Takwimu za ukusanyaji wa maoni ya wananchi kwenye tume ya Katiba

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,982
1.0 Historia na Hali ya Nchi
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayojumuisha iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika ambayo kwa sasa inajulikana kama Tanzania Bara zilizoungana tarehe 26 Aprili 1964. Tanganyika ilipata uhuru wake tarehe 9 Disemba 1961 na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ilijikomboa kutoka Utawala wa Kisultani kwa Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964.

Tanzania ipo kati ya nyuzi 0 na 12 Kusini mwa Ikweta na nyuzi 12 hadi 40 Mashariki mwa Greenwich. Tanzania inapakana na Kenya na Uganda (Kaskazini); Rwanda, Burundi na Kongo (Magharibi); Zambia, Malawi na Msumbiji (Kusini); na Bahari ya Hindi kwa upande wa Mashariki.

Tanzania ina eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 945,203 yakiwemo maziwa makuu ya Viktoria, Tanganyika na Nyasa pamoja na Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu zaidi Afrika. Nchi hii ina vivutio vikubwa vya kitalii zikiwemo mbuga za wanyama, hifadhi za taifa, fukwe za bahari, milima na mabonde. Tanzania ina rasilimali nyingi zikiwemo ardhi, madini, gesi asilia, misitu, mazao ya kilimo, mifugo na samaki ambazo ndiyo nguzo kuu za uchumi wa taifa.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Tanzania ina idadi ya watu wapatao milioni 45. Tanzania Zanzibar ina jumla ya watu milioni 1.3 wakati Tanzania Bara ina idadi ya watu milioni 43.6. Taifa hili linaundwa na watu wenye makabila zaidi ya 120 na jamii zenye tamaduni mbalimbali. Pamoja na wingi wa makabila, kiungo kikuu cha utaifa ni lugha ya Kiswahili inayozungumzwa na Watanzania wote.

Tanzania inafuata mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi vya siasa inayoongozwa na Rais mtendaji chini ya misingi ya usawa, undugu, haki na utawala wa kisheria. Katiba na sheria mbalimbali hutumika kufikia misingi hii. Kiutawala, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imegawanyika katika mikoa 30 (Tanzania Bara – 25 na Tanzania Zanzibar - 5), wilaya, kata/shehia na vijiji/mitaa. Mihimili mikuu ya dola ni Bunge/Baraza la Wawakilishi, Mahakama na Serikali ya Jamhuri ya Muungano/Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Pamoja na dola, asasi za kiraia na sekta binafsi hushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi kwenye nyanja za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.

1.1 Mchakato wa Kukusanya na Kuchambua Maoni ya Katiba
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inaongozwa na Katiba ya 1977, iliamua kuifanyia mabadiliko Katiba hiyo kwa kuwashirikisha wananchi. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kuratibu kazi hiyo. Baada ya kukamilisha matayarisho, Tume ilikwenda kwa wananchi ambao walijitokeza kutoa maoni yao juu ya mabadiliko ya Katiba kwa kutumia njia mbalimbali. Pamoja na uchambuzi wa hoja na sababu za maoni hayo ili kupata masuala muhimu ya kuingiza katika Rasimu Katiba, ushiriki huo pia umezalisha takwimu ambazo zimechambuliwa kwa vigezo mbalimbali vya kidemografia na kijiografia.

1.2 Njia za Utayarishaji wa Takwimu za Maoni ya Katiba (Methodology) Mchakato wa kukusanya na kuhifadhi maoni ya wananchi ulihusisha njia mbali mbali ambazo kwa pamoja zimewezesha kupatikana kwa takwimu zilizomo katika taarifa hii. Njia hizo ni pamoja na ukusanyaji wa maoni, utayarishaji wa mfumo wa kuhifadhi maoni, ubunifu wa mfumo wa kutafsiri maoni, na uchambuzi wa maoni kwa njia za kitakwimu.

1.2.1 Njia za Ukusanyaji wa Maoni
Maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya yalikusanywa kupitia njia zifuatazo:

1. Mikutano miwili ya hadhara kwa siku iliyodumu kila mmoja kwa muda usiopungua saa tatu katika ngazi ya kata au shehia ambayo wananchi walijitokeza na kutoa maoni yao;

2. Mikutano ya ziada ya ndani ilifanyika kwa taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali katika baadhi ya kata/shehia kwa vyombo vya ulinzi na usalama, vyombo vya habari na wanafunzi wa vyuo vya mafunzo/wafungwa/mahabusu.

3. Katika mikutano ya hadhara na ile ya ziada, fomu maalumu za kukusanyia maoni zilizotayarishwa na kusambazwa kwa wananchi waliohitaji kutoa maoni yao kwa njia ya maandishi zilitumika;

4. Mikutano ya ndani kwa ajili ya watu mashuhuri wakiwemo viongozi waandamizi na wakuu wa serikali, viongozi wastaafu, wawakilishi wa wananchi na viongozi wa kijamii;

5. Mikutano ya ndani kwa ajili ya makundi ya taasisi za kiserikali na kijamii ambapo wazungumzaji wakuu kutoka taasisi hizo waliwasilisha maoni;

6. Wataalamu wa fani na nyanja mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi walialikwa kutoa mada ili kujenga uwezo wa wajumbe wa Tume kwa kutoa uzoefu na mapendekezo juu masuala mahsusi ya kikatiba[1];

7. Barua za maoni kutoka kwa wananchi nazo ziliwasilishwa Tume;

8. Njia za mtandao kama vile barua pepe, facebook, tovuti na ujumbe mfupi wa maandishi wa simu ya mkononi nazo zilitumika kupokea maoni ya wananchi;

9. Mikutano ya Mabaraza ya Katiba ya wilaya na yale ya Asasi, Taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana ilitumika kupokea maoni kuhusu Rasimu ya Awali ya Katiba ambapo kumbukumbu za mikutano hiyo ziliandikwa na kuwasilishwa Tume; na

10. Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora) walitoa maoni yao kwa kufika Makao Makuu ya Tume na kwa kuandika.

Baada ya mchangiaji kuwasilisha maoni yake ufafanuzi ulitolewa pale ambapo Wajumbe wa Tume walihitaji. Aidha, taarifa ya maandishi ya mchangiaji nayo ilipokelewa. Ili kuweka kumbukumbu ya maoni hayo kwa ajili ya uchambuzi na kupata takwimu, sauti na picha za video za wachangiaji zilinaswa na kuhifadhiwa kwenye majalada ya kompyuta.


[1] Majaji Wakuu wa nchi jirani za Kenya na Uganda na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba ya Kenya walialikwa kutoa uzoefu wa nchi zao.

Habari zaidi soma kiambatanisho
 

Attachments

  • TAKWIMU ZA UKUSANYAJI WA MAONI YA WANANCHI (1).pdf
    3.6 MB · Views: 55
Back
Top Bottom