TANESCO yakarabati vituo 9 kupoza umeme

TANESCO yakarabati vituo 9 kupoza umeme

diana chumbikino

JF-Expert Member
Joined
May 29, 2018
Posts
428
Reaction score
368
1582615103720.png


SHIRIKA la Umeme Tanzania(Tanesco) limepata Euro milioni 139 kwa ajili ya mradi wa ukarabati wa vituo tisa vya kupoza umeme sambamba na kujenga mfumo wa kisasa wa kudhibiti umeme, ambao utakuwa na uwezo wa kutambua tatizo la kukatika umeme lilipoanzia na kufanyiwa kazi mapema.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Usafirishaji Umeme wa Tanesco, Isaac Chanji wakati akitoa maelezo kwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo, iliyotembelea Kituo cha Kupooza na Kusafirisha umeme wa Gridi cha Ubungo, kukagua utendaji kazi wa shirika hilo.

Akizungumzia kazi na miradi iliyo mbioni kuanza ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma za upatikanaji wa umeme nchini, Chanji alisema hivi sasa umeme upo wa kutosha, lakini changamoto za kukatika kwa nishati hiyo, zinatokana na hitilafu na sio uhaba wa nishati hiyo. “Hivi sasa Tanesco tuko vizuri tunazalisha umeme wa kutosha kwenye maeneo mengi, kukatika kwa umeme kwa sasa kunatokana na hitilafu za umeme ambazo ni pamoja na athari za mvua ambazo wakati mwingine huleta mafuriko, upepo mkali na sio uhaba wa umeme,”alisema Chanji.

Kutokana na changamoto hizo na nyingine, alisema shirika hilo limepata Euro milioni 139 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ukarabati wa vituo tisa vya kupooza umeme nchini sambamba na ujenzi wa mfumo wa kisasa wa udhibiti umeme. Akifafanua, alisema mradi huo unatarajiwa kuanza muda wowote na utakamilika mwaka 2029, ambapo Euro milioni 69 zitatumika kufanya ukarabati kwenye gridi ya Taifa kwa kukarabati vituo tisa vya kupooza umeme.

Alisema Euro milioni 70 zitatumika awamu ya pili ya mradi kwa kujenga mfumo wa kisasa wa udhibiti umeme. Mfumo huo utakuwa na uwezo wa kutambua tatizo la umeme lilipo na kutatuliwa kwa wateja wakubwa .

Akizungumzia ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Dk Alexander Kyaruzi alisema wameridhishwa na utendaji kazi wa shirika hilo na kushauri viongozi kuboresha mfumo wa kudhibiti umeme ili kuleta ufanisi wa huduma zao kwa wateja.

“Bodi yetu ina muda mfupi tangu ianze kufanya kazi, tumetembelea kujua na kuelewa utendaji kazi wa Tanesco ulivyo ili tuweze kutoa maelekezo yetu kwa lengo la kuboresha na kuleta ufanisi, tumebaini kwamba umeme unaozalishwa kwa sasa ni wa kutosha changamoto za kukatika zinatokana na hitilafu na sio uhaba wa umeme,”alisema Dk Kyaruzi.
 
Back
Top Bottom