Hakuna sababu ya kuendelea na Taifa la Tanzania kama Jamhuri (ya muungano au vinginevyo). Tanzania ni nchi dhaifu, maskini, dunia ya tatu, ambayo haiwezi kabisa kupambana na nchi za magharibi.
Nchi jirani zetu -- Uganda, Burundi, Rwanda na Kenya zina shida kubwa ya Ardhi. Ukiziunganisha nchi hizo zote, bado hazifikii Tanzania kwa ukubwa wa Ardhi. Tanzania ni nchi ya 31 kwa ukubwa wa ardhi duniani. Matokeo yake majirani zetu
wanauana kwa vile tu
msongamano wa watu umekuwa
mkubwa.
Hatuwezi kuwaaangalia hivihivi wenzetu wanapata taabu, wakati sisi tunayo ardhi ya bwelele. Kwa kuanzia tutafuta mipaka kati yetu na wao, ili waweze kuja
kujihomolea sehemu ya nchi yetu wanavyopenda! Hii ndio tunaloita soko la pamoja. Tanzania itabaki na taasisi muhimu -- Rais anayesindikizwa na misafara, anayekaa Ikulu, na akienda nje ya nchi, anapigiwa mizinga 21. Wabunge wanaofanya vikao, na wataendelea kuitwa Waheshimiwa. Vyama vya siasa 'vya upinzani' vitaendelea kuwepo, na kutambuliwa na mabalozi wa nje ya nchi. Jeshi letu tukufu litaendelea kusubiri adui aje na vifaru na mizinga kuchukua nchi. Hao ambao tunawagawia, ni kwa hiari yetu, si kwamba wametushinda vitani, hata kama wapo watakotuona sisi ni mazuzu kwa kufanya hivyo. Huo ni ufinyu wao wa kufikiri. Sisi tutaendelea kupata sifa duniani kwamba 'hata Waafrika tunaweza kuungana'. Baada ya miaka miwili mitatu, hata madaraka ya kisiasa tutayaunganisha, wasije wakadhani tunawaogopa.
Halafu wapo baadhi ya Watanzania
vidomidomi wanaong'ang'ania mawazo ya kizamani kwamba tuendelee kuwa na taifa letu wenyewe. Wanaabudu mipaka bandia iliyowekwa na wakoloni. Wanataka Tanzania iendelee kuwa
Jamhuri huru. Kuthibitisha kwamba sisi ni '
advanced' tunaifuta hiyo mipaka hata kama
wananchi hawataki.
Siyo tu hivyo, tunaandaa wizara nzima, tunayoitengea bajeti, kuhakikisha Tanzania inafutwa kikwelikweli pasi na uwezo wa kurudi tena.
Kwa kuanzia, mipaka ya Tanzania
tutaifuta Julai 01 mwaka huu 2010, isije ikawa mambo ya uchaguzi Tanzania ukaja utawala mwingine utakaozinduka na kubadili mawazo. Ofkozi hiyo ni mpaka Bunge lipitishe makubaliano ambayo Rais Kikwete
keshayasaini -- bunge la nani litakalothubutu kukataa?
Miaka ya zamani Watanzania walikuwa '
brainwashed' kuwa tayari hata kutoa maisha yao kulinda mipaka, uhuru, umoja na ardhi ya Tanzania. Hivyo pale Iddi Amin alipotaka kuchukua 'ardhi kidogo tu' ikawa vita! Watu walijitolea kwa hiari na kwa lazima kumng'oa 'nduli' mvamizi. Lakini leo tunaigawa nchi nzimanzima, tunafuta hiyo mipaka ambayo watu walijitolea muhanga kuilinda. Tukiwa wazima, hatukunywa, wala hatukulewa. Nchi tunaigawa kwa watu wengine watokao mbali, kwa nini isiwe Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi?
Lazima tuwaonee huruma. Wao wako kwenye ile
Jumuia Nyingine ya Afrika Mashariki - Igad. Lakini kule watachukua ardhi ya wapi? Somalia? Jibuti? Ethiopia? Jumuia yao ni kubwa, ya zamani, na ina malengo yote sawa na EAC. Lakini kule bado suala la msingi linabaki kuwa ni ardhi. Siyo ardhi ya jangwa, ardhi ya kilimo! Kilimo kwanza! Hata wale wengineo wako kwenye
jumuia ile nyingine. Lakini lazima tuonyeshe sisi hatuogopi kupoteza uhuru wetu, mradi tu unaenda kwa wenzetu wenye ngozi nyeusi kama sisi.
Ni kweli
walisherehekea pale EAC ilipovunjika mwaka 1977 kwa vile walijua tutapata taabu, lakini sasa hivi
tunawapatia nchi nzima, pasipo na uwezo wa kusema 'ajua' kama ya 1977.
Tanzania mwisho Julai 01 2010,
Viva Afrika Mashariki!