Candid Scope
JF-Expert Member
- Nov 8, 2010
- 11,897
- 6,933
Mkutano wa Kumi wa Bunge unaanza leo huku kukiwa na viporo vilivyochacha vya hoja, miongozo na taarifa mbalimbali za wabunge ambazo zimeibuka tangu Bunge la Kumi lilipoanza mwaka 2011.Itakumbukwa pia, ni katika Mkutano huu mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, atawasili bungeni baada ya kusimama kwa takribani mwaka mmoja tangu Mahakama ilipotengua ubunge wake Aprili 4, mwaka jana.Baadhi ya viporo hivyo ni kile cha Februari 10, 2011 cha mbunge huyo alipotakiwa na Spika kuwasilisha ushahidi wa kauli yake aliyosema kwamba mbunge anaweza kuchukua hatua gani ikiwa atabaini kiongozi mkuu wa serikali amelidanganya Bunge.
KIPORO CHA LEMA
Lema alitaka ufafanuzi huo wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. Lema alilazimishwa kuwasilisha ushahidi bungeni kwa kauli yake hiyo kwa kuwa ilionekana kama alikuwa akimtuhumu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa kuwa aliomba ufafanuzi baada ya kujibiwa swali lililohusu maandamano ya Chadema yaliyofanyika Arusha Mjini Januari 5, 2011.
Ilikuwa katika kikao cha tatu cha Mkutano wa Pili wa Bunge Lema alipoomba kupata ufafanuzi kwamba Mbunge anaweza akachukua hatua gani kama anaona mtu mwenye nafasi kubwa katika nchi kama Waziri Mkuu analidanganya taifa na kulidanganya Bunge. Baada ya kauli hiyo, Spika Anne Makinda, alingaka na kusema: Mheshimiwa Mbunge, Bunge hili lazima liwe na adabu inayostahili. Kwa hiyo kama tutafanya Bunge letu hili ikawa ni mahali, sasa unataka kusema Waziri Mkuu kwa ahadi aliyoweka ndani ya Bunge hili anadanganya? Kama anadanganya naomba ukaiandike vizuri kabisa kuhusu kudanganya kwake, halafu nitakuambia tufanye nini. Spika alitoa siku nne kwa Lema kuwasilisha maelezo yake na Februari 14, 2011, mbunge huyo aliwasilisha maelezo, lakini hadi sasa umma haukuwahi kuelezwa ninini hasa kiliamuliwa au nini ukweli wa kauli ya Pinda au Lema.
KIPORO CHA OPULUKWA
Kiporo kingine ni kile cha Juni 19, mwaka jana baada ya mbunge wa Meatu (Chadema), Meshack Opulukwa, kumlipua Mkuu wa Wilaya ya Momba, Abihudi Saideya, bungeni kuwa yeye na Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo walihongwa gari la kifahari aina ya Toyota Land Cruiser GX na mwekezaji wa Kampuni ya Mwiba Holding ili awahamishe wananchi wa kijiji cha Makao kwenye eneo la hifadhi tengefu (WMA).
Opulukwa alitoa madai hayo bungeni alipokuwa akiuliza swali la nyongeza kwa Wizara ya Maliasili na Utalii. Alisema kuwa Saideya alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Meatu, alihongwa gari hilo aina ya GX lenye namba za usajili T 147 ASX na kampuni hiyo ili awaondoe wananchi katika eneo hilo. Mara baada ya kumaliza kuuliza swali hilo, alisimama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, na kuomba mwongozo wa Spika. Lukuvi alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge, Mbunge haruhusiwi kumzungumzia bungeni mtu ambaye hawezi kujitetea ndani ya Bunge. Alitaka Mbunge huyo kupeleka vielelezo na ushahidi wa tuhuma hizo kwa sababu serikali haiwezi kumvumilia mkuu wa wilaya anayehongwa.
Katika uamuzi wake, Naibu Spika, Job Ndugai, alimpa siku saba Opulukwa kuwasilisha vielelezo vinavyothibitisha kuwa Mkuu huyo wa Wilaya na mkuu wa polisi wa wilaya walihongwa gari.Mheshimiwa Opulukwa ameongea kwa uhakika mambo haya na ametaja jina la mtu, namuomba ama namtaka ndani ya siku saba alete vielelezo vinavyothibitisha jambo hilo kuwa wamehongwa gari, alisema Ndugai. Opulukwa alikiri kwamba anao ushahidi ambao aliuwasilisha mezani kwa Spika, lakini hadi leo hakuna taarifa zozote.
KIPORO CHA LISSU
Jambo lingine ambalo halijapatiwa ufafanuzi kutoka mezani kwa spika ni lile la Julai mwaka jana la Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, kutakiwa kuwasilisha vielelezo vya kuthibitisha kwamba Rais Jakaya Kikwete aliteua majaji wa Mahakama Kuu bila kushauriwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.Lissu alitoa taarifa hiyo alipokuwa akiwasilisha hotuba ya kambi hiyo alipokuwa akitoa maoni ya kambi ya Upinzani katika makadirio ya Wizara ya Katiba na Sheria ya mwaka 2012/13.
Katika maoni hayo ya Upinzani, Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, alisema madhara ya ukiukwaji huo wa Katiba katika uteuzi wa majaji wa Mahakama Kuu ni makubwa na yameanza kujitokeza wazi.Madhara hayo kwa mujibu wa madai ya Lissu, ni kuwapo kwa majaji ambao kwa sababu ya kutofanyiwa usaili na Tume ya Utumishi wa Mahakama, hawana uwezo wa kuandika mwenendo wa mashauri na hukumu zinazosomeka kutokana na ama kutokuwa na uwezo na ujuzi wa sheria au kutokuwa na weledi wa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo lugha rasmi.
Julai 13, mwaka jana Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama alilazimika kutumia Kanuni ya 2 ya Bunge, kuamuru suala hilo kupelekwa kwenye Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.Kutokana na maneno hayo dhidi ya majaji, Naibu Spika Job Ndugai aliyekuwa akiongoza kikao cha Bunge, alimuagiza Lissu awasilishe waraka maalumu ili kuomba kufuta maneno hayo.Pamoja na kupewa agizo hilo, Lissu hakuwasilisha waraka wowote kwenye meza ya Katibu wa Bunge ili kuthibitisha au kufuta maneno hayo badala yake alisema pamoja na kuelewa umuhimu wa majaji, lakini hawezi kuondoa maneno yaliyopo kwenye hotuba yake kwa vile taratibu na mwenendo mzima uliotumiwa na Kiti cha Spika hazikufuatwa hatua iliyomfanya Mhagama kuamuru suala hilo kupelekwa kwenye Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
KIPORO CHA MNYIKA
Suala lingine ni lile la Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, kufikishwa katika Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, baada ya kumtuhumu Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba, kwamba alihusika na wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
KIPORO CHA MSIGWA
Suala lingine ni lile la ujangili lililoibua mvutano baina ya Kambi ya Upinzani bungeni na Kiti cha Spika kwa upande mmoja na kambi hiyo na wabunge wa CCM.Akiwasilisha hotuba ya kambi hiyo Agosti 9, mwaka jana, Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, alimtuhumu mmoja wa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyemtaja kwa jina moja la Lazaro kwamba ni mshirika wa ujangili. Katika hotuba hiyo Msigwa alimtaja Lazaro kwamba anamiliki silaha aina ya Rifle 375 na kwamba ni mshirika wa mtandao mkubwa wa ujangili nchini unaoongozwa na mtu aliyemtaja kwa jina la Bryson Baloshingwa.
Alisema Baloshingwa ni kiongozi wa mtandao wa ujangili kwa kufadhili uwindaji wa faru na biashara haramu ya meno ya tembo; uharamia unaofanyika katika hifadhi za Serengeti, Katavi, Tarangire, Ziwa Manyara na Ngorongoro.Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alikanusha tuhuma zilizotolewa na Msigwa akieleza kwamba Lazaro aliyetajwa kuwa ni Mwenyekiti wa CCM wilayani Karatu si kweli kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Karatu ni John Tipa.Alisema kiongozi huyo hana silaha yoyote na wala hahusiki na ujangili au uharamia wowote.Alisema anachofahamu ni kwamba Lazaro aliyetajwa anaweza kuwa ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu (Chadema).Alisema taarifa zinaonyesha kwamba Februari mwaka 2010, gari yenye namba SM 4117 mali ya Halmashauri ya Karatu inayoongozwa na Chadema ilikamatwa na nyara za serikali zilizokuwa zikisafirishwa na Diwani wa Kata ya Lotya (Chadema) pamoja na Ofisa Wanyamapori wa Halmashauri hiyo na watu wengine saba.
Lukuvi ambaye alisimama kuomba mwongozo wa Spika ili kumtaka Msigwa athibitishe au afute tuhuma hizo, alikitaka pia kiti cha Spika kisimamie kanuni za Bunge ili kikomeshe tabia ya baadhi ya wabunge kuwatuhumu baadhi ya wananchi ambao hawana uwezo wa kujitetea ndani ya Bunge.Akieleza kuhusu mwongozo huo, Naibu Spika, Job Ndugai, alionya tabia ya wabunge kuwatuhumu viongozi au wananchi ambao hawana uwezo wa kujitetea ndani ya Bunge kwa kuwa ni kinyume cha kanuni.Alisema kutokana tuhuma hizo, atapeleka hotuba ya Msigwa kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili iijadili na kushauri hatua za kuchukua dhidi ya Msigwa na wabunge wengine wenye tabia ya kutaja majina ya watu wasio wabunge ndani ya Bunge. Mwongozo huo haukuwahi kutolewa ufafanuzi.
KIPORO CHA CHC
Hoja nyingine ni ile ya kulituhumu Baraza la Mawaziri kwamba lilirubuniwa ili kuliongezea muda Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC).
Kauli hiyo ilitolewa Julai, 2011 na ushahidi uliwasilishwa kwa Spika Makinda, lakini uamuzi ni kama uliwekwa kapuni hadi sasa.
KIPORO CHA MA-DC KUPORA MIFUGO
Hoja nyingine ni ile ya Julai 6, 2011 ya mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Magdalena Sakaya, ya ushahidi wa tuhuma kwamba baadhi ya wakuu wa wilaya wanakwenda katika mazizi ya mifugo ya wananchi na kujichukulia wanyama kwa ajili ya kitoweo kama wanavyopenda.Sakaya alikuwa akichangia hotuba ya bajeti ya makadirio ya matumizi kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma pamoja na Uhusiano na Uratibu katika mwaka wa fedha wa 2011/12.Katika mchango wake, mbunge huyo aliwalaumu baadhi ya viongozi kwa kutozingatia utawala bora na kwamba hali ilivyo inaashiria kuwa wakuu wa wilaya wanaweza kutumia nafasi zao kuwadhulumu wananchi wao.Alisema viongozi wa aina hiyo wanaweza hata kwenda kwenye mazizi ya mifugo ya wananchi wa wilaya yake na kuchukua ndafu kwa ajili ya kitoweo.
Lakini baada ya Sakaya kumaliza kuchangia, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika, alisimama na kusema yeye ndiye mwenye dhamana ya wakuu wa wilaya na kwamba hajawahi kusikia au kupata malalamiko ya namna hiyo.Kufuatia hali hiyo, Mkuchika alimuomba Mwenyekiti wa Bunge, Silvester Mabumba (Dole-CCM), amuamuru Sakaya athibitishe usemi wake.Mabumba alimtaka mbunge huyo kuthibitisha na bila kuchelea, alisema hana wasiwasi kuhusu kauli yake na siku iliyofuata, mbunge huyo aliwasilisha ushahidi, lakini hadi sasa bado uamuzi haujawekwa hadharani.
Wakati huo huo, Mkutano wa Kumi wa Bunge unaanza leo mjini Dodoma kwa kipindi cha maswali na majibu; na baada ya hapo Bunge litaahirishwa ili kuruhusu kikao cha Kamati ya Uongozi kukaa na kupanga ratiba ya mkutano huu.Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Deogratias Egidio, alisema ratiba ya mkutano huu ilishindwa kupangwa jana kwa kuwa viongozi wakuu wa kamati ya uongozi walikuwa na udhuru wa kikazi.Alisema Spika wa Bunge, Anne Makinda, yupo Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo (DRC) kikazi wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, yupo ziara ya kikazi mkoani.Alisema hata idadi ya wabunge waliowasili Dodoma ni ndogo. Kufuatia hali hiyo, Kamati ya Uongozi itakutana leo baada ya
kipindi cha maswali na majibu huku pia kamati za vyama vya siasa zikikutana.
Mkutano wa Kumi wa Bunge unatabiriwa kuwa na hoja mbalimbali ikiwamo ya ujangili ambayo inatarajiwa kuwasilishwa na Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa. Aidha, Mbunge wa Arusha Mjini, Lema, anatarajiwa kulitikisa Bunge atakapowasili kwa mara ya kwanza tangu aliporejeshwa na Mahakama ya Rufani baada ya matokeo ya ubunge wake kutenguliwa na Mahakama Kuu kanda ya Arusha, Aprili mwaka jana.