropoka mambo yaliyomtia mara kadhaa katika mizozo ,hata kama aliyoyasema yalikuwa na ukweli ndani yake.

Pia aliwahi kuwa na mzozo na wabunge ambao aliwataka wakatwe posho zao wakalipwe askari Polisi, baada ya kutokea malumbano fulani ya kiutendaji, Mahita hakupenda kuonekana mwoga kwa mtu yeyote Huku akitumia nguvu ambazo mara nyingi zilimfanya anase kirahisi katika mitego ya wanasiasa.

Alipoamini kwamba haki ipo upande wake hakujizuia kuinadi yaani aliamini zaidi nguvu ya ukweli na haki kuliko taratibu za uendeshaji. Ilielezwa kwamba haya yote yalimfanya Mahita kila siku awe Katika mizozo ,iwe na taasisi au mtu binafsi, mbaya zaidi mara nyingi alijikuta amesimama peke yake kama Mahita na siyo kama IGP ,ukimsikiliza miaka yake katika hotuba yake iliyoukuza mzozo wake na CUF, utasadiki hili.

Hakuwa akiongea kama mkuu wa jeshi , ila binafsi kama Mahita, hata hivyo Mahita ,mengi aliyoeleza akiwa IGP yalikuwa na ukweli ndani yake ,yalifuatia uchunguzi wa kina wa jeshi la Polisi na alisema akiwa na uhakika wa kutosha, tatizo lake lilibaki palepale katika kutojali taratibu za utendaji zilizomweka kwenye migogoro kadhaa.

CUF mara nyingi walikuwa wakimlaumu kwa kutowatendea haki kwamba alitumia jeshi kuwakandamiza kwa operesheni Kali za kijeshi pamoja na kuwanyanyasa viongozi wao. Hivyo katika mazingira hayo hatuwezi kuamini wangeweza kuwa na uswahiba na Mahita, hatuwezi kudhani walipenda aendelee kuwa madarakani.

Kwa upande mwingine haikuwa mara ya kwanza kwa CUF kulaumiwa kwa Kwenda kinyume cha taratibu za vyama vya siasa tulizojiwekea ,wala Mahita sio wa kwanza kutamka hadharani kwamba CUF ni chama cha kijambazi ,wengine walishafika hata mahakamani kumshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakihoji kwanini anaruhusu chama cha kigaidi nchini mwetu.

Kilishalaumiwa mara nyingi miaka hiyo, kujihusisha na mambo ya udini, kule visiwani kilisemwa kuwagawa wananchi kwa Sera za upemba na Uunguja ,kikasemekana kumiliki vikosi vya "Blue Guard" ambavyo vilituhumiwa kwenda mbali zaidi ya ulinzi wao binafsi na viongozi wao.

Tanzania ilishuhudia vurugu zilizopelekea mauaji ya januari 27 kule Pemba . Kadhalika ilishuhudiwa mara nyingi maandamano na fujo za ovyo za Vijana wa CUF zilizobarikiwa na viongozi wao.

Wachambuzi wa mambo waliwahi kueleza kwamba, Iliwezekana kuwa Mahita baada ya kubanwa ,alitumia silaha ya kisiasa ili kuwagawa wananchi walioanza kuungana kifikra dhidi yake, akaona kwa kuihusisha CUF na hujuma dhidi ya Serikali ingekuwa rahisi kuaminika na zaidi kujipatia ulinzi toka kwa vyama pinzani na hasa CCM pamoja na kulalia kwa Serikali aliyodai anatuhumiwa kuiingiza madarakani kwa hila zake ,kwa bahati mbaya hakufanikiwa.

Hata hivyo baada ya mzozo wa muda mrefu Mahita alistaafu katika namna ambayo mpaka sasa haipo wazi sana kwa wananchi, na tangu hapo hatukusikia tena mzozo ule kuongelewa. Sio na Mahita ,CUF wala Serikali yenyewe.


*World Stories Group The Home Of Great Stories Whatsapp 0623782805*
IMG-20200903-WA0004.jpg
IMG-20200903-WA0005.jpg
 
Bora cuf walimiliki majambia ila Chadema ya lissu imewaahidi Mabeberu kutuuza Watanzania

Tuwaogope Chadema km ukoma
 
Back
Top Bottom