Taazi: Sheikh Alhad Omar Kawambwa

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,925
30,273
SHEIKH ALHAD OMAR MWALIMU WA QUR'AN ALIYEWAFUATA WANAFUNZI BADALA YA WANAFUNZI KUMFUATA MWALIMU

Jana asubuhi na mapema hata hapaja pambazuka vyema Tawfik Kazaliwa mmoja wa vijana wa marehemu Sheikh Alhad Omar akawa keshanifikia nyumbani kunitaarifu kuhusu msiba.

Nikamfahaisha kuwa taarifa ninazo.

Tawfiq katoka mbali Buguruni na mida hii keshafika zawiyyani Magomeni ulipo msiba na amekwishafika kwangu.

Nimejiinamia uzito wa msiba wa Sheikh Alhad unaninyong'onyeza.
Akili yangu inapita kwanza Masjid Badawy, Kisutu.

Sheikh Ismail Mohamed alikuja Badawy na akawa mwanafunzi akisomeshwa na Sheikh Alhad Omar na Ustadh Adam Ahmad.

Wote hawa na mwanafunzi Ismail Mohamed wakaja kuwa mabingwa katika usomaji wa tajwid.

Wote hawa mabingwa katika usomaji wa Qur'an.
Sheikh Ismail Mohamed tumemzika miezi michache iliyopita.

Sijaweza kujua nani katika hawa watatu ni bingwa aliyemshinda mwenzake katika usomaji wa tajwid.

Kasema msemaji, ''Ikiwa wewe unaisikia Qur'an inasomwa na moyo wako haujaathirika basi jua wewe si mzima unahitaji kulazwa hospitali uaguliwe kwani wewe ni mgonjwa.''

Hakika ikiwa utamsikia Sheikh Alhad Omar anasoma Qur'an na wewe ikawa inaingia sikio moja inatoka la pili basi jua moyo wako una maradhi.

Sheikh Abubakar Mwilima anahadithia anasema walikwenda bara sehemu ambayo wenyeji wao wengi si Waislam.

Walikwenda kule kuwafikishia watu wa huko ujumbe wa Allah na ulikuwa mhadhara wa wazi.

Sheikh Alhadi Omar alifungua mhadhara ule kwa kusoma Qur'an Tukufu.
Alisoma, ''Surat Maryam,'' sura katika Qur'an ambako anaelezwa mama yake Nabii Issa.

Sheikh Mwilima anasema, ''Sijapata hata siku moja kumsikia Sheikh Alhad anaisoma Qur'an kama siku ile.

Watu hawa walikuwa hata siku moja hawajapata kuisikia Qur'an katika masikio yao kwa wao kuwa kitako hadhir kuisikiliza.

Sisi Waislam wachache tulikuwa tunafikisha ujumbe wa Allah kwa hawa ndugu zetu malaika katika miili yetu ilikuwa imesimama.

Wenyeji wetu nawaangalia wametuia tuli wanasikilza jambo ambalo katika mihadhara ya watu wengi huwa si kawaida kwa ajili ya pitapita ya watu.

Palikuwa na utulivu wa ajabu.
Sauti pekee iliyokuwa ikisikika kutoka vipaza sauti ilikuwa sauti ya Sheikh Alhad Omar.

Kati kwa kati, anatoka njia moja ya usomaji anaingia nyingine, anatoka hii, anaingia nyingine.'''

Sheikh Mwilima alimaliza.
Nilimwelea Taufik Kazaliwa kuwa nikifahamiana na Sheikh Alhad Omar kwa miaka mingi.

Taufik akanishangaza aliponiambia kuwa hilo analijua.

Nikamuuliza kajuaje?
"Sheikh Alhad kanieleza," akanijibu.

Ikawa sasa ni zamu yangu kushangaa.
Nilisikia furaha moyoni kwa sheikh kujinasibisha na mtu mdogo kama mimi.

Leo tuko Msikiti wa Kichangani katika maziko ya Sheikh Alhad Omar wanafunzi wake mmoja baada ya mwingine wakawa wanasoma Qur'an kwa si zaidi ya dakika tano.

Naam kwangu mimi niliyekuwa namfahamu sheikh na usomaji wake nilikuwa pale namsikia Sheikh Alhad Omar mwenyewe kupitia wanafunzi wake.

Umri ukisogea machozi hayawi mbali na macho.

Lakini haiwezekani kumtaja Sheikh Alhad Omar bila kumtaja Ustadh Adam Ahmed Abdallah kwani hawa walikuwa mfano wa watoto pacha.

Sheikh Alhad Omar akiwa kijana mdogo sana alitoka kijijini kwao Kitiku kuja Kaole, Kisiju kusoma kwa Maalim Abubakar aliyekuwa akisomesha Madrasa Nur.

Kipindi hicho hicho na yeye Ustadh Adam akatoka kwao kisiwani Kwale kuja Kaole kusoma kwa Maalim Abubakar na hapo ndipo vijana hawa wawili walipofahamiana na wakawa pamoja hapo chuoni.

Kipindi hicho Shariff Hussein Badawy alikuwa ametoka Lamu amekuja Dar es Salaam kwa nia ya kusomesha Uislam.

Sheikh Ramadhani Abbas aliyekuwa na madras yake maarufu Mtaa wa Mkunguni karibu na New Street (sasa Lumumba Avenue) akamwambia aende Kisiju kwa Maalim Abubakar.

Ilikuwa hapo Madras Nur, Kisiju ndipo Shariff Hussein alipowakuta watoto wawili, Alhad Omar na Adam Ahmed wanasoma wakiwa wanafunzi wa Maalim Abubakar.

Shariff Hussein aliwasomesha vijana hawa kwa miezi sita kisha akaamua kuwachukua kujanao mjini Dar es Salaam waendelee na masomo.

Vijana hawa wakaendelea na masomo yao katika madrasa ya Sheikh Ramadhani Abbas.

Katika kipindi hicho palikuwa na msikiti mdogo Kisutu jirani na Soko Mjinga uliokuwa umetelekezwa.

Liwali Ahmed Saleh aliyekuwa Liwali wa Dar es Salaam wakati ule akamwambia Shariff Hussein Badawy aende akautengeneze msikiti ule ili upate kutumika na yeye afungue chuo hapo.

Msikiti ulikuwa wa udongo na kulikuwa na ukuta uliokuwa umeanguka.

Mpashaji habari wangu kaniandikia kunieleza kuwa, ''Sheikh Alhad ndiye katika waliokandika ukuta uliobomoka, na kuanza kusoma hapo.''

Msikiti huu ukaja kujulikana kama Masjid Badawy na ukapata umaarufu mkubwa kwa kosemesha Qur'an na usomaji wa tajwid.

Hapa Badawy pakawa na darsa kubwa akisomesha Sheikh Hassan bin Ameir aliyekuwa mufti wa Tanganyika na darsanhii ilitia fora kwa kuhudhuriwa na masheikh wakubwa wa Dar es Salaam kama Mzee Ali Comorian, Shekh Digila, Sheikh Ramadhani Abbbas kwa kuwataja wachache.

Darsa hii haikuwa na uchache wa wasomaji wa Qur'an kama Sheikh Alhad Omar, Ustadh Adam Ahmed na Shekh Ismail Mohamed.

August Nimtz katika kitabu chake maarufu, ''Islam and Politics in East Africa,'' ametaja darsa hii kwa sifa kubwa.

Uhuru wa Tanganyika mwaka wa 1961 ulikuja na changamoto ambazo hakuna aliyezitegemea.

Masjid Badawy ilikuja kukutwa na msiba mkubwa pale mwaka wa 1963 serikali ilipomfukuza muasisi wake Shariff Hussein Badawy Tanganyika kama muhamiaji asiyetakiwa na kurudishwa kwao Kenya yeye na nduguye Seyyid Mwinyibaba.

Nimemsikia Shariff Hussein akisema kuwa yeye binafsi alishiriki mara kadhaa katika dua za kuiombea Tanganyika ijitawale.

Juu ya pigo hili Sheikh Alhad Omar na wenzake waliendelea kuwapo Masjid Badawy bado vijana wakawa wanasoma na wanasomesha.

Darsa la Mufti Sheikh Hassan bin Ameir likawa linaendelea hapo msikitini darsa nyingine akifanya Msikiti wa Ngazija.

Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa Zanzibar na Tanganyika mwaka wa 1964 ulileta changamoto mpya Masjid Badawy.

Msikiti huu ukawa unatazamwa kwa jicho baya kuwa huenda kwa kuwa waumini wengi kutoka Zanzibar walikuwa wakisali pale basi hao ni wapinga mapinduzi.

Lakini kwa ukweli kwa ajili ya kuwa jirani na Kariakoo msikiti wa Badawy uliwavutia waumini wengi kusali hapo na kusikiliza darsa za Sheikh Hassan bin Ameir.

Mwaka wa 1968 Masjid Badawy ika ikapata pigo jingine pale Sheikh Hassan bin Ameir alipokamatwa usiku na akapakiwa ndani ya ndege na kurudishwa kwao Zanzibar.

Kipindi hiki pakawa na kamata kamata ya masheikh na kuwekwa kizuizini chini ya Preventive Detention Act ya mwaka wa 1962.

Hakika uhuru wa Tanganyika ulikuwa umekuja na changamoto ambazo hakuna hata mtu mmoja alizitegemea.

Masheikh waliokuwa mstari wa mbele katika kusoma na kusomesha pale Masjid Badawy kama Shariff Adnan, Maalim Matar na Mzee Ali Comorian wakawekwa kizuizini.

Haya yote Ustadh Alhad Omar kayashuhudia kwa macho yake.
Ustadh Alhad Omar bila shaka alipata somo kubwa sana.

Kwake yale yalikuwa darsa tosha lililomfunza mengi.

Ukiangalia maisha yake kuanzia pale alipoamua kukaa kitako na kusomesha alichukua mwelekeo mwingine kabisa.

Sheikh Alhad Omar alisomesha Dar es Salaam na pia alitoka na kwenda nje ya mipaka ya jiji kusomesha.

Sheikh Alhad Omar alifanya kazi hii kimya kimya.

Kupitia njia hii ya usomeshaji na akikubali kuwa nyakati zimebadilika na yeye kubuni njia mpya za kusomesha Sheikh Alhad Omar alipata mafanikio makubwa kupita kiasi.

Lakini si wengi walikuwa wanajua mafanikio haya.

Baada ya maziko Makaburi ya Mwinyimkuu nikawa nimekaa kivulini na Abdallah Tambaza wakapita vijana wadogo watano akawaita kwa kuwa walikuwa hawakutuona.

Baada ya kusalimiana na wale vijana sasa wanatumba rukhsa ya kuondoka Tambaza aliwaomba dua.

Tulifanya dua kisha vijana wale wakaondoka.
Tambaza akaniambia, ''Usiwano wale vijana kwa udogo ule ukawadharau.

Wale ni wanafunzi wa Sheikh Alhad Omar na wote wale watano ni maimamu katika msikiti mitano tofauti hapa Dar es Salaam.

Hawa vijana pia ni walimu wa Qur'an wamekuja hapa kumzika sheikh wao.''
Allah amghufirie dhambi zake ndugu yetu Sheikh Alhad Omar na amtie pepo ya Firdaus.

Amin.

PICHA: Ndani ya Msikiti wa Kichangani, Shariff Badawy katika ujana akiwa na mwanafunzi wake Sheikh Ismail Mohamed na picha ya mwisho Ustadh Adam Ahmad Abdallah.

Screenshot_20220410-071815_Facebook.jpg
 
Ngome...
Ukisoma historia ya sheikh na misukosuko iliyopitia Masjid Badawy utapata jibu.

Rejea soma hiyo taazia.

Ondoa BALUKTA katika swali lako ibaki BAKWATA.
Kuna haja ya wewe kuandika historia ya uislam na wanazuoni wake.Unayafahamu mengi kuhusu hayo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom