'Taifa liko hatarini’ | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

'Taifa liko hatarini’

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Oct 24, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Oct 24, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,805
  Likes Received: 83,184
  Trophy Points: 280
  'Taifa liko hatarini'

  Mwandishi Wetu Oktoba 22, 2008
  Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

  Zitto asema dalili zote mbaya ziko wazi

  Askofu aonya kuna hatari ya kuibuka machafuko

  WANASIASA, viongozi wa dini na wananchi wameelezea kushitushwa kwao na hali ya kisiasa na kiuchumi inavyoendelea nchini, wakisema kwa sasa nchi iko hatarini kutokana na kuibuka kwa matabaka ya wazi ya kijamii miongoni mwa wananchi, watawala na watu waliowazunguka.

  Matukio ya hivi karibuni kuhusiana na migomo, maandamano, ‘zomea-zomea' na hata urushaji wa mawe dhidi ya msafara wa Rais wa Jamhuri, yameelezewa kuwa ni dalili za wazi za kuwapo ombwe la kisiasa na hatua nyingine katika mmomonyoko mkubwa wa maadili na kutoweka kwa utangamano wa kitaifa.

  Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza ameliambia Raia Mwema kwamba hali ikiendelea na kuonekana ya kuwa ndiyo maisha ya kila siku, "kinachofuata ni machafuko kama haya yanayoendelea na kushuhudiwa."

  Katika mahojiano hayo maalumu, Askofu Bagonza alisema kwa sasa uongozi wa dola umeshindwa kujitofautisha na uongozi wa kisiasa na sasa viongozi wa dola wamekuwa wanasiasa.

  "Kiongozi wa dola anatakiwa afanye kazi ya wananchi wote lakini sivyo ilivyo, kwani viongozi wa dola wanaonekana kufanya kazi kama bado wako kwenye kampeni. Ukifanya kazi kama uko kwenye kampeni, si watu wote watakaokufurahia, wale unaotofautiana nao kiitikadi watakuwa hawana imani nawe, utakosana nao tu; ndiyo maana kuna hizi vurugu," anasema Askofu Bagonza.

  Pamoja na hali hiyo, Askofu huyo mwenye msimamo wa pekee, alisema watu wengi sasa wamekata tamaa kutokana na jinsi mambo mengi yanavyofanyika nchini, kiasi cha kuwafanya waanze kuhisi kutokuwapo kwa hata dalili ya mwangaza mbele yao.

  Alisema baada ya kuvutiwa mno na hamasa wakati wa kampeni, watu walikuwa na matumaini makubwa kwamba haki itatendeka lakini badala yake hali halisi imekuwa kinyume cha matarajio yao.

  "Sisi tunaokaa vijijini ni mashuhuda wakubwa wa hali hii. Kuna kero nyingi huku, kama kwa mfano za ardhi lakini mtu ukimwambioa aende polisi atakukatalia kwa sababu anajua kupata haki yake huko ni ndoto", alisema.

  Alisema mambo hayo yakiendela ikaonekana kuwa ndiyo maisha ya kila siku, kinachofuata ni machafuko kama haya yanayoendelea na kushuhudiwa, akirejea matukio ya migomo, maandamano na baadhi ya matukio ya viongozi kuzomewa ama kurushiwa mawe.

  Akofu Bagonza anaelezwa kuwa ni mmoja wa maaskofu vijana na wasomi katika kanisa la Tanzania ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, alikuwa miongoni mwa wanateolojia wanaoheshimika nchini.

  Mara kadhaa Askofu Bagonza amekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na maaskofu wenzake katika kusimamia haki ikiwa ni pamoja na wakati fulani kutofautiana na Katibu Mkuu wao katika mashitaka yaliyofunguliwa mahakamani dhidi ya Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya.

  Hivi karibuni, Askofu Dk. Bagonza alinukuliwa akisema kwamba mfumo wa utandawazi umesababisha watu wengi kujikuta wanakuwa masikini zaidi na hivyo idadi ya maskini na wenye mizigo ni kubwa kuliko utayari wa kuwasaidia na kuwabebea.

  Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, ameliambia Raia Mwema kwamba hali si nzuri kiuchumi, kisiasa na kijamii na kwamba kwa sasa kuendelea kukiachia Chama cha Mapinduzi (CCM) kutawala ni kuhatarisha usalama na ustawi wa Taifa la Tanzania.

  "Ndiyo maana kwa sasa tuko Mara tukianzia mikakati yetu na Kanda ya Ziwa. Tumeona kuiachia CCM kuendeleza ukiririmba wa nchi yetu ni hatari kwa usalama na ustawi wa nchi yetu. Ni hatari sana kwani kwa sasa rushwa imekuwa ‘order of the day'. Tulipita mahali fulani juzi, watu wakawa wanatuomba fedha; imefikia mahali hata mwanakijiji sasa akiona mwanasiasa anaona kwamba kuna fedha zimekuja kugawanywa," alisema.

  Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POC), alisema hali ya kisiasa ni mbaya sana na hata mwananchi wa kawaida tu anaona kuna ombwe kubwa la kiuongozi.

  "Hizi ni dalili za wazi za matatizo makubwa. Matatizo ya walimu, wanafunzi kugoma hadi wanafunzi wa sekondari wanaandamana. Hii si dalili nzuri hata kidogo, na lazima kama Taifa tuzinduke na kuchukua hatua badala ya kuendeela kulala usingizi," alisema.

  Alisema kwa sasa kuna tatizo kubwa la kuachiwa kiongozi mmoja kufanya kila kitu huku mwenyewe akiendelea kuamini kuwa na uwezo huo, jambo ambalo alisema ni la hatari katika utawala wa pamoja na zaidi katika kipindi kigumu kilichopo.

  "Hakuna anayejali, imekuwa business as usual (mambo kama kawaida). Hizi ni dalili za wazi za kuwapo ombwe (vacuum). Kila waziri na kiongozi anasubiri Rais aseme, na yeye anafikiri kila kitu anaweza mwenyewe. Duniani inapofika hali hii viongozi wanakaa na kuondoa tofauti zao. Sasa hata mawaziri hawasikiki; ni Rais pekee," alisema.

  Zitto amezungumzia suala la uchunguzi na hatua dhidi ya wizi wa Fedha za Mfuko wa Madeni ya Nje (EPA) na matumizi mengine ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kusema kwamba kuna tatizo la msingi la kuchanganya mambo kunakofanywa na watawala kwa nia ya kuwalinda watuhumiwa halisi.

  "Tulikosea toka mwanzo kuunganisha Shilingi bilioni 90 zilizochotwa kwa kughushi na shilingi bilioni 42 ambazo ushahidi wake haukuwapo kwa wakati ule. Sasa kuna juhudi za kuanza kutaka kutafuta mbuzi wa kafara ili wezi halisi wasikamatwe. Hii ni ishara ya uongozi mbovu. Nashangaa wanataka kushitaki watu wa Mwananchi Gold! Pale hakuna wizi, ni uamuzi mbovu tu," alisema Zitto. POC ndiyo hupitia pia hesabu za BoT.

  Zitto alisema kuwa kuhusiana na Mwananchi Gold hakuna kesi ambayo serikali inaweza kufikisha mahakamani na badala yake wanalenga kumdhalilisha mwenyekiti wa bodi ya kampuni hiyo, Jaji Joseph Warioba, kutokana na msimamo wake katika kupiga vita ufisadi, lengo likiwa ni kuwapa ahueni mafisadi.

  Alisema hali hiyo ya ‘kuwazuga' wananchi ikiendelea nchi itaingia katika vurugu, na akato mfano wa mgomo wa walimu na kitendo cha walimu hao kumpiga rais wao, akiongeza kuwa ni dalili za wazi za wananchi kuchoshwa na jinsi nchi inavyoendeshwa.

  "Angalia walimu walichofanya kwa rais wao; huwezi kufanya hivyo kwa kiongozi wako bali hizo zilikuwa ni hasira ndio zilizofanya hivyo. Walimu wana hasira na kimsingi ni ishara za mmomonyoko wa misingi ya kitaifa," alisema Zitto.

  Akirejea takwimu za serikali zilizotolewa na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo, Zitto alisema takwimu zilizotolewa zinapingana na hali halisi kwa kuwa pamoja na serikali kusema kwamba umasikini umeshuka kwa asilimia mbili, bado Watanzania wanazidi kuwa masikini.

  "Takwimu za serikali zinaonyesha kwamba umasikini umeshuka kwa 2.6% lakini kwa upande wa watu mwaka 2005 kulikuwa kuna Watanzania masikini milioni 11.7 na sasa wameongezeka hadi milioni 12.7. Ilani ya Uchaguzi ya CCM inasema kwamba watapunguza umasikini kwa kiasi cha nusu. Kwa maana hiyo ilitakiwa mwaka 2010 upungue na kuwa na masikini milioni tano lakini sasa unaongezeka kwa watu milioni moja," anasema na kuongeza;

  "Inaonyesha kwamba sera za CCM zimeshindwa kufanya kazi japo uchumi unakuwa kwa asilimia sita (6%); kumekuwa na fedha nyingi za wafadhili; uzalishaji wa madini na utalii vimeongezeka lakini kwa kipindi cha mwaka 1991-2007 umasikini ulishuka kwa asilimia tano tu wakati wenzetu wa Uganda kwa kipindi cha 1995-2006, umasikini umeporokoka kwa asilimia 25, hii ikiwa na maana wamepunguza umasikini kwa robo, kwetu, sisi pamoja na hadithi nyingi na kuwakumbatia Marekani na mataifa makubwa, umasikini umeongezeka," alisema.

  Alisema wananchi wamekwisha kugundua kwamba hali ilivyo sasa ni dalili za wazi za kushindwa kwa sera, uchovu wa ubunifu huku nchi ikigawanyika kwa matabaka kati ya watu ambao uchumi wao unakua na wengine ambao wanaangamia.

  "Uchumi unaokua ni uchumi wa sekta ya mawasiliano, utalii na madini wakati uchumi wa wakulima unadidimia bila ya kuwapo kwa ubunifu wowote wa kuwainua watu masikini, halafu utegemee wananchi wakushangilie?" alisema Zitto.

  Aliibeza serikali kudharau misukosuko ya kiuchumi inayoikumba dunia kwa sasa na kusema kudharau hali hiyo ni uvivu wa kufikiri.

  "Watu wanaamini kwamba sisi huku Tanzania hatutaathirika; wanabweteka huku viongozi wetu hawatulii. Ukweli ni kwamba nchi yetu itaathirika mno kutokana na kuyumba kwa uchumi wa dunia," alisema.

  "Ukiangalia, tunategemea madini na utalii na katika sekta ya madini utaona kwamba makampuni yote yanaendeshwa kwa kusaidiwa na mikopo ya benki za nje, benki ambazo ndizo ama zimeyumba ama kufa, na sasa hazina fedha za mikopo. Tumeanza kusikia makampuni yameanza kusimamisha watu kazi.

  "Sekta ya utalii tunayoitegemea nayo lazima itaguswa kwani tunategemea watalii kutoka Marekani na Ulaya. Tutarajie fedha tulizotegemea katika sekta ya utalii zitashuka, hatutakuwa na watalii wengi," alisema Zitto.

  Kuhusu mikopo na misaada kutoka mataifa makubwa, Zitto alisema kwa sasa mataifa hayo yanatumia fedha nyingi kuokoa mabenki yao na uchumi wao, na hivyo kuna kila dalili kwamba fedha za misaada zitapungua kwani IMF na Benki ya Dunia wanajadili jinsi ya kupunguza misaada.

  Alisema ni lazima kwa taifa masikini kama Tanzania kuchukua hatua kwa kubana matumizi ili kujiandaa na wimbi la kuyumba kwa uchumi wa dunia, badala ya kuendelea kutumia fedha nyingi kwa shughuli zisizo za lazima kama safari za viongozi kwa kutumia madaraja ya juu ya ndege.

  "Pamoja na uchumi duniani kuyumba, kuna bidhaa hazitaathirika kama vile dhahabu na fedha. Bei ya dunia ya dhahabu na fedha haitaathirika kwani Wazungu hununua dhahabu na fedha kutunza mali zao. Ni lazima tufanye mabadiliko ili tuweze kunufaika kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa hizi, vinginevyo tutaikosa fursa hii kama wakati wa mwanzo wa uwekezaji katika sekta ya madini. Viongozi wetu kama vile hawaoni," alisema.

  Katika siku za karibuni kumekuwapo na matukio ya kukata tamaa ikiwa ni pamoja na migomo, maandamano na kuhitimishwa na vurugu dhidi ya viongozi na matatizo yote hayo yamekuwa yakitatuliwa na serikali kwa mtindo wa ‘zimamoto', na baadhi kuzimwa kwa propaganda bila kuwapo kwa utatuzi wa kudumu.

  Migomo ya wafanyakazi wakiwamo walimu, ilitanguliwa na maandamano ya wanafunzi wa shule za sekondari wa Dar es Salaam, ambao walibeba mabango yakiwa na maneno makali yanayoushutumu uongozi wa serikali baada ya kupandishwa kwa nauli ya daladala kutoka shilingi 50 na hadi shilingi 100.

  Mbali ya walimu kumekuwapo na maandamano ya mara kwa mara ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, sambamba na migomo ya madaktari na wanafunzi wa vyuo vikuu vilivyoko Dar es Salaam na hivi karibuni mgomo ulihamia Chuo Kikuu cha Dodoma.

  Hayo yakiendelea nchi imekuwa ikiyumbishwa na tuhuma za ufisadi, wananchi wengi wakiwamo wanafunzi wakitaka hatua za dhahiri kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa; huku serikali ikionekana kuyumba katika kufanya maamuzi ya kufikisha mahakamani wahusika.

  Tayari chombo chenye jukumu la kupambana na rushwa, Taasisi ya Kuzuia ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kimeshindwa kutekeleza ahadi yake ya muda mrefu ya kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa kesi za ufisadi; huku watuhumiwa wa wizi wa fedha za EPA wakiendelea kubembelezwa walipe fedha hizo kabla ya mwisho wa mwezi huu.

  Wiki hii, imeripotiwa kwamba watuhumiwa dhaifu wa EPA na wa tuhuma nyingine ndio watakaofikishwa mahakamani kama kafara, huku watuhumiwa wakubwa wakiwa salama kutokana na kuwa na uwezo wa kulipa fedha walizokwapua BoT.
   
Loading...