Tujenge utamaduni wa kufuata sheria

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Miongoni mwa mambo yanayokera katika miji mingi ya nchi hii ni utaratibu usiozingatia sheria wala kanuni wa wachuuzi wanaovamia maeneo ya kandokando ya barabara, sehemu ya waenda kwa miguu, kwenye vituo vya mabasi na hata mbele ya malango ya kuingia kwenye majumba mbalimbali na kuyafanya kuwa ni maeneo yao ya kutafuta riziki.
Ni kweli riziki ni popote, lakini popote huko ni lazima wakati wote utafutaji uzingatie sheria kanuni na taratibu; kwa kufanya hivyo wote, wachuuzi na wateja wao wataishi kwa maisha ya amani na staha.
Juzi Rais Jakaya Kikwete akiweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa barabara New Bagamoyo kutoka Mwenge hadi Tegeta yenye urefu wa Km 12.9, miongoni mwa mambo yaliyojitokeza ni hoja dhaifu zinazojengwa na baadhi ya wafanyabiashara waliovamia maeneo ya pembezoni mwa barabara na kudai kwamba eti wameruhusiwa kufanya hivyo kwa amri ya Rais ya kuitaka Wizara ya Ujenzi isifanye ubabe katika kubomoa waliovamia kwenye eneo la hifadhi ya barabara.
Baada ya kauli ya Rais tulitoa kauli katika safu hii, tukisema ‘kweli bomoabomoa iwe na utu’ bado tunasimamia kauli yetu kuwa zoezi hili liwe na utu, lakini haiingii akilini kwamba watu wamepanga bidhaa zao kwenye maeneo ya pembezoni mwa barabara, kwenye vituo vya mabasi, kwenye eneo la waenda kwa miguu na hata kwenye malango ya kuingia katika majengo ya watu eti wadai wameruhusiwa kufanya hivyo.
Tunakumbuka Rais alifafanua kauli yake kwamba kuna maeneo Wizara ya Ujenzi ilizembea hadi watu wakavamia hifadhi ya barabara; lakini pia kuna maeneo mengine mabadiliko ya sheria na kanuni za barabara yamesababisha watu wengine kujikuta wakiangukia kwenye hifadhi ya barabara.
Rais alitaka watu wa namna hiyo wapewe muda wa kuondoka na utafutwe uwezekano wa kuwafidia kwa sababu kimsingi barabara imewafuata na si wao walioifuata barabara.
Leo tunajitokeza tena kuunga mkono hoja hiyo, tukisisitiza kwamba bomoabomoa iwe na utu kwa maana ya kutazama mazingira yote kuwa walioko kwenye hifadhi ya barabara walifikaje na kisha hatua stahili zichukuliwe. Tunaweka msimamo wetu wazi kabisa katika hili.
Lakini tungependa kuwaeleza wale wote wanaotaka kuchukulia maelekezo haya kiujanjaujanja ili kuendelea kuvunja sheria kama hawa ambao wanaendesha uchuuzi kwenye eneo la barabara la waenda kwa miguu, au kugeuza vituo vya mabasi kuwa masoko kama ilivyo pale Mwembechai, Kagera, Ubungo, Mbezi Mwisho, Tegeta kutaja kwa uchache tu, si watu wa kufikiriwa katika agizo la Rais. Hawa wanatakiwa waondoke mara moja.
Wanatakiwa waondoke mara moja iwe kuna mradi wa upanuzi wa barabara au hakuna. Hawa wanachangia makali ya kero ya msongamano wa magari jijini Dar es Salaam. Ukiukaji wa sheria wa kiwango hiki haukubaliki hata kidogo.
Sote tunakumbuka kuna wakati Jiji la Dar es Salaam lilikuwa na mpangilio na watu kuheshimu sheria, hii ilitokea wakati wa Tume ya Jiji, lakini pia wakati wa utawala wa Mkuu wa Mkoa Abbas Kandoro.
Operesheni kabambe ilifanyika kusafisha vurugu za uchuuzi zilizokuwa zimebisha hodi hadi lango la Ikulu.
Tunafikiri alichosema Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, juzi mbele ya Rais kwamba wapo watu watakaomfuata kumlilia kuwa wanabomolewa awapuuze kwa sababu wamekiuka sheria na kanuni za barabara, ni jambo sahihi katika kutibu janga hili la watu kutaka tu kukaa mjini bila kufuata sheria na kanuni.
Pia tunafikiri wakati umefika sasa wa Halmashauri za Manispaa za Dar es Salaam; yaani Kinondoni, Ilala na Temeke, kujifunza kwa manispaa nyingine kama ya Moshi katika kusimamia taratibu na sheria za ukazi wa mijini.
Ni aibu na fedheha kwa manispaa hizi miaka na miaka kushindwa hata kusimamia sheria ndogo ndogo za kuwadhibiti wachuuzi ambao kila uchao wanaota kama uyoga kila kwenye upenyo huku wakiongeza kero kwa watumiaji wengine wa barabara. Hawa nao kwa hakika ni lazima waelekezwe na ikibidi walazimishwe kufuata sheria, hatuwezi kuendelea kuishi mijini kwa kuhama na tabia za vijijini.
Wakati sasa umefika wa kuleta mabadiliko ya kweli kwa wakazi wa mijini, kubwa ni kuishi kwa kufuata sheria; kama kutokutupa taka ovyo, kuheshimu maeneo yaliyotengwa kwa shughuli maalumu, kutambua kwamba bila kufuata taratibu tunajitengenezea maafa yetu wenyewe.
 
Kama wanaotunga sheri na kutakiwa kuzisimamia wanajichanganya sisi wananchi tufanyeje? tatizo hapa ni mfumo mzima wa sheria na kiutawala,mfano kama waziri baada ya kusimamia sheria anaambiwa ni kosa huku uswazi tumfate nani?anayesimamia sheria ama anayeionea sheria huruma?
 
Jiji la Dar es Salaam ni chafu,mno,fujo kila mahala barabara ndio zimekuwa gereji,viwanja vya wazi gereji,viwanja vya wazi ni bar na makontena,hakuna ustaarabu kabisa yaani hata mameya,madiwani,wabunge,wakurugenzi ,maafisa afya,waganga,wahandisi,wapima mji,maafisa ardhi,afisa biahsara,watendaji wa kata wenyeviti wa serikali za mitaa wa mkoa wa Dar es Salaam,hovyo,hovyo kabisa,hawana ubunifu watu waliochoka kifikra,kazi yao kuuza sura tuu,wameshindwa kabisa kusimamia sheria,kuu na zile ndogondogo zinaoongoza utawala wa miji,Kenja aliweza na watu wote tuliheshimu sheria,nashauri halmashauri za Dar es salaam zivunjwe mara moja
 
hakuna kitu kinachoniuzi hapa dar kama kuweka kila sehemu soko kusingizia soko la jioni huu niupuuuzi sana! kama ni ajila wananchi walizoahidiwa ni sawa na ile aliyosema jk kuwa wawekezaji wakiwekeza kwenye bar kunawatu wataajiliwa kufungua vizibo! EEETI HUYO NDO MHESHIMIWA RAISI!
 
hahaaaaaaaaa yaani anahalalisha watanzania wakafungue vizibo vya bia!!!
hakuna kitu kinachoniuzi hapa dar kama kuweka kila sehemu soko kusingizia soko la jioni huu niupuuuzi sana! kama ni ajila wananchi walizoahidiwa ni sawa na ile aliyosema jk kuwa wawekezaji wakiwekeza kwenye bar kunawatu wataajiliwa kufungua vizibo! EEETI HUYO NDO MHESHIMIWA RAISI!
 
Back
Top Bottom