SoC03 Tujibu Ripoti ya C.A.G

Stories of Change - 2023 Competition

Dira Yetu

New Member
May 10, 2023
3
5
Ripoti ya mwaka ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Tanzania kwa mwaka wa fedha 2021/22, ilibainisha mapungufu mbalimbali katika nyanja tofauti za uendeshaji wa Serikali. Hii ni ishara tosha kuwa, kuna haja ya kutafuta njia mbadala na makini za kutatua changamoto hizo ili kuhakikisha na kuimarisha ufanisi wa utendaji wa Serikali kuwa bora na wenye tija kwa wananchi na Taifa.

Katika andiko hili, zitajadiliwa njia mbadala za kutatua changamoto hizo zilizobainishwa na Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Utendaji usioridhisha wa menejimenti wa Uwanja wa Taifa wa michezo wa Benjamin Mkapa. Uchakavu wa miundombinu, usalama na ubovu wa mitambo ya umeme. Njia madhubuti za kuhakikisha viwanja vya michezo vinadumu kwa muda mrefu kiusalama na kimiundombinu kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo izingatie vile viwango vya ubora kimataifa kama kiwango cha kimataifa kinachohusiana na usimamizi wa ubora ISO 9001, kiwango cha mataifa kuhusiana na usimamizi wa mazingira ISO 14001, kiwango cha kimataifa kinachohusiana na usimamizi wa afya na usalama ISO 45001, The Green Guide, The International Building Code kulingana na shirika la kimataifa linalotoa viwango vya kuboresha ujenzi na matengenzo ya viwanja vya michezo ASTM International.

Halikadhalika Wizara itumie vifaa bora na teknolojia kama vile teknolojia ya Laser, teknolojia ya mifumo ya usambazaji na uthibiti umeme, matumizi ya nyasi bandia na miundombinu ya usafi kama vile vyoo, mfumo wa kamera za usalama, mifumo ya utoaji tahadhari na uthibiti wa majanga ya moto na vitendo vya uhalifu.

Usimamizi wa deni la Serikali. Kuna njia kadhaa ambazo wananchi na viongozi wa Serikali wanaweza kufuata ili kuhakikisha kuwa nchi inalipa madeni yake ya ndani na nje na kujikwamua kutoka kwenye mzigo wa madeni hayo licha ya jambo hili kuhitaji muda mrefu, nia na juhudi.

Mfano, kupitia utawala bora na uwazi katika usimamizi wa rasilimali za umma, kuongeza mapato ya Serikali kupitia kutoza kodi kwa ufanisi na kuhakikisha zinatumika kwenye mahitaji yenye tija zaidi, kuweka sera na sheria za kodi zinazofaa, kuvutia uwekezaji, kuzidisha uzalishaji wa bidhaa za ndani kwa kuhimiza sera ya viwanda na kukuza sekta ya utalii na kilimo, kudhibiti matumizi ya serikali kwa kuzingatia vipaumbele vyake vya maendeleo, kurekebisha sera za kiuchumi na kupanga bajeti za kisasa itakayosaidia kupunguza matumizi ya serikali na badala yake kuibua vyanzo stahimilivu vya mapato ya serikali.

La muhimu zaidi kuzingatias ni kuhakikisha matumizi stahiki ya mikopo hiyo hasa katika miradi yenye tija na manufaa kuwezesha ulipaji wa madeni hayo.

Ukosefu wa ajira na tatizo la upungufu wa watumishi wa umma. Hatua zifuatazo zizingatiwe ili kutatua changamoto ya ajira katika kumeneji rasilimali watu kupitia Wizara ya Kazi na Ajira kwa kushirikiana na Sekretarieti ya ajira.

Hatua hizo ni pamoja na kuhamasisha ujasiriamali kupitia Tanzania Entrepreneurship Network, pia Serikali iweke sera na mipango ya kukuza uchumi wa kijani kwa kukuza sekta mbalimbali kama kilimo, uvuvi, viwanda, utalii, kuboresha sera za kodi katika sekta za uzalishaji ili kuvutia wawekezaji wapya na kuongeza ushindani katika soko la kimataifa, kuweka sera za kulinda watumishi na kuhamasisha maendeleo ya jamii.

Pia Wizara ya Kazi na Ajira kwa hisani ya Serikali kuu kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iwekeze katika elimu na kuhamasisha uvumbuzi na teknolojia kwa kufadhili tafiti, mafunzo na ukuzaji wa fani. Pia ipunguze urasimu na kuongeza ajira katika sekta ya umma na itoe ruzuku na misaada kama motisha kwa makampuni ili kuajiri watu wengi zaidi pamoja na ruzuku kwa wafanyabiashara wadogo.

Hasara zitokanazo na uendeshaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) zinaweza futiliwa mbali kwa kudhibiti matumizi na kupunguza gharama za rasilimali za Shirika ikiwa ni pamoja na mafuta, wafanyakazi na vifaa vya ndege.

Pia, kwa kutafuta njia za kuboresha ufanisi na kupunguza na kuongeza mapato. Halikadhalika, Uongozi wa Shirika la Ndege la Tanzania inabidi isimamie rasilimali watu kwa kusimamia malipo na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi ili waweze kufanya kazi kwa weledi. Vilevile, Uongozi usimamie mtandao wa ndege wa kimataifa ili kuongeza mapato na kuimarisha ushindani.

Hii ni inajumuisha kuongeza idadi ya vituo vya ndege, kuongeza idadi ya safari, kuboresha huduma kwa wateja na kuendeleza teknolojia ya ubunifu kwenye tasnia ya ndege. Lakini pia, Uongozi wa Shirika la Ndege la Tanzania ijenge na kusimamia mikakati ya masoko ili kuongeza mauzo yake na kushindana na mashirika mengine ya ndege. Hii inajumuisha kuongeza idadi ya wasafiri, kubuni sera za bei na kufanya kazi na wadau wa tasnia ya utalii.

Aidha, Shirika la Ndege la Tanzania lianze kuwekeza katika masoko ya uuzaji wa bidhaa na huduma zao ili kuongeza ushindani. Hii ni pamoja na kutoa ofa na punguzo kwa wateja, kupitia kampeni za matangazo na kushiriki katika matukio ya kibiashara na kuhakikisha Shirika linajenga ushirikiano na washirika wengine wa maswala ya usafiri wa anga na wadau wengine kama vile mahoteli, makampuni ya kukodisha magari, na wahudumu wengine wa usafiri.

Mwisho, hizi ni baadhi tu ya hoja za CAG nilizozijibia mapendekezo katika uchambuzi wa ripoti ya mwaka ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Tanzania kwa mwaka wa fedha 2021/22. Ni jukumu la Serikali na wadau wote kushiriki kutatua changamoto hizi ambazo zinahitaji mikakati ya kina na thabiti na usimamizi mzuri wa rasilimali na bajeti.​
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom