Tanzania na India kusaini mikataba kadhaa

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
WAZIRI Mkuu wa India, Narendra Modi anatarajia kuweka saini mikataba mbalimbali ya ushirikiano kati ya India na Tanzania katika sekta za viwanda, maji, elimu, sayansi na teknolojia.

Pia, atazungumza na waandishi wa habari na wafanyabiashara wa hapa nchini. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga alisema hayo juzi alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Modi atakuwepo nchini kwa ajili ya ziara ya kitaifa ya siku mbili, kwa lengo la kudumisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kati ya nchi hizo mbili. Dk Mahiga alisema Modi atatumia fursa hiyo kukuza uhusiano wa kihistoria baina ya nchi hizi mbili na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi.

Alisema Modi atakutana na Rais John Magufuli na kufanya naye mazungumzo Ikulu; na pia kuweka saini kwenye mikataba ya ushirikiano kati ya sekta mbalimbali.

Dk Mahiga alisema Modi pia atazungumza na jumuiya ya wafanyabiashara wakubwa, ambao baadhi yao wameshaonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya ujenzi wa viwanda vya kutengeneza chuma, saruji, dawa ya binadamu na maji ya matunda.

“Natoa mwito kwa wafanyabiashara wa hapa nchini watumie fursa hii kushiriki ili waweze kukutana na wenzao. Kongamano hilo litafanyika kwenye ukumbi wa Benki Kuu (BoT) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi,” alisema.

Dk Mahiga alisema Modi atatumia pia fursa hii kutangaza hatua zilizochukuliwa na serikali yake katika kutekeleza ahadi zilizotolewa kwenye mkutano wa wakuu wa nchi wa India na Afrika, uliofanyika New Delhi, India Oktoba mwaka jana. Ahadi hizo ni pamoja na kutenga dola bilioni 10 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa miradi ya maendeleo kwa Afrika.
 
Back
Top Bottom