MANGI MASTA
Senior Member
- Jul 14, 2011
- 175
- 56
Waziri kivuli wa kambi rasmi ya upinzani mh.Sugu analihutubia bunge..ila jamaaa kweli ni mtetezi wa wasanii kwani analia sana kuhusu wizi wa kazi za wasanii.
HOTUBA YAKE HII HAPA:
ZAIDI Soma post hii
HOTUBA YAKE HII HAPA:
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHE.JOSEPH MBILINYI, (MB) WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO, KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012
UTANGULIZI
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai, afya njema na kunipa fursa ya kipekee ya kufanya maajabu yenye manufaa kwa taifa langu; kwa baraka zake, niliweza kung'ara kwenye sanaa na kuwa nyota wa muziki wa Bongofleva; kwa uwezo wake, leo nimekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini; na kwa mapenzi yake, mimi Msanii wa Bongofleva sasa nimekuwa Waziri Kivuli wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha maoni na mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni, na Michezo, kwa mwaka wa fedha 2011/2012, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99 (7) toleo la 2007.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua na kuthamini imani na heshima kubwa niliyopewa na wananchi wa Jimbo la Mbeya Mjini, katika uchaguzi mkuu uliopita. Licha ya kuletewa mabomu ya machozi, virungu na bado hakuna yeyote kati yetu aliyeogopa. Uwongo haukuweza kufunika ukweli na hata rushwa haikuweza kurubuni akili. Wananchi kwa umoja wao walijitoa mhanga kulinda kura zetu bila woga, na hatimaye dunia nzima inajua na imekubali kuwa mimi ndiye SUGU na CHADEMA si chama legelege, bali ni chama makini na kinachoaminika mbele ya jamii.
Mheshimiwa Spika, namshukuru na kumpongeza kwa moyo wa dhati kabisa Katibu Mkuu wa chama changu, Dk. Willibrod Peter Slaa, na makamanda wote wa CHADEMA nchi nzima kwa kazi kubwa tuliyoifanya katika uchaguzi mkuu uliopita, na kwa harakati nzito tunazoendelea kuzifanya za kuielimisha jamii juu ya haki zao za msingi. Watapiga kelele sana, lakini hatutarudi nyuma, tunasonga mbele mpaka kieleweke.
Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima namshukuru Kiongozi Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani na Mwenyekiti wa CHADEMA, Mhe. Freeman Aikael Mbowe (Mbunge) kwa kuniamini na kuniteua kuwa Waziri Kivuli wa wizara hii nyeti; Naibu Kiongozi Mhe. Kabwe Zuberi Zitto (Mbunge) na Mnadhimu Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani, Mhe. Tundu Lissu, kwa ushirikiano wao mkubwa wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu ya kibunge.
Mheshimiwa Spika,nachukua fursa hii pia kuwashukuru kwa dhati wadau wote wa Sekta ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kwa kutuamini na kuthamini kazi kubwa ya uwakilishi inayofanywa na Kambi rasmi ya Upinzani bungeni, hata kuamua kutupa ushirikiano mkubwa katika maandalizi ya hotuba hii.
Naomba niwatambue baadhi ya wadau hao kwa shukrani kama ifuatavyo: ·Baraza la Habari Tanzania (MCT) ·Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) ·Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na, ·Rulu Arts Promotion SEKTA YA HABARI Weledi na Maadili ya Uandishi wa Habari.
Mheshimiwa Spika, vyombo vya habari ni taasisi muhimu sana katika ujenzi wa taifa lenye kufuata misingi ya demokrasia na utawala bora. Vyombo vya habari vina dhima kubwa ya kutoa habari na taarifa kwa umma wa Watanzania kuhusu mambo yanayohusu maisha yao na vilevile kutoa elimu na burudani. Vyombo vya habari ni kiungo muhimu cha kuunganisha jumuiya mbalimbali, kujenga utaifa, umoja na kuhimiza maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Vyombo vya habari kwa ujumla wake ni taasisi yenye nguvu. Ina uwezo mkubwa wa kujenga na vilevile kubomoa ikiwa vitatumiwa na kujiendesha vibaya au kuingiliwa uhuru wake. Hivyo basi, wakati vyombo vya habari vina wajibu wa kufanya kazi kwa kuzingatia umakini, weledi na maadili ya uandishi wa habari, Serikali nayo ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha uhuru na haki za kutafuta na kupata habari vinalindwa.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiotiliwa shaka kuwa baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikikiuka kabisa maadili ya uandishi wa habari. Kinachosikitisha zaidi ni pale ambapo baadhi ya waandishi wa habari na baadhi ya vyombo vya habari na ambavyo vimepewa dhamana kubwa na jamii wanapokubali kutumiwa na baadhi ya watu wenye nguvu ama za kisiasa au za kifedha ili kuendeleza ajenda zao binafsi. Hili ni jambo lisilopendeza hata kidogo na halina mustakabali mzuri kwa amani na maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kinachosikitisha zaidi, vyombo vya habari vya Serikali na hapa nalizungumzia gazeti la serikali Daily News kuongoza katika ukiukwaji wa maadili ambapo katika kipindi cha mchakato wa uchaguzi mkuu uliyopita gazeti hili lilichapisha tahariri ya uchochezi iliyosema, "Kamwe Dk. Slaa hatakuwa rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania." Maoni haya ya Mhariri yalilenga kuleta uchochezi na kujenga hoja kwamba hata kama Watanzania watamchagua Dk. Slaa kuwa rais wao, lakini kamwe hatakabidhiwa jukumu la uongozi, jambo ambalo ni la hatari kwa usalama wa taifa.
Mheshimiwa Spika, jambo la hatari zaidi hapa ni kwamba walioendesha vitendo hivi vya uchochezi ni wahariri wa gazeti la serikali ambalo lilitakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa vyombo vingine vya habari nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inaitaka serikali ilieleze Bunge hili tukufu imemchukulia hatua gani Kaimu Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo ambaye aliidhinisha kuchapishwa kwa tahariri hiyo? Je, Idara ya Habari na Maelezo iliwahi kuandika barua kwa mhariri huyu kumuonya kama ambavyo imekuwa ikifanya hivyo kwa magazeti mengine; hata kabla ya habari haijaandikwa, tayari barua inakuwa imeandaliwa na kinachosubiriwa ni gazeti kuchapishwa na barua hiyo kufika kwa wahusika?
Kama serikali haijamchukulia hatua, waziri anaweza vipi kuwa na mamlaka ya kuadhibu vyombo vingine vinavyodaiwa kukiuka maadili ya uandishi wa habari wakati yenyewe imeshindwa kuwajibisha wahariri wa gazeti lake? Mheshimiwa Spika, kuna tabia imezuka ya viongozi wa Serikali kuvitisha vyombo ya habari pale vinapotoa udhaifu wa watendaji Serikalini, kama ilivyotokea hapa Bungeni wakati Mhe. Waziri Ofisi ya Rais mahusiano alipotoa vitisho kwa gazeti la Mwananchi. Kambi ya Upinzani inalaani kitendo hicho na kuitaka Serikali iache mara moja.
Mheshimiwa Spika, hili ni jambo ambalo wote tunatakiwa tulikemee kwa nguvu zetu zote na kila inapowezekana tuwaumbue na tuwataje wale wote wanaoshiriki katika matendo haya ambayo hayana nia njema sio tu kwa tasnia yenyewe ya habari kwa kuipa jina baya na kuipaka matope, bali pia kwa nchi yetu kwani tuna mifano dhahiri hapa Afrika na kwingineko duniani juu ya athari ambazo zimewahi kutokea vyombo vya habari vilipotumika vibaya. Na sote tunakumbuka yaliyofanywa na vyombo vya habari vya serikali kule Rwanda na maafa yaliyotokea. Sheria ya Haki ya Kupata Habari.
Mheshimiwa Spika,haki ya kupata habari ni haki ya msingi ya binadamu na inalindwa na Ibara ya 18 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni haki ambayo inamhusu kila Mtanzania bila ya kujali wadhifa au daraja lake kwenye jamii, umri au jinsia. Mwaka 2006, na nataka niamini kwa nia njema kabisa, Serikali ilianzisha mchakato wa kutunga sheria ya Uhuru wa Habari kwa kutoa rasimu ya muswada wa sheria hiyo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo rasimu ya muswada huo ilikataliwa na wadau kwa sababu haikukidhi haja wala viwango vya sheria kama hiyo vinavyotakikana. Mwaka 2007, Serikali iliitikia wito wa wadau wa habari na haki za binadamu wa kutaka kuwepo na sheria mbili tofauti na kutenganisha rasimu yake ya Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Habari na kutengeneza rasimu mbili, moja ya sheria ya Haki ya Kupata Habari na nyingine ya sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari.
Mheshimiwa Spika, hoja ya kutenganisha muswada huo ilikuwa na bado, ni muhimu sana, kwa sababu sheria ya haki ya kupata habari ni mtambuka na inahusu haki ya kikatiba ya Watanzania wote. Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ni ya kisekta na inahusiana zaidi na kutoa mwelekeo wa jinsi vyombo vya habari vitakavyofanya kazi nchini.
Mheshimiwa Spika, mchakato huo ulipata muitiko mzuri kutoka kwa wadau mbalimbali wa habari na wanaharakati wa haki za binadamu ambao kwa umoja wao walitembea nchi nzima kukusanya mawazo na mapendekezo ya wananchi kuhusu Sheria ya Haki ya Kupata Habari. Walipeleka mapendekezo yao kwa Serikali ili yaweze kujumuishwa katika mchakato wa utungaji wa sheria.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inasisitiza kuwa Sheria hii ni muhimu sana, kwani itaimarisha utawala wa wazi na uwajibikaji. Utawala ulioshamiri katika mila za usiri ndio ulioifikisha Tanzania yetu mahali pabaya. Ndio chanzo cha mikataba mibovu na kushindwa kwa uwajibikaji kwa sababu tu watendaji wabovu wanaweza kujificha katika kinga ya usiri.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa ahadi mwaka hadi mwaka kuhusu mchakato wa utungaji wa sheria hii muhimu. Lakini hadi leo hatujaona muswada wa sheria hiyo ukiacha ule ambao wadau wamependekeza. Kambi rasmi ya Upinzani tunaitaka Serikali kuuleta bungeni muswada wa sheria hiyo ndani ya mwaka huu, ili tuujadili na kupitisha sheria hiyo bila ya kukawia zaidi.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani tunaitahadharisha serikali kuwa isijaribu kuchakachua hata kidogo maoni hayo ya wadau, kwa sababu tumejiridhisha kuwa yana msingi na dhamira ya dhati ya kuboresha tasnia nzima ya habari na uhuru wake. Pendekezo la wadau limo katika Kiambatanisho Na. 1 cha hotuba hii. Tunachukua fursa hii kuwataarifu mapema wadau wote wa habari kwamba tutakuwa pamoja nao wakati wote wa harakati za kushinikiza muswada huo uletwe bungeni ndani ya mwaka huu. Tunataka sheria hiyo ipatikane mapema iwezekavyo ikiwa imebeba maoni yote ya wadau.
Mheshimiwa Spika, pamoja na umuhimu wa kupata sheria mpya ya vyombo vya habari, ni muhimu pia kuwapo kwa sheria inayokidhi mahitaji na inayokubalika kwa jamii yote ya wananchi. Sheria ya habari katu, si mali ya waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari pekee yao. Ni sheria ya Watanzania wote. Hii ni kwa sababu, haki ya kupata na kutoa habari, ni haki ya asili.
Mheshimiwa Spika, wakati wananchi wanasubiri sheria mpya ya habari, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuleta bungeni muswada wa kufuta sheria ya magazeti ya mwaka 1976 kwa kuwa sheria hiyo ni kinyume na Katiba. Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari.
Mheshimiwa Spika, katika sera ya Habari na Utangazaji iliyotolewa na Serikali na kupitishwa na Bunge lako tukufu mwaka 2003, kipengere cha 2.2.2 kinaelekeza kwamba; "Sheria mbovu za habari ambazo zimekuwa zikikosolewa na kulalamikiwa kwa kuwa haziendani na misingi ya kidemokrasia zitadurusiwa, kurekebishwa au kufutwa." Hivyo basi, Serikali iliahidi kuwa itatunga sheria mpya zinazoendana na wakati na kukidhi mahitaji ya kidemokrasia ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, tunasisitiza kuwa mapendekezo ya wadau yanakidhi kwa kiwango kikubwa ahadi hiyo ya Serikali na wadau walizipitia sheria 27 zinazogusa habari na kupendekeza sheria 17 miongoni mwa hizo ama zidurusiwe, zirekebishwe au kufutwa. Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka serikali isiendelee kusuasua katika jambo hili na ilete muswada bungeni wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ndani ya mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa shirika linalochapisha magazeti ya Serikali (DAILY NEWS NA HABARI LEO) halina Mtendaji Mkuu, toka alipoondolewa Mtendaji aliyekuwepo. Tangazo la kumtafuta mtendaji mpya mwenye sifa na hadhi ya kuongoza liliondolewa katika mazingira tatanishi. Hivi sasa shirika hilo limeyumba kiuongozi jambo ambalo limesababisha kushuka kwa uzalishaji. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuanzisha mchakato wa kumpata Mtendaji mkuu wa shirika hilo mwenye sifa na hadhi, kabla ya mwaka huu haujamalizika. MAENDELEO YA VIJANA Benki ya Taifa ya Vijana Ianzishwe.
Mheshimiwa Spika, sehemu kubwa ya watu wa taifa hili ni vijana, tukiendeleza vijana basi tutakuwa tumeendeleza sehemu kubwa ya taifa. Ni muhimu kama taifa tuweke vipaumbele vya makusudi vya kibajeti vya kuhakikisha vijana wanapewa kipaumbele cha kutosha na kujengewa mazingira mazuri ya kujikomboa.
Mheshimiwa Spika, ili kuanza kujenga mazingira mazuri ya kuchochea ajira nyingi kwa vijana kupitia shughuli za ujasiriamali na shughuli nyingine za kiuchumi, Kambi rasmi ya Upinzani, inaitaka Serikali ianzishe Benki ya Taifa ya Vijana. Tunapendekeza kuwa mchakato wa kuanzishwa kwa benki hiyo uanze ndani ya mwaka wa fedha wa 2011/2012, na benki hiyo iwe na masharti nafuu kwa manufaa ya vijana. Mchakato wa Baraza la Vijana la Taifa.
Mheshimiwa Spika, kwa mara ya kwanza Serikali iliahidi kuanzisha Baraza la Taifa la Vijana kupitia Sera ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 1996, na tangu wakati huo kila mwaka Serikali imekuwa ikiahidi hivyo hivyo, lakini hadi leo hakuna kilichofanyika.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani haiko tayari tena kuona Serikali hii ikiwapotezea muda vijana wa nchi hii. Tunamtaka Waziri atoe kauli ya moja kwa moja ya kuhakikisha kuwa mchakato wa kuanzishwa kwa Baraza la Taifa la Vijana unaanza mara moja na Baraza linapatikana ndani ya mwaka huu wa fedha. Haja ya Mabadiliko Idara ya Maendeleo ya Vijana.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inaamini kuwa hali mbaya ya maendeleo ya vijana nchini, pia inachangiwa na uongozi dhaifu usiokuwa na ubunifu wa kutosha wa Idara ya Maendeleo ya Vijana, ambao kwa takribani miaka 10 umekuwa na watu walewale kwenye nyadhifa takribani zote ikiwemo ile ya Mkurugenzi. Kwa hiyo, tunataka Serikali kuifanyia mabadiliko ya viongozi Idara hii ili kuleta ari na ubunifu mpya kikazi. Sanjari na hilo, tunapendekeza Idara hii iongezewe nguvu na raslimali. SEKTA YA UTAMADUNI.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli ulio wazi kuwa sekta ya utamaduni kwa sasa imepoteza mwelekezo kwa sababu mipango mingi ya maendeleo haizingatii umuhimu wa utamaduni wetu kwa tafsiri pana. Maendeleo ya jamii yoyote ile yanategemea utamaduni wa nchi husika, hivyo Kambi ya Upinzani inasisitiza kuwa ni lazima Serikali irudi nyuma na kujitathimini vizuri katika sekta ya Utamaduni.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tunaishi katika kipindi muhimu cha mpito wa historia na utamaduni ya tangu kizazi cha uhuru na kile kilichozaliwa baada ya uhuru, ni muhimu kuhakikisha kuwa historia na utamaduni wetu, unakusanywa, unachambuliwa na kuhifadhiwa vizuri kwa ajili ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo; Kambi rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa Serikali iunde Kamisheni Maalum ya Rais ya Historia, ambayo pamoja na mambo mengine, iwe na majukumu yafuatayo:
(i)Kufanya utafiti wa watu wote waliotoa mchango mkubwa wa kihistoria katika kupigania Uhuru wa Tanganyika, Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano ili waweze kukumbukwa na michango yao kuenziwa.
(ii)Kutambua maeneo, majengo, na sehemu mbalimbali zenye umuhimu mkubwa wa kihistoria.
(iii)Kupitia matukio muhimu ya historia yetu ili yaweze kuelezewa katika mwanga wa kihistoria. Hii ni pamoja na Uhuru, Mapinduzi, Muungano, Uasi wa Jeshi, Azimio la Arusha, Operesheni Vijijini, Vita ya Kagera, Enzi za soko huria, n.k.
(iv)Kukusanya vielelezo mbalimbali vyenye umuhimu mkubwa wa kihistoria kutoka watu binafsi, taasisi binafsi na nje ya nchi ili hatimaye vitu hivyo, viweze kuingizwa katika historia yetu kwa ajili ya kuwa ni urithi wa vizazi vijavyo.
(v)Kuandika ripoti maalum juu ya historia yetu na matukio mbalimbali ili yaweze kutunzwa kama sehemu ya historia yetu maalum.
(vi)Kutoa mapendekezo ya jinsi ya kuenzi utamaduni wetu muhimu pamoja na watu mbalimbali ambao walichangia katika matukio mbalimbali kwa namna ya pekee na ambao historia yetu haijawakumbuka ipasavyo.
SEKTA YA SANAA
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kutangaza maslahi kwenye sekta hii, kuwa mimi ni msanii wa muziki wa kizazi kipya (Bongofleva) na nimekuwa kwenye fani hii kwa muda mrefu sasa. Kwa uzoefu wangu na kwa niaba ya Kambi rasmi ya Upinzani, nachukua fursa hii kuieleza serikali kwamba: "Sanaa si mapambo au burudani tu kama ilivyozoeleka, bali Sanaa ni ajira inayoweza kubadilisha maisha ya Mtanzania yeyote anayejihusisha nayo na inaweza kabisa kuwa moja ya vyanzo vikubwa vya mapato ya Bajeti ya Serikali, ikiwa Serikali yenyewe itadhamiria kwa dhati kufanya mapinduzi makubwa katika tasnia hii".
Mheshimiwa Spika, taarifa mbalimbali kutoka nchini Marekani za mwaka 2007 zilionyesha kuwa; "Makampuni yanayotengeneza na kuuza kazi za hatimiliki yataendelea kuwa moja ya nguvu kubwa za uchumi wa Marekani, kwani mapato yatokanayo na filamu, muziki, michezo ya video, na mifumo ya kompyuta yanachangia zaidi ya asilimia 6.5 ya Pato la Taifa na kuajiri takribani watu milioni 5.4…" mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa sekta ya Sanaa ikifanyiwa mapinduzi makubwa inaweza kabisa kuwa moja ya vyanzo vikubwa vya bajeti ya Serikali yetu na kuchangia maendeleo ya taifa hili. Ikiwa Sanaa inachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa taifa kubwa kama Marekani; Je, Tanzania tuna maendeleo gani ya kujivunia hata tupuuze Sanaa? Bado hatujaipa sekta hii umuhimu wake unaostahili.
Mheshimiwa Spika, wasanii pamoja na Serikali bila kujua, wamekuwa wakinyonywa kimapato na wadhamini, wazalishaji, na wasambazaji wa kazi za Sanaa, hususan kwenye biashara ya kuuza muziki na filamu. Kwa mujibu wa utafiti wa Dkt. Jehovaness Aikaeli ambaye ni mchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema sekta ya muziki pekee ikifanyiwa maboresho, inaweza kuiingizia Serikali mapato ya kodi ya wastani wa shilingi bilioni 50 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, tafiti chache zilizowahi kufanyika, ukiwemo utafiti wa Taasisi ya RULU/BEST – AC, wa mwaka 2007/08, zimeonyesha kuwa Wasanii na Serikali kwa pamoja, wamekuwa wakipoteza mapato mengi yatokanayo na biashara ya kazi za sanaa, hususan muziki na filamu kama ifuatavyo: ·Maharamia wameendelea kurudufisha santuri na kanda za muziki, filamu na kazi nyingine za sanaa, na kujipatia mapato haramu kwa jasho la Wasanii, lakini hakuna hatua kali zinazochukuliwa kukomesha hali hii. ·
Wasanii wengi wamekuwa wakiingia mikataba isiyo na manufaa kwao baina yao na Wadhamini, Wazalishaji, Wasambazaji wa kazi za Sanaa na hivyo kunyonywa kimapato, kwa sababu tu ya kukosa uelewa mzuri wa masuala ya mikataba na kutokuwepo udhibiti wa kutosha wa Serikali. ·Serikali kwa mwaka 2007 pekee, ilipoteza mapato ya muziki, ya jumla ya shilingi bilioni 71.
·Kodi inayokusanywa na Serikali katika Sekta ya Muziki, inapatikana katika asilimia 12 tu ya kiwango cha mapato kinachotakiwa kulipiwa kodi kwenye sekta hiyo. ·Wakati wa utafiti iligundulika kuwa ni asilimia 12.5 tu ya Wafanyabiashara wa kazi za Sanaa, ndio waliokuwa wamelipa mirabaha, asilimia 87.5 hawakuwa wamelipa.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na wizi na uharamia huu wa kazi za Sanaa na kuokoa mapato ya Wasanii na ya Serikali, Kambi rasmi ya Upinzani inapendekeza yafuatayo:
COSOTA iwe Mamlaka.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Na.7 ya mwaka 1999 ifanyiwe marekebisho kwa lengo la kuipa meno zaidi ya kulinda haki na kuhakikisha Wasanii wananufaika na kazi zao. Moja ya mapendekezo ni kuifanya COSOTA kuwa chombo chenye nguvu zaidi katika kulinda kazi za Wasanii kuliko ilivyo hivi sasa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyokatika sehemu ya marekebisho tunayopendekeza, Kambi rasmi ya Upinzani tunataka Sura Na. 218 ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki, ifanyiwe marekebisho ili kuunda Mamlaka ya Hakimiliki Tanzania (COPYRIGHT REGULATORY AUTHORITY OF TANZANIA (CORATA) badala ya kuiacha COSOTA kama ilivyo hivi sasa.
Mamlaka haya yakishaundwa yatakuwa na nguvu zaidi ya kushughulikia mambo mbalimbali ya kazi za wasanii,yawe ndio msimamizi na mratibu wa masuala ya Hakimiliki kwa kushirikiana na vyama vya msingi vya wasanii vilivyopo chini ya BASATA,kama vile Chama Cha Muziki Wa Dansi Tanzania(CHAMUDATA) na kile cha wasanii wa muziki wa kizazi kipya yaani Tanzania Urban Music Association (T.U.M.A), tofauti na sasa ambapo COSOTA imebakiwa na kazi ya kusajili kazi za wasanii na kukosa nguvu ya kuzilinda.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa mwenye Hakimiliki ana jukumu la kulinda haki zake kwa kwenda mahakamani pale anapoona haki yake imepokwa na mtu au kikundi chochote, bado ipo haja ya kuhakikisha kuwa Polisi wetu wa upelelezi wanahusika moja kwa moja katika kulinda haki za Wasanii. Mathalan, nchini Marekani hawana polisi wa kulinda hakimiliki moja kwa moja, lakini Shirika lao la Upelelezi (FBI), limekuwa likifanya uchunguzi wa mara kwa mara kuhusu hakimiliki za wasanii, kila kunaporipotiwa suala la wizi wa kazi za msanii, na limekuwa linahusika moja kwa moja katika kutoa ushahidi na kusaidia kupatikana kwa haki ya msanii husika.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa taasisi za Serikali, Polisi na Forodha washirikiane kwa karibu na Mamlaka ya Hakimiliki na Hakishiriki tunayotaka ianzishwe (CORATA), kukomesha uharamia wa kazi za Sanaa. Forodha watengeneze utaratibu wa kutoza kodi kikamilifu kwenye kazi za muziki, filamu na Sanaa nyingine zote zinazouzwa nje ya nchi. Na mashirika ya uzalishaji wa kazi za muziki –waunde ushirikiano na taratibu zao za kukabiliana na uharamia wa kazi za sanaa kwa mapana yake.
Mheshimiwa Spika, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Februari mwaka huu, wakati akizindua kampeni ya kuzuia malaria ambayo iliwashirikisha baadhi ya wasanii, aliahidi kuundwa kikosi kazi (task force) kitakachowashirikisha COSOTA, Polisi, Tume ya ushindani, TRA, BRELA, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na wasanii mbalimbali wanaojihusisha na sanaa ili kutafuta ufumbuzi dhidi ya uharamia na wizi wa kazi za Sanaa.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka wizara kuliarifu Bunge hili, je kikosi kazi hicho kiko wapi mpaka leo? Na kama kiliundwa, kiliundwa kwa taratibu zipi, na kwanini suala hilo haliko wazi?
Mradi wa Stickers kwenye kazi za Sanaa
Mheshimiwa Spika, mbali na marekebisho hayo ya kisheria na kimfumo tuliyopendekeza, Kambi rasmi ya Upinzani pia tunaitaka Serikali ndani ya mwaka wa fedha wa 2011/2012, itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kuanzisha utaratibu rasmi wa kuwa na Stickers kwa ajili ya kazi zote za Sanaa, hususan kwenye kanda na Santuri za muziki, filamu, na kazi zote za Sanaa zinazoshikika na kuuzika. Hapa tunashauri kuwa mamlaka tunayotaka ianzishwe, yaani COPYRIGHT REGULATORY AUTHORITY OF TANZANIA) ishirikiane kwa karibu na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kuandaa utaratibu mzima wa kuwa na Stickers hizo na jinsi ya kuusimamia.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inaamini kuwa utaratibu rasmi wa kuwa na Stickers ukitumika sekta ya Biashara ya Kazi za Sanaa inaweza kupata mafanikio ya kuridhisha ndani ya muda mfupi. Mfano mzuri ni Sticker yenye nembo ya TRA inayowekwa kwenye bidhaa za Konyagi. Faida kubwa ambayo itapatikana kwa kuwa na Stickers kwenye kazi za Sanaa ni kuwa stickers hizi zitawezesha kubaini kazi halisi (Original) iliyofanywa na msanii mhusika dhidi ya kazi za bandia zilizorudufishwa au kughushiwa.
Sambamba na hilo, mapato ya Wanamuziki, Watunzi wa filamu na washirika wao pamoja na Serikali yataongezeka na hivyo mchango halisi ya sekta hii kwenye uchumi wa nchi utakuwa wazi. Mheshimiwa Spika, pia tuna taarifa kuwa Wasanii wengi kutoka nje ya nchi wanaofanya maonyesho mbalimbali hapa nchini wamekuwa hawatozwi kodi licha ya kulipwa fedha nyingi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Spika, tunaitaka Serikali kuanzia mwaka wa fedha wa 2011/2012, ihakikishe kuwa Wasanii hao wa nje ya nchi ambao wamekuwa wakilipwa dola laki 1hadi dola laki 4 kwa onyesho moja hapa nchini, wawe wanatozwa kodi ya kutosha, ili fedha hizo ziongezee bajeti kuu ya Serikali na kuwasaidia Watanzania wengi maskini.
Mheshimiwa Spika, tunaitaka Serikali kwa kushirikiana na vyombo husika, iweke utaratibu wa kuhakikisha kuwa pale Msanii wa ndani anapofanya onyesho au kazi ya pamoja na Msanii kutoka nje, basi kuwe na mgawanyo mzuri na wa haki wa mapato kati ya Msanii huyo wa Nje na Msanii Mzawa.
Mheshimiwa Spika, ili kuboresha Sekta nzima ya Sanaa nchini, na kuhakikisha inaongeza ajira zenye tija, na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji uchumi, Kambi rasmi ya Upinzani inapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe; ·Serikali ndani ya mwaka wa fedha wa 2011/2012,pamoja na kufanyia kazi tafiti zilizokwishafanywa na wadau mbalimbali wa sanaa, ifanye utafiti mahsusi na wa kina kuhusu Sekta nzima ya Sanaa (Feasibility Study), ili kubaini fursa na vikwazo vyote vilivyopo, na kuainisha njia na mikakati kabambe ya kuboresha na kuisimamia sekta husika, kwa manufaa ya Wasanii na uchumi wa nchi. ·
Kupitia matokeo ya utafiti huo, Wizara ndani ya mwaka wa fedha 2011/2012, iandae Mpango mahsusi wa Maboresho ya Sekta ya Sanaa, ambao pamoja na mambo mengine, ulenge kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato ya Sanaa na kuchochea ajira nyingi na zenye tija kwa vijana.
·Chuo Kikuu cha Sanaa cha Bagamoyo kipandishwe hadhi na kuwa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Kawawa cha Bagamoyo (Kawawa Memorial University – Bagamoyo). Lengo liwe ni kuhakikisha kuwa chuo hiki kinatoa mafunzo yote ya hali ya juu ya mambo ya sanaa, michezo na utamaduni kwa vijana wa Kitanzania na wale wanaotoka ng'ambo, huku tukimuenzi Hayati Mzee Rashid Mfaume Kawawa, kwa mchango wake mkubwa katika taifa hili alioutoa kwenye uongozi na Sanaa. ·
Serikali ihakikishe kuwa asilimia 90 ya bajeti zote za Wizara, Idara, Taasisi na Wakala wa Serikali zinazotengwa kwa ajili ya kunaksisha ofisi, iwe inatumia kazi za sanaa na samani zinazopatikana hapa Tanzania au zinazotokana na ubunifu wa Watanzania. Hii itachochea ajira katika kazi za Sanaa na kuweka ushindani wa kibiashara ambao utainua ubora wa kazi hizo.
·Masomo ya Sanaa yarudishwe katika ngazi zote za elimu katika shule za binafsi na serikali, ili kuchochea ubunifu na umahiri wa vijana katika kazi za sanaa na kuinua vipaji vyao mbalimbali. ·Serikali ihakikishe mafunzo ya Sanaa yanatolewa kwa vyuo vya elimu ili kuweza kupata walimu wa kutosha wa sekta hii. ·Mashindano ya ubunifu wa kazi za Sanaa yaanzishwe yakiwa ni sehemu ya mashindano ya michezo ya UMISHUMTA na UMISETA.
Kashfa ya Nyumba ya Sanaa
Mheshimiwa Spika, Nyumba ya Sanaa ilianzishwa mnamo 1972 kwa madhumuni ya kutoa mafunzo ya Sanaa kwa vijana, wanawake na wasiojiweza pamoja na kutafuta masoko ya Sanaa na kazi za mikono. Hata hivyo, kuanzia mwaka 1995 kumekuwepo hali ya kutoelewana baina ya wajumbe wa Bodi ya wadhamini baada ya kutiliana shaka wenyewe kwa wenyewe, pia kati ya Bodi ya Wadhamini na Wanachama waanzilishi wa Nyumba ya Sanaa.
Mheshimiwa Spika, matokeo ya hali hiyo ni kufunguliwa kwa kesi mahakamani. Katika kesi hiyo, iliyotolewa hukumu tarehe 24 Februari, 2005, Msajili aliamua kufuta rasmi usajili wa Bodi ya Wadhamini ya Nyumba ya Sanaa akiwataka wakabidhi mali na shughuli za NYUMBA kwa asasi mbadala. Uchunguzi uliofanywa na Kambi rasmi ya Upinzani umebaini kuwa tangu kutolewa kwa hukumu hiyo, Bodi haijawahi kukasimisha amali na majukumu ya Nyumba ya Sanaa kwa asasi mbadala, na badala yake imeendelea kuwepo na kupelekea Nyumba hiyo kuendeshwa kama kampuni binafsi kwa faida ya wajumbe wachache wa Bodi.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani ina taarifa kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo iliyofutwa na baadhi ya wajumbe wake wameleta mwekezaji ambaye wameshaingia naye ubia kimkataba, kwa ajili ya kujenga jengo la ghorofa katika eneo lenye jengo la sasa. Izingatiwe hapa kuwa mwekezaji atapaswa kulivunja au kubadilisha mfumo wa jengo la sasa la Nyumba ya Sanaa, ndipo aweze kujengwa la ghorofa.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani, inaitaka serikali na Bunge lako tukufu lizingatie yafuatayo; ·Tujue kuwa Nyumba ya Sanaa hivi sasa inawanufaisha wachache ambao si walengwa waliokusudiwa. Tufahamu kwamba wanufaika hawa hawana rekodi ya uwekezaji katika Nyumba ya Sanaa, hivyo wanavuna matunda yaliyopandwa na wengine hasa kupitia ushirikiano mwema baina ya serikali ya Tanzania (kupitia Ikulu), Norway (kupitia shirika la NORAD) na Uholanzi (kupitia shirika la NOVIB).
·Tutambue kuwa Nyumba ya Sanaa ilikuwa ni mlango wa masoko ya Sanaa na kazi za mikono, hivyo kutokuwepo kwake kunakwamisha juhudi za wazalishaji kazi za sanaa wa Tanzania kuweza kushiriki vyema masoko na hasa soko la pamoja la Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, kwa kuyazingatia yote hayo na kwa manufaa ya wadau wote wa Sanaa na taifa zima kwa ujumla, Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ichukue hatua zifuatazo kuhusiana na Nyumba ya Sanaa:-
Mheshimiwa Spika, kwanza tunataka Nyumba ya Sanaa irudishwe Serikalini kwa Mdhamini Mkuu wa Serikali ili mchakato wa uanzishwaji wa Bodi huru ya kusimamia malengo yake anuai ufanyike. Uhuishaji wa Nyumba ya Sanaa utachangia sana kuongeza ajira na pato la taifa, hivyo kupunguza tatizo la uzururaji na kilio cha masoko ya kazi za sanaa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tangu kufutwa kwake mnamo mwaka 2005, Nyumba ya Sanaa imeendelea kufanya biashara pamoja na kuingia mikataba ya biashara mpaka sasa, Kambi rasmi ya Upinzani tunaitaka serikali ifanye tathmini na ilipwe kodi kutokana na faida ya biashara zilizoendeshwa mara baada ya kusitishwa uendeshaji wake.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani tunaitaka Serikali isitishe mara moja uvunjwaji wa jengo lililopo sasa, kwani ni utalii na ni alama ya taifa inayoonyesha jinsi serikali za Norway na Tanzania zilivyothamini juhudi za wasanii na wazalishaji kujikwamua kiuchumi na kuchangia pato la Taifa. Tunataka Nyumba ya Sanaa ifufuliwe upya bila kubadili malengo yaliyopelekea kujengwa kwake, na badala yake kila kitu kiboreshwe kwa kuheshimu malengo yale yale.
Tunaamini Serikali hii inayojiita Serikali sikivu, itaheshimu matakwa ya Watanzania hususan Wasanii ambao pasipo shaka yoyote ile wanataka Nyumba yao irudi kwenye mikono salama kama tulivyopendekeza.
Ahadi ya Studio ya Wasanii
Mheshimiwa Spika, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kupitia Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano alitangaza kuwa amewapa Wasanii Studio ya kufanyia kazi zao. Hata hivyo, baadaye wananchi na wadau wengi wa sanaa, nikiwemo mimi binafsi, tulishangaa kusikia Studio hiyo wamepewa NGO binafsi ya Tanzania House of Talent (THT)! Pia Rais aliahidi na kutoa nyumba ya Serikali kwa Wasanii ambayo ingetumika kuendeshea Studio husika, lakini nyumba hiyo ya Serikali iliyotolewa na Rais sasa iko chini ya THT na ndio makao ya THT!
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inahoji, kwanini ahadi hizo zitolewe kwa kikundi kimoja tu cha THT, tena kilichojikita zaidi katika biashara ya kazi za Sanaa, wakati ahadi hizo za Rais zililenga Wasanii wote wa Tanzania? Kambi rasmi ya Upinzani inatambua na kuthamini mchango wa THT katika Sekta ya Sanaa ya nchi hii, lakini si sahihi kwa taasisi hiyo binafsi kupewa jukumu la kuhodhi Studio na Nyumba iliyotolewa na Rais kwa ajili ya Wasanii wote.
Mheshimiwa Spika, badala yake, Kambi rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa Studio na Nyumba hiyo iliyotolewa na Rais iwe chini ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)kwa manufaa ya Wasanii wote na si THT peke yao kama ilivyo sasa. Tunatahadharisha kuwa hili lisipozingatiwa, jina la Rais na hadhi ya Urais itachafuka kwa kuonekana kufanya kazi kwa maslahi ya watu binafsi (THT) badala ya kufanya kazi kwa maslahi ya umma (Wadau wa Sanaa).
SEKTA YA MICHEZO
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inaamini kuwa Michezo ni Afya, Michezo ni Burudani, Michezo ni Ajira na Michezo ni Uchumi. Hata hivyo, mwenendo na hali halisi ya Sekta ya Michezo nchini, vinadhihirisha kuwa sekta hii imekuwa ikichukuliwa kuwa ni ya burudani pekee. Timu zetu za taifa zifungwe au zitolewe kwenye michuano ya kimataifa, limekuwa ni jambo la kawaida, hakuna hatua zozote kali zinazochukuliwa kuwajibishana wala kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha hali ya kufanya vibaya haijurudii tena.
Mheshimiwa Spika, ushahidi kuwa Sekta ya Michezo haijapewa umuhimu unaostahili upo wazi. Taifa letu limeendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu, kwa timu zetu za taifa kuendelea kufanya vibaya na kuambulia mafanikio kidogo kwenye michuano ya kimataifa. Kama taifa tumeshindwa kuzalisha walimu wa kutosha wa michezo mbalimbali, na mbaya zaidi hata walimu wachache wazalendo hususan wa mpira wa miguu, wenye ujuzi na umahiri wa kuridhisha wamekuwa hawapewi motisha, pindi wanapoteuliwa kufundisha timu za taifa. Badala yake, Serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kuwapa ajira Walimu wa kigeni.
Kambi ya Upinzani inamtaka Mhe. Waziri alieleze Bunge katika kipindi chote timu ya taifa ya vijana ilipokuwa chini ya kocha Tinoco toka Brazil, mkataba wake kwa mwezi alilikuwa akilipwa kiasi gani na Kocha wa sasa Jamhuri Kiwelu (Julio) mzawa analipwa kiasi gani?
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ilieleze Bunge ni kwanini kocha wa netiboli, Simone Mcknnis raia wa Australia aliyetia saini Septemba mwaka jana kwa mkataba wa miaka mitatu kufundisha mchezo huo alikatiza mkataba wake na kuondoka kurudi kwao Australia kwa kile kilichoelezwa kuwa serikali kushindwa kutimiziwa masharti ya mkataba wake na haswa malipo yake.
Mheshimiwa Spika, mkakati wa kuagiza makocha kutoka nje, ni sharti uende sambamba na mpango wa kuwapatia ujuzi na uzoefu makocha wetu wa ndani ili pale makocha wa nje wanapoondoka tuweze kuwatumia makocha hao wazalendo kuendeleza michezo nchini.
Kambi ya Upinzani, inashauri kuwa pale ambapo makocha wa kigeni wanapoajiriwa nchini kufundisha timu mbalimbali basi wapewe sharti la kuwa na wasaidizi ambao ni wazawa ili mikataba yao itakapomalizika basi wazawa wabakie na ujuzi na kuweza kuendeleza michezo husika. Aidha, Kambi ya Upinzani inatoa hoja kuwa Bunge hili tukufu liweze kuutambua mchango mkubwa uliofanywa na makocha wazalendo na ikiwezekana waweze kupata nishani ya Bunge kutokana na mchango mkubwa kwenye sekta ya michezo.
Mheshimiwa Spika, miaka 50 baada ya Uhuru, Tanzania ina uwanja mmoja tu wenye hadhi ya kimataifa ambao ni Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam uliojengwa kwa msaada wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu. Lakini kiwanja hicho sawa na viwanja vingine nchini kimekuwa hakiendeshwi vizuri hata kulitia aibu taifa kwa huduma mbovu, ikiwemo ya kukatika kwa umeme kama ilivyotokea hivi karibuni wakati wa fainali za michuano ya Kombe la Kagame ambalo Tanzania ilikuwa mwenyeji. Mamlaka ya Viwanja vya Michezo ianzishwe. Mheshimiwa Spika, Serikali ianzishe Mamlaka ya Viwanja vya Michezo nchini, na kuipa jukumu la kusimamia na kuendesha viwanja vyote vya michezo vilivyopo. Aidha, Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya Serikali, ipewe jukumu la kuhakikisha kila mwaka inajenga Vituo vya Kisasa vya Mazoezi na Hosteli kwa ajili ya Wanamichezo, na angalau kiwanja kimoja kikubwa cha michezo chenye hadhi ya kimataifa inayolingana na hadhi ya Uwanja mpya wa Taifa uliopo Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, kwa pendekezo hilo, baada ya miaka tisa, nchi yetu itakuwa na jumla ya viwanja 10 vya kimataifa. Mbali ya kuchochea maendeleo ya michezo nchini na kuajiri Watanzania wengi kutoa huduma mbalimbali, Viwanja hivi pia vitakuza hadhi ya nchi na kuiwezesha nchi kukidhi vigezo vya kuwa Mwenyeji wa michuano mikubwa ya kimataifa kama kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN).
Mheshimiwa Spika, kwa hiyosanjari na mpango huo wa Ujenzi wa Viwanja vya Kisasa, Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuweka lengo la kuhakikisha Tanzania inakuwa Mwenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) mwaka 2018, na mwenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019. Aidha, Serikali iandae programu na kampeni kabambe ya kuhakikisha timu ya taifa ya mpira wa miguu (Taifa Stars) inaandaliwa vema na kupatiwa mechi nyingi na ngumu za kujipima nguvu, kwa ajili ya kuhakikisha inafuzu kuingia kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 iliyopangwa kufanyika nchini Brazil.
Mheshimiwa Spika, pili viwanja vyote vya michezo, kama Uwanja wa Majimaji Songea, Sheikh Amri Abeid Arusha, Uwanja wa Jamhuri Morogoro, Uwanja wa Jamhuri Dodoma, ule unaoitwa Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, na viwanja vingine vyote vilivyomilikishwa kwa CCM, virejeshwe Serikalini na viwe chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Michezo tunayotaka ianzishwe, ili viboreshwe na kutumika kwa maslahi ya Watanzania wote.
Mheshimiwa Spika, badala ya kutegemea tu vituo vya michezo vichache vilivyoanzishwa na sekta binafsi, Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iandae mpango wa kukuza vipaji vya wanamichezo wadogo kwa kuanzisha vituo vya michezo (Sports Academy) katika kila halmashauri kwa kushirikiana na Mamlaka ya Viwanja vya Michezo tuliyopendekeza ianzishwe.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hali mbaya ya sekta ya michezo nchini, bado zipo timu na wapo wachezaji ambao wamekuwa wajitutumua na kufanya vizuri kwenye ushindani wa kimataifa. Kambi rasmi ya Upinzani inachukua fursa hii kuzipongeza timu za soka za Simba na Yanga kwa kufanikiwa kufika fainali ya Kombe la Kagame baada ya kuzitoa timu nyingine za Afrika Mashariki na Kati.
LUGHA YA KISWAHILI NA UTAMADUNI WETU Mheshimiwa Spika, Kuhusu maendeleo ya Kiswahili, Tanzania inasifika kwa kuongea Kiswahili fasaha, lakini leo ukiingia katika tovuti yeyote duniani, ukiuliza Kiingereza utaambiwa asili yake ni Uingereza, Kifaransa asili yake Ufaransa, Kijapan asili yake Japan, Kijerumani asili yake Ujerumani, Kispanyola asili yake Hispania, lakini unapouliza Kiswahili, wanasema asili yake ni Kenya.
Mheshimiwa Spika, elimu bora hutolewa kwa lugha ya taifa inavyosemwa na karibu kila mtu, na lugha hiyo hapa kwetu ni lugha ya Kiswahili. Kwa mujibu wa wataalamu na watafiti wa masuala ya lugha na maendeleo(Kwa mfano Prof. Kahigi), ni kwamba hakuna nchi yoyote Duniani ambayo imeendelea kwa lugha ya kukopa. Hivyo basi, Tanzania haiwezi kuendelea kwa kutumia lugha ya Kiingereza tuu katika kutoa elimu kwa vijana wetu kwa hiyo lugha zote mbili zitumike kikamilifu katika kufundishia. Hata hivyo, Kambi ya Upinzani tunapongeza taasisi zote ambazo zimeendelea kukikuza Kiswahili.
Mheshimiwa Spika, hivi tumeshindwa hata kulinda huu utamaduni wetu wa asili? Kwa sababu hata juhudi ambazo Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) wanazifanya kuendeleza Kiswahili duniani, zinaishia kutolisaidia taifa kwa sababu ya mtazamo wa serikali juu ya lugha ya kufundishia shule za sekondari na vyuo vya juu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya kambi ya upinzani, naomba kuwasilisha............................
Joseph O. Mbilinyi (Mb)Waziri Kivuli Habari, Utamaduni, Michezo na Vijana
11.08.2011