Tanzania yatoswa uenyeji Afcon 2017

Tanzania yatoswa uenyeji Afcon 2017

Rugby Union

JF-Expert Member
Joined
Nov 21, 2012
Posts
402
Reaction score
257
CAF_logo.gif

NDOTO za Rais wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ya kutaka Tanzania iwe mwenyeji wa fainali za Kombe la Soka la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2017, zimeyeyuka.

Hali hiyo imetokana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kuifahamisha TFF kuwa haiwezi kuwa mwenyeji wa fainali hizo zilizoachwa wazi na Libya, kwa sababu Tanzania haijawahi kuwa mwenyeji wa fainali zozote za vijana Afrika.

Malinzi aliyeingia madarakani Oktoba mwaka 2013, amekuwa na ndoto za kuandaa fainali hizo baada ya kutangaza azma hiyo kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Celestine Mwesigwa, Agosti 25, mwaka huu.

"Tunatambua kuwa moja ya masharti ya kuandaa fainali hizo ni pamoja na nchi kuwa imeandaa moja ya mashindano ya vijana. Lakini kwa kuwa suala hili liko katika mazingira maalumu, tunaamini CAF watafikiria ombi letu kwa msingi huo," Mwesigwa aliwaambia waandishi wa habari siku hiyo akitangaza uamuzi huo wa Kamati ya Utendaji.

Lakini jana, TFF ilituma taarifa kwa vyombo vya habari ikieleza kuwa imefahamishwa na CAF kuwa Tanzania haitaweza kuwa mwenyeji wa fainali za Afrika- AFCON 2017 kwa kuwa haijawahi kuandaa fainali zozote za vijana Afrika.
Fainali hizo ni zile za vijana wenye umri chini ya miaka 17 na 20.

"Hivyo, TFF inaelekeza nguvu zote katika kuandaa Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka U17 mwaka 2019," ilieleza taarifa ya TFF na kuongeza: "Tunapenda kuchukua fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwa kututia moyo katika kuomba uenyeji wa AFCON 2017. "Pia tunamshukuru Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara kwa juhudi binafsi alizozionesha katika jitihada za Tanzania kuomba uenyeji wa AFCON 2017."

Shirikisho hilo lilieleza kuwa linaamini kwa dhati kuwa uenyeji wa Afrika U17 2019 utaifungulia Tanzania milango ya kuandaa mashindano makubwa zaidi.

Awali, Libya ilipewa uenyeji wa fainali hizo za 2015, lakini zikahamishiwa Afrika Kusini kutokana na sababu za kiusalama. Hivyo Libya ikapewa fainali za 2017, lakini baadaye ikajitoa. Fainali za 2015 sasa zitafanyika Morocco.

CAF ilitenga Septemba 30, mwaka huu kuwa siku ya mwisho ya kutuma maombi ya kuandaa fainali hizo za 2017, na Tanzania ilikuwa imepanga kuungana na Kenya na Rwanda kuandaa fainali hizo kwa pamoja, lakini Tanzania na Rwanda zilishindwa kuafikiana na Kenya, nchi hiyo ikatuma maombi peke yake.

Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya CAF, hadi kufikia tarehe ya mwisho iliyowekwa ya Septemba 30, mwaka huu ya kutuma maombi ya uenyeji wa fainali hizo za 2017, nchi saba zilipokewa maombi yake.

Nchi hizo ni Algeria, Misri, Gabon, Ghana, Kenya, Sudan na Zimbabwe. Mwenyeji wa fainali hizo za 31 atateuliwa na Kamati ya Utendaji ya CAF katika moja ya vikao vyake mwakani.

Habari Leo
 
Back
Top Bottom