Tanzania yataka hatua udhibiti athari tabianchi

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Tanzania imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na za pamoja kushughulikia suala la mabadiliko ya tabianchi na athari zake.

1576214901301.png

Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mussa Sima, alitoa wito huo jana wakati wa mkutano wa 25 wa mawaziri wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaondelea jijini Madrid, Hispania.

Aliwataka wajumbe wanaoshiriki katika mkutano huo kuendelea kuchukua hatua mahsusi za kushughulikia matatizo ya mabadiliko ya tabia nchi. “Tunahitaji kuendeleza kasi ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kwa kubainisha malengo mahsusi ya kupunguza tatizo hili na kuchukua hatua zote muhimu zinazohitajika," alisema.

Alibainisha kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi tayari zimeonekana Tanzania kupitia matukio makubwa ya hali ya hewa ikiwamo mvua kubwa na kuongeza kwa joto, kunakosababisha mafuriko na kusambaa kwa magonjwa ambukizi, upotevu wa mali na maisha ya wanadamu na uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja katika maeneo mengi ya nchi.

Alisema kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Oktoba mwaka huu, kulikuwa na mvua kubwa kulinganisha na kipindi kingine kama hicho kwa karibu muongo mmoja uliopita na kuathiri sekta zote muhimu, kama vile kilimo, afya, uvuvi, mifugo, maji na afya, hivyo kuongeza kwa magonjwa yakiwamo dengue na malaria.

Sima pia alisema Serikali ya Tanzania, imekuwa ikichukua hatua thabiti ambazo zinachangia katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la gesijoto licha ya ukweli kuwa haikuchangia katika chanzo cha tatizo hilo.

Aliuarifu mkutano huo kuwa Tanzania imenunua rada mbili zitakazotumiwa na TMA kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utabiri hali ya hewa na majanga yatokanayo na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema serikali pia inaendelea kupanua na kujenga mtandao wa barabara za mabasi ya mwendo wa haraka katika Jiji la Dar es Salaam; inajenga reli ya viwango vya kimataifa (SGR) na Bwabwa la Mwalimu Nyerere ambalo litazalisha MW 2115.

“Utekelezaji wa miradi hii siyo tu unachochea maendeleo ya taifa na ukuaji wa uchumi, bali unachangia pia katika upunguzaji wa gesijoto ambazo zinasabaisha ongezeko la joto la dunia ambalo husababisha mabadiliko ya tabianchi," alisema.

Pamoja na hayo, Sima pia aliuarifu mkutano kuwa, Tanzania imedhamiria kuendelea kuongeza maeneo yanayonyonya gesijoto na kutunza uoto wa asili kwa kuwa na eneo la misitu lenye ekari takriban milioni 48, kuendelea kuongeza eneo ambalo limehifadhiwa kwa kuongeza idadi ya hifadhi za taifa na kuendelea na kampeni ya upandaji miti nchi nzima.

Alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono jitihada za Tanzania katika kushughulikia suala la mabadiliko ya tabianchi na kuziomba nchi zilizoendelea kuongeza juhudi zaidi katika kushughulikia suala la mabadiliko ya tabianchi kwa kutekeleza miradi na kutoa fedha na teknolojia kwa ajili ya kushughulikia tatizo hilo.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo ulioanza Desemba 2, ukitarajiwa kuhitimishwa leo, unaongozwa na Sima. Mkutano huo unahudhuriwa na washiriki zaidi 20,000 kutoka serikali za kitaifa, majimbo, majiji na halmashauri, asasi za kiraia, sekta binafsi na jumuiya ya wafanyabiashara.

Mkutano huo una ajenda ya kujali utekelezaji wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi na makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi.


Chanzo: IPP Media
 
Back
Top Bottom