Tanzania na mawaziri watano tu, kati ya 28 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tanzania na mawaziri watano tu, kati ya 28

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, May 14, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  May 14, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,409
  Likes Received: 81,442
  Trophy Points: 280
  Tanzania na mawaziri watano tu, kati ya 28

  Godfrey Dilunga Mei 13, 2009

  Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

  UENDESHAJI wa Serikali ni gharama kubwa, na hasa tukirejea hatua ya hivi karibuni ya kusitisha ununuzi wa magari yasiyo ya lazima uliookoa zaidi ya Sh. bilioni 50.

  Lakini gharama hizo za uendeshaji serikali huzidi mara dufu pale tija kutoka katika serikali husika inapokuwa haba au ya kubahatisha katika baadhi ya sekta.

  Kwa hali ya mambo ilivyo nchini, unaweza kudhani kuwa nchi inaundwa na Baraza la Mawaziri wasiozidi watano hivi. Kumbe kuna mawaziri 27, na kama utamjumuisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, basi mawaziri wanafikia 28. Wakati mawaziri wakiwa 28, naibu mawaziri ni 21.

  Je, wako wapi wengine (kwa maana ya utendaji wenye tija ya wazi) hadi tuanze kuamini kuwa nchi ina mawaziri wasiozidi watano, akiwamo Waziri John Magufuli? Wako wapi mawaziri wengine zaidi ya 20?
  Tujiulize na kutafakari ni kwa nini kila kukicha kero zisizo stahili, na ambazo zinapaswa kutatuliwa na wizara zinaongezeka badala ya kupungua? Ni kweli nchi hii yenye mawaziri 28 na naibu mawaziri 21 inastahili kuzubaa kimaendeleo kiasi hiki. Ni kweli Tanzania inastahili kuendelea kutuwama katika dimbwi la matatizo yasiyo ya lazima?

  Je, inaingia akilini nchi hii yenye mawaziri 28 na naibu mawaziri 21 iendelee kuishi katika kero lukuki za sasa, ikiwamo kero ya kuyumba kwa utawala bora? Mawaziri na naibu mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya na viongozi wengine wako wapi katika kuliletea Taifa tija ya ziada kutokana na utendaji wao wa kazi ofisini?

  Sababu hasa ni nini? Je, sababu ni mawaziri na naibu mawaziri na viongozi wengine kucheleweshewa mishahara au kulimbikiziwa mafao yao kama walimu? Walimu ambao licha ya malimbikizo yao kulipwa kwa utata bado wanafunzi wanafaulu.


  Je, sababu ni marupurupu na mishahara ya viongozi wetu haitoshi kama ilivyo kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

  Au mfumo wa utendaji wao wa kazi ni dhaifu, usio na fursa thabiti za kudhibiti uwajibikaji wa waziri mmoja mmoja kila siku? Tujiulize, kwa mfano, kwa nini nchi hii yenye Wizara ya Ardhi karibu katika kila awamu ya Serikali, iendelee kukumbwa na kashfa za kutoa kiwanja kimoja kwa mtu zaidi ya mmoja, huku tukitambua kuwa ardhi ni chanzo cha machafuko katika jamii yoyote ulimwenguni?

  Kutokana na mwenendo wa mambo ambao naamini ni shaghala baghala, nadhani sasa ni wakati muafaka tukaanza kuhoji uzito wa vikao vya Baraza la Mawaziri. Tunaweza sasa kuhoji uzito wa vikao vya Baraza la Mawaziri kwa kuhusisha hali zetu za maisha.

  Tujiulize, ni kweli wanajadili matatizo yetu wanayoshuhudia mitaani wakati wa ziara zao kwa lengo la kuyaondoa, au wanaishia tu kutafakari namna ya kujipanga kutumia matatizo hayo ili kuomba fedha za wafadhili ili kuendeleza utawala wa kuegemea zaidi uzoefu hata kama uzoefu huo hauna manufaa tena kwa wananchi?

  Uko wapi ubunifu wa Baraza la Mawaziri katika kubuni mbinu za kukabili kero za wananchi kwa kasi inayostahili?

  Tutafakari tukijiuliza, vikao vya Baraza la Mawaziri vimetuletea mabadiliko gani ya kujivunia kuanzia katika MKUKUTA (Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania) hadi Mpango wa zima moto wa mabilioni ya JK, ambao umefikia hatua ya viongozi kuanza kukiri kuwa hawakujipanga vema katika usimamizi. Ni aibu nchi yenye mawaziri wa kutosha wakiendelea kuongoza nchi yenye umeme wa kubahatisha.

  Swali linalotia uchungu hapa ni kwamba kwa nini nchi yenye mawaziri 28 na naibu mawaziri 21, Rais na Makamu wa Rais, ishindwe kuwa na umakini mkubwa kiasi cha kushindwa hata kujipanga katika usimamizi wa mabilioni ya JK, ambayo leo hii karibu katika kila wilaya kuna malalamiko?

  Je, tatizo ni mfumo wa uteuzi wa viongozi husika? Hili ninalojadili si geni, nakumbuka katika gazeti hili, mwandishi Lula wa Ndali Wananzela aliwahi kuandika mara kadhaa akiweka bayana kuwa tatizo kubwa nchini ni uongozi. Kwamba kuna viongozi wenye elimu nzuri lakini hawana uwezo wa kuongoza. Jenerali Ulimwengu naye aliwahi kuandika kuhusu suala hili.

  Leo napenda kuungana na wenzangu hao kwa kumtazama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utawala Bora, Sophia Simba. Nitamjadili Waziri Simba kwa kuwa naamini kuwa nchi yoyote yenye Waziri wa Utawala Bora imara na mwenye msimamo, kamwe nchi hiyo haiwezi kuyumba katika masuala ya utawala, na hata kama waziri ataingizwa katika majaribu ya kutingishwa na wakubwa wake basi atakuwa tayari kujiuzulu kwa notisi ya saa 24.

  Nakumbuka maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyewahi kuzungumzia sifa za Rais wa Tanzania, akisema ni lazima awe na uwezo wa kuwaambia rafiki zake kuwa Ikulu ni mahali patakatifu na achukie rushwa si tu kwa kutamka, bali hata tukimwangalia usoni tuamini hivyo.

  Maelezo haya ya Mwalimu Nyerere yanajidhihirisha kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Nina imani kwa asilimia kubwa kuwa mafisadi wanafahamu Waziri Mkuu Pinda kuwa si mla rushwa wala mtovu wa maadili. Ni muungwana anayetambua matumizi sahihi ya nguvu zake za kiuongozi alizokabidhiwa na Taifa.

  Kwa hiyo tunaye Waziri Mkuu anayetazamika machoni kama mtu safi. Hali hii ya Pinda ndiyo tungepaswa kuishuhudia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Utawala Bora, Sophia Simba. Waziri ambaye vyombo nyeti kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) vipo chini ya ofisi yake.

  Sina hakika na uadilifu wa Waziri huyu, lakini jambo moja la dhahiri ni kuwa uwezo wake katika ofisi hiyo umepwaya na hili amelithibitisha mwenyewe. Turejee mfano wa hivi karibuni tu mara baada ya Mwenyekiti Mtendaji wa IPP kutaja orodha ya matajiri wenzake aliowaita mafisadi papa: Yusuf Manji, Jeetu Patel, Rostam Azizi, Tanil Somaiya na Subash Patel.

  Binafsi nilitarajia kujivunia uwezo wa Waziri huyo wa Utawala Bora mara baada ya shutuma hizo nzito za Mengi kwa wenzake. Lakini kabla ya kuendelea niweke wazi kuwa, nitamjadili Waziri Simba na Mengi kutokana na nafasi zao katika jamii.

  Kwa haraka, baada ya kumsikia Mengi akiwataja wale aliowaita mafisadi papa nilitaraji kumsikia Waziri huyo akionyesha mikondo ya utawala bora na wa sheria ilivyo wazi kwa watu waliotajwa na Mengi.

  Nilitarajia Waziri huyo atatosheleza katika wadhifa wake huo kwa kueleza fursa walizonazo hao walioitwa mafisadi papa, pamoja na fursa alizonazo Mengi katika sakata hilo, mara baada ya waandishi wa habari kumuuliza maswali Waziri Simba.

  Hakika, sikutarajia kumsikia Waziri wa Utawala Bora akijificha katika upande mmojawapo, bila hata kwanza umma kusikia utetezi au hatua wanazochukua watu waliotwa na Mengi kuwa ni mafisadi papa.

  Binafsi, sikutaka kujadili hatua hiyo ya Waziri Simba mapema kwa sababu kadhaa, lakini kubwa zaidi ikiwa ni kusubiri namna ambavyo waziri huyo angejirudi na kusawazisha makosa yake ya kukurupuka na kujihifadhi upande mmojawapo wa mvutano, wakati akitambua kuwa pande zote zina fursa ndani ya wigo wa utawala bora na wa sheria.

  Kwa mfano, nilitaraji Waziri Simba angejirudi na kueleza kuwa maneno yake ya kuhoji; “Mengi ni nani katika hii nchi” angeyafuta au kuomba radhi. Angeomba radhi kwa kuwa akiwa kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utawala Bora, alipaswa kujua kuwa Mengi ni raia wa halali wa Tanzania.

  Lakini kubwa zaidi, Waziri huyo angepaswa kujua kuwa Mengi ni Mtanzania ambaye haki zake zimetamkwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ilikuwa kosa kubwa kwa Waziri kupandwa na jazba, na kuhoji kuwa “Mengi ni nani katika hii nchi.”

  Jambo la hatari katika kauli ya Waziri huyo ni kwamba kama leo ameanza kuhoji Mengi ni nani katika hii nchi, basi kesho anaweza kuhoji Waziri mwenzake ni nani katika hii nchi, au anaweza hata kuhoji muuza nazi au nyanya sokoni ni nani katika hii nchi.

  Kama Waziri huyo ameweza kuhoji Mengi ambaye ni mfanyabiashara ni nani katika nchi hii, si ajabu siku nyingine atakapokuwa na jazba akahoji mkulima wa chai, Mufindi ni nani katika nchi hii, au mkulima wa ndizi kule Kinole, Morogoro ni nani kwenye hii nchi.

  Kikubwa ninachojaribu kukiweka wazi hapa ni hatari iliyo ndani ya maelezo ya Waziri Simba, maelezo ambayo binafsi nimeyatafakari kwa takriban wiki kadhaa sasa. Ni imani yangu kuwa si busara kwa kiongozi wa umma kuanza kuhoji uhalali wa Mtanzania huku akijua wazi kuwa uhalali wa mhusika unatambuliwa ndani ya Katiba.

  Katika mazingira kama haya wapo Watanzania wanaoweza kumtamfsiri Waziri huyu kuwa ameanza kulewa madaraka. Watanzania hao wanaweza kuamini hivyo wakizingatia kuwa akiwa kama Waziri alipaswa kujua Mengi ni Mtanzania ambaye Katiba imemtambua pamoja na Watanzania wenzake, akiwamo yeye Waziri Simba.

  Si ajabu vile vile wakaibuka Watanzania wengine wanoamini kuwa katika kauli hiyo Waziri Simba ameyumba na ametumia vibaya madaraka yake ya uwaziri. Amehoji uhalali wa raia wa Tanzania, ambaye tayari mamlaka husika zinamtambua. Je, anahoji kwa malengo gani na kwa manufaa ya nani? Je, kuhoji huko kwa Waziri Simba kunalenga kumwondolea Mengi sehemu ya uhalali wake wa kikatiba au ni jazba tu za Waziri?

  Kwa mfano, Waziri angepaswa kuhoji Mengi ni nani baada ya kuchunguza na kutambua kuwa si Mtanzania, hati zake za kusafiria hazina mihuri ya Serikali inayomtambua kama Mtanzania. Hapa Waziri angekuwa na hoja katika kuhoji Mengi ni nani, kwa kuwa angekuwa hatambuliki na Serikali.

  Kwa ujumla, kauli hiyo ya Waziri Simba kuhoji Mtanzania maarufu anayetambulika na Serikali kwa kuwa hati zake za kusafiria bila shaka zina mihuri ya Serikali ni nani, ametoa ujumbe wa kuitisha jamii. Ni kweli, Mengi anaweza kuwa na makosa kama walivyo Watanzania wengine wengi, wakiwamo viongozi, lakini tukianza leo kuhoji fulani ni nani kwenye nchi hii maana yake ni kwamba nchi yetu haitakuwa na mustakabali unaoeleweka.

  Tutakuwa tunajenga nchi yenye jamii iliyojaa hofu katika kutuhumu uovu wa wazi hata kwa wale ambao wanachunguzwa kwa tuhuma husika na vyombo vinavyotambulika rasmi katika mfumo wa utawala nchini. Kama Waziri Simba na wenzake wanakusudia tufike huko kwenye jamii yenye hofu katika kuhoji, wengine ambao ni wengi tunaamini malengo hayo hayana manufaa kwa nchi. Ukichambua kwa upana zaidi, utabaini kuwa Waziri Simba ameitishia jamii kuhoji, kuuliza na kufuatilia pale wanapobaini kuwa kuna kasoro.

  Lakini ukitazama kwa kina na umakini mkubwa utabaini kuwa ni kauli yenye kuibua enzi mpya za vitisho dhidi ya Watanzania waliomstari wa mbele kuhoji hadharani mambo wanayoona hayako sawa. Ni kauli inayolenga kutisha Watanzania kuhoji viongozi wao wanaoyumba katika kutekeleza ahadi zao kwa wananchi.

  Kwa bahati nzuri, hivi karibuni Waziri Mkuu Mizengo Pinda alizungumza na wakuu wa mikoa na wilaya wa mikoa ya nyanda za juu kusini, akiwa huko Pinda alikumbushia kauli za Mwalimu Nyerere kwamba nchi inahitaji mambo manne - watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

  Katika mambo hayo yote, Waziri Mkuu Pinda akaonyesha kutilia shaka hili la uongozi bora. Sasa tafakari ni kwa nini Waziri Mkuu atilie shaka suala la uongozi bora wakati nchi inayo Wizara ya Utawala Bora na pia yupo Waziri wa Utawala Bora? Hii maana yake ni kwamba chimbuko la matatizo ya kiuongozi nchini linaanzia katika Wizara Nchi, Ofisi ya Rais – Utawala Bora.

  Kutokana na maelezo hayo ya Waziri Mkuu, inawezekana Wizara hiyo haijawahi kupata Waziri anayejua kwa kina malengo na majukumu ya wizara, na mwenye uwezo mkubwa wa kuongoza wizara hiyo ili hatimaye kukidhi matarajio ya umma. Je, ni kwa nini nchi yenye mawaziri 28 iwe na tija ndogo mfano wa nchi yenye mawaziri watano? Tafakari.

  Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

  Simu: 0787-643151
   
 2. K

  Kidatu JF-Expert Member

  #2
  May 14, 2009
  Joined: Jun 11, 2008
  Messages: 1,491
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 135
  Mkuu hapo juu umelonga ukweli bin haki. huyo mwana mama alifaa sana kuwa kiongozi wa kikundi cha taarabu.
   
Loading...