Taifa lililopiga kambi kwenye bonde la kashfa! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Taifa lililopiga kambi kwenye bonde la kashfa!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mzee Mwanakijiji, Feb 13, 2009.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Feb 13, 2009
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Na. M. M. Mwanakijiji

  Hatuendi mbele, wala hatutoki tuliko. Kama ni jeshini tunaweza kusema tuko kwenye marktime! Na kama ni lori basi tumekwama kwenye matope na magurumu yanazunguka kwa kasi na ngurumo ya gari inapasua anga huku harufu ya moshi wa matairi ikichafua pua zetu. Hata hivyo, hatuendi kokote. Tumebakia kama tumefungwa kamba karibu na vundo la uchafu, na kama tuliokaribishwa karamu kwenye shimo la uchafu, tumeketi, tunajaribu kuziba pua na huku tunajisikia kichefu chefu, lakini hatutoki.

  Ni mfano mbaya ninaotumia, lakini inabidi.

  Tumepiga kambi kwenye bonde la kashfa. Tulipoanza kujenga Taifa letu tulitaka tuendelee mbele, tulitaka tulete mabadiliko kwa watu wetu na siyo majengo yetu, tulitaka kuona katika Taifa letu watu wote wanakuwa sawa na wenye kufurahia haki zote za msingi za binadamu na huku wakifurahia pia haki zao kama raia. Na sisi tulitaka kujenga taifa la kisasa ambalo lina mazingira mazuri ya maisha na lenye kutoa nafasi sawa ya mafanikio. Bahati mbaya haya sasa yanaendelea kuwa ndoto inayofikiwa na wachache, huku wengi wetu kama taifa tumeendelea kukaa pembeni na kunung'unika kwenye bonde hili la kashfa.

  Taifa letu kwa miaka karibu mitatu sasa limejikuta katika mijadala yake limekwama kwenye ile ya kashfa. Sipendi kuziorodhesha tena lakini wingi wake unajulikana na gharama yake inashtua mioyo. Na kama vile watu wasioona mbele tayari tumeshatengeneza kashfa zijazo kwa kuahirisha kushughulikia yanayowezekana sasa! Hatuwezi kuishi bila kashfa.

  Tatizo kubwa nilionalo (na nimewahi kuandika huko nyuma) ni kutokuwa tayari kushughulikia jambo la kitaifa na kulimaliza na kufunga mjadala. Inashangaza mwaka mmoja baadaye suala la Richmond bado lipo, miaka nane baadaye suala la rada ndio hata halijaanza kushughulikiwa, miaka karibu kumi na kitu suala la IPTL bado linatoa harufu yake, na miaka karibu 20 uchafu wa BoT bado tunao! Hatuwezi kuendelea mbele kwa kadiri ya kwamba tunaendelea kuketi kwenye kambi hii ya kashfa za ufisadi.

  Hatuwezi kwenda mbele kama katika mawazo na fikra zetu tunahangaika na mambo ambayo yangepaswa kushughulikiwa mara moja na daima. NI tabia hii ya kuvumilia uchafu na uovu ndiyo imetufanya tuuzoee kiasi kwamba usafi na wema vinaonekana kuwa ni tunu za "watakatifu" wachache na sehemu ya "waadilifu wateule".

  Hatuwezi kwenda mbele na kujadali masuala ya mabadiliko ya taifa ambayo yatachochea kupiga hatua "ile kuu" ya maendeleo kwa kadiri ya kwamba tumeng'angania utamu wa kashfa mbalimbali tukikwepa kuzishughulikia mara moja. Tunaendelea kuchechema kama kulungu aliyenaswa mtegoni!

  Tumefika mahali pa kuelezea na kusifia "hatua za maendeleo" ambayo yamo mawazoni mwetu. Tunapita kati ya watu wetu na kuwataka waimbe nyimbo za maendeleo ya kitu ambacho hawakuwa nacho. Unapojenga kisima mahali ambapo hakuna kisima ulichofanya siyo maendeleo bali kukutana na mahitaji ya watu. Maendeleo yatakuwa ni pale ambapo wakazi wa sehemu hiyo wanaweza kupata maji safi ya bomba kwenye nyumba zao!

  Unapojenga kliniki mahali ambapo hapana kliniki ya msingi siyo umeendelea bali umekutana na mahitaji ya watu. Maendeleo hapo yatakuwa ni huduma ya kisasa, wataalamu wa kutosha na mchakato bora wa kupata tiba.

  Unapojenga barabara ya lami unaweza kuona ni maendeleo. Hata hivyo hilo ni jambo la lazima katika ulimwengu wa leo. Maendeleo basi hapo yatakuwa ni kutengeneza mitaro ya maji machafu, taa zinazofanya kazi za kuongezea magari na zile za kumulika njia, alama nzuri za usalama wa barabarani n.k

  Ndiyo maana wengine tulitakaa pale kina Lowassa walipotaka tuimbe wimbo wa kupaa ati kwa sababu tumejenga shule nyingi za msingi kupitia MMEM na miradi mingine. Tulikataa kwa sababu walikuwa wanatuonesha ongezeko la vitu. Walitaka tuone idadi ya wanaffunzi wanajiunga na sekondari na shule ya msingi. Lakini walikwepa kabisa kuangalia kufaulu kwa watoto hao.

  Leo hii tulichokisema karibu miaka minne iliyopita kinaendelea kuwa kweli. Tumeongeza mashule, tumeongeza idadi ya wanafunzi wanaoingia shule lakini tumepunguza kiwango cha kufaulu, na kwenye masomo ya sayansi na kiingereza bado tuko nyuma sana. Siyo kwenye shule za awali bali hata kwenye vyuo! Tumepiga kambi kwenye kashfa nasi tumezizoa.

  Naamini wakati upo, na haja ipo ya kubadili fikra zetu na kukataa kucheza mdumange wa kashfa huku tukipiga filimbi za ufisadi. Ni lazima tukatae kulazimishwa kucheza mganda wa sifa za uongo huku tukiruka ruka kamba za kudanganyana.

  Kama taifa ni lazima tutoke kwenye kambi hii ya kashfa na kuingia katika uwanja wa ujenzi mpya wa taifa la kisasa. Tuweze kukusanya nguvu zetu za kifikra kujadiliana jinsi ya kuboresha vilivyopo na vipya. Tuweze kutoka katika kashfa za BoT, Bunge, n.k na kuanza kujadiliana jinsi ya kuiboresha BoT, Bunge, Mahakama n.k Tuweze na sisi kutumia uwezo wetu na vipaji vyetu tulivyopewa na Mungu bure kutatua matatizo yetu.

  Vinginevyo, tutaendelea kukodoleana macho, kutukanana, kutafutana wachawi, kubezena, kupigana vijembe, huku tukicheka cheka, tukiremburiana macho na kukonyezana, katika bonde hili la kashfa na ufisadi, kiasi kwamba kizazi kijacho kitakapoamka kitatulaani kwa kupoteza muda katika shimo la takataka!

  Tuamue kutoka, na wale ambao hawataki tuwafukie na takataka zao!

  Mwenzenu,
  Ndugu yenu,
  Rafiki yenu,
  Na kwa wengine....
  Adui yenu


  Na isimame kama ushahidi na mashtaka dhidi yetu!
  M.M. Mwanakijiji
  Feb 13, 2009
   
  Last edited: Feb 13, 2009
 2. Zero

  Zero JF-Expert Member

  #2
  Feb 13, 2009
  Joined: Mar 8, 2008
  Messages: 301
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 0
  Naamini kabisa tunaweza kutoka ndani ya bonde hili. Suluhisho ni kuwa na bunge lenye meno. Na bunge lenye meno litatokana na sisi wananchi kuchagua wabunge makini ambao watatuwakilisha sisi kama wananchi, na sio kuwakilisha maslahi ya chama. Imefika mahali sasa, lazima watanzania watambue bunge ni chombo muhimu sana katika mustakabali wa nchi. Bunge ndio linatunga sheria, na kikubwa zaidi, bunge ndio linaisimamia serikali. Tukiwa na bunge makini, basi serikali itawajibika ipasavyo. Wananchi lazima watambue kwamba kuwa na uwiano mzuri wa vyama vya siasa bunge ni jambo zuri sana. Bunge linapokuwa la chama kimoja, ni vigumu sana kuwa na meno ya kuiwajibisha serikali. Watanzania tuamke na kuchagua wabunge wengi wa upinzani wenye utashi wakuleta maendeleo ya kweli nchini, na kututoa bondeni.
   
 3. Steve Dii

  Steve Dii JF-Expert Member

  #3
  Feb 13, 2009
  Joined: Jun 25, 2007
  Messages: 6,416
  Likes Received: 67
  Trophy Points: 145
  Mkjj, you are one great soul. Mungu akubariki.... it's an exceptionaly inspiring article, thank you!

  SteveD.
   
 4. Nemesis

  Nemesis JF-Expert Member

  #4
  Feb 13, 2009
  Joined: Feb 13, 2008
  Messages: 3,833
  Likes Received: 1,089
  Trophy Points: 280
  True man, somebody to print and hand to JK and Sitta.
   
 5. M

  Morani75 JF-Expert Member

  #5
  Feb 13, 2009
  Joined: Mar 1, 2007
  Messages: 619
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 0
  M.M.M, hapo kweli inaonyesha jinsi JF ilivyo na watu wenye uchungu wa nchi yao.... Hii ni one great article, nadhani itabidi wanafunzi wa vyuo mbalimbali hapa nchini wawe wanaingia kwenye JF ili waweze soma na kutumia mawazo kama haya especially wale wanaofanya political science!!

  I salute............
   
 6. zomba

  zomba JF-Expert Member

  #6
  Feb 13, 2009
  Joined: Nov 27, 2007
  Messages: 17,081
  Likes Received: 49
  Trophy Points: 0
  Umeng'aka sana katika maelezo yako marefu ambayo nadhani kwa mzoefu wa kuwasilisha mada, angeya kusanya kwenye sentensi tano au kumi na angeeleweka vizuri.

  Kwanza, uandikapo hebu jaribu kwenda moja kwa moja kwenye unalokusudia na sio kuzunguka mbuyu kama ufanyavyo.

  Pili, baada ya kulalama sana kwenye nukuu zako za matakataka, jee ufumbuzi ni nini? Sijauona kwenye nukuu zako! au unataka ushauri? hujaeleza kusudio haswa la nukuu zote za takataka, au na nukuu zenyewe ni taka taka za kutupwa kwenye debe la taka? au ndio debe tupu haliishi kutika-tika?
   
 7. Azimio Jipya

  Azimio Jipya JF-Expert Member

  #7
  Feb 13, 2009
  Joined: Nov 27, 2007
  Messages: 3,370
  Likes Received: 14
  Trophy Points: 135
  Very intersting!
   
 8. K

  KGM Senior Member

  #8
  Feb 13, 2009
  Joined: May 21, 2007
  Messages: 188
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  Ha ha ha ha ha ha ha ha ha ha ha ha
  Kwenye tope twawezaje kutoka sasa kwa mtindo huu. Na huyu hayuko pekee.

  Imebidi nicheke tu. TZ kazi ipo. Mafisadi yamechachamaa na wananchi tongotongo zinaanza kuwatoka. Nashindwa kutabiri nini kitatokea

  UWIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIII
   
 9. Gamba la Nyoka

  Gamba la Nyoka JF-Expert Member

  #9
  Feb 13, 2009
  Joined: May 1, 2007
  Messages: 6,594
  Likes Received: 6,755
  Trophy Points: 280
  Makala nzuri lakini nadhani ni bora Mzee Mwanakijiji ukatumia Tafsida wakati mwingine, Maneno kama takataka, harufu mbaya, unapoyatumia kuashiria kwamba Watanzania hatuyachukii hayo, kwa maoni yangu ni kwamba inaweza isilete picha nzuri kwa wananchi wachukia ufisadi.

  nadhani ingekuwa bora kama ungefanya distinction iliyowazi baina ya "Wao" mafisadi na "sisi" wapenda maendeleo na wachukia ufisadi, lakini wote kutukusanya katika kundi moja la nafsi ya pili wingi "Tu", hataaa Mzee hilo sikubaliani nalo.

  WORDS MATTER.
   
 10. H

  Hofstede JF-Expert Member

  #10
  Feb 13, 2009
  Joined: Jul 15, 2007
  Messages: 3,584
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 0
  Mkuu zero umeongea kitu cha hakika na kweli kabisa kuwa ni lazima mabadiliko yaanzie bungeni. Ila kwa Tanzania hilo haliwezekani kwani Bunge lina maana kubwa sana, kwanza ni ruzuku ya chama toka serikalini, pili ni chaka la kupitishia maamuzi yenye maslahi ya chama, tatu ni ulaji na si huduma kwa wananchi

  Hivyo basi kutokana na sababu hizo plus tume ya uchaguzi ya chama tawala, kamwe usitarajie wapinzani kuongezeka bungeni hata kama wananchi wote wataamua kuchagua upinzani, system yetu hairuhusu hilo, kwani wao wanamsemo wao kuwa "KWA VYOVYOTE LAZIMA TUSHINDE", Tuongee hapa mwisho wa siku wao ndiyo wanajua wawape wapinzani viti vingapi na si wananchi.
   
 11. Mag3

  Mag3 JF-Expert Member

  #11
  Feb 13, 2009
  Joined: May 31, 2008
  Messages: 9,094
  Likes Received: 6,188
  Trophy Points: 280
  Tatizo watanzania wengi tunaanza kulizoea hili bonde na kuliona kama makao yetu ya kudumu. Ndiyo, na aliyetupeleka bondeni anajua fika kuwa nje ya bonde atapoteza nguvu kwa kuwa huko kuna hewa safi isiyoruhusu ustawi wa uvundo. Bunge limegeuzwa kuwa baraza la kutunga sheria kudhibiti na kuzima mawazo yoyote ya kuhama bondeni. Serikali inalinda huu uvundo kwa nguvu zake zote kwa kisingizio cha amani na utulivu bila kujua inatafuna watu wake pole pole kama kansa. Wengi baada ya kuathirika na uvundo wamepoteza kabisa uwezo wa kunusa, kusikia wala kuona na wanachapa usingizi bila wasiwasi. Wachache ambao hawajaathirika sana wamefungwa kamba miguuni na kuzibwa midomo wasije wakawakosesha wenzao usingizi.
   
 12. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #12
  Feb 13, 2009
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Nawapata vizuri kabisa..

  a. Utaona kuwa nazungumzia zaidi sisi "kama taifa".. siyo kama mtu mmoja mmoja. Kuelewa hii distinction ni muhimu kwani kama kweli tunataka kubadili na kujenga taifa la kisasa, utamaduni, taswira, na taamuli ya kitafa ni lazima ibadilike. Leo hii tukijiuliza ni sifa gani zinamtambulisha Mtanzania kulinganisha na mwafrika mwingine? majibu yanaweza yakawa ya kushangaza sana. Miaka tya 80 na 70 majibu yalikuwa karibu yanalingana.

  b. Kuhusu suala la mapendekezo mara zote limo humo ndani. Hata hivyo kunawatu wanaopenda siyo tu kulimiwa, kuvuniwa, kupikiwa na kulishwa wao wangependa hata kumezewa pia. Kwa ufupi utaona kuwa pendekezo ninalotoa limo ndani, kwani kimsingi ni kuwa "tutoke kwenye bondel la kashfa"! To me that was a metaphor for our nation..

  c. Lengo letu hasa siyo kuuonesha uchafu kwani wengi tayari tunaujua ulipo na upo vipi. Lengo ni kuonesha kuwa ni lazima tutoke kwenye uchafu lakini kubwa zaidi kama hatuwezi kutoka eneo la uchafu, basi tuundoe uchafu na kupasafisha hapo..

  Wazo hili la makala nililipata kwenye ile picha walioonesha daraja la Manzese na lundo la uchafu ambapo pembeni kuna kijana ameketi kama anaushangaa kwanini upo pale, lakini wakati huo huo yuko comfortable enough to relax there! To me that was a metaphor for our nation.
   
 13. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #13
  Feb 13, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,607
  Likes Received: 82,181
  Trophy Points: 280
  Yanasikitisha sana yanayoendelea ndani ya nchi yetu. CCM imeng'ang'ania madarakani pamoja na hakuna chochote wanachokifanya kuiendeleza nchi yetu. Watafanya juu chini kuwatetea mafisadi na viongozi wabovu bila kujali athari ya utetezi wao.

  Nafarijika sana ninapoona kwamba bado wanaJF hatujakata tamaa katika kupambana na viongozi wabovu na mafisadi waliojaa ndani ya CCM na serikali isiyojali maslahi ya wananchi wake. Yaliyotokea ndani ya Bunge katika kikao cha Bunge kilichokwisha yamemaliza matumaini yangu yote niliykuwa nayo ndani ya Bunge letu. Kama wawakilishi wa Watanzania katika majimbo mbali mbali wanalipwa mishahara na marupuru chungu nzima lakini Wabunge wa CCM wanapokuwa bungeni huweka mbele maslahi ya chama chao badala ya yale ya Watanzania matokeo yake nchi sasa inaelekea pabaya.

  Bado mapambano ni mazito na yatachukua muda mrefu na yanahitaji juhudi za Watanzania wengi ili kuikwamua nchi yetu toka kwa mafisadi. Hili ni kwa faida yetu sote na faida ya vizazi vyetu vijavyo. Kamwe tusikubali tena kuambiwa nchi yetu ni maskini wakati tunagawa bure dhahabu yetu kwa kuwaachia wachukuaji 97% ya dhahabu yetu. Kamwe tusikubali kuambiwa nchi yetu wakati tunaona vingozi ndani ta chama na seriali wanakuwa na utajiri wa kutisha kutokana na ufisadi wanaoufanya ndani ya nchi yetu. Tunao sasa mabilionea hata matrilionea wanashindana kila kukicha nani atakuwa tajiri zaidi kuliko mwenzake ili wanunue magari na majumba ya kifahari UK, Dubai, na nchi nyingine za magharibi.

  Tuendeleze mapambano kwa faida ya nchi yetu na wale wote wanaoitakia mema Tanzania.

  Alutta Continua!

  Mungu ibariki Tanzania.
   
 14. Kiranga

  Kiranga JF-Expert Member

  #14
  Feb 13, 2009
  Joined: Jan 29, 2009
  Messages: 34,607
  Likes Received: 6,185
  Trophy Points: 280
  What a shame!

  Ni vigumu kulishughulikia jambo la "kitaifa"n kama watu wengine hata hawataki kulitambua hivyo.

  Kingunge anaweka mbele chama kuliko taifa, wengine hata utaifa wanaona ni nyimbo tu zisizo na uhalisi.Tutashughulikiaje mambo ya kitaifa wakati tunafikiri kibinafsi? (That car, that foreign vacation, that obscenely expensive house on the hill, that 10% etc)
   
 15. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #15
  Feb 13, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,607
  Likes Received: 82,181
  Trophy Points: 280
  Mkjj,

  Hii article ni nzuri sana. Nakuomba uisambaze kwenye magazeti yote ya kiswahili nchini ambayo yatakuwa tayari kuichapisha.
   
 16. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #16
  Feb 14, 2009
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Mag3.. nimependa sana hii!!! naomba kuiiba kwenye updated makala wiki ijayo..!!
   
 17. Mag3

  Mag3 JF-Expert Member

  #17
  Feb 14, 2009
  Joined: May 31, 2008
  Messages: 9,094
  Likes Received: 6,188
  Trophy Points: 280
  Hamna taabu, karibu.
   
 18. U

  Utatu JF-Expert Member

  #18
  Feb 14, 2009
  Joined: Dec 31, 2008
  Messages: 436
  Likes Received: 111
  Trophy Points: 60
  Watu wengine bwana. Yaani, kwa aina yeyote ile ni kujaribu kukosoa kila kitu tu. Mkuu, huwezi kusoma katikati ya mistari? Unataka utafuniwe kila kitu?

  Wewe kwani ufumbuzi wako ni nini?

  Akina Mag3 wanaoelewa kiurahisi, si unaona mchango wao?
   
 19. zomba

  zomba JF-Expert Member

  #19
  Feb 14, 2009
  Joined: Nov 27, 2007
  Messages: 17,081
  Likes Received: 49
  Trophy Points: 0
  Action speaks louder than words!
   
 20. U

  Utatu JF-Expert Member

  #20
  Feb 14, 2009
  Joined: Dec 31, 2008
  Messages: 436
  Likes Received: 111
  Trophy Points: 60
  Na vitendo vyako wewe ni ......?
   
Loading...