TRT DARASA #7: Uchaguzi Wa Njia Za Kutengeneza Fedha Kwenye Ardhi Na Majengo

Aliko Musa

Senior Member
Aug 25, 2018
156
240
Lengo kuu la maandishi yangu, maisha yangu ya uandishi na makala zangu na vitabu vyangu ni kuwasaida watu nikiwemo mimi mwenyewe jinsi ya kutunza utajiri au kujenga utajiri kupitia ardhi na majengo.

Leo ninakushirikisha falsafa mbili (2) tu ambazo wawekezaji wenye mafanikio makubwa huamini na huzitumia kutunza au kujenga utajiri kupitia ardhi na majengo. Falsafa hizo ni kama ifuatavyo:

Falsafa Namba Moja.

Platifomu ya kujenga faida (Cash-building platform).

Hii ni ile mbinu inayobeba njia zote za kutengeneza faida (na sio kipato endelevu) kupitia uwekezaji kwenye ardhi na majengo. Njia ambazo zipo kwenye kundi hili ni kama ifuatavyo;-

✓ Kununua na kuuza viwanja,

✓ Kununua na kuuza mikataba ya ardhi na majengo (wholesaling real estate),

✓ Kutoa huduma za udalali wa ardhi na majengo,

✓ Kutoa huduma za ukaguzi wa viwanja na majengo,

✓ Kutoa huduma za usimamizi wa majengo ya kupangisha,

✓ Kutoa huduma za usimamizi wa mashamba ya kukodih

Falsafa hii hutofautishwa na falsafa ya hapo chini kwa namna mbili:

✓ Ukubwa wa kiwango cha kazi.

✓ Kiwango cha kutengeneza faida.

Njia zote za kutengeneza faida kupitia uwekezaji katika ardhi na majengo zipo kwenye makundi manne (4).

Makundi 4 Ya Kutengeneza Faida.

Moja.

Kununua, kuendeleza na kuuza majengo au ardhi.

Hii ni njia ya kutengeneza faida ambayo inataka ufanye mambo makuu mawili ili uweze kukua haraka. Moja, ni kununua na kuuza viwanja vingi au majengo mengi na kwa muendelezo.

Mbili, kulenga katika uwiano wa faida kwa kila dili unayofanya. Mfano: ni vizuri zaidi kuuza viwanja 5 ndani ya mwezi mmoja kwa faida ya milioni 10 kuliko kuuza viwanja 30 ndani ya mwezi mmoja kwa faida ya milioni 12.

Mbili.

Kununua na kuuza ardhi au majengo (bila kufanya maendelezo ya aina yoyote.

Hapa unanunua na kuuza bila kuongezea thamani.

Tatu.

Kununua mikataba ya ardhi na majengo na kuiuza.

Nne.

Kutafuta na kutoa rufaa hapa huhusisha huduma za udalali.

Njia ya kwanza ndiyo njia bora ya kutengeneza kiasi kikubwa cha faida ukilinganisha na njia ya pili. Mfano; ukinunua ekari tano na kuzigawa vipande vidogovidogo. Baada ya hapo ukauza kwa faida ndani ya miezi sita, utaweza kutengeneza kiasi kikubwa sana faida kuliko ungenunua ekari 5 na kuziuza bila kuziongezea thamani (Njia ya pili ya kutengeneza faida).

Njia ya pili ni njia bora ya kutengeneza kiasi kikubwa cha faida ukilinganisha na njia ya tatu ya kutengeneza faida.

Njia ya tatu ni njia bora ya kutengeneza kiasi kikubwa cha faida ukilinganisha na njia ya nne.

Njia ya nne ndiyo njia inayotengeneza kiasi kidogo cha faida ukilinganisha na njia zote za hapo juu.

Huu ni ukweli ambao hauhitaji tusikie uzoefu wa kutoka kwa walengwa wa kila njia. Tofauti ni utendaji wa mtu husika.

Falsafa Namba 2.

Platifomu ya kujenga utajiri (wealth-building platiform).

Kama jinsi jina la falsafa linavyojieleza. Hii ni jumla ya mbinu zote zinazohusiana na kutengeneza kipato endelevu. Ni njia zilizoonyesha uwezo wa kumfanya mtu kuwa tajiri japo inachukua muda.

Hivyo, njia bora ninayo washauri rafiki zangu ni kutumia kwanza falsafa namba 1. Kisha, unatumia faida ipatikanayo kutoka kwenye falsafa namba moja kuanza platifomu ya ujenzi wa utajiri.

Hii ni falsafa ya uhakika ya kuwa tajiri kwa miaka kadhaa. Sio njia ya kujiingizia kipato kikubwa haraka haraka. Ili uweze kufanikiwa kwenye falsafa hii unahitaji umakini wa hali juu sana.

Mfano; ukianza kumiliki mabanda ya biashara ya kukodisha itakufanya ufike haraka na kwa usalama kwenye safari yako ya ujenzi wa utajiri kupitia kipato endelevu.

Makundi 3 Ya Kutengeneza Kipato Endelevu.

Njia zote za kutengeneza kipato endelevu zilizopo kwenye uwekezaji huu huingia katika makundi haya matatu. Nayo ni;

Moja.

Kununua, kuendeleza na miliki ardhi au majengo kwa miaka mingi.

Kipato endelevu kwenye njia hii ni kikubwa sana ukilinganisha na njia namba mbili ya hapo chini.

Mbili.

Kununua na kumiliki ardhi au majengo kwa miaka mingi.

Njia hii huingiza kiasi kikubwa cha kipato endelevu ukilinganisha na njia namba tatu ya hapo chini.

Tatu.

Njia tofauti tofauti za ukodishaji wa ardhi au kupangisha majengo.

Njia hii huingiza kiasi kidogo cha kipato endelevu ukilinganisha na njia zote za hapo juu.

Mfano halisi huu.

Umenunua nyumba kwa lengo la kupangisha, kwa kanuni yangu ya kiuwekezaji ya 2% unatakiwa kuingiza kodi ya 1% kila mwezi. Huku 1% ikibaki kwenye usimamizi, kulipia bili na kadhalika.

Hivyo mtaji fedha wako utarudi ndani ya miaka 10 hii inakuwa ni sahihi endapo nyumba yako haitakosa kabisa wapangaji.

Lakini ukinunua nyumba ukaiendeleza na kuiuza baada ya miaka kumi. Utatakiwa kuuza mara nne ya gharama zote ulizotumia kununua na kufanya maendelezo.

Ardhi ndiyo inapanda thamani sana. Ardhi inakuwa mara 10 (1,000%) ndani ya miaka 10. Hii inakuwa kweli endapo utafanya uchaguzi wa viwanja kutoka katika mitaa inayopanda thamani muendelezo.

Kwa ufupi, hivyo ndivyo ambavyo nimeweza kugusia jinsi ya kufanya uchaguzi wa NJIA ZA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE ARDHI NA MAJENGO.

Muhimu; Fungua kitabu kiitwacho NJIA 120 ZA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE ARDHI NA MAJENGO. Baada ya hapo fanya uchambuzi wa njia ulizopendezwa nazo. Kisha nishirikishe hapa hapa kwenye makundi yetu ya TZ REAL ESTATE TEAM.

Rafiki yako,

Aliko Musa.

Mbobezi majengo.

Whatsapp: +255 752 413 711
 
Back
Top Bottom