Taasisi za dini, ujasiriamali vipi huko?

Samahani

JF-Expert Member
Oct 29, 2018
222
335
Najitahidi kukumbuka miaka kadhaa nyuma ambapo, lilikuwa ni jambo la kawaida kukuta taasisi nyingi sana za dini zikiwekeza sana kujenga tabia ya ujasiriamali, tena hasa kwa vijana na akina mama.

Navikumbuka baadhi ya vikundi vya vijana wakati ule walikuwa na shughuli kama kutengeneza tofali, ufundi seremali, uashi, kusuka na kutengeneza vifaa mbalimbali na vilikuwa vikiuzwa karibu na majengo ya taasisi, hasa siku za ibada na zilikuwa zina soko kubwa sana kutokana na wingi wa waamini pia.

Hata katika shule za sekondari, nakumbuka kulikuwa na vikundi vya wanafunzi kama UKWATA, CASFETA, TAMSA, TAYOMI, TYCS, ASSA na vingine ambavyo vilikuwa na miradi iliyokuwa inafanya shughuli hizi, wengine palepale shuleni na wakati mwingine, kwenye taasisi zao. Kule seminari ndiko sasa kilimo na ufugaji vilishamiri mpaka kuwa na ziada la kuuza baada ya kula.

Hebu ipitie bajeti ya sabuni, tofali, mbogamboga na matunda, nyama, kuku, mafuta ya kula, mikate, mavazi na vingine kwa mwaka ilivyo kubwa!!! Hivi hatuna fursa tunaweza kuwapa waamini, wakawa wajasiriamali kwa mahitaji haya, wakayatengeneza na kuuza huku na kule kwa kuwasaidia zaidi wakue kiuchumi ili walete sadaka pia?

Shughuli hizi, kama tutakumbuka vema, zilisaidia sana kuondoa utegemezi katika familia na pia, kuondoa msukumo wa makundi rika. Hata mimi niliwahi kuwa mnufaika wa semina moja ya ujasiriamali ambayo ilikuwa msaada mkubwa kwelikweli.

Ziko wapi hizi shughuli kwenye taasisi zetu za dini? Uko wapi msukumo wa dhati kutoka kwa tasisi hizi ili kuendeleza kundi kubwa la wanaohitaji haya?Tunakubaliana kuwa, miaka ya nyuma, taasisi hizi zilikuwa zikijiendesha kwa kiwango kikubwa kutoka kwa wahisani, mashirika ya misaada na nchi wafadhili. Lakini tulishaambiwa tujitegemee, na tunapaswa kuwa tumejiwekea mazingira ya kusimama wenyewe.

Sasa mbona tunaua tena miradi ya ufugaji kwenye makanisa, maduka misikitini, shughuli za utengenezaji mali kule tunapoabudu na kuwajengea uwezo waamini kulisaidia na kusaidia na kuzijenga taasisi wao wenyewe?

Badala yake sasa, kila taasisi ya dini inawaza kuanzisha shule tu!! Tumekuwa na utitiri wa shule na vituo vya malezi kuliko idadi ya 'maombi' tunayoyatoa. Si jambo baya hata kidogo. Kazi hii ya miradi katika taasisi iendane basi na fursa tunazozitengeneza kwa makundi muhimu ya waamini wetu!

Ni rahisi zaidi kwa taasisi ya dini kumiliki mashamba makubwa, maduka ya bidhaa, saluni na sehemu nyingine.

Mosi, kitaasisi tuna maeneo ya kutosha ambayo mengi hayajaanza kutumika. Viwanja, mashamba, visima na vingine ni miundombinu muhimu sana katika kujiajiri

Pili, taasisi zina muingiliano wasomi wazuri wa kitaifa na kimataifa ambao ni viongozi wa kidini. Sasa hawa si ndio injini ya kutunoa kimwili ili tuwe mguu sawa pia kiroho? Mbona hatuwatumii kwa namna ya mwili baada ya kuwatumia kiroho pale madhabahuni na katika mimbari?

Tatu, taasisi inamiliki watu wengi kwa wakati mmoja na hivyo kurahisisha masoko. Ibadani mnatoka watu 5000 kwa siku, kwanini kikundi cha vijana kisifanyiwe hamasa wakauza kuku wao ambao wamevunwa katika viunga vya eneo la taasisi, tukalipia kodi ya eneo na huduma zingine muhimu, kisha faida vijana wakachukua, wakatoa sadaka na kilichobaki wakapeleka dagaa makwao?

Nne na muhimu zaidi, taasisi zina uwezo wa kuwakutanisha vijana hawa na Mungu wao kwa kuwasaidia katika kuutafuta mkate!! makundi mengi ya wajasiriamali wana vipaji na bidhaa nzuri, lakini hawana masoko wala wa kuwasemea Leo hii taasisi yoyote ya dini ikaamua kuanzisha sehemu ambako vijana wanajifunza na kisha kuendelea na shughuli za kilimo, sio swala la muda mrefu. Na huko watakutana na wataalamu wa kilimo ambao wanaweza kutoa elimu, ushauri, vitendea kazi na hata masoko. Matokeo yake, vijana hawa watamtumikia Mungu kwa tija zaidi.

Tano, nimesema hapo juu kuwa, wajasiriamali wengi wanahitaji kusemewa. Tuache kuwa na harambee za kuchangia ujenzi na magari ya taasisi tu. Twende mbali kwa kuwatambulisha wajasiriamali hawa na pia, kuzitumia bidhaa zao. Taasisi ndio wawe wanunuzi pia ili mambo yaende!!!

Binadamu ni mwili na roho. Mwili dhaifu unazidi kuidhoofisha hata roho. Taasisi za dini zitusaidie katika yote mawili. Mwili upate mahitaji, na roho ipigwe msasa, iache wizi na ukahaba na mengine "yatuzikayo", baadae kila kimoja kiende kinapostahili.

Huu sio wimbo wa taifa!
Hapana sehemu nimesema kuwa huu ni mwarobaini wa yanayotusumbua na wala sijasema haya yanaweza kufanyika kila mahala, kwa matokeo yanayofanana kwa wote. Lakini kwakuwa ni njia zinazoweza kuwasaidia wachache, tuzijaribu!!!

Wasalaam,

Mwenye kunoa Lubu...
 
Back
Top Bottom