Tujifunze kwa taharuki ya Dar juzi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tujifunze kwa taharuki ya Dar juzi

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, Apr 17, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Apr 17, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,613
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Maoni ya katuni


  Jana katika safu hii tuliandika tahariri ikikumbusha umma juu ya umuhimu wa kujiandaa kwa majanga yawe ya asili au hata ya kusababishwa na binadamu.

  Tulisema kuwa majanga mengi yanayotokea nchini, kama ya mioto, mafuriko na hata ajali za magari yanathibitisha kwamba uelewa wa watu wetu kwa ujumla juu ya kinga ya matukio kama hayo ni mdogo sana na hata pale janga linapotokea, basi njia za kukabiliana nalo imekuwa si yenye ufanisi wa kutosha kiasi cha kusaidia ama kuokoa maisha au mali.

  Tulizungumzia majanga hayo kwa kukumbushia matukio ya hivi karibuni kabisa ya moto, ule uliotokea jijini Arusha ukikumba baa ya Pentagon na nyumba moja yenye maduka manane, ambazo ziliungua na kutekekea kabisa.

  Tulisema kuwa tukio la Arusha lilitokea siku chache tu baada ya janga jingine la moto kutokea katika soko kuu la samaki la Feri, Dar es Salaam, ambao uliunguza sehemu ya paa la soko hilo sehemu ambayo samaki hukaangwa na wachuuzi. Kwa soko la Feri tukio hilo lilikuwa ni tatu, madhara yake kwa uharibifu wa mali yamekuwa ni makubwa sana.

  Kabla hata wino ulioandika tahariri ya jana haujakuka, jana hiyo hiyo Jiji la Dar es Salaam lilikumbwa na taharuki kubwa. Hii ilisababishwa na tangazo la Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kwamba Jiji hilo na mikoa yote ya pwani ya bahari ya Hindi ilikuwa katika hatari ya kukumbwa na tsunami kutokana na tetemeko la ardhi la chini ya bahari lilitokea nchini Indonesia.

  Ingawa baadaye hadhari hiyo ilipunguzwa kiwango cha hatari yake baada ya taarifa za madhara ya tsunami na kimbunga hicho kupunguzwa, hali ya usalama katika jiji la Dar es Salaam hasa barabara kuu ilikuwa ya taharuki kubwa.

  Kwa hakika baada ya taarifa za tsunami kutolewa watu wengi wanaofanya kazi katika ofisi mbalimbali katikati ya mji na shughuli nyingine za biashara walifunga na kuanza kuukimbia mji kuwahi nyumbani kwao nje ya katikati ya mji.

  Hali hii ikichangiwa na mvu zilizonyesha kwa wingi juzi jijini Dar es Salaam, ilisababisha msongamano mkubwa mno wa magari. Kwa ujumla barabara zote za kutoka katikati ya mji kwenda pembezoni zilikuwa hazipitiki, kwa maneno machache tunaweza kusema kuwa mji ulisimama kwa saa kadhaa.

  Katika mazingira hayo, wale wote waliokuwa wameitikia wito wa hadhari ya TMA na kuamua kuondoka ofisini mapema, hawakuwahi kufika nyumbani kwao maeneo mbalimbali ya mji kwa sababu magari yalikuwa hayasogei. Hali ilikuwa ni ya wasiwasi mkubwa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

  Jana tulisema kuwa kama taifa tuna tatizo katika kujipanga kukabiliana na majanga, tulitoa mfano wa vikosi vya Zimamoto na Uokoaji kuwa utendaji wake ni wa kiwango cha chini sana; hawana vifaa, weledi duni na hata ari ya kutenda kazi ni ya chini sana. Kwa kifupi vina hali mbaya

  Mara nyingi vikosi hivi havifanikiwi kuzima moto kabla ya ama kulete madhara au kuteketeza kabisa nyumba au kokote unakowaka. Sababu ni nyingi za udhaifu huu, lakini itoshe tu kusema kuwa hali yetu kama taifa ni mbaya katika utayari wa kukabili majanga.

  Sasa katika hali ya juzi ya tahadhari ya tsunami, huku magari barabarani yakikwama kwa saa kadhaa maana yake ni kwamba wale wote walioitikia wito wa kuchukua tahadhari kama vile kuondoka karibu na fukwe za bahari, wasingefanikiwa kujiokoa kama kweli tsunami hiyo ingelipiga jiji la Dar es Salaam kama ilivyokuwa imebashiriwa awali.

  Isingekuwa ajabu kuona watu wakibebwa na mawimbi ya bahari eneo lote la barabara ya Ocean, Ali Hassan, Old Bagamoyo, Kurasini Shimo la Udongo (Bandari) na kokote barabara inakopakana na bahari kwa kuwa magari yalikuwa hayatembei.

  Hali ya Juzi ni kielelezo cha juu kabisa kuwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam wamekalia bomu kwa sababu ya mfumo wa miundombinu. Barabara za jiji hili ni nyembamba sana kiasi kwamba haziwezi kwa vyovyote vile kuhimili wingi wa magari na watumiaji wengine wa barabara hizo, ndiyo maana juzi hata pikipiki hazikufua dafu katika msongamano uliosababishwa na taharuki ya kuikimbia tsunami.

  Usimamizi wa magari barabarani juzi ulikuwa wa kiwango cha chini kabisa, kwa ujumla hali iliyojitokeza inatukumbusha sote kuwa kama hatutajipanga vizuri hakika huko tuendako tutalipukiwa na bomu baya kwa kuwa mpangilio wa miundombinu yetu ni duni mno. Tujiulize tumejifunza nini kwa hali ya juzi jijini Dar es Salaam na kuchukua hatua sasa.

  CHANZO: NIPASHE

   
Loading...