Tanzania yaanza mafunzo ya nuklia | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tanzania yaanza mafunzo ya nuklia

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, Jun 5, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jun 5, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,611
  Trophy Points: 280
  Na Dennis Luambano

  MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Taifa ya Nguvu za Atomiki (TAEC), Profesa Iddi Mkilaha, amesema kwa sasa Tanzania inao wataalamu wasiozidi 10 ambao ni wabobezi katika teknolojia ya nyuklia inayozalisha umeme wa bei nafuu unaotokana na madini ya urani (uranium).

  Kutokana na hali hiyo, anasema Tume yake iko katika mchakato wa kuandaa mpango maalumu wa kuvifanya baadhi ya vyuo vikuu nchini viweze kufundisha masomo yaliyojikita zaidi katika teknolojia ya nyuklia ili Taifa liweze kuwa na wataalamu wengi waliobobea katika fani hiyo.

  Akizungumza katika mahojiano maalumu na Rai mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Profesa Mkilaha anasema wataalamu waliopo kwa sasa, ambao wamesomea fani ya nyuklia ni wachache mno, ingawa wapo wengi waliosomea sayansi na kugusia kidogo tu somo la teknolojia ya nyuklia katika shahada zao za kwanza.

  Kwa mujibu wa Profesa huyo, itaichukua Tanzania miaka 10 kuanzia sasa ili kuweza kuwa na kiwanda chake cha kuzalisha umeme kwa kutumia teknolojia hiyo kutokana na ukweli kwamba mwanafunzi wa fani hiyo anatumia kati ya miaka minne hadi mitano kusoma shahada ya kwanza ya teknolojia ya nyuklia, kabla ya kutumia mwaka mwingine mmoja wa masomo kwa ajili ya kuhitimu rasmi.

  “Kwa hivi sasa tuko katika mchakato wa kutengeneza programu za maandalizi za kujenga kiwanda cha kufua umeme unaotokana na uranium. Tutataanza na kiwanda kidogo ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 300, huku tukiendelea na programu yetu ya kawaida ya umeme unaotokana na maji pamoja na gesi, hali itakayotufanya kufikia mwaka 2020 tuwe na uwezo wa kuzalisha umeme unaotokana na madini,” anasema Profesa Mkilaha na kuongeza:

  “Tunapaswa kuanza na kiwanda kidogo kabla ya kikubwa ili tujifunze kutokana na makosa tutakayoyafanya.”

  Anasema kiwanda kidogo cha kufua umeme unaotokana na madini ya urani, ili kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi na tija, kinatakiwa kiwe na wafanyakazi kati ya 100 na 150 wakati kikubwa kabisa kinatakiwa kiwe na wafanyakazi 200.

  Wafanyakazi hao, anasema wanatakiwa wawe ni wazawa kwanza kwa mujibu wa kanuni za Tume ya Kimataifa ya Nguvu za Atomiki (IAEA), ambayo iliwekwa kwa makusudi kutokana na unyeti wa madini hayo ambayo yanatengeneza mabomu hatari ya maangamizi.

  Anasema Profesa Mkilaha: “Kanuni za kimataifa zinataka wafanyakazi wa kiwanda hicho kuwa wazawa kwa sababu urani inatengeneza mabomu hatari ya maangamizi. Sasa ukiwa na wafanyakazi ambao si wazawa, bila shaka wanaweza kufanya usaliti na kisha wakafanya uhalifu utakaoleta madhara makubwa katika nchi na kizazi chake kwa ujumla.

  “Wakati kanuni inatutaka tufanye hivyo, ukweli unabaki pale pale kwamba hatuna wataalamu wa kutosha ambao ni wabobezi katika teknolojia ya nyuklia. Hiyo ndiyo sababu tunataka sasa vijana wa Kitanzania wasome masomo hayo kwa idadi kubwa kadiri itakavyowezekana, iwe ndani au nje ya nchi.”

  Aidha, anasema kutokana na unyeti wa madini hayo, lazima ulinzi na usalama uimarishwe katika eneo la kiwanda, kazi itakayosimamiwa na Tume yake hiyo.

  Lakini pia, anasema maandalizi pekee ya kujenga kiwanda cha kufua umeme unaotokana na nyuklia yanachukua kati ya miaka saba na 10, na kwamba wataalamu wa kufunga mitambo ya kiwanda hicho watatoka nje ya nchi lakini watakaokiendesha lazima wawe wazawa.

  “Kujenga kiwanda kimoja tu, tunahitaji fedha nyingi sana, na ndiyo maana Tume ya Kimataifa (IAEA) inalazimika kutoa misaada mikubwa ya fedha kuwezesha ujenzi huo, ikiwa ni pamoja na mikopo,” anasema Profesa Mkilaha na kuongeza:

  “Uhai wa kiwanda kimoja ni kati ya miaka 60 na 100. Lakini ndani ya miaka 20 unaweza kurudisha fedha ulizokopeshwa na baada ya hapo ukawa unapata faida tu.

  “Uhai wa kiwanda hiki ni tofauti na vile vinavyotumia nishati ya gesi au maji kwani hivyo vinaishi miaka 15 na gharama ya kuikarabati mitambo yake ni sawa na kuinunua mipya.”

  Kwa mujibu wake, unafuu wa gharama ya umeme unaotokana na madini ya urani unasababishwa na gharama za uendeshaji wa mitambo yake kuwa katika kiwango cha chini kulinganisha na mitambo mingine.

  Akielezea hali ya upatikanaji wa madini hayo hapa nchini, Profesa Mkilaha anasema: “Madini ya uranium yanapatikana ardhini yakiwa yamechanganyika na udongo na vitu vingine, na kwa maana hiyo kiasi cha madini hayo kinakuwa ni kidogo wakati udongo na vitu vingine vinakuwa vingi.

  “Karibu maeneo mengi ya ardhi yetu yana uranium lakini kuna maeneo machache kama Bahi (Dodoma) ndiyo yenye kiasi kikubwa cha madini hayo, na hatari ya madini hayo ni kwamba yanatoa mionzi ambayo haionekani, haisikiki wala haina harufu ambayo unaweza kuitambua.

  “Mionzi hiyo inasababisha ugonjwa wa saratani, na kwa hiyo ili mtu ajikinge na mionzi hiyo, lazima awe na kifaa maalumu kwani ikishakupata inaharibu chembechembe za mwili na kutokana, na ndiyo maana kuna sheria kali za kimataifa za kudhibiti madini hayo.”

  Wakati madini hayo yakirutubishwa kiwandani, anasema huwa yanatoa joto kali, mtikisiko, mwanga na mionzi.

  Profesa Mkilaha anazungumzia utapeli unaofanyika kwa sasa, kwa baadhi ya Watanzania wanatapeliwa kuuziwa mchanga wanaoambiwa kuwa una madini ya urani ndani yake.

  Anasema: “Hivi sasa kuna watu wanauziwa mchanga kwa bei kubwa baada ya kuambiwa kuwa una uranium, hao wanatapeliwa kwani mchanga huo una kiasi kidogo sana cha uranium.

  “Nawasihi (Watanzania) wasidanganyike kununua udongo huo kwani wanapoteza fedha zao. Isitoshe uuzaji wa udongo huo unafanywa kwa vibali maalumu na pia hata wakinunua hautakuwa na thamani kwa sababu mchanga huo una kiasi kidogo mno, na process yake ya kuurutubisha hadi upate yellow cake inahitaji mitambo ya kisasa.”

  Aidha, anasema kabla ya Serikali ya Tanzania kuamua kujenga kiwanda cha kufua umeme kwa kutumia teknolojia ya nyuklia inatakiwa kuwaelimisha wananchi juu ya hatari ya madini hayo.

  Baada ya elimu hiyo, anasema Serikali italazimika kuwaita waangalizi wa kimataifa ili waje nchini kujiridhisha juu ya usalama wa kiwanda hicho kabla ya kuanza uzalishaji.

  “Kwa kuwa na kiwanda hicho, hatutakuwa na migongano ya kidiplomasia na nchi ya Marekani na nchi za Ulaya kwa kuwa uranium itakayopatikana hapa nchini itauzwa nje kwa kufuata taratibu zote zilizowekwa,” anasema.

  Akizungumzia maandalizi ya Serikali katika kukabiliana na uhaba wa wataalamu katika fani hiyo ya nyuklia, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, anasema Serikali imejipanga kuwafundisha vijana wa Kitanzania masomo ya teknolojia ya nyuklia ili Taifa liweze kuwa na wataalamu wa kutosha.

  “Vijana wetu tunawasomesha teknolojia ya nyuklia na tutaendelea kuwasomesha hadi hapo tutakapopata wataalamu zaidi,” anasema na kuongeza:

  “Kwa kuanzia ni kwamba katika Chuo Kikuu cha Dodoma, tumeanzisha shule ya sayansi ya ardhi wakati katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuna Idara ya Jiolojia ambapo kwa pamoja wanafunzi wanafundishwa masomo hayo.”


  Tanzania yaanza mafunzo ya nuklia
   
 2. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #2
  Jun 5, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,611
  Trophy Points: 280
  Uranium: Hatuzalishi mabomu


  [​IMG]"Teknolojia imebadilika. Haturudi nyuma, tupo makini na tumedhamiria. Kiwango gani, hapo siwezi kusema
  Na Mwandishi Wetu
  SERIKALI ya Tanzania imeanza mazungumzo na kampuni binafsi kwa lengo la kuzalisha umeme kutokana na nishati ya madini ya uranium ambayo yamegunduliwa hivi karibuni nchini.
  Uzalishaji wa madini hayo unatarajiwa kuondoa kabisa tatizo la uhaba wa umeme ambao umekuwa sugu hapa nchini kwa miaka mingi sasa.
  Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili mjini Dodoma, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema mazungumzo yamefikia katika hatua nzuri. Hata hivyo, alikataa kuyataja majina ya kampuni hizo kwa maelezo kwamba mazungumzo yapo katika hatua za awali.
  Waziri huyo alisema, kampuni mbili zinazochimba madini hayo nchini, zimeithibitishia Serikali kwamba ifikapo mwaka 2013, tayari madini hayo yanaweza kupatikana tayari kwa kuzalisha umeme.
  Madini ya uranium yanatumiwa kwa mambo mengi, lakini jambo moja kubwa ambalo linayahangaisha mataifa makubwa duniani ni matumizi kwa ajili ya kutengeneza mabomu ya nyuklia.
  Hata hivyo, Waziri Ngeleja aliyatoa wasiwasi mataifa yanayotuzunguka na yale makubwa kwamba Serikali ya Tanzania, haiwezi kuruhusu madini yake kutumika kutengeneza milipuko mibaya.
  Ngeleja alisema anataka kuyatoa wasiwasi mataifa makubwa duniani kwamba uranium ya Tanzania haitatumika kutengeneza silaha na akaahidi kwamba Tanzania itafuata itifaki zote za kimataifa zinazohusu matumizi ya madini hayo.
  Waziri huyo hakutaka kuyataja majina ya kampuni ambayo serikali imeanza mazungumzo nayo ya kuzalisha nishati ya uranium, lakini alithibitisha kwamba mazungumzo na kampuni hizo tayari yameanza na umeme wa uranium utakuwa tayari ifikapo mwaka 2013.
  "Suala la kuwapo kwa uranium nchini ni suala halisi. Huko nyuma kulikuwa na hisia, kulikuwa na viashiria tu vya kuwapo kwa madini hayo mpaka hivi karibuni tulipogundua kuwapo kwake.
  Waziri huyo alisema kwa sasa, maeneo makubwa matatu yamethitibika kwamba yana madini hayo kwa kiwango cha kufanya biashara na kuzalisha nishati ya umeme.
  Alisema zipo kampuni mbili zinazofanya utafiti katika maeneo hayo matatu tofauti. Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Mantrax Resources inayofanya utafiti wake katika Wilaya ya Namtumbo na Kampuni ya Uranex inayofanya utafiti wake katika Wilaya za Manyoni mkoani Singida na Bahi mkoani Dodoma.
  Alisema kampuni ya Mantrax Resources, ndiyo inayofanya utafiti wake katika Wilaya ya Namtumbo eneo la Mto Mkuju.
  "Hawa tayari wamethibitisha kuwapo kwa mashapo yanayowezesha mgodi wa kuchimba uranium kwa zaidi ya miaka 12," alisema Ngeleja.
  Alieleza kuwa wataalamu wa kampuni hiyo, wameeleza kuwa ugunduzi huo, unaipaisha Tanzania na kuiweka katika nafasi ya saba au nane duniani kwa wingi wa madini hayo. Kampuni hiyo imethibitisha kwamba watajenga mgodi na ifikapo mwaka 2012 wataanza uzalishaji.
  "Wanasema wakati wa ujenzi wataajiri wafanyakazi wapatao 1,500 lakini ukishakamilika, watatoa ajira kwa wafanyakazi 400 na hii na kwa sababu kazi kubwa itakuwa imeshakamilika," alisema waziri huyo .
  Ngeleja alisema kampuni hiyo imethibitisha kuwa uwekezaji wa kampuni hiyo utakuwa ni wa dola milioni 350 za Marekani.
  Mojawapo ya matumizi makubwa ni kuzalisha nishati ya umeme ambapo serikali ya Tanzania imejipanga kushirikiana na makampuni kutoka katika sekta binafsi kuzalisha umeme kwa kutumia madini ya uranium.
  "Teknolojia imebadilika. Haturudi nyuma, tupo makini na tumedhamiria. Kiwango gani, hapo siwezi kusema kwa sasa," alisema Ngeleja.
  Kuhusu suala la udhibiti, Waziri Ngeleja alisema serikali inafahamu kwamba uchimbaji na biashara ya madini ya uranium unahitaji kuzingatia sheria za nchi na itifaki za kimataifa.
  "Kwa kuzingatia umuhimu wake, shughuli zinazohusiana na madini haya zinaratibiwa kwa pamoja na Wizara yangu ya Nishati na Madini na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia," alisema.
  Ngeleja alisema Tanzania haipangi kutengeneza silaha za maangamizi au silaha yoyote itokanayo na uranium badala yake itayauzia mataifa yanayohitaji lakini kama nchi, imeweka kipaumbele katika kuzalisha nishati ya umeme.
  Ngeleja aliitaja kampuni ya pili inayojishughulisha na utafiti na uchimbaji wa madini hayo kuwa ni Uranex ambayo inafanya utafiti wake katika Wilaya za Manyoni na Bahi na tayari kampuni hiyo imethibitisha kuanza uzalishaji kabla ya mwaka 2013.
  Waziri Ngeleja alisema lengo la wizara yake ni kutaka kuzalisha umeme mwingi wa kibiashara.
  "Umeme ni bidhaa sawa na bidhaa nyingine. Kwa hiyo tunapata kufanya biashara ya umeme tukizingatia kuwa hii ni mojawapo ya bidhaa adimu duniani. Kuna mipango inaendelea ya kuunganisha kwenye gridi ya kimataifa," alisema na kuongeza:
  "Na tukishaunganisha tutaweza kufanya biashara vizuri kwa kuwa umeme unaotokana na madini ya uranium, una bei ndogo ukilinganisha na umeme utokanao na vyanzo vingine.
  Uranium: Hatuzalishi mabomu
   
 3. G

  Godwine JF-Expert Member

  #3
  Jun 9, 2010
  Joined: Jan 15, 2010
  Messages: 1,369
  Likes Received: 45
  Trophy Points: 145
  yah kama tukifanikiwa kujenga na kuzalisha umeme basi hilo litakuwa ni moja ya mafanikio ya serikali lakini bado tunatakiwa kudhibiti madini yetu na tunufaikenayo kwa kiwango kikubwa
   
 4. U

  Ubungoubungo JF-Expert Member

  #4
  Jun 9, 2010
  Joined: Jul 28, 2008
  Messages: 2,508
  Likes Received: 24
  Trophy Points: 135
  lakini wabongo, maneno mingimingiiii vitendo vichache..
   
 5. Nyambala

  Nyambala JF-Expert Member

  #5
  Jun 9, 2010
  Joined: Oct 10, 2007
  Messages: 4,470
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 135
  More barks than bites, time will tell!
   
Loading...