Heche kuongoza Vijana Chadema
Imeandikwa na Lucy Lyatuu; Tarehe: 30th May 2011
JOHN Heche amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Katika uchaguzi uliofanyika jijini Dar es Salaam, Heche amewabwaga wagombea wenzake sita waliokuwa wakiwania nafasi hiyo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa aliliambia gazeti hili jana kuwa wagombea wanne walienguliwa katika kinyanganyiro hicho kutokana na kukosa maadili pamoja na rushwa, katika mkutano Mkuu wa Bavicha uliofanyika juzi.
Aliwataja walioenguliwa katika kinyanganyiro hicho kwa kampeni chafu, rushwa, kukosa maadili na uongo kuwa ni Grayson Nyakarundu, Bernard Saanane, Mtella Nampamba na Habib Mchange.
Dk. Slaa alisema Mchange alienguliwa na Kamati Kuu wakati wagombea wengine walienguliwa na Kamati ya Wazee baada ya kuagizwa na Kamati Kuu kuchukua hatua zozote zinazofaa dhidi ya wagombea wenye kutuhumiwa.
Alisema nafasi ya Mwenyekiti ilikuwa ikigombewa na Aidan Sadik, Bernard Mao, Saanane, Deogratias Kisandu, Edwin Soko, Nyakarungu, Mchange, Heche, Masood Suleiman na Mtela Mwampamba.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti Bara, Dk. Slaa alisema ilichukuliwa na Juliana Shonza ambaye alikuwa akigombea pamoja na Emmanuel Somon, Gwakisa Mwakasendo, Joseph Patrick na Julieth Rushuli.
Dk. Slaa alisema kwa upande wa Zanzibar, alichaguliwa Sharifa Khamis na kuwabwaga Sharim Khamis, Zainab Bakari na Ally Akalipo Ally.
Alisema wagombea waliorudisha fomu kwa nafasi za Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Mratibu wa Uhamasishaji, Mweka Hazina watatangazwa katika ratiba ya baadaye.
Dk. Slaa alisema kwa nafasi ya Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Mratibu wa Uhamasishaji na Mweka Hazina, watapendekezwa na Kamati ya Utendaji ya Bavicha kwa mujibu wa ratiba itayopangwa baadaye na uteuzi wao utathibitishwa na Kamati Kuu ya chama, hivyo wataalikwa katika vikao vya baadaye.
Uchaguzi wa Bavicha ulikwama kufanyika mwaka jana kutokana na sababu mbalimbali na hivyo kuahirishwa hadi ulipofanyika Mei 28.