Teuzi Kama Zawadi - Chanzo cha Umaskini wa Tanzania

Bams

JF-Expert Member
Oct 19, 2010
16,505
41,014
Nchi yetu hii imebarikiwa kwa mambo mengi lakini imenyimwa watu wenye kuonesha njia ya kutumia vile tulivyobarikiwa navyo.

Wengi, watu wakiongelea upatikanaji wa katiba mpya, mawazo yao wanayaelekeza kwenye kutwaa au kupokonywa madaraka badala ya kufikiria kuwa ni mahali pa kuanzia ili kuweza kulikwamua Taifa letu.

Wapo wanaosema kuwa nchi yetu haiendelei kwa sababu ya ufisadi na rushwa unaofanywa na viongozi na watendaji ndani ya Serikali ya CCM. Ni kweli kuna wizi wa fedha za umma na kuna rushwa pia, lakini hivi vitu kwa Taifa letu vina mchango mdogo katika umaskini wetu.

TATIZO KUBWA LA UMASKINI WA TANZANIA NI NINI?

Ni mfumo mbaya wa kuwapata watu wa kufanya maamuzi. Siyo kwamba nchi hii haina watu wenye uwezo wa kupanga, kuamua na kusimamia majukumu ya Taifa ili kuliondoa Taifa kutoka kwenye umaskini, bali nafasi ya hao watu kushiriki katika mambo hayo, haipo kutokana na katiba kuwa mbaya.

Nafasi nyingi za kufanya maamuzi, kupanga na kusimamia, zinategemea uteuzi, na uteuzi unatumika kama zawadi au shukrani kuliko kuangalia mtu anayeteuliwa, anayepewa nafasi fulani anaenda kufanya nini.

Mwaka 1961, Tanzania uchumi wake ulikuwa sawa na wa Malaysia, Singapore na Thailand. Lakini kwa taarifa ya miaka ya karibuni ya UNDP, kwa spidi ambayo Tanzania inaenda, Malaysia ikisimama pale ilipofika bila kwenda mbele zaidi, Tanzania itahitaji miaka 250 kufika. Sijaongelea Singapore, ambayo ipo mbele zaidi.

Hakuna muujiza eti Rais awafahamu watu wote Tanzania wenye uwezo mkubwa katika kutambua, kupanga, na kusimamia mambo muhimu ambayo yangeweza kulibadilisha Taifa hili. Lakini Rais amerundikiwa majukumu ya kumteua kila mtu wa kufanya maamuzi katika vitengo mbalimbali ndani ya Serikali.

Katiba mpya ingeweza kutupatia nafasi ya mahali pa kuanzia. Nafasi zote za kiutendaji zinastahili kuondolewa kuwa nafasi za kuteuliwa badala yake ziwe ni nafasi za weledi, yaani kuwa nafasi za ajira.

Mawaziri, walistahili wasiwe wabunge, bali wateule wa Rais ili Rais awe na uhuru wa kumteua mtu kutoka mahali popote alimradi mtu huyo siyo mbunge.

Wabunge ili waweze kuishauri, kuikosoa na kuiwajibisha Serikali, ni lazima sifa zao ziwe za kiwango cha juu, kwa kuhusisha uadilifu na weledi (nadharia na ule wa uhalisia. Mathalani mtu anaweza asiwe na shahada lakini mambo aliyoyafanya yadhihirishe kuwa ana uadilifu na weledi mkubwa).

Kama watu, vyama vya siasa, taasisi mbalimbali na asasi mbalimbali, zimechoshwa na umaskini wa Tanzania, ni lazima tukubaliane tupate katiba mpya, itakayotoa mwongozo mzuri, pamoja na mambo mengine, la muhimu zaidi, ni namna tunavyowapata watendaji wa Serikali.

Ifahamike kuwa, mwananchi, mmoja mmoja, hata tukijitahidi kiasi gani, utafika mahali fulani, utaihitaji Serikali kwenda mbele zaidi. Mahali hapo ka yupo mtoa maamuzi ambaye uwezo, uelewa na weledi wake ni duni, huwezi kwenda mbele zaidi. Na kushindwa kwenda mbele wananchi ndiko kushindwa kwenda mbele kwa Taifa.

Hebu fikirieni, kuna wakati wakulima wa mazao ya nafaka walivuna vizuri, wakapata masoko mazuri nje ya nchi, wakapata bei nzuri (jambo ambalo lingechochea uzalishaji zaidi) tayari wafanyabiashara wakiwa wanapeleka mazao nje, Waziri Mkuu Majaliwa akatangaza kuwa eti imeonekana kutakuwa na uhaba wa mahindi, kuanzia tarehe hiyo, ni marufuku kupeleka mahindi nje!! Hii ilikuwa ni kauli duni kabisa toka kwa kiongozi mwenye uelewa duni. Hajui kuwa masoko hutafutwa na hulindwa. Lakini ni mtu asiyejua maana ya friendly policies.

Ukiona kiongozi, kila mara anasema kuwa eti hiki kuanzia siku fulani ni marufuku wakati kitu hicho kabla yake ilikuwa ni halali, tambua huyo kiongozi uelewa wake ni duni. Hajui watu wamewekeza kiasi gani wakati sheria ilikuwa ikiruhusu jambo hilo, hafikirii wale waliowekeza wataingia hasara gani na hiyo hasara itakuwa na athari gani kwenye uchumi na maendeleo ya nchi. Yeye anafikiri kutoa amri zile zisizotumia akili, ndiyo umadhubuti wa uongozi.

Tatizo kubwa kuliko yote katika nchi hii, tumebarikiwa kila kitu, tukanyimwa uongozi wenye maono. Angalia hata sasa, badala ya viongozi kuonesha njia ya namna bora ya kupata msingi mzuri wa utawala ili kuyafikia maendeleo haraka, wao ndio wanakuwa kikwazo cha kupata katiba mpya ambayo ndiyo msingi wa awali, wanageuza suala la katiba mpya kuwa suala la vyama vya siasa. Na kama vile katiba kazi yake kubwa ni kusimaia uchaguzi. Wengine wanaona katiba itawanyang'anya ubunge na Urais, na wengine wanafikiria itawapa ubunge na Urais.

Wananchi, katiba ni yetu, siyo ya Rais, siyo ya vyama vya siasa, wala msajili wa vyama vya siasa. Anayepinga sisi wananchi kuweka msingi mzuri wa kuiondoa nchi yetu kwenye dimbwi la umaskini na maendeleo duni kwa kuwa na katiba inayotoa mwongozo thabiti, huyo tumwone kuwa ni adui wa Watanzania wote, ni adui wa Taifa letu.

Tuondoke kwenye ushabiki, tuishi katika ukweli.
 
Ndiyo maana hawataki kabisa kusikia lolote kuhusu Katiba Mpya! Wanajua wanachokifanya.
 
Ndiyo maana hawataki kabisa kusikia lolote kuhusu Katiba Mpya! Wanajua wanachokifanya.
Ni kweli. Ni ubinafsi wa hali ya juu. Wanafikiria manufa yao. Wanafikiria uhuru wa kuwanufaisha watu wao hata kama watu hao hawana msaada kwa Taifa. Huu ni udhalimu wa hali ya juu.

Lakini laana iliyo kubwa ni kwa sisi wananchi, tunaoamua kuwa mashabiiki wa viongozi badala ya kuwa mashabiki wa Taifa letu.

Watu wanastahili kufuata matakwa na milengo yao katika masuala madogo madogo, lakini wanastahili kuungana katika masuala ya makubwa ya msingi. Kwetu hapa haipo hivyo. MwanaCCM yupo tayari kumpigania kiongozi mwanaCCM mwizi kwa vile tu ni mwanaCCM badala ya kuwa mkali na kumwambia, "wewe ni mwanaCCM mwenzetu, lakini katika uovu wako sisi siyo wenzako". Kwetu hilo halipo. Hakuna wanaiweza kusimama na kusema, "ni kweli wewe na kiongozi wetu, lakini katika jambo la msingi kama kayiba mpya, hjna uwezo wa kulikataa kwa sababu ni maamuxi ya wananchi"

Wale vijana ambao Mwalimu Nyerere alisema, "tunataka vijana jeuri, wanaoweza kumwambia kiongozi kupepesa macho", sasa hivi hakuna. Wamebakia vijana mashabiki wa watu, wa kushangilia kwa unafiki ili kuvizia teuzi.
 
Back
Top Bottom