#COVID19 Tanzania na UVIKO-19

Sep 20, 2018
20
7
Ni muda sasa umepita tangu tangu janga la korona liikumbe dunia yetu.
Wengi wetu tunafahamu kuhusu historia ya ugonjwa huu; mahali ulikoanzia na namna ilivyoenea hadi ukafika hapa nchini kwetu.
Sitozungumzia sana huko, badala yake nataka tujikite zaidi katika madhara yaliyosababishwa na ugonjwa huu, lakini zaidi tutamalizia juu ya nini kifanyike kuondokana na madhara hayo.

Kwa uzoefu nilionao, korona ni changamoto ya kisiasa na uchumi iliyojificha chini ya mwamvuli wa ugonjwa. Wakati wananchi wakifanya kila linalowezekana kujilinda na kujikinga dhidi ya korona, kulingana na ushauri kutoka kwa watalamu wa afya, serikali, asasi zisizo za kiserikali na mataifa mengine duniani, hali inazidi kuwa mbaya katika siasa na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Utaratibu wa lockdown na baadhi ya madharti ya kufungwa kwa mipaka ya nchi yetu yamepelekea sekta ya utalii kushuka, ijapokuwa kwa sasa hali inazidi kuimarika kila kukicha. Lakini pato la serikali katika sekta hii limeshuka kwa ujumla ukilinganisha na hali ilivyokuwa kabla ya korona.

Watu wengi wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huu kwa sababu kuna wakati korona ilikuwepo lakini wataalamu wa afya walipewa vizuizi vya kisiasa wasiseme kuwa watu wanaugua. Korona ikapata jina la "Political pneumonia". Hali hii imegharimu maisha ya wengi ambao wangepata matibabu sahihi na pengine kuwalinda na ndugu zao.

Licha ya taifa kuwa na msimamo fulani juu ya namna ya kutokomeza ugonjwa huu, shinikizo kutoka mataifa yaliyoendelea umeifanya nchi yetu kukosa msimamo thabiti na hivyo kukubali na kupokea kwa hali zote yale yote yanayoletwa kutoka nje kwa ajili ya kupambana na korona.

Katika kipindi kama hiki, nchi inahitaji viongozi wazalendo watakaofanya na kuamua mambo yenye maslahi mapana kwa taifa. Nchi inahitaji viongozi watakaofikiria vyema na kupigania mambo yenye tija kwa wananchi wao.

Endapo viongozi watashindwa kulitambua hili, afya za watanzania zitakuwa mashakani, hali ya uchumi na siasa itazidi kuwa mbaya zaidi pia.

Katika kipindi hiki, ambapo tayari chanjo imeshakuja. Napendekeza mambo yafuatayo yafanyike;

Mosi, baadhi ya wananchi wana maswali na wasiwasi kuhusu usalama wa chanjo ya uviko-19. Maswali yao yajibiwe kitaalamu na elimu itolewe kote nchini ili watu wafanye maamuzi kwa uzuri zaidi kutokana na elimu na ufahamu unaotolewa kuhusu chanjo hii.

Pili, Watalaamu wa afya wapewe uhuru wa kutoa mawazo yao na kufanya chochote kama sehemu ya kupambana na ugonjwa huu, wasiwe watu wa kupokea miongozo tu kila wakati pasipo kutumia akili zao za kitaaluma katika kutatua majanga ya kiafya kama haya.

Tatu, Serikali ioneshe utofauti wa siasa na afya za watu. Siasa zina mahali pake na afya nayo ina mahali pake. Kuleta siasa kwenye afya ni kuangamiza taifa lote.

Mwisho, Tuendelee kushirikiana katika juhudi za kutokomeza ugonjwa huu.
 
Back
Top Bottom